Tuesday, August 3, 2021

Udugu Social Help welfare yawafariji mayatima Mbagala

 







Na Mwandishi wetu





Taasisi ya Udugu Social Help Welfare yenye Makao Makuu yake Buguruni Jijini Dar es Salaam imefanikisha nia yake ya kuwafariji mayatima wa kituo cha Al-Azim kilichopo Mbagala kwa kujumuika nao na kupata chakula cha pamoja.

Aidha Taasisi hiyo imetoa wito kwa wadau kuendelea kuwakumbuka na kuwajali mayatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu popote pale walipo kwani bado wanazo changamoto nyingi zinazohitaji ufumbuzi.

Akizungumza mara baada ya kupata chakula cha mchana na mayatima, mratibu wa kundi hilo lenye wanachama Zaidi ya 20, Hajat Neema Maumba amesema kilichowasukuma kushiriki chakula pamoja na mayatima ni kuwafariji, wasijione wapweke katika maisha yao.

Amesema ni utaratibu wao wa kila mwaka kushiriki chakula na watoto yatima na wamekuwa wakifanya hivyo katika maeneno mbalimbali katika jiji la Dar es salaam.

Amesema taasisi yao ya Udugu Social Help welfare sio ya kidini na lakini wengi wao ni waislam, wanasaidia watu mbalimbali bila kujali dini zao.

 

“Sisi tunaitwa Udugu Social Help welfare, Makao makuu yetu yapo Buguruni Malapa, tuko wakina mama 20, tulianza kazi mwaka 2009, tumefanya kazi sehemu nyingi na bado tunaendelea,” alisema

Tumesikia majonzi mengi baada ya watoto kueleza changamoto zao, tunamuomba mwenyezi Mungu atuafikishe sisi na wengine tuweze kusaidiana, yatima sio mtoto wa mtu mmoja, ni watoto wetu, kama alivyosema Mtume wetu Muhammad (saw) kwamba katika nyumba yenye yatima wakalala njaa na nyumba nyingine wakala basi watu wote katika mtaa huo wanapata dhambi,” aliongeza

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa taasisi ya kulelea watoto yatima na wenye mazingira hatarishi cha Al-Azam Orphanage center Sheikh Musa Chele ametoa wito kwa wafadhili kuacha kuwatumia watu wa kati kufikisha sadaka zao katika makao ya watoto yuatima.

Amesema kwa muda mrefu watu hao wa kati (agent) wamekuwa wakitumia fursa hiyo vibaya kwa kujinufaisha wao wenyewe badala ya watoto mayatima.

Ametoa mfano katika kituo chake pekee jumla ya milioni 80 zimeliwa na watu wa kati jambo ambalo lina muudhi sana na kuamua kulitolea ufafanuzi.

Aidha akielezea historia ya kituo chao, Sheikh Musaa alisema Kituo chao kimeanzishwa mwaka 2009 kikiwa na watoto 10, wavulana 5 na wasichana 5, hadi kufika mwaka 2021, walikuwa na watoto 60, kati yao wanawake 35 na wanaume 25, aidha kati ya watoto 60, 45 wanaishi katika kituo na wengine wanalelewa wakiwa majumbani mwao.

Amesema Kituo kinakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa ni huduma za afya, watoto wengi hawana bima za afya ili kuwasaidia kupata matibabu bila hofu.

Pia amesema kuna changamoto ya rasilimali fedha za kulipa pango la nyumba, ada za wanafunzi, na chakula,  kwa mwezi wanalipa shilingi 300,000 fedha ambazo ni nyingi kwa uwezo wao.

Aidha kwenye upande wa mafanikio kituo kimeweza kununua kiwanja na kuwaomba wadau kuwajengea nyumba ili watoto wakaishi huko na kuepukana na adha ya kupanga.


 

No comments:

Post a Comment