Tuesday, November 19, 2019

Rais Magufuli ateua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa TMA


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Description: Description: Description: Description: Description: Coat of ArmsKURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Simu: 255-22-2114512, 2116898
Baruapepe: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz              

Nukushi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
      IKULU,
 1 BARABARA YA BARACK OBAMA,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ikulu, Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Buruhani Salum Nyenzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

Dkt. Nyenzi (Tanzania Bara) anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Makame Omar Makame kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TMA.

Dkt. Makame (Zanzibar) ni Mhadhiri Mwandamizi wa Jiografia katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hao umeanza tarehe 18 Novemba, 2019.





Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Mfumo wa TANePS Kuleta Tija na Ufanisi Katika Sekta ya Ununuzi ya Umma





Na Jovina Bujulu, MAELEZO, Dar es Salaam

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kujidhihirisha jinsi inavyofanya kazi kwa ufanisi na weledi kwa kuhakikisha inatekeleza mipango yake kwa kasi inavyotakiwa. 

Hatua hiyo inapelekea utendaji wa kazi za Serikali kuwa bora na zenye tija kwa wananchi siku hadi siku na zenye nia ya kuleta mabadiliko katika utekelezwaji wa miradi mbalimbali ambayo hutumia pesa nyingi za umma inayoendana na thamani ya pesa.

Kwa kuzingatia kuwa fedha zitumikazo katika utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa kiasi kikubwa hutumika kupitia mfumo wa ununuzi wa umma. Ili kuleta tija kwa taifa, Serikali imeamua kuimarisha eneo hilo kwa kuanzisha Mfumo wa Ununuzi kwa njia ya Kielektroniki (TANePS) ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Ili uwe endelevu, mfumo umetayarishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuziwa Umma ya Mwaka 2011na Kanuni za Ununuzi wa Umma chini ya Tangazo la Serikali Na. 446 la Mwaka 2013. Sehemu ya XI ya Kanuni hizo inabainisha utaratibu wa mfumo wa manunuzi kwa njia ya mtandao kwa mujibu wa Kanuni ya 343,mambo yatakayotekelezwa kwa mfumo ni pamoja na usajili wa watumiaji, mchakato wa zabuni, ununuzi wa bidhaa, mnada wa mtandaoni, malipo ya ada mbalimbali pamoja na usimamizi wa mikataba mbalimbali.

Akizungumza mfumo huo hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema kuwa mfumo umeanzishwa ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika kupitia ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi.

Mfumo wa ununuzi umeanza kutumika tayari kuanzia mwezi Machi 2018 kwa mujibu wa Kanuni ya 342(1) ambapo baadhi ya taasisi za umma zimeunganishwa baada ya kukamilisha taratibu muhimu ikiwemo mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo na mfumo huo upo wazi kwa wafanyabiashara kujisajili.

Akielezea baadhi ya faida za mfumo huo, Katibu Mkuu James alisema kuwa ni pamoja na kurahisisha ushiriki wa wazabuni kwenye michakato ya ununuzi na hivyo kuongeza ushindani na ufanisi na kupunguza muda unaotumika katika mchakato wa zabuni.

“Mfumo huu utaongeza uwazi na kupunguza vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha uwajibikaji kutokana na urahisi wa uhakiki wa michakato ya zabuni inayoendeshwa, kupunguza gharama za ununuzi kutokana na uokoaji wa muda,  pamoja  na kupunguza  muda wa kuandaa vikao na tathmini yake pamoja na kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu za ununuzi.” alisisitiza Katibu Mkuu James.

Inakadiriwa kwamba kuanzishwa kwa mfumo huu kutaokoa wastani wa shilingi bilioni 34 katika miaka mitano ya kwanza, hali ambayo itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa uliokuwa unatokana na matumizi yasiyo na tija ambayo yalikuwa kwenye mfumo wa kawaida.

Kwa kuzingatia manufaa ya mfumo huo, Serikali imeagiza PPRA kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 31, Desemba, mwaka huu ihakikishe kwamba taasisi zote za nunuzi nchini ziwe zimeungwa katika mfumo huo.

“ Natoa wito kwa wazabuni, taasisi binafsi na za umma  na wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma ya Serikali  ya kuwa na mfumo wenye tija kwa taifa” alisema James.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Leonard Kapongo alisema baada ya kupatiwa maelekezo hayo Mamlaka ilianza kutoa  mafunzo kuhusiana na matumizi ya mfumo wa TANePS kwa maafisa wa ununuzi na TEHAMA wa taasisi za Umma.

