Monday, June 17, 2024

RC LINDI AZIAGIZA HALMASHAURI KUANZISHA NA KUHUWISHA MADAWATI YA ULINZI MASHULENI

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.



Mkuu wa Mkoa wa Lindi ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha zinafufua au kuunda madawati ya ulinzi ya watoto  sambamba na kuunda klabu za watoto mashuleni zitakazowasaidia kuelezea na kutatua changamoto zao


Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa huko katika kijiji cha chienjele halmashauri ya Ruangwa Jana Juny 16/2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi , Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Patrick Sawale  amesema vyombo hivyo ni  muhimu  kwa ajili ya kutetea maslahi yao pindi watoto wanapokuwa wamefanyiwa ukatili. 



Amesema ili Taifa liweze kuendelea kupiga hatua ni muhimu kutilia maanani mahitaji  ya watoto  ikiwa pamoja na watoto  masikini , walemavu na walio na mazingira magumu zaidi kutengewa mafungu toka katika bajeti kuu ya serikali na zile za Halmashauri.



hata hivyo ameendelea  kuikumbusha Jamii kuwa inawajibu wa  kutoa taarifa na ushahidi kuhusu mtoto ambae haki zake zinakiukwa na wazazi na walezi au ndugu yoyote kwenye  serikali za mitaa na kwenye vyombo vya dola kwa vitendo vya ulawiti, ubakaji na ukatili  wanaofanyiwa  watoto  ili serikali ichukue hatua na adhabu zitolewe.



Akitoa salamu za Wilaya ya Ruangwa Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Ngoma amesema siku hiyo ya Mtoto wa Afrika ni muhimu kwa Nchi za Afrika kutathimini na kueleza Dunia mabadiliko Makubwa yaliyofanywa na Nchi hizo Katika kuwapambania watoto hao Katika kuondoa changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rangi unyanyapaa Elimu na kadhalika


 


Awali afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Lindi ndugu Charles Kigahe alieleza changamoto kadhaa zinazowakabili watoto wa Mkoa huo wa Lindi 


Miongoni changamoto hizo ni pamoja na Watoto kutotimiziwa haki ya kupata elimu, hii imetokana na wazazi kutoona umuhimu wa kuwafuatilia watoto pindi wakiwa shuleni ambapo imesababisha watoto kuacha shule.



Watoto kukosa malezi ya wazazi, hii imetokana na wazazi kutengana ambapo mtoto anaendelea kulelewa na mzazi mmoja au bibi. Watoto kukosa mahitaji ya msingi kwa sababu ya kutoelewana kwa wazazi,

Watoto kufanyiwa ukatili wa kingono.



Changamoto nyingine ni Migogoro ya ndoa kwa wazazi,  ambapo wazazi wanaachana inapelekea mtoto kuendelea kuhangaika na hatimaye kuacha shule.

Wazazi na walezi hawatimizi wajibu wao wa kuwalea watoto ambapo inasababisha kuongezeka kwa watoto wa mtaani.


Kauli mbiu ya siku ya Mtoto wa Afrika 2024 ni Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maadili, maarifa na stadi za kazi










Wednesday, June 12, 2024

SERIKALI YAENDELEZA JITAHADA ZA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA TEMBO

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na utalii imeendelea kujenga vituo  kupeleka asikari wa wanyama pori pamoja na vitendea kazi Katika maeneo yote yenye changamoto ya wanyama wakali na waharibifu aina ya Tembo ili kukabiliana na changamoto hiyo


Hayo yameelezwa na Mratibu wa Mradi wa kutatua changamoto ya migongano baina ya binaadamu na Wanyama pori unaotekelezwa Katika wiliya za Liwale Mkoani Lindi, Namtumbo na Tunduru Mkoani Ruvuma Bw.Gideon Mseja alipokuwa anafungua mafunzo ya siku moja kwa waadishi wa vyombo mbalimbali vya habari yaliyofanyika huko Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma


Mafunzo hayo yamewakutananisha waandishi 10 kutoka Katika Maeneo ya utekelezaji wa Mradi maafisa habari wa halmashauri , wawakilishi kutoka kitengo cha  mawasiliano wizara ya maliasili na utalii pamoja na maafisa Wa Serikali 



Amesema changamoto hiyo ya wanyama wakali na waharibifu imeathiri Katika wilaya 44 ambapo Serikali imeendelea kuchukua Hatua mbalimbali Katika kukabiliana nayo ikiwa ni pamoja na kufanya Doria za mara kwa mara kujenga vituo vya asikari wa wanyama pori.


