Saturday, May 25, 2024

DKT. MPANGO AWASILI COMORO.

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Kilimo wa Comoro Mhe. Houmed Mssaidie mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Prince Said Ibrahim uliopo Moroni nchini Comoro tarehe 25 Mei 2024. Makamu wa Rais anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uapisho wa Rais Mteule wa Comoro Azali Assoumani unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Mei 2024.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Prince Said Ibrahim uliopo Moroni nchini Comoro tarehe 25 Mei 2024. Makamu wa Rais anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uapisho wa Rais Mteule wa Comoro Azali Assoumani unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Mei 2024. (Kulia ni Waziri wa Kilimo wa Comoro Mhe. Houmed Mssaidie na kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu)



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitazama ngoma ya asili ya Comoro mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Prince Said Ibrahim uliopo Moroni nchini Comoro tarehe 25 Mei 2024. Makamu wa Rais anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uapisho wa Rais Mteule wa Comoro Azali Assoumani unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Mei 2024.

Friday, May 24, 2024

NAWASHUKURU KWA DUA ZENU - DK.MWINYI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj  Dk.Hussein Ali Mwinyi amewashukuru Wazee wa Vijiji vya Ukongoroni na Charawe kwa kumuombea dua baada ya kukamilika barabara ya  Ukongoroni hadi Charawe na kuipongeza Serikali.


Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipojumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa na dua ya kumuombea iliyoandaliwa na Wazee wa Ukongoroni na Charawe iliyofanyika Ukongoroni, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja tarehe: 24 Mei  2024.


Aidha Rais Dk.Mwinyi amewahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kuiombea dua nchi ili Mwenyezi Mungu aidumishe katika amani na kutimiza ahadi za maendeleo kwa wananchi.









 

SOME AANZA KUWATETEA WANAFUKAYOSI.

 

MRISHO SOME Diwani wa Kata ya Fukayosi, akisalimiana na mmoja wa Madiwani baada ya kuapishwa rasmi kuwa diwani. Picha na Omary Mngindo.


Mrisho Some akila kiapo. Picha na Omary Mngindo.


Mrisho Some (kushoto pichani) diwani mpya Kata ya Fukayosi akiwa katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo ikiwa ni mara yake ya kwanza. Picha na Omary Mngindo.

...................................

Na Omary Mngindo, Bagamoyo.


DIWANI mpya wa Kata ya Fukayosi halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani  Mrisho Some ameanza kuwapigania wakazi wake, kwenye baraza lake la kwanza kuanza kutekeleza majukumu yake.


Some alianza kazi hiyo katika Baraza la robo ya tatu ambapo alianza kwa kuiomba TARURA wilaya hiyo kuiangalia barabara itokayo Kijiji cha Fitina haina Posho kuelekea shule ya sekondari ya fukayosi.


Akiwa katika kikao hicho Some alisema kwamba ndani ya Kata hiyo kuna changamoto kadhaa huku akianza na barabara kutokea Fitina haina Posho kuelekea shuleni huko.


"Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza niwashukuru wanaFukayosi wenzangu, viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Mkuu wa Wilaya, Madiwani wenzangu na wataalamu wote kwa kunipokea," alisema Some.


Aliongeza kwamba "Katika Kata yangu ya Fukayosi kuna changamoto ya miundombinu ya barabara ya kuelekea shule ya Kata ya Fukayosi, ambapo barabara ni mbaya kupita maelezo, naiomba TARURA iiangalie barabara ile," alisema Some.


Katika baraza hilo diwani wa Viti Maalumu Ummy Matata Kisebengo alilalamikia kitendo cha kuhamishwa kwa wataalamu sekta ya afya, akielezea changamoto ya uchache wa watumishi huku akiomba halmashauri kuangalia adha hiyo.


"Mheshimiwa Mwenyekiti katika Hospitali yetu ya Wilaya tuna changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya, kuna watumishi ambao walipelekwa kuongeza ujuzi nasikia wamehamishwa, hili Mwenyekiti tulifanyie kazi," alisema Ummy.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mohamed Usinga alisema kwamba changamoto hiyo wameipokea, huku akiahidi kuifisha ya Mkoa kwa taratibu zaidi


MWENGE WA UHURU WATUA LINDI, KUTEMBELEA MIRADI 53

 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack leo, Mei 24, 2024 amepokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa  mkuu wa Mkoa wa kusini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, ambapo unatarajiwa kuwekwa mawe ya msingi, na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 45.9


Makabidhiano ya Mwenge huo  yamefanyika katika viwanja vya Ndege Wilayani Kilwa Mkoani Lindi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali sambamba na wananchi wa maeneo hayo.