“Mpaka sasa Mamlaka imefanikiwa kuunganisha taasisi 418, huku  wataalamu waliopatiwa mafunzo kutoka taasisi nunuzi ikifikia 1,600 ambapo mara baada ya kupatiwa mafunzo taasisi zao huunganishwa kwenye mfumo na kuendelea kutekeleza michakato yote ya ununuzi inayofuata” alisema Mhandisi Kapongo.

Mhandisi Kapongo alitoa rai kwa wakuu wa taasisi kuhakikisha kwamba wanatumia mfumo huo kwani ni takwa la Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake, na kwamba PPRA watafuatilia kwa karibu kuhakikisha matumizi sahihi ya mfumo huo.

Watoa huduma mbalimbali, wazabuni na makandarasi wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kushiriki kwenye michakato ya zabuni kwa kujisajili TANePS kupitia tovuti ya mfumo ambayo ni, www.taneps.go.tz ambapo watapata maelekezo mbalimbali ya namna ya kujisajili.

Akizungumzia faida ya mfumo huo kwa wazabuni, Mhandisi Kapongo alisema kuwa ni mfumo uliorahisishwa sana kwa vile hawatahitaji tena kutumia makabrasha au kusafiri kwa ajili ya kuwasilisha zabuni zao.

“Mambo yote hayo yatafanyika kwa njia ya mtandao, yakihusisha kutangazwa kwa mipango ya ununuzi ya mwaka, matangazo mahsusi ya zabuni na Wazabuni waliosajiliwa kuweza kupakua nyaraka za zabuni na kuziwasilisha kwa taasisi nunuzi kwa njia ya mtandao na majibu ya washindi wa zabuni yatatangazwa kwenye mtandao wa mfumo” alisema Mhandisi Kapongo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Dkt, Marten Lumbanga ameunga mkono mfumo huo na kuongeza kuwa utarahisisha kazi na kuweka uwazi kwa mapato ya Serikali yanayoingia kupitia ununuzi kwa taasisi za umma.


Uchaguzi Mkuu CHADEMA Kufanyika Desemba 18, 2019

 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimetangaza ratiba ya uchaguzi wa viongozi wake ngazi ya Taifa.

Mchakato huo unaanza na uchukuaji na urejeshaji fomu kuanzia  Novemba 18 hadi Novemba 30, 2019 huku mkutano mkuu ukifanyika Desemba 18, 2019.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji akizungumza na wanahabari makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam alisema uchaguzi huo utaanza kwa kuchagua viongozi ngazi ya mabaraza na kufuatiwa na viongozi wakuu wa chama ngazi ya Taifa.

"Tutakuwa na Mkutano Mkuu wa Taifa itakuwa December 18, 2019, tushapeleka mialiko kwa watu mbalimbali, miongoni mwa mambo tutakayoyafanya siku hiyo ni kuchagua Viongozi Wakuu wa Chama

"Mchakato tunaoanza nao ni kuchukua na kurudisha fomu za Wagombea, huu mchakato unaanza November 18, 2019, wote ambao wangependa kugombea nafasi mbalimbali wanakaribishwa kuja kuchukua fomu, kujaza kwa ufasaha na kwenda kugombea" Amesema 
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji

Amesema baada ya kupitia majina ya wote walioomba, Desemba 8, 2019 kamati tendaji ya baraza la vijana na wazee watakutana na kufuatiwa na mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa mabaraza hayo Desemba 9, 2019.

Dk Mashinji amesema Desemba 10, 2019 kamati tendaji ya baraza la wazee na vijana itakutana ambapo ni vikao vinavyofanyika kufuatiwa na mkutano mkuu.

Serikali yalifunga Kanisa la Mfalme Zumaridi Jijini Mwanza

Uongozi wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza umepiga marufuku ibada zinazoendeshwa na kiongozi wa kanisa la Mfalme Zumaridi lililoko mtaa wa Iseni kata ya Butimba hadi hapo Serikali itakapojiridhisha kuwa ibada hazikinzani na sheria za nchi.
 
Agizo la kupiga marufuku limetolewa  jana Novemba 18, 2019 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza Daktari Philis Nyimbi akiwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo katika eneo la kanisa hilo.

Amesema kanisa hilo limekuwa likitumia katiba ya kanisa lingine ambalo ni Pentecoste Christian Church of Tanzania  na pia limekuwa likitembea na Katiba ya Kanisa hilo.

