Tuesday, June 4, 2024

MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI UGANDA-TANZANIA WAFIKIA ASILIMIA 29.

 

Na Alodia Babara, Bukoba

Mradi wa bomba la mafuta ghafi unaotekelezwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani  Tanga nchini Tanzania umefikia asilimia 29.


Mradi huo ambao utagharimu zaidi ya  sh.trilioni 8 ulisainiwa mkataba wake mwaka 2021 kati ya Rais wa Uganda Yowel Kaguta Museven pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, mradi unaendelea kutekelezwa na umefikia asilimia 29.


Afisa katika kitengo cha mawasiliano bomba la mafuta EACOP Abass Abraham akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani Kagera June 03, mwaka huu juu ya mwongozo kuhusu mradi wa bomba hilo amesema kuwa, hadi sasa mabomba yaliyopokelewa ni ya kusambaza umbali wa kilomita 500 na kituo cha kupokea mabomba na kuyaboresha kiko mkoa wa Tabora.


"Asilimia 80 ya bomba la mafuta ziko nchini Tanzania na asilimia 20 ziko upande wa Uganda, kwa Uganda ni kilomita 296 na upande wa Tanzania ni kilomita 1,147 bomba litapita katika wilaya nane"amesema Abraham


Abraham ameeleza kuwa, bomba litafukiwa ardhini ili kukwepa athari za kimazingira, vitajengwa vituo sita vya kusukuma mafuta ili mafuta yaweze kufika kwa wakati Tanga na mafuta kuweza kuingia kwenye matenki ambapo vituo viwili vitakuwa nchini Uganda na vinne vitakuwa hapa nchini Tanzania.


Akizungumzia upande wa fidia amesema hadi kufikia Januari,2024 asilimia 99 ya waguswa wa mradi walikuwa wameshapata fidia kwa Tanzania na idadi ya waguswa ni zaidi ya watu 8,363 miongoni mwao waliojengewa nyumba ni waguswa wapatao 339 na kufikia Machi,2024 walikuwa wamekabidhiwa nyumba hizo.


Kwa Kagera waguswa hao toka mwaka jana wanasaidiwa kutayarisha mashamba kupata pembejeo hadi hatua ya kuvuna na wanasaidiwa ufugaji mdogo mdogo mfano, mbuzi na ngombe, kabla ya program hiyo waguswa walikuwa wanapewa chakula.


Aidha, baada ya mradi huo kuanza itatumika nguvu ya aina tatu ya umeme ili mradi usiweze kukwama katika kusukuma mafuta ghafi ikiwemo, umeme wa Tanesco, generator pamoja na umeme wa nguvu ya jua (solar).


Gharama za kukamilisha ujenzi wa mradi wa bomba zinatarajiwa kufikia takribani shilingi trilioni 8 za Kitanzania, bomba hilo litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya China na TULLOW ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)


No comments:

Post a Comment