Jitihada zingine ni pamoja na kuwezesha vifaa vya kuondoa tembo maeneo ya wananchi, kufuatilia mienendo ya wanyamapori, kutumia helikopta na mabomu baridi kuwaondoa tembo kwenye makazi, kuwezesha wananchi kiuchumi na kutoa elimu ya tabia ya tembo na mbinu ya kutatua migongano hiyo kwa jamii ili kujenga uhimilivu wa matukio hayo.


"Lakini pia Serikali imekuwa ikifuatilia mienendo ya wanyama kuona mzunguko wao ambapo  kupitia  TAWIRI Tembo wamefungwa vifaa vinavyoweza kutoa taarifa mapema endapo wanyama wanakaribia Maeneo ya Jamii basi asikari waweze kusogea pale ili wanyama hao wasisababishe madhara kwa wananchi"


Hata hivyo ameongeza kuwa Katika kuendelea kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imeanzisha Mradi wa mashirikiano kati ya Tanzania na ujerumani unaolenga kutatua migongano baina ya Binaadamu na Wanyama pori  unaotekelezwa kwenye ukanda wa Ruvuma unaolenga kutoa elimu ya namna sahihi ya kuandika habari zinazohusu migongano hiyo  kwa usahihi


Kwa upande wake Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa habari za mazinginra (JET) Bw.John Chikomo amesema Mradi huo wa kudhibiti migongano baina ya binadamu na Wanyama pori upo chini ya   wizara ya maliasili na utalii kupitia ufadhili  wa Serikali ya Ujerumani  (MBZ) kupitia Shirika la maendeo la ujerumani (GIZ) unatekelezwa na (JET) kwa kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuripoti vyema habari hizo za migongano baina ya Binaadamu na Wanyama pori


"Mradi huu utawawezesha waandishi wa habari kuweza kuandika habari hizo kwa usahihi ili wananchi wanaoishi Katika Maeneo ya shoroba za wilaya hizo tatu wapate uelewa wa kujua namna gani ya kupambana na hiyo Hali ambayo wanakutana nayo"


" Ni wazi kuwa maswala haya ya migongano baina ya binadamu na Wanyama pori yamekuwa ni mengi kwenye magazeti tunasoma, kwenye TV tunaona kwamba Kumekuwa na ongezeko la wanyama kuingia Katika Maeneo ya makazi, mashamba kwa hivyo lengo kubwa ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa Tanzania hususani wa wilaya hizi waweze kuandika habari za ufasaha zaidi bila kuleta taharuki kwa wananchi hao" alisema Chikomo




Kwa Upande wake Mtaalam Mshauri wa Mradi huo  wa kutatua  Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori kutoka  Shirika la maendeo la ujerumani GIZ, Bi. Ana Kimambo alitumia fursa hiyo kuwaasa waandishi wa habari waliopatiwa mafunzo , kuyatumia mafunzo hayo Katika kuleta matokeo chanya Katika Jamii zao kwa kuandika habari zenye usahihi




" Baada ya mafunzo haya tutapenda kuona sasa taarifa zile zinazo ripotiwa hasa  ukanda huu zinakuwa na mabadiliko ya kuelimisha zaidi pamoja na kufikisha ujumbe wa uhalisia , hakikisha unachokiandika  unaandika kwa usahihi kulingana na taarifa yenyewe ilivyo"


Kumekuwa na upotoshaji unaofanywa na baadhi ya waandishi wa habari ambao ndio unaozua taharuki kwa wananchi na hiyo ndio inayopelekea wananchi waweze kuona kuwa haya matukio kwamba yana ukubwa zaidi tofauti na uhalisia wenyewe  usiiandike Tu kwa sababu unataka gazeti lako liweze kuuzwa,  amesema waandishi hao wanapatiwa mafunzo hayo ili wanapoenda kwenye Jamii waweze kuielimisha kwa ufasaha