DC Nyimbi amesema kiongozi wa Kanisa hilo la Mfalme Zumarid amekuwa akiendesha kanisa hilo bila kufuata sheria za nchi wala maandiko matakatifu kwa kujiita Mungu wa Dunia, Mfalme wakati yeye ni Mwanamke.

Diamond Platnumz atunukiwa tuzo ya kujali na kuthamini jamii..wasema anastahili kupewa hongera na kutiwa moyo




Taasisis ya The Foundation for Conserving Natural Resources Based for Future Generation (FCRFG) na wadau wengine wametangaza nia yao ya kumtuza msanii maarufu hapa nchini Nasib Abdul maarufu Diamond Platnumz tuzo maalum ikiwa ni sehemu ya kutambua jitihada zake anazozifanya katika jamii.

Diamond ameweza kujitoa na kusaidia jamii kwa njia tofauti, ameweza kuwalipia watoto gharama za upasuaji wa moyo katika hospitali ya Taifa Muhimbili, kufuturisha watu wa makundi maalum, kutoa michango ya madawati, kutoa bodaboda kwa vijana na kusaidia wakina mama wajasiliamali.

Akizungumza na wanahabari mapema hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya TCRFG Bw. Omary Kalekela amesema wameamua kufikia maamuzi hayo baada ya kutafakali kwa kina kazi anazofanya msanii huyo kwa jamii.

“sisi kama wadau wa maendeleo tumeona msanii huyu amefanya mengi mazuri lakini kubwa ambalo limetugusa ni suala la kujitolea kuwalipia watoto wenye matatizo ya moyo pale hospitali ya taifa ya Muhimbili, ni kitendo ambacho kinatia moyo na faraja kwa jamii, kukaa kimya bila kumpa pongezi na kumtia moyo itakuwa si uungwana na ni uchoyo wa fadhila, sisi kama wadau wa maendeleo hatupo tayari kuwa wachoyo wa fadhila” alisema Kalekela.

Alisema tuzo hiyo inatarajiwa kutolewa katika ofisi za wasafi media, Jumamosi hii, pia siku hiyo Diamond Platnumz atavalisha joho maalum na kukabidhiwa Jogooo ikiwa ni ishara ya ujemedari wake wa kufanya kazi bila kuchoka licha ya kwamba hakusoma na kufikia ngazi ya digrii.

Pia Taasisi hiyo ilitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujitoa kwake na kuwathamini wasanii hadi kufikia hatua ya kutoa milioni 100 kwa ajili yao, lakini pia amesema wataendelea kumuombea Rais na wasaidizi wake wawe na afya njema na waendelee kutekeleza majukumu yao wakiwa na afya njema.

Sunday, November 17, 2019

Chuo kikuu cha Dar es salaam chafanya mahafali ya 49 kwa duru ya pili, zaidi ya wanafunzi 8,000 wahitimu









Selemani magali

Chuo Kikuu cha Daresalaam kimefanya mahafali yake ya 49 dulu ya pili na tatu huku ikiwashauri wahitimu kwenda kuyafanyia kazi yote waliyojifunza ikiwemo kuwa wabunifu na kujitengenezea ajira kwa kufanya ujasiliamali.

Mahafili hayo ambayo yalifayonyika katika ukumbi wa mlimani city yalishuhudia wahitimu wa digrii za uzamili, awali, astashahada na vyeti wakitunukiwa tuzo mbalimbali.

Akizungumza kabla ya kuwatunuku wahitimu, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuuu cha Dar es salaam Prof William A.L Anangisye alisema kwa ujumla katika mwaka 2019 wahitimu 8,313( wanawake 3201 au asilimia 38.5) wamefuzu na wamestahili kutunukiwa tuzo mbalimbali za Chuo kikuu cha Dare salaam.

Alisema kwa duru la pili kulikuwa na jumla ya wanafunzi 5, 444 (wanawake 2,194 sawa na asilimia 40.3) kati yao, 95 (wanawaker 33 sawa na asilimia 34.7) wamefuzu na wanastahili kutunukiwa shahada ya uzamivu; 575 (wanawake 223 sawa na 38.9%) wamefuzu na wanastahili kutunukiwa shahada za umahili; 250 (wanawake 102 sawa na 40.8%) wamefuzu masomo ya stashahada za uzamili; na 4,276 (wanawake 1,747 sawa 40.9%) wamefuzu na wanastahili kutunukiwa shahada za awali.

