Wednesday, June 5, 2024

MOTO WATEKETEZA BWENI BUKOBA

 


Na Alodia Babara, Bukoba,

Bweni la wavulana katika shule ya sekondari Mugeza Mseto iliyopo kata ya Kahororo manispaa ya Bukoba mkoani Kagera limeteketea kwa moto na mali zote zilizokuwemo kuungulia humo chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.


Kaimu kamanda wa jeshi la zima moto na uokoaji mkoa wa Kagera George Mrutu akizungumzia tukio hilo Juni 05, mwaka huu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, limetokea Juni 04, mwaka huu saa 8:15 usiku wakati wanafunzi wakiwa darasani wanajisomea.


Mrutu amesema kuwa, jeshi hilo lilipokea taarifa kupitia simu yao ya 114 kutoka kwa mkuu wa shule juu ya kuwepo tukio la moto katika shule hiyo ndipo kikosi cha zimamoto kilielekea eneo la tukio walifika na kukuta moto ukiwa umeshasambaa kwenye bweni zima na kuanza juhudi za kuuzima.


“Baada ya kufika tulikuta moto umeshasambaa bweni zima miali ya moto ikiwa inatokea madirishani moto umeshashika kwenye paa tulifanya juhudi za kuuzima moto huo ili usiendelee kuleta madhara, hatukuweza kubaini chochote kwa kuwa ilikuwa usiku hivyo tunaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hili ili kubaini chanzo” amesema Mrutu.


Amemtaja mwangalizi wa wanafunzi (Matron) katika shule hiyo Savera Revelian ambaye alipata mshtuko na kukimbizwa hospitali.

Aidha ameongeza kuwa, bweni hilo lina uwezo wa kulaza wanafunzi 100 lakini wakati linaungua walikuwa wanalala wanafunzi 58 wa kidato cha pili 28 na kidato cha nne 30 kutokana na kwamba wengine wapo likizo.


Aidha Mrutu amezitaka shule zote kuwepo walinzi maeneo ya shule ili kuweza kudhibiti kama kuna watu wanaingia mabwenini wanafunzi wakiwa madarasani.


Kwa upande wake, afisa elimu sekondari manispaa ya Bukoba Frances Nshaija ameeleza kuwa, baada ya kufika eneo la tukio moto ulikuwa unaendelea kuzimwa na jeshi la zimamoto, yeye kwa kushirikiana na uongozi wa shule waliwaweka wanafunzi eneo salama la kulala.


Baadhi ya wananchi waliomba serikali kupitia jeshi la zimamoto na uokoaji baada ya kubaini chanzo cha moto huo waweke mikakati ya kudhibiti moto katika mabweni na kusababisha hasara.


Matukio ya moto kuunguza mabweni yamekuwa yakitokea mara kwa mara mkoani hapa ambapo mwaka jana lilitokea tukio la moto katika shule ya sekondari Omumwani na kuteketeza mali zote zilizokuwa katika bweni.


No comments:

Post a Comment