Akitoa taarifa ya Mkoa wakati wa Makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru, Mhe Telack amesema kuwa katika Mkoa wa Lindi Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 45.9


Akipokea Mwenge huo Telack amesema Mwenge huo wa uhuru ukiwa Mkoani Lindi unatarajiwa kukimbizwa kwa umbali wa kilometa 1128.7 katika Wilaya 5 na halmashauri 6 za Mkoa huo ambapo jumla ya miradi 15 itawekwa mawe ya msingi, miradi 13 itazinduliwa na miradi 25 itatembelewa.


Telack amesema kwa kuzingatia Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 unaolenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu "Uhifadhi wa mazingira na Uchaguzi wa serikali za Mitaa", Mhe. Telack ameeleza kuwa Mkoa wa Lindi umeweza kuongeza kasi ya upandaji miti ambapo hadi kufikia April mwaka huu, jumla ya miti 6,544,230 imepandwa.


Pia, Mkoa huo umeendelea kushirikiana na OR- TAMISEMI katika kuhakikisha maandalizi ya awali ikiwemo uhakiki wa vituo vya uchaguzi pamoja na kutoa hamasa na elimu kwa wananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa katika mikutano mbalimbali vinafanyika.

Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Eliakim Mzava , amewatahadharisha viongozi wa mkoa na wilaya kuwa na nyaraka zote muhimu katika miradi husika ambayo itatembelewa na Mwenge huo ili waweze kuzipitia kwa kina na kujiridhisha.


“Naomba niwakumbushe viongozi wangu wa Mkoa wa Lindi katika miradi yote tutakayotembelea huko wilayani kwenu naomba nyaraka zote zinazohusika ziwepo na tuzipate asubuhi mapema kabla hatujaanza kutembelea miradi yenyewe hii itatupa sisi urahisi wa kuzipitia taarifa mapema,” amesema Mzava






UMARUKI WATUMIA MILIONI 7, KUSAIDIA WAATHIRIKA WA MAFURIKO PWANI.

 


Viongozi wa Umoja wa Maendeleo wa Watu wa Rufiji mkoani Pwani na Kilwa mkoani Lindi (UMARUKI) waishio Morogoro, wakikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa mkoa wa Pwani ambao umepokelewa na Katibu tawala mkoani Pwani (RAS)  Rashid Mchata kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo.

....................................

Na Rashid Mtagaluka, Kibaha.


Umoja wa Maendeleo wa Watu wa Rufiji mkoani Pwani na Kilwa mkoani Lindi (UMARUKI) waishio Morogoro, jana Mei 23/2024 umekabidhi msaada wa nguo kwa wananchi waliopatwa na athari ya mafuriko mkoani Pwani.


Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo kwenye ofisi za Mkuu wa mkoa wa Pwani, Katibu Mkuu wa UMARUKI Bwana Juma Mtumbei alisema umoja huo umeguswa na tukio hilo, hivyo kama binadamu wameona wanao wajibu wa kuwasaidia.


Kwa mujibu wa Mtumbei, msaada waliotoa kwa waathirika hao ni pamoja na nguo za watoto, wanawake, wanaume pamoja na nguo maalumu za kujistiri wakati wa baridi zote zikiwa na  thamani ya shilingi Milioni Saba na laki saba.


Kwa upande wa Katibu tawala mkoani Pwani Rashid Mchata aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, amewashukuru UMARUKI kwa moyo wao  wa kujitolea kuwasaidia wananchi wa wilaya za Rufiji na Kibiti zilizokumbwa na athari za mafuriko.


Mchata ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa taasisi nyingine za kiraia kufuata nyayo za UMARUKI kwa kuona umuhimu wa kuisaidia serikali katika jukumu la kujitolea kwa watu waliopatwa na majanga kama hao wa mkoani Pwani.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Mwalimu Habib Salim Muhinge ameishukuru ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Pwani kwa kukubali kwao kupokea mchango wao huo ingawa ni mdogo lakini ofisi hiyo haikuona tabu kuupokea.


Aidha Muhinge amewashukuru wanajumuiya ya UMARUKI waishio Morogoro na kuwataka wasiishie hapo tu, bali moyo huo wa kujitolea wauendeleze kila inapotokea watu kuhitaji msaada popote pale nchini.