Aidha akitoa nasaha zake kwa wanafunzi, Anangisye aliwataka wanafunzi hao kwenda kuwa chachu ya maendeleo, akisema wameandaliwa vizuri kupambana kuleta maendeleo kwao wenyewe na Taifa kwa ujumla na kwamba Chuo kinawategemea kwenda kuleta mabadiliko na kukiletea heshima katika jamii.

“Mnapoondoka hapa na kujiunga na jamii  kama sehemu ya nguvu kazi ya muhimu, mnafahamu kwamba mnaingia katika ulimwengu unaobadilika haraka mno. Ni muhimu nanyi mkawa wepesi mno wa kujifunza mambo mapya na kubadilika kwa haraka ili msiachwe nyuma na wakati. Ni vyema kuzingatia msingi huu katika kutekeleza kazi zenu za kitaaluma mtakaozokuwa mkizifanyana katika maisha yenu ya kila siku” Alisema Anangisye

Pia amewataka wanafunzi kuwawatu wa kutafuta fursa badala ya kusubili fursa kuwafuata jambo ambalo si rahisi kutokea kwa ulimwengu wa sasa, lakini pia amewashauri kuacha woga na wawe na hulka ya kujaribu mambo ambayo yanaonekana ni magumu n ahata pale watakaposhindwa kufikia mafanikio , wasife moyo, bali waendelee kuwa na ari ya kujaribu tena na tena mpaka mafanikio yapatikane


ADC YAGOMA KUFUATA MKUMBO...YASEMA WATASHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2019

Katibu Mkuu wa Chama cha ADC  Doyo Hassan Doyo akizungumza na waandishi wa habari katika makao mkuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es salaam wakati alipotangaza msimamo wa chama hicho kushiriki uchaguzi wa serikali ya mtaa, amesema chama hicho kitashiriki uchaguzi, Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa ADC Bi. Queen Sendiga.


Chama cha Alliance For Democratic Change’ (ADC) kimetangaza kushuriki katika uchaguzi wa serikali wa mitaa wakisisitiza kuwa hawaoni sababu ya kutoshiriki huku kuna wagombea wao ambao wamepitishwa katika uchaguzi huo.
Akizungumza na Waandishi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo amesema Chama chao kitashiriki uchaguzi huo licha ya ‘figisu figisu’ zilizojitokeza zilizosababisha baadhi ya wagombea wake kukosa kuenguliwa huku akikiri kuwa baadhi yao ‘walijichanganya’ katika mchakato wa ujazaji fomu za uteuzi.
Tunao wagombea wetu ambao wamepitishwakugombeamaeneo mbalimbali, kujitoa katika uchaguzi huu ni kuwanyima haki ya wananchi ya kuchagua viongozi wanaowataka, lakini pia kuwanyima wanachama wetu haki ya kugombea. Ndiyo maana tunagombea.

SERIKALI YASISITIZA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA 2019 UKO PALEPALE