Kwa upande wake Joyce Joliga mwandishi wa habari wa Gazeti la mwanachi amesema kupitia mafunzo hayo ameeleza kujifunza namna Bora ya kuandika habari hizo za migongano ya Binaadamu na Wanyama pori kwa weledi tofauti na hapo awali ambapo alikuwa akiandika habari hizo kwa kutumia uzoefu wa uandishi wa habari kimazoea








WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO KWA WATUMISHI WA UMMA

 

Awataka waondoe urasimu na kutowasumbua wananchi wanaowahudumia

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini kote wawatumikie wananchi ipasavyo na wahakikishe wanaondoa urasimu kwa kutowasumbua wananchi wanaokuja kupata huduma za kiserikali katika ofisi zao.


“Epukeni tabia ya kuomba na kupokea rushwa, rushwa inaharibu maendeleo. Tusitumie maneno magumu kwa wananchi wetu maana eneo hili bado ni changamoto, tunalishughulikia au bado tupo kwenye mchakato, tunafanya tathmini, upembuzi yakinifu, tumieni lugha rahisi.“


Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wazingatie taaluma zao na watoe ushauri kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, wafike sehemu ya kazi kwa muda uliopangwa na watumie muda huo kufanya kazi za Serikali na waepuke kuwa na migongano ya maslahi katika kutekeleza majukumu na kusimamia rasilimali za umma.


Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 12, 2024) kwenye Mkutano Mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania (TOA) unaofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.


“Viongozi wote tuwahudumie wananchi kwa heshima, staha, unyenyekevu na umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwapa majibu sahihi ya maswali yao na majawabu sahihi ya kero zinazowasumbua. Toeni ufafanuzi au maelekezo juu ya masuala yatokanayo na sheria, kanuni na taratibu za Serikali kwa haraka, uwazi na bila upendeleo wowote au ubaguzi wa aina yoyote.”


Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo na huduma mbalimbali za msingi.


Amesema chombo muhimu cha kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wa ngazi ya msingi ni Mamlaka za Serikali za Mitaa na maendeleo hayo yatakuwa dhahiri na endelevu endapo wananchi watashirikishwa katika kuainisha changamoto zinazowakabili na watawezeshwa kukabiliana nazo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.


Pia, Waziri Mkuu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanakuwa na mifumo madhubuti ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato pamoja na kuweka mkakati wa udhibiti wa mali zilizopo ndani ya halmashauri na mapato watakayoyapata wayaelekeze katika kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri zao.





RAIS DK.MWINYI AISHUKURU TAASISI YA AL MAZRUI

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Al Mazrui Charitable Organisation ya Abu Dhabi kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya , elimu na maji.


Pia ameishukuru taasisi hiyo  kwa kutoa jengo lao kwa Serikali ilitumie kwa huduma za afya.


Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo akizungumza na vijana wa Chuo cha ufundi Mubarak AL Mazrui  na alipotembelea eneo hilo Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe :11 Juni 2024.


Aidha Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imetoa kibali cha kuajiri vijana waliokuwa wanajitolea katika mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwemo Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).


Wednesday, June 5, 2024

MOTO WATEKETEZA BWENI BUKOBA

 


Na Alodia Babara, Bukoba,

Bweni la wavulana katika shule ya sekondari Mugeza Mseto iliyopo kata ya Kahororo manispaa ya Bukoba mkoani Kagera limeteketea kwa moto na mali zote zilizokuwemo kuungulia humo chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.


Kaimu kamanda wa jeshi la zima moto na uokoaji mkoa wa Kagera George Mrutu akizungumzia tukio hilo Juni 05, mwaka huu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, limetokea Juni 04, mwaka huu saa 8:15 usiku wakati wanafunzi wakiwa darasani wanajisomea.


Mrutu amesema kuwa, jeshi hilo lilipokea taarifa kupitia simu yao ya 114 kutoka kwa mkuu wa shule juu ya kuwepo tukio la moto katika shule hiyo ndipo kikosi cha zimamoto kilielekea eneo la tukio walifika na kukuta moto ukiwa umeshasambaa kwenye bweni zima na kuanza juhudi za kuuzima.


“Baada ya kufika tulikuta moto umeshasambaa bweni zima miali ya moto ikiwa inatokea madirishani moto umeshashika kwenye paa tulifanya juhudi za kuuzima moto huo ili usiendelee kuleta madhara, hatukuweza kubaini chochote kwa kuwa ilikuwa usiku hivyo tunaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hili ili kubaini chanzo” amesema Mrutu.