Salha Mbonde ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa UMARUKI aliyeongozana na viongozi kupeleka msaada huo Mkoani Pwani, amewaomba kina mama kote nchini kutumia fursa hii kuona umuhimu wa kuisaidia jamii kila inapoonekana kuna haja ya kufanya hivyo.


Umaruki ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa na wananchi wa mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara waishio Morogoro kwa lengo la kusaidiana, na  ambayo imesajiliwa serikalini kwa namba S.A.19402.


Thursday, May 23, 2024

MAJALIWA: TUMEDHAMIRIA KUONGEZA KIPATO CHA WANANCHI

 

Asema lengo ni kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na vijijini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya imedhamiria kuongeza ushiriki wa wananchi katika kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza kipato kwa wananchi wengi na kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na vijijini.

“Ili kufikia lengo hilo, Serikali inatekeleza Mpangokazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini kwa kufanya mapitio na maboresho ya sera, sheria na kanuni ambazo zinakuwa ni kikwazo katika ufanyaji wa biashara nchini.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 23, 2024) kwenye ufunguzi wa Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji baina ya Uganda na Tanzania, katika Hoteli ya Johari Rotana jijini, Dar-es-Salaam.

Amesema Serikali imeimarisha utoaji huduma kwa kuunganisha mifumo ya kielektroniki 55 ya taasisi 50, pia sheria 13 zimeshafanyiwa marekebisho ili kupunguza au kuondoa kodi, ada na tozo na kupunguza au kuweka misamaha ya ushuru wa forodha.

“Mifumo hiyo imeunganishwa ili kubadilishana taarifa na kukamilisha uundaji wa mfumo wa kielektroniki wa dirisha moja la utoaji huduma kwa wawekezaji (Tanzania Electronic Investiment single window).”

Amesema mbali na maboresho ya mifumo, Serikali imeendelea kuimarisha nidhamu katika utendaji kazi, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara na uwekezaji.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa ahueni za kikodi kwa wawekezaji katika viwanda vya ndani na kuanza utekelezaji wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara Tanzania (Blueprint Regulatory Reforms to Improve the Business Environment for Tanzania).

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani kutoka sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa jumla ya kampuni mpya 15 zenye mitaji ya Dola za Marekani milioni 215.48 zinazojishughulisha na uchakataji wa mazao ya kilimo na madini zimesajiliwa na kupewa leseni.

“Kutokana na jitihada mbalimbali, Serikali imewezesha uanzishaji wa viwanda 332 vya kimkakati na kurejesha viwanda 20 vilivyobinafsishwa. Tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua ya kugawa viwanda hivyo ambapo, EPZA wamepewa  viwanda nane  kwa ajili ya kuviendeleza, NDC na SIDO wamekabidhiwa viwanda viwili na viwanda kumi vilivyobaki bado vinatafutiwa wawekezaji wapya.”

Amevitaja viwanda hivyo kuwa ni  Mbeya Ceramics Company Ltd, Nachingwea Cashewnuts Processing Factory, Mafuta Ilulu Ltd, Mkata Sawmills Ltd, Tanganyika Packers Limited (TPL) Shinyanga Plant, Mwanza Tanneries Ltd, Mang’ula Mechanical and Machine Tools, National Steel Corporation, pamoja na Mbeya Meat Processing Plant.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa masuala ya uwekezaji na biashara watumieni makongamano hayo kubaini fursa za uwekezaji wa pamoja kati ya wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kuweka bayana faida zinazotokana na uwekezaji wa pamoja. “Ikiwezekana andaeni maonesho ya fursa hizi ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi zetu.”







Tuesday, May 21, 2024

JKT RUVU WAUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA SEKTA YA UTALII.

 

Kanali Peter Mnyani (Mwenye suti) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John wakifunua kitambaa kuashiria kuzinduliwa kwa zuu hiyo. Picha na Omary Mngindo.

....................................

Na Omary Mngindo, Ruvu.

JESHI kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, imeunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Saluhu katika suala la kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo vikiwemo vya wanyamapori kupitia sekta ya utalii.

Hatua hiyo inatokana na kambi ya Ruvu kuanzisha kitalu cha kuhifadhia wanyama hao, kwa kutenga ardhi yenye ukubwa wa eka 70, pembezoni mwa kambi wakianza na Twiga, Swala, Pundamilia na wengine wadogowadogo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kikosi hicho Kanali Peter Mnyani, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, wakati wa uzinduzi wa zuu hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wanajeshi wastaafu na mamia ya wananchi.