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Nyamuhanga akizungumza na waandishi wa habari leo wakati walipotangaza msimamo wa serikali kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji ambapo Kampeni zinatarajiwa kuwanza kesho.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Nyamuhanga alipokuwa akizungumza nao leo ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change ADC Bw. Doyo Hassan Doyo akizungumza na waandishi wa habari katika makao mkuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es salaam wakati alipotangaza msimamo wa chama hicho kushiriki uchaguzi huo amesema chama hicho kinashiriki kikamilifu, Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa ADC Bi. Queen Sendiga.
Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change ADC Bw. Doyo Hassan Doyo Naibu Katibu Mkuu wa ADC Bi. Queen Sendiga wakiwa katika picha ya pamoja na wagombea wao wanaoshiriki katika nyazifa mbalimbali za uchaguzi huo.
Naibu Katibu Mkuu wa ADC Bi. Queen Sendiga akizungumza na kusisitiza jambo katika mkutano huo.
Baadhi ya wagombea wa chama cha Chama cha ‘Alliance For Africa Farmers Party’ (AAFP) wameenguliwa katika uchagzui huo kwa makosa mbalimbali ya kikanuni na kisheria..
Katibu Mkuu wa AAFP Rashid Rai akizungumzzia kuhusu makosa mbaimbali ambayo wagombe wa chama chake walifanya na kisha kuengeuliwa kikanuni na wasimamizi wa uchaguzi.
Katibu Mkuu wa AAFP Rashid Rai akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu yao yaliyopo Tandika wilayani Temeke jijini Dar es salaam.
……………………………………………………….
SERIKALI imeweka wazi kwamba uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 24 mwaka 2019 uko pale pale huku ikitangaza kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi huo zikitarajiwa kuanza kesho. 
Hivyo vyama vyote ambavyo vitashiriki uchaguzi huo zimetakiwa kupeleka ratiba ya mikutano yao ya kampeni kwa wakuu wa Polisi wa Wilaya kwa lengo la kupatiwa ulinzi kuhakikisha kampeni hizo zinakuwa salama na wagombea kupata fursa ya kujinadi kwa wapiga kura.
Wakati Serikali ikitoa msimamo huo baadhi ya  vyama kadhaa vya upinzani kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Chama cha Wananchi(CUF) ,Chama cha ACT Wazalendo , Chama cha Chauma na NCCR Mageuzi wao walishatangaza kujitokea ,huku Chama Cha Mapinduzi(CCM) na vyama kadhaa vya upinzani vimetangaza kutoshiriki.
Akizungumza leo Novemba 16,mwaka 2019 Katibu Mkuu  wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Nyamuhanga amesisitiza uchaguzi huo utafanyika kama ambavyo imepangwa na kampeni itaanza kesho nchini na kila kitu kiko sawa.
Amefafanua kuwa kwamba Watanzania waajiandae kusikiliza mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa na kisha Novemba 24 wakachague viongozi wao .Tunaomba vyama ambavyo vitashiriki kujiandaa na kampeni ambazo zinaanza kesho( leo) , ushauri wetu kwa vyama hivyo ni kupeleka ratiba ya mikutano yao ya kampeni za uchaguzi huu kwa wakuu wa polisi wa wilaya ili wapatiwe ulinzi,”alisema.
Kuhusu kampeni za uchagzi huo, ameeleza kuwa baada ya kuanza kesho,zitahitimishwa Novemba 23 mwaka huu ambayo itakuwa siku moja kabla ya upigaji wa kura kwa vyama vyote ambavyo vimebakia katika uchaguzi huo.Amesisitiza hakuna sababu ya uchaguzi huo kuusogeza mbele wala kuuahirisha.
Ameongeza kuwa kampeni  za uchaguzi huo zinazoanza kesho zitafanyika katika maeneo yenye wagombea pekee na kuyaacha maeneo ambayo wagombea wake wamejitoa au kupita bila kupingwa jambo ambalo pia limevifanya vituo vya uchaguzi kupungua kwa kiwango fulani kutoka vituo 1,10000.
Nyamuhanga amesema  kwa ujumla wagombea waliopita bila kupingwa katika mchakato wa uchaguzi huo nchi nzima ni 1,2319 sawa na asilimia 55 ya wagombea wote waliokuwa wamejitokeza kuomba kuteuliwa huku akitoa msisitizo kwa vyama vyote kufanya kampeni za kistaarabu.
Amesisitiza kuwa Wasimamizi wa uchaguzi, askari Polisi, mgambo wote wanapaswa kuwa katika sare kipindi chote cha kampeni  hadi uchaguzi utakapofanyika ili kuondoa mkanganyiko wowote unaoweza kujitokeza huku akitoa onyo kwa vyama hivyo  na kuvitaka kuacha kutumia vikundi vya sungusungu na vinginevyo na kwamba sheria itachukua mkondo wake pale ambapo agizo hilo utekelezaji wake utakiukwa.
Katibu Mkuu Nyamuhanga amesema maandalizi ya uchaguzi huo yameshakamilika ikiwemo wino maalumu utakapakwa kidoleni mara baada ya kupiga kura pamoja na rakiri itakayotumika kufungia masanduku mara baada ya kuhitimishwa kwa zoezi la kupiga kura.
 Wakati Serikali ikisisitiza kufanya uchaguzi huo, vyama vya ‘Alliance For Democratic Change’ (ADC) pamoja na Chama cha ‘Alliance For Africa Farmers Party’ (AAFP) vimetangaza kushiriki uchaguzi huo kwa kudai havioni sababu yoyote ya wao kujitoa.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Vyama vya Tanzania Labour Party(TLP) na chama cha National Reconstruction Party (NRA) kutangaza kushiriki mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa vikidai kuwa kufanya hivyo ni kuitendea haki demokrasia iliyopo nchini.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo amesema Chama chao kitashiriki uchaguzi huo licha ya ‘figisu figisu’ zilizojitokeza zilizosababisha baadhi ya wagombea wake kukosa kuenguliwa huku akikiri kuwa baadhi yao ‘walijichanganya’ katika mchakato wa ujazaji fomu za uteuzi.
Amesema ni kweli wapo waliofanya makosa ya aina mbalimbali katika ujazaji fomu hatua iliyosababisha kukiuka kanuni,  kilichosababisha hayo kutokea hatuwezi kukilaumu kwa kuwa mengine yalitokana na uzembe wao kwa  kutowapa elimu wagombea wao kabla ya kuzijaza fomu hizo.
 Wakati  Katibu Mkuu wa AAFP Rashid Rai, pamoja na kusisitiza kushiriki katika uchaguzi huo, amesema  changamoto iliyojitokeza katika chama chake na kusababisha wagombea wake kuenguliwa ni kukiuka kanuni katika ujazaji fomu.
Hata hivyo amesema licha ya kujitokeza kwa changamoto mbalimbali wao bado watashiriki katika uchaguzi huo kwa kuwa bado wanao wagombea katika baadhi ya maeneo nchini.’Kwetu  hata tukipata mtaa mmoja ni ushindi wa zaidi ya asilimia hamsini, haijarishi wenzetu wameshinda viti vingapi,”ameongeza.
Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa ulioanza Oktoba mwaka huu  kwa mchakato wa uandikishaji wapiga kura na baadae uchukuaji fomu, urejeshaji wa fomu, ukataji rufaa na sasa.kuanza kwa kampeni ambazo zitahimitishwa kwa kufanyika uchaguzi huo Novemba 24 kwa wananchi kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