Amemtaja mwangalizi wa wanafunzi (Matron) katika shule hiyo Savera Revelian ambaye alipata mshtuko na kukimbizwa hospitali.

Aidha ameongeza kuwa, bweni hilo lina uwezo wa kulaza wanafunzi 100 lakini wakati linaungua walikuwa wanalala wanafunzi 58 wa kidato cha pili 28 na kidato cha nne 30 kutokana na kwamba wengine wapo likizo.


Aidha Mrutu amezitaka shule zote kuwepo walinzi maeneo ya shule ili kuweza kudhibiti kama kuna watu wanaingia mabwenini wanafunzi wakiwa madarasani.


Kwa upande wake, afisa elimu sekondari manispaa ya Bukoba Frances Nshaija ameeleza kuwa, baada ya kufika eneo la tukio moto ulikuwa unaendelea kuzimwa na jeshi la zimamoto, yeye kwa kushirikiana na uongozi wa shule waliwaweka wanafunzi eneo salama la kulala.


Baadhi ya wananchi waliomba serikali kupitia jeshi la zimamoto na uokoaji baada ya kubaini chanzo cha moto huo waweke mikakati ya kudhibiti moto katika mabweni na kusababisha hasara.


Matukio ya moto kuunguza mabweni yamekuwa yakitokea mara kwa mara mkoani hapa ambapo mwaka jana lilitokea tukio la moto katika shule ya sekondari Omumwani na kuteketeza mali zote zilizokuwa katika bweni.


Tuesday, June 4, 2024

RUNALI YAWAJENGEA WAKULIMA  KITUO CHA MALIPO RUANGWA 

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.

HATIMAYE ucheleweshwaji wa Fedha za malipo ya wakulima wa Wilaya ya Ruangwa wanaohudumiwa na chama kikuu cha Ushirika Runali kinachojumuisha wakulima wa Wilaya za Ruangwa, Liwale na Nachingwea mkoani Lindi, itabaki historia baada ya chama hicho kujenga kituo cha malipo kitakachotumika kuandaa na kuhakiki malipo ya wakulima hao kwa haraka zaidi.

Kituo hicho cha malipo kimejengwa katika Kata ya Lipande  Wilayani Ruangwa ambapo kimewekwa jiwe la msingi na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack  na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali Wilayani humo pamoja na viongozi wa vyama vya Msingi, Amcos za Mkoa wa Lindi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Katibu Tawala wa Mkoa huo (RAS) Zuwena Omary baada ya kukagua jengo hilo na kuweka jiwe la msingi amekipongeza chama hicho kwa namna kinavyoendelea kuwekeza na kutoa huduma bora kwa wanachama wake kwa kuzikabili changamoto wanazokutana nazo.

Pamoja na pongezi hizo  pia aliutaka uongozi wa Bodi wa chama hicho cha Runali kutunza mradi huo na kuutumia kama walivyokusudia na kuendelea kusogeza  huduma hiyo katika maeneo ambayo yana wanachama wao na wakulima wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Chama kikuu cha Ushirika RUNALI, Jahida Hasani alisema kuwa ujenzi huo wa kituo cha malipo mpaka kukamilika kwake utagharimu Sh milioni 110  na kwamba kitaanza kutumiwa na viongozi hao katika msimu huu wa Ufuta.

" katika eneo hili pamoja na ujenzi wa kituo hiki umeenda sambamba na uwepo wa ghala kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi mazao  tani elfu 10 kwa pamoja  lakini pia kama chama tunamuendelezo wa kujenga hivi vituo ambapo tumejenga Nachingwea,  tumejenga Liwale na sasa ni hapa Ruangwa "

Nae Mwenyekiti wa chama kikuu hicho Odas Mpunga amesema  kuwa lengo kubwa la kujenga kituo hicho ni kuendelea kuwaweka pamoja viongozi na watendaji wa vyama vya msingi (AMCOS) kuchakata na kurahisisha mchakato wa malipo ya wakulima.