"Mkuu wa Wilaya uanzishwaji wa zuu ya wanyama tunalenga kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu, ambae amedhamiria kuifungua nchi katika sekta mbalimbali pia tunakumbuka alizindua filamu ya Royal Tour iliyochangia kupatikana kwa watalii wengi," alisema Mnyani.

Kanali Mnyani aliongeza kuwa "Mwezi wa sita tunataraji kuleta Simba, ambae hatokuwa na madhara kwa wanamchi watakaokuja kuangalia wamyama hapa katika kambi yetu ya Ruvu," alisena Kanali huyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kibaha Nickson John, alipongeza ubunifu huo unaolenga kuwawezesha wananchi wa Kibaha na maeneo mbalimbali kufika kujionea wanyama hao, ambao wengine huwangalia kupitia TV.

"Uwepo wa zuu hii utasaidia wana Kibaha, lakini si wao tu ukizingatia ipo mita chache kutoka barabara Kuu ya Dar es Salaam kuelekea mikoani, hapa abiria wanaopita eneo hili wanaweza kuja kuangalia wanyama hawa," alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Wakazi Athumani Semsega na Zainabu Issa wameelezea kufurahishwa kwao kufuatia ubunifu huo, huku wakisema kuwa umesaidia kuwaona wanyama hao kwa karibu ambapo pia waliweza kuwalisha chakula.

Kanali Peter Mnyani akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,  Nickson John eneo litakalokuwa linapatikana vinywaji. 
Picha na Omary Mngindo.

Mkuu wa Wilaya Nickson John akimlisha chakula mmoja wa Pundamilia wanaopatikana katika zuu hilo. Picha na Omary Mngindo.


Friday, May 17, 2024

BENKI YA NBC YAZINDUA BIMA YA AFYA KWA WAKULIMA

 

YATAMBULISHA KAMPENI YA KUHAMASISHA KILIMO CHA UFUTA LINDI NA MTWARA

Na Hadija Omary 

LINDI

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Assemble Insurance imezindua huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima nchi nzima ikilenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa kundi hilo. Hatua hiyo inatajwa kuwa itasaidia kuimarisha sekta ya afya ambayo ni moja ya nguzo muhimu katika ukuaji wa kilimo nchini.

Kupitia huduma hiyo wakulima na familia zao wanaweza kupata huduma ya bima ya afya kwa malipo ya kiasi cha Sh. 450,000 kwa mwaka.

Hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo imefanyika leo mkoani Lindi ikienda sambamba  na uzinduzi wa kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ mahususi kwa wakulima wa zao la ufuta mkoani Lindi na wilaya za Masasi na Nanyumbu mkoa wa Mtwara.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bi Zuwena Omary aliongoza hafla hiyo iliyohusisha viongozi wa vyama vya msingi na ushirika mkoani Lindi na Mtwara huku Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Theobald Sabi kwenye tukio hilo muhimu.

Akizungumzia hatua ya benki hiyo Bi Zuwena pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kutoa kipaumbele kwa wakulima nchini alisema ujio wa huduma ya Bima ya Afya mahususi kwa wakulima ni  ukombozi muhimu kwa kundi hilo na inaunga mkono na dhamira ya serikali ya kuhakikisha makundi yote ya wananchi yanapata huduma ya bima ya afya.

“Ujio wa huduma hii ya Afya ya NBC ni mkombozi muhimu kwa wakulima kwasababu watoa huduma wengi wa bima ya afya wameshindwa kuwa na mifumo rafiki katika kuwafikia wakulima. NBC wameiona changamoto hii na kwa kuwa wapo karibu na wakulipa kupitia huduma mbalimbali za kibenki wataweza kufanikisha mpango huu kwa urahisi na ufanisi zaidi. Sasa wakulima na familia zao watakuwa salama kuanzia sasa.’’ alisema Bi Zuwena huku akitoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa hiyo.

Akizungumzia kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ Bi Zuwena alionyesha kuridhishwa zaidi na namna kampeni hiyo ilivyohusisha suala zima la utoaji wa elimu ya fedha kwa wakulima, hatua aliyosema itasaidia zaidi kukabiliana na changamoto ya matumizi ya pesa yasiyozingatia vipumbele muhimu inayowakabili wakulima wengi mkoani humo.

