Thursday, March 26, 2020

CUBA KUONGEZA NGUVU ZAIDI ITALIA

Na Albert Kawogo.

Cuba inatafakari namna ya kuongeza kikosi kingine cha madaktari ili kuongezea nguvu kasi ya huduma kwa wagonjwa wa corona nchini Italia.

Tayari kikosi cha kwanza Cha madaktari 100 na vifaa tiba kilikwisha ingia nchini humo mwanzoni mwa juma hili huu ukiwa ni uamuzi uliofikiwa na serikali ya Cuba kusaidia jitihada za nchi ya Italia kuokoa uhai wa raia wake.

Zaidi ya waitaliano 80,000 wameambukiwa virusi vya corona hii ikielezwa kuwa ni idadi kubwa kufikiwa na nchi moja barani Ulaya tangu ugonjwa huo ulipoingia Italia miezi miwili iliyopita.

Wizara ya afya ya Cuba imeonyesha nia ya kuongeza madaktari zaidi ili kuunganisha juhudi za serikali ya Italia kupambana na ugonjwa huo ambao wastani wa watu 600 hufariki kila siku nchini humo.

Pamoja na serikali ya Cuba kuishi katika kisima cha vikwazo vya kiuchumi kwa miaka 56 sasa vinavyotokana na shinikizo la Marekani bado serikali hiyo imekuwa ni ya pili kuonyesha nia ya kuisaidia Italia baada ya awali China pia kupeleka madaktari wake nchini humo.

Umoja wa Ulaya EU umekuwa lawamani kwa kushindwa kuweka mikakati ya kuisaidia Italia iliyoathirika zaidi na corona ambapo siku kadhaa zilizopita waitaliano wamekata tamaa na umoja huo hatua iliyowafanya baadhi yao kushusha bendera ya Umoja huo kwenye miji mbalimbali na kupandisha bendera za Cuba na China kama mbadala wake.

Waziri Mkuu wa Italia Giusepe Conte ameonya kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi iwapo waitaliano watapuuzia amri ya kukaa ndani.

"Virusi havitembei bali vinatembezwa na watu, tusipotembea navyo havitatembea na baadae vitakufa vyenyewe" Alisema Conte.

Conte ametoa wito kwa EU kuona namna ya kusaidia nchi zote wanachama zilizoathirika sana ili kupunguza kasi ya kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo barani Ulaya.

RAIS MAGUFULI AMTEUA BRIGEDIA JENERALI MBUNGO KUWA MKURUGENZI WA TAKUKURU

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jenerali John Mbungo kuwa Mkurugenzi wa taasisi hiyo kwa kazi nzuri aliyoifanya ikiwemo ya kurejesha bilioni 8.8 walizodhulumiwa wananchi.

Rais amefanya uteuzi huo leo, Machi 26, 2020 katika hafla ya kupokea ripoti kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali CAG na ripoti ya TAKUKURU katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma.


HADI SASA TUMEWEZA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA NDANI KWA NDANI YA CORONA-WAZIRI UMMY

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Ummy Mwalimu, akiwa na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid na Naibu Katibu Mkuu wake wakati akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Corona (COVID-19) Jijini Dodoma.
...................................


Na WAMJW-DOM.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Ummy Mwalimu, amebainisha kuwa, hadi sasa Tanzania imeweza kudhibiti maambukizi ya ndani kwa ndani ya ugonjwa (COVID-19) na kuwasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga.


Amesema, wasafiri 245 walioingia Tanzania Bara na Zanzibar tangu Machi 23, mwaka huu, wametengwa kwenye hoteli na maeneo yaliyoandaliwa na Serikali kwa gharama zao.


Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa Corona nchini.
Amesema hadi sasa hakuna maambukizi ya ndani (Local transmission) na wagonjwa 13 waliothibitika kuwa na virusi vya ugonjwa huo wanaendelea vizuri.


“Hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa lengo lakutimiza dhamira nzuri ya serikali ya kupunguza hatari ya kusambaa kwa haraka maradhi haya nchini, tunashukuru Mungu bado hatuna ‘Local transmission,”amesema.


Aidha, amesema mgonjwa wa kwanza wa Arusha, amepona Corona na taratibu za kumruhusu kurudi nyumbani zinaendelea.


“Mgonjwa wetu amepona COVID19 na amepimwa mara tatu hana, tumeanza utaratibu wa kumrudisha nyumbani, kazi ambayo nimemuelekeza Katibu Mkuu aifanye sasa hivi suala la kutoa elimu ili kuondoa unyanyapaa, kulaumiana na kunyoshewa vidole Isabela,” amesema.


Kadhalika, amesema wasafiri hao 245 wamewekwa karantini kwa siku 14 kwenye maeneo maalum ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt.John Pombe Magufuli.


“Tangu agizo la Rais wasafiri 111 kwa Tanzania barana 134 kwa Zanzibar wametengwa kwenye hayo maeneo, na tunasisitiza mikoa yote nchini kuendelea na zoezi la kubainisha sehemu zitakazo tumika kuweka wasafiri bila kuleta usumbufu usio wa lazima,”amesema.


Pamoja na hayo, Waziri huyo amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Zanzibar imeendelea kufanya ukaguzi kwa kupima joto lamwili kwa wasafiri wote wanaoingia nchini.


“Kuanzia Januari mosi mwaka huu hadi sasa wasafiri 1,890,532 wamefanyiwa ukaguzi wa kupimwa joto kwenye vituo 27 vya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandarini na kwa saa 24 zilizopita jumla yawasafiri 3,471 wamefanyiwa ‘screening’,”amesema.


Amefafanua kuwa watu 273 wamepimwa sampuli za kupima virusi vya Corona katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii hadi Machi 26,2020.


“Kati ya sampuli hizo zilizopimwa 260 hazikuonesha uwepo wa virusi hivyo na sampuli 13 zilithibitika kuwa na virusi, wagonjwa hawa ni kutoka Mkoa wa Arusha (2), Dar es salaam(8), Zanzibar (2) na Kagera (1),”amesema.


Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameshukuru msaada wa vifaa mbali mbali ikiwemo vya kupima virusi haraka (Rapid test kits) kutoka kwa Taasisi zilizopo Jamhuri ya watu wa China za Jack Ma na Alibaba na vitasambazwa kwenye hospitali zilizotengwa maalum kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hao.

Waziri Ummy amesema maabara iliyopo haijazidiwa na utaratibu mzuri umeandaliwa wa upimaji wa sampuli kutoka mikoani.


Aidha, amesema serikali inatarajia kuongeza maabara sita na Zanzibar moja.


“Tumeona pia kuna haja ya kuongeza maabara, tayari maabara ya Chuo Kikuu Sokoine (Sua) inaweza kupima sampuli, pia maabara za NIMR Mbeya, Tanga, Mwanza na Arusha ile maabara ya St.Nelson Mandela, hili tumeliona lakini tumeona kuna haja ya kuwa na ‘rapid test’, tupo vizuri hatujazidiwa na sampuli zinafika kwa wakati kwenye maabara yetu,”amesema.


Waziri huyo amesema vipimo vya kupima virusi kwa haraka vitawekwa kwenye Hospitali za Mikoa, Kanda na kwenye mipaka.


“Jumuia ya ya Afrika Mashariki pia jana tumepata msaada wa maabara zinazotembea, na tuta pata mbili kwa Tanzania ambazo zitapelekwa Arusha na Zanzibar,”amesema.


Naye, Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad RashidMohammed, amewataka Watanzania kujikinga na ugonjwa huo huku akisisitiza kuwa Serikali haina nia ya kumuweka mtu kambini kumtesa.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Ummy Mwalimu, akieleza jambo, wakati akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Corona (COVID-19) Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula wakifuatilia neno kutoka kwa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha, wakati akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Corona (COVID-19) Jijini Dodoma.