Hata hivyo Mpunga ameeleza kuwa  chama hicho  kinaendelea na uwekezaji kwa kununua lori aina ya Scania lenye uwezo wa kubeba Tan 20 za mazao ya wakulima kwa pamoja kutoka shambani mpaka kwenye maghala.






MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI UGANDA-TANZANIA WAFIKIA ASILIMIA 29.

 

Na Alodia Babara, Bukoba

Mradi wa bomba la mafuta ghafi unaotekelezwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani  Tanga nchini Tanzania umefikia asilimia 29.


Mradi huo ambao utagharimu zaidi ya  sh.trilioni 8 ulisainiwa mkataba wake mwaka 2021 kati ya Rais wa Uganda Yowel Kaguta Museven pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, mradi unaendelea kutekelezwa na umefikia asilimia 29.


Afisa katika kitengo cha mawasiliano bomba la mafuta EACOP Abass Abraham akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani Kagera June 03, mwaka huu juu ya mwongozo kuhusu mradi wa bomba hilo amesema kuwa, hadi sasa mabomba yaliyopokelewa ni ya kusambaza umbali wa kilomita 500 na kituo cha kupokea mabomba na kuyaboresha kiko mkoa wa Tabora.


"Asilimia 80 ya bomba la mafuta ziko nchini Tanzania na asilimia 20 ziko upande wa Uganda, kwa Uganda ni kilomita 296 na upande wa Tanzania ni kilomita 1,147 bomba litapita katika wilaya nane"amesema Abraham


Abraham ameeleza kuwa, bomba litafukiwa ardhini ili kukwepa athari za kimazingira, vitajengwa vituo sita vya kusukuma mafuta ili mafuta yaweze kufika kwa wakati Tanga na mafuta kuweza kuingia kwenye matenki ambapo vituo viwili vitakuwa nchini Uganda na vinne vitakuwa hapa nchini Tanzania.


Akizungumzia upande wa fidia amesema hadi kufikia Januari,2024 asilimia 99 ya waguswa wa mradi walikuwa wameshapata fidia kwa Tanzania na idadi ya waguswa ni zaidi ya watu 8,363 miongoni mwao waliojengewa nyumba ni waguswa wapatao 339 na kufikia Machi,2024 walikuwa wamekabidhiwa nyumba hizo.


Kwa Kagera waguswa hao toka mwaka jana wanasaidiwa kutayarisha mashamba kupata pembejeo hadi hatua ya kuvuna na wanasaidiwa ufugaji mdogo mdogo mfano, mbuzi na ngombe, kabla ya program hiyo waguswa walikuwa wanapewa chakula.


Aidha, baada ya mradi huo kuanza itatumika nguvu ya aina tatu ya umeme ili mradi usiweze kukwama katika kusukuma mafuta ghafi ikiwemo, umeme wa Tanesco, generator pamoja na umeme wa nguvu ya jua (solar).


Gharama za kukamilisha ujenzi wa mradi wa bomba zinatarajiwa kufikia takribani shilingi trilioni 8 za Kitanzania, bomba hilo litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya China na TULLOW ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)


KESI YA WANANDOA KUJERUHI JIRANI YAPIGWA KALENDA

 


Na Mwandishi Wetu

SHAHIDI wa upande wa mashitaka, Kiran Lalit Ratilal, ameshindwa kutoa ushahidi katika kesi  ya kujeruhi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54), kwa sababu wakili wa utetezi katika kesi hiyo yupo Mahakama ya Rufani kwenye shauri lingine.


Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


Kesi hiyo ililetwa jumatatu tarehe 3 Juni mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka, mashahidi watatu wameshatoa ushahidi wao.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga alidai kuwa wana shahidi mmoja na wapo tayari kuendelea na ushahidi, baada ya kudai hayo, upande wa utetezi ulidai kuwa ni kweli kesi ipo kwenye hatua ya ushahidi, lakini kwa bahati mbaya siku ya ijumaa walipata barua kutoka Mahakama ya Rufaa.


"Ni kweli kesi imekuja kwa kusikilizwa, lakini kwa bahati mbaya siku ya ijumaa tulipokea barua kutoka Mahakama ya Rufaa, kwa hiyo wakili ameenda huko,"alidai Wakili Mwanaisha Mshobozi


Baada ya Mshobozi kudai hayo, Wakili Mwanga alidai kutokana na maombi hayo hawana pingamizi, wanaomba wapangiwe tarehe nyingine ya usikilizwaji ambayo alipendekeza iwe Julai, mwaka huu ambapo hakimu alisema ni mbali sana.


Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 25, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji, ambapo shahidi Kiran Lalit alionywa na mahakama kufika tarehe hiyo kwa ajili ya kutoa ushahidi.


"Shahidi kwa bahati mbaya Wakili wa washtakiwa hayupo, tumeelezwa hapa yupo Mahakama ya Rufani, unatakiwa tarehe tutakayopanga uwepo mahakamani,"alisema Hakimu


Awali, Fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) aliileza mahakama jinsi mshitakiwa Bharat Nathwan allivyomshambulia jirani wake, Lalit Ratilal kwa kumpiga kichwa kifuani kisha akadondoka chini na nakupoteza fahamu kwa muda.


Aidha, alidai kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya mke wa Bharat (Sangita Bharat) na mke wa Lalit, (Kiran) ambao walikuwa wakirushiana maneno kwa ukali kwa lugha ya kihindi huku, baada ya muda kidogo waume zao walifika kwa pamoja na kuingilia ugomvi huo.


Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa nyumbani kwa Lalit Ratilal maeneo ya mtaa wa Mrima katika jingo la Lohana, alimuita kwa ajili ya kuifanyia kazi zinazohusiana na mbao na kazi zingine ndogo ndogo.


Alidai kuwa alifika katika jengo hilo saa tatu asubuhi ambapo bosi wake huyo anakaa floor ya tatu, wakati anaendelea na kazi alidai kuwa Sangita alikuwa amesimama kwenye mlango lake na Kiran alikuwa amesimama kwenye mlango wake, ambapo Sangita Bharat alianza kuzungumza kwa ukali na kwa jaziba akitumia lugha ya kihindi.


"Lakini nilimsikia mke wa Bharat, Sangita akimwambia mke wa Lalit kwamba uchafu wake apeleke huko ambapo vitu vyote vilikuwa vimewekwa katika eneo la Lalit na hakuna kitu chochote kilichokuwa katika eneo la Sangita. Baada ya dakika kadhaa sijui walipiga simu au vipi waume zao walikuja kwa wakati mmoja na malumbano ya maneno yakaendelea kwa wote wanne," alidai Fundi Mpakani.


Shahidi huyo alidai kuwa, wakati malumbano ya maneno hayo yanaendelea wote walikuwa wamesimama kwenye mlango wa Lalit, baada ya muda Bharat akampiga kichwa Lalit na Lalit akadondoka chini na kupoteza fahamu.


Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania jinsia ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.


Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga kichwa, ngumi na mateke kichwani.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.


Monday, June 3, 2024

WADAU WA USHIRIKA WATOA MSAADA HOSPITALI YA WILAYA YA RUANGWA 

 





Na Mwandishi wetu, Lindi.

Kuelekea siku ya jukwaa la ushirika linalotarajiwa kufanyika hapo kesho juni 04, 2024 wadau wa ushirika Mkoa wa Lindi wamekabidhi misaada mbalimbali ya kibinaadamu kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Wilaya ya Ruangwa pamoja na kupanda miti hospitalini hapo



Misaada hiyo iliyokabidhiwa ni pamoja na sabuni za unga pamoja na sukari ambavyo vimegawiwa kwa akina Mama waliojifungua katika hospitali hiyo


Akizungumza na Waandishi wa Habari, Bi. Cesilia Socitenes amesema kuwa huduma zilizofanyika katika Hospitali ni moja ya utekelezaji wa misingi Saba ya ushirika ambapo msingi wa saba unaelekeza kuijali jamii.


Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa msingi huo wa Saba, wanachama wa Vyama vya Ushirika watachangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wengi ambao matibabu yao yanauhitaji wa damu.


Kwa upande wake, Ndg. Richard Zengo, Mrajisi Msaidizi anayesimamia Sehemu ya Vyama Visivyo vya Kifedha kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika amesema kuwa moja ya malengo makuu ya Jukwaa la Ushirika ni kuhimiza utekelezaji wa msingi wa saba wa Ushirika ambao ni kujali jamii.