“Pamoja na zawadi mbalimbali kwa wakulima ikiwemo pampu za kupulizia dawa, dawa za kuua magugu na konokono, baiskeli na pikipi ambavyo ni muhimu sana kwa wakulima, ubora wa kampeni hii upo zaidi kwenye eneo la elimu ya fedha kwa wakulima na hapa nawasihi sana washiriki wa semina hizi mzingatie zaidi,’’ alisema Bi Zuwena ambae pia alitumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi hao wa vyama vya msingi na ushirika kuisaidia serikali katika kusimamia udhibiti za pembejeo za kilimo zinazotolewa bure na serikali.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo alisema ujio wa huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima pamoja na uzinduzi wa kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ ni muitikio wa benki  hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali kuboresha sekta muhimu za afya na kilimo nchini kupitia mapinduzi ya huduma za kifedha.

“Kupitia program hizi mbili tulizizindua leo NBC tunakwenda kugusa maeneo muhimu kitaifa na yanayogusa watu wengi zaidi ambayo ni sekta ya afya na kilimo ambavyo kimsingi vinaingiliana sana na vinategemeana.’’

“Kwa kushirikiana na kampuni ya BIMA ya Assemble wakulima kote nchini  wanafikiwa moja kwa moja na huduma ya afya kwa kiasi cha sh 450,000 tu kwa mwaka na kupitia kampeni yetu ya  ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ wakulima wa zao la ufuta mkoani Lindi na wilaya za Masasi na Nanyumbu watanufaika kupitia elimu za fedha na elimu ya kilimo cha kisasa pia wakipata huduma bora za kibenki mahususi kwao huku wakiwa kwenye nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali zikiwemo pikipiki, baiskeli na dawa kuua wadudu waharibifu wa mazao yao,’’ alisema.

Wakizungumza kwa niaba wakulima hao, Wenyeviti wa vyama vya ushirika vya TANECU na MAMCU, Bw Hamis Chipola na Azam Mfaume ‘Jula jula’ msawalia, pamoja na kuishukuru na kuipongeza benki hiyo kwa program hizo muhimu walielezea namna wakulima wanavyopata wakati mgumu kutokana changamoto ya ukosefu wa huduma ya bima za afya huku wakibainisha kuwa ujio wa huduma hiyo kupitia NBC itakuwa ni msaada mkubwa kwao na familia zao.

“Hata hivyo tunaendelea kutoa wito kwa taasisi za fedha ziendelee kuwa karibu na sisi wakulima kwa kuwa nasi pia kwasasa tumeazimia kuwa karibu na taasisi zinazotujali kupitia huduma zinazotugusa kama hizi za NBC. Wakulima tunahitaji mikopo hususani mwanzo wa msimu ili itusaidie kuboresha uzalishaji wetu na sio waje kipindi cha msimu wa mauzo nasi tutawakataa,’’ alisema  Mfaume kauli iliyoungwa mkono na mwenzie Chipola.

 









 


Thursday, May 16, 2024

WAZAZI NA WALEZI MKOANI LINDI WATAKIWA KUTUMIA MIFUMO RASMI KATIKA KUMALIZA MIGOGORO YAO

 

NA HADIJA OMARY

LINDI.


Wazazi na walezi Mkoani Lindi wametakiwa kuitumia vyema mifumo iliyowekwa na Serikali katika kushughulikia migogoro na tofauti zinazojitokeza katika familia zao  ambayo kwa kiasi kikubwa huchangia kuachana na  kusababisha watoto kuathiriwa kwa kukosa  malezi imara.



Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo  katika maadhimisho ya siku ya Familia ambayo kwa ngazi ya Mkoa yamefanyika katika viwanja vya soko la majengo halmashauri ya Mtama Mkoani humo.


Ndemanga amesema  Mifumo hiyo ni pamoja na madawati ya jinsia na Ofisi  za ustawi wa jamii zilizopo kwenye kila halmashauri.


Ndemanga ametaka wazazi kuitumia siku hiyo kutafakari namna ya kuimarisha ubora wa familia ikiwemo kutafuta suluhu ya tofauti zao kwa njia zinazofaa ili zisiendee kuathiri malezi na makuzi ya watoto.


“Watoto wetu wakati wanaimba wamekuambia kwa lugha nyepesi sana kwamba tunapogombana baba anakuwa na lakwakwe na mama pia anakuwa na lakwakwe hakuna anauejihusisha na malezi tunawapa shida watoto, lakini kwa hapa Lindi tunautamaduni wetu, wazazi tunapofarakana na kuachana tunaacha jukumu la ulezi kwa babu na bibi na wazazi hawawajibiki tena’ Alisema Ndemanga.