Friday, November 15, 2019

WANANCHI KISARAWE WAFURAHIA ELIMU YA KODI TOKA TRA.

Na Shushu Joel.

WANANCHI wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wamefurahishwa na huduma ya elimu kwa mlipa kodi inayotolewa na mamlaka ya mapato nchini (TRA).

Wakizungumza mara baada ya kutembelewa na wahudumu kutoka TRA walisema kuwa elimu imekuwa kubwa na yenye mashiko kwa wafanyabiashara.

James Joackim ni mmoja wa wafanyabiashara wa muda mrefu katika wilaya hiyo anasema kuwa tangu aanze biashara kipindi hiki amefurahishwa na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo kwa jinsi wanavyojitoa kuwaelimisha wafanyabiasha.

"Miaka ya nyuma ilikuwa ukiwaona watu kutoka TRA unakuwa kama umewaona polisi hata ilifikia hatua ya kuwaona watu wa mapato unafunga duka lakini kipindi hiki ni raha sana"Alisema Joackim.

Aidha aliongeza kuwa elimu hii iendelee kutolewa mara kwa mara ili wafanyabiasha waweze kupata elimu zaidi.

Kwa upande wake Bi' Mariam Mbaga ameishukuru mamlaka ya mapato kwa kuelimisha juu ya utoaji wa risiti kwa wateja.

Pia amesema kuwa amewataka wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi katika zoezi linalofanywa na mamlaka ya mapato kwani elimu ni nzuri sana hivyo ukikosa elimu hii utajutia sana.

Naye Mkurugenzi wa huduma ya elimu kwa walipa kodi Richard Kayombo alisema kuwa mamalaka ya mapato nchini imeamua kuwafuata wananchi katika mkoa wa Pwani na Morogoro kwa madhumuni ya kuwaelimisha na kuwasaidia kutatua changamoto zao.

"Kampeni hii ya kuwaelimisha wananchi juu ya ulipaji wa kodi kwa hiyari ni endelevu na litafika kila mkoa kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara na wananchi juu ya malipo ya kodi" Alisema Kayombo.

Aliongeza kuwa sio kila mtu anatakiwa alipe kodi hivyo ni muhimu sana kuwasikiliza watoa huduma kutoka TRA ili waweze kukuelimisha juu ya nani anastahili kulipa au kutokulipa.

Aidha Kayombo aliongeza kuwa dhamira ya mamlaka ni kuwaelimisha wananchi juu ya upataji wa namba ya utambulisho kwa mlipa kodi (TIN) na uchukuaji wa risiti kwa wanunuzi ni jambo la muhimu sana.

Akitoa ufafanuzi juu ya faida za kulipa kodi mkurugenzi huyo wa huduma ya elimu kwa walipa kodi alisema kuwa miradi yote inayotekelezwa kwa pesa za ndani ni matokeo ya ulipaji kodi.

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la ulipaji kodi za majengo, biashara na kodi zjngine ili kuisaidia serikali katika ufanikishaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wingi.