Zengo amesisitiza kuwa shughuli zote zinazofanyika ni kuonesha kwa vitendo namna Ushirika unavyoungana na Serikàli ya Awamu ya Sita katika kutekeleza masuala ya kusaidia jamii inayotuzunguka.

JELA MIAKA 50, KWA UBAKAJI, WIZI NA UHUJUMU UCHUMI.

 

Na Mwandishi wetu, Lindi

Mahakama ya hakimu mkazi Lindi chini ya hakimu mkazi mfawidhi consolata singano imewahukumu kazili kafanya  mwenye umri wa miaka 47 mkazi wa dare es salaam na jonh mondo  maarufu kama kikwete kwa jina  la utapeli mwenye umri wa miaka 55 mkazi wa msavu mororgoro kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka na kwenda jela miaka 20 kwa kosa linguine la utakatishaji fedha.


Hili ni shauri  la uhujumu uchumi namba tatu la mwaka 2022 ambapo kulikua na  jumla ya mashahidi 32 kutoka mikoa ya lindi, mtwara, Ruvuma, dar es salaam, Dodoma na morogoro  na vielelezo 35.


Kesi hii ilikua chini ya hakimu mkazi mfawidhi  consolata singano ambapo upande wa jamuhuri ukiongozwa na wakili wa serikali godfrey mramba  ambapo ameiambia mahakama yakwamba watuhumiwa walifanya vitendo vya uzalilishaji wa kingono kwa kuwaingilia wanawake wawilia  bila ridhaa yao na kuwasababishia hasara kiuchumi kwa kuwaibia kiasi hicho cha fedha huku upande wa watuhumiwa wakiongozwa na wakili hagai mwambingu wakikana makossa yote 16.


Hukumu hii imesomwa ndani ya saa nne na dakika 40 ambapo baada ya kusikiliza pande zote mili ndipo hakimu akatoa hukumu kwenda jela kila mmoja miaka 30  kwa kosa la kubaka.


Makossa manne yaan   la 3,4,5,6,7  la wizi kila kosa kutumikia kifungo cha miaka mitano kila mmoja.


Kuhusu kosa la nane la mtuhumiwa  jonh mkondo  kughushi nyaraka za benki yeye amehukumiwa kwenda jela miaka saba  na kosa la tisa la kufoji nyaraka kwa wote waili nalo wataenda jela miaka saba kila mmoja.


Aidha kosa la kumi la kutoa nyaraka za uongo wote wawili watatumikia kifungo cha miaka saba  kila mmoja  na kosa la 12,13 na 14  kwa  mshatakiwa wa kwanza kazili kaftani  kusajili laini za simu kwa kutumia majina ya watu na kuzitumia bila ridhaa yao kinyume na sharia ya mawasliano na posta atatumikia kifungo cha miezi 36 jela au kulipa faini ya shilingi milioni 15.


Kosa la 15 la utakatishaji fedha kwa mtuhumiwa wa kwanza ataenda jela miaka 20 na huku kosa la 16 pia la utakatishaji fedha wote wawili watatumikia pia kifungo cha miaka 20 jela.


 Bada ya kuwahukumu kisha hakimu singano akasema mtuhumiwa wa kwanza kazili atatakiwa kumlipa fidia muhanga wa ubakaji shilingi milioni 5 na kosa la tatu kwa mshatkiwa wa pili nae atalipa fidia kwa muhanga wa kubakwa shilingi milioni 5.


WIZI WA MTOTO MWENYE UALBINO MULEBA, WATATU WAKAMATWA.

 

Alodia Babara, Muleba,

Noela Asimwe Novath mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu mwenye ualibino  ameibwa katika mikono ya mama yake baada ya mtu mmoja  asiyejulikana kupiga hodi nyumbani kwao na kuomba msaada wa chunvi akidai amenga’twa na nyoka katika kijiji cha Bulamula kata ya Kamachumu  wilaya ya Muleba mkoani Kagera.


Mama mzazi wa mtoto huyo Judith Richard amesema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 30, mwaka huu saa 7:30 jioni wakati mama huyo akiwa amekaa ndani na mtoto wake ndipo mtu huyo alipokuja na kupiga hodi bila kutaja jina lake na kusema kuwa, amenga’twa na nyoka hivyo  anaomba msaada wa chunvi.