Awali, Akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Omari, Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt Kheri Kagya ameweka wazi namna ambavyo migogoro ndani ya familia inavyoathiri watoto ambapo amesema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 Mkoa wa Lindi unajumla ya Watoto 3797 walio katika mazingira magumu ambao wametokana na familia ambazo zina migogoro na malezi yasiyofaa huku katika madawati ya jinsia na ustawi wa jamii kukiwa na mashauri ya migogoro ya familia 13796 ambayo kwa sehemu kubwa yanahusu wazazi waliotelekeza watoto na kutotoa matumizi.


Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Lindi Joyce Kitesho amesema Jeshi la Polisi wanayo kampeni ya ushirikishwaji wa jamii isemayo familia yangu haina muhalifu kwani uhalifu huwa unaanzia kwenye ngazi ya familia endapo wazazi  hawatotimiza majukumu yao kikamilifu na akatumia nafasi hiyo kuwaomba wazazi kuwa walezi na sio watoa huduma.


Siku ya Familia Kimataifa Imeenda sambamba na kauli mbiu isemayo tukubali tofauti zetu kwenye familia kuimarisha malezi ya watoto.






BUWASA IPO TAYARI KUSAIDIA KPC

 

Na Alodia Babara, Bukoba

Mwakilishi wa mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba BUWASA mhandisi Matage Doto amesema mamlaka hiyo iko tayari kushirikiana na wadau wengine kusaidia  chama cha waandishi wa habari mkoa wa Kagera (KPC) katika ujenzi wa ofisi ya chama hicho.

Hayo yamekuja baada ya mwenyekiti wa club ya waandishi wa habari mkoani hapa Mbeki Mbeki, kumuomba mgeni rasmi kutoa msaada katika ujenzi wa ofisi ya waandishi wa habari kutokana na club hiyo kuwa na kiwanja ambacho tayari kimeishapata hati miliki.

Mhandisi Doto wakati akihutubia waandishi hao Mei 15,2024 wakati akiwa mgeni rasmi kwa niamba ya Mkurugenzi wa BUWASA katika maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika kimkoa mjini Bukoba ametoa pongezi kwa club hiyo kwa mawazo ya ujenzi wa ofisi na kusema kuwa, endapo club hiyo itaanza ujenzi ishirikishe wadau mbalimbali ikiwemo mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA.)

“Niwapongeze kwa kuwa na mawazo ya kuwa na ofisi yenu, mtakapoandaa mchanganuo wa bajeti ya ujenzi wa ofisi yenu pamoja na kubainisha taasisi zilizopo mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuwapa msaada na pale mtakapoona kwamba na sisi BUWASA tunaweza kusaidia tutakuwa tayari” amesema Mhandisi Doto

Aidha, akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi amesema waandishi wanapaswa kubobea katika kuandika habari Fulani ili waweze kuingia kwa undani juu ya makala wanazokuwa wanaandika.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Club ya waandishi wa habari mkoa wa Kagera Mbeki Mbeki amesema kuwa, maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu ni ya 31, na kutokana na takwimu kutoka World Press Freedom 2024 zimeonyesha Tanzania kufanya vizuri katika kuheshimu uhuru wa habari kwa kushika nafasi ya 97 kwa mwaka 2024 kutoka nafasi ya 142 kwa mwaka 2023.

Amesema Tanzania imepanda kwa kasi kwa nafasi 46 na kuziacha nchi nyingine za ukanda wa Afrika mashariki nyuma.

Mathias Byabato ni mwandishi wa habari mkoani Kagera akichangia juu ya kauli mbiu ya mwaka huu amesema kuwa, licha ya waandishi wa habari kuwa na wajibu wa kuelimisha jamii juu ya changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi pia wataalamu wa mazingira kutoka serikalini wanao wajibu wa kulinda maeneo ya vyanzo vya maji kwa kusimamia sheria.

Byabato ametolea mfano wa eneo la Kasalani na Rwamishenyi manispaa ya Bukoba ambalo ni eneo la maji ya mto Kanoni lakini kimemwagwa kifusi kikionyesha kuna mtu anahitaji kufanya ujenzi katika eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa, siku ya uhuru wa vyombo vya habari huadhimishwa kimataifa kila mwaka Mei 3 na mwaka huu imeadhimishwa Kitaifa jijini Dodoma kwa kusimamiwa na Muunganiko wa Umoja wa Vilabu nchini UTPC na mgeni rasmi alikuwa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasimu Majaliwa na Kimataifa iliadhimishwa nchini Ghana na baada ya siku yenyewe yameadhimishwa ngazi ya mkoa.