Tuesday, June 4, 2024

RUNALI YAWAJENGEA WAKULIMA  KITUO CHA MALIPO RUANGWA 

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.

HATIMAYE ucheleweshwaji wa Fedha za malipo ya wakulima wa Wilaya ya Ruangwa wanaohudumiwa na chama kikuu cha Ushirika Runali kinachojumuisha wakulima wa Wilaya za Ruangwa, Liwale na Nachingwea mkoani Lindi, itabaki historia baada ya chama hicho kujenga kituo cha malipo kitakachotumika kuandaa na kuhakiki malipo ya wakulima hao kwa haraka zaidi.

Kituo hicho cha malipo kimejengwa katika Kata ya Lipande  Wilayani Ruangwa ambapo kimewekwa jiwe la msingi na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack  na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali Wilayani humo pamoja na viongozi wa vyama vya Msingi, Amcos za Mkoa wa Lindi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Katibu Tawala wa Mkoa huo (RAS) Zuwena Omary baada ya kukagua jengo hilo na kuweka jiwe la msingi amekipongeza chama hicho kwa namna kinavyoendelea kuwekeza na kutoa huduma bora kwa wanachama wake kwa kuzikabili changamoto wanazokutana nazo.

Pamoja na pongezi hizo  pia aliutaka uongozi wa Bodi wa chama hicho cha Runali kutunza mradi huo na kuutumia kama walivyokusudia na kuendelea kusogeza  huduma hiyo katika maeneo ambayo yana wanachama wao na wakulima wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Chama kikuu cha Ushirika RUNALI, Jahida Hasani alisema kuwa ujenzi huo wa kituo cha malipo mpaka kukamilika kwake utagharimu Sh milioni 110  na kwamba kitaanza kutumiwa na viongozi hao katika msimu huu wa Ufuta.

" katika eneo hili pamoja na ujenzi wa kituo hiki umeenda sambamba na uwepo wa ghala kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi mazao  tani elfu 10 kwa pamoja  lakini pia kama chama tunamuendelezo wa kujenga hivi vituo ambapo tumejenga Nachingwea,  tumejenga Liwale na sasa ni hapa Ruangwa "

Nae Mwenyekiti wa chama kikuu hicho Odas Mpunga amesema  kuwa lengo kubwa la kujenga kituo hicho ni kuendelea kuwaweka pamoja viongozi na watendaji wa vyama vya msingi (AMCOS) kuchakata na kurahisisha mchakato wa malipo ya wakulima.

Hata hivyo Mpunga ameeleza kuwa  chama hicho  kinaendelea na uwekezaji kwa kununua lori aina ya Scania lenye uwezo wa kubeba Tan 20 za mazao ya wakulima kwa pamoja kutoka shambani mpaka kwenye maghala.






No comments:

Post a Comment