Judith amefungua mlango na kumuona mtu ambaye alikuwa akitembea kwa kuchechemea bila kujua kumbe alikuwepo mtu mwingine amejibanza  ukutani ambapo aliyekuwa amejibanza ukutani alimkaba koo na aliyekuwa anachechemea  aliingia ndani na kutokomea na mtoto kusikojulikana.


 “Kuna mtu alipiga hodi akaniita mama Asimwe naomba unisaidie chunvi  nikamuuliza wewe nani akajibu mie Kelvin, nikamuuliza  wa wapi? akajibu wa humu humu kitongojini Mbare awali roho ikasita baadaye nikawaza siwezi kujua atakayenisaidia nikafungua mlango nikiwa nimewasha tochi ya simu yangu nilimuona mtu amaejibanza ukutani muda huo huo alikuja haraka akanikaba shingo  dakika kama nne amenikaba na aliyekuwa anajifanya anachechemea aliingia ndani na kutokomea na mtoto wangu” amesema Richard.


Amesema baada ya mtu huyo kumwachia alianza kupiga kelele za kuomba msaada ndipo mke wa shemeji yake alitoka  na yeye kuanza kumsaidia kupiga kelele za kuomba msaada wanakijiji walikusanyika.


Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga  amesema kuwa, jeshi la polisi limeshaweka mtego kila sehemu kwa ajili ya kuwakamata watu waliofanya kitendo cha wizi wa mtoto huyo.


Dkt Nyamahanga ameitaka jamii ya wakazi wa Muleba kuendelea kuonyesha mshikamano katika kumtafuta mtoto huyo kama ambavyo walifanya toka tukio lilivyotokea.


“Sisi kama serikali kwa kushirikiana na jeshi la polisi tunaendelea kupambana na mitego yote tuliyoitega tulitoa taarifa kila kona ili kuwanasa wahalifu, maelekezo yetu kama serikali ukiona matukio haya yameanza, wameanza kutikisa kiberti kijiji chochote ndani ya wilaya ya Muleba wenye binadamu mwenye ualibino kupitia kwa maafisa ustawi wa jamii waripoti kila siku juu ya usalama wa watu hawa”


“Na nyie wanawake msiwaache watoto wenu bila mtu yeyote mkaenda kuchota maji umbali wa mita kadhaa tuwalinde kwa kila namna na kwa gharama yoyote kwa sababu ni binadamu wenzetu” amesema Dkt Nyamuhanga.


Aidha, kaimu kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoa Kagera Yusuph Daniel amesema wanaendelea na msako wa kutafuta wahalifu waliohusika kupora mtoto huyo na wamefanikiwa kuwakamata watu watatu washukiwa wa tukio hilo akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo.


Kamanda Daniel amesema katika uchuguzi wanaoendelea nao bado ni mapema kusema tukio hilo la kupora mtoto mwenye Ualbino limehusisha  imani za kishirikina na bado hakuna mwananchi yeyote ambaye amethibitisha hilo.


Jeshi la polisi mkoa Kagera linatoa wito kwa wananchi  kushirikiana na polisi kata kufanya msako  kwa ajili ya kumpata mtoto huyo na kutoa taarifa za uhalifu unaotokea kwenye maeneo yao.


Saturday, June 1, 2024

NMB YATOA MSAADA VIFAA TIBA VYA MILIONI 10 HOSPITALI YA BAGAMOYO

 

Benki ya NMB yatoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo ikiwa ni kutekeleza majukumu yao ya kusaidia wananchi katika kuimarisha afya zao.


Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Meneja wa kanda ya Dar es salaam, Ferdinand Mpona, amesema NMB imetekeleza msaada huo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali chini ya uongozi wake Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda, amesema wanaishukuru Benki ya NMB kwa kutoa vifaa hivyo kwani vitasaidia katika matibabu ya afya za wananchi.


Amesema serikali imetenga fedha za kujenga na kukarabati majengo mbalimbali ya Hospitali ya Bagamoyo hivyo inapokea taasisi binafsi zikajitolea kusaidia vifaatiba inasaidia kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.


Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Vitanda vitano vya kujifungulia kinamama wajawazito, pamoja na magodoro yake, na viti vya magurudumu (wheelchairs) ishirini kwaajili ya kubebea wagonjwa ambavyo vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 10.