Wednesday, February 27, 2019

Manispaa Ya Ubungo Yapitisha Bajeti Ya Billioni 84, Mwaka Wa Fedha 2019/2020


Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo yapitisha Makadirio ya beti ya 2019/2020 Kutumia Kiasi cha Tsh Billioni 84.6 kwa mwaka wa fedha 2019/2020. 

Akisoma Hotuba yake Mstahiki Meya Manispaa ya Ubungo,Mh Boniface Jacob, amefanunua kuwa katika pesa hizo serikali itatoa ruzuku ya Billioni 65.5,Millioni 750 ni  michango ya Wananchi na billioni 18.4 ni Makusanyo ya ndani.

Ambapo katika matumizi yake fedha hizo,Billioni 72.3 ni Mishahara ya watumishi,Na kiasi cha billioni 12.3 zimeelekezwa katika miradi Mbalimbali ya Maendeleo

Aidha ameweka msisitizo kuwa Kiasi cha billioni 8.3 sawa na Asilimia 60,za mapato yanayokusanywa na Halmashauri zitatumika kwa ajili ya Miradi ya maendeleo

Mstahiki meya ametaja Vipaumbele 11 vya Halmashauri vilivyomo katika Bajeti hiyo

kuboresha utoaji huduma kwa jamii kwa kuongeza pesa za kujengea Makao makuu ya Halmashauri kiasi cha Millioni 700, Kuanza kujenga Hospitali ya wilaya kwa kiasi cha Tsh Millioni 250

Kutenga fedha za kujenga machinjio ya kisasa kiasi cha  Tsh Millioni 250 pia Kutenga fedha Kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Mbezi ( kwa ajili ya wamachinga) Kiasi cha Tsh millioni 300. 

Kuimarisha Utawala bora kwa kuwatengea fedha za kiinua Mgongo wenyeviti wa Serikali za mitaa wanaomaliza muda wao mwaka 2019

Kuongeza Mapato kwa kuboresha miundombinu ya ukusanyaji, kubuni vyanzo vipya, Uanzishaji wa stendi za daladala Mloganzila na Msumi, Uanzishwaji wa Masoko mapya Kiasi cha Tsh Billioni 1.7 zimetengwa

Kuongeza kiwango cha Uzoaji taka Ngumu kwa manispaa kwa Kununua Vifaa vya ubebaji taka kama magari na mitambo,Kiasi cha Tsh billioni 3.02 kimetengwa

Ujenzi wa Mabweni ya Wavulana na Wasichana shule ya Sekondari Goba TshMillioni 230 zimetengwa

Kutoa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake,Vijana na Walemavu Kiasi cha Tsh billioni 1.38 zimetengwa

Kupima maeneo ya Umma,kwa kutoa hati miliki na kutwaa Maeneo ya miradi ya uwekezaji Kiasi cha Tsh billioni 1.4 zimetengwa

Kwa kuboresha na Kujenga Miundombinu ya Elimu Msingi na Sekondari kwa kujenga madarasa na Nyumba za walimu,Kiasi cha Tsh billioni 1.168 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Aidha Mstahiki meya amesisitiza kuwa,Halmashauri ni chombo cha wananchi  ambacho kimewekwa kisheria  katika kukuza uchumi na kusogeza ajira kwa Vijana ili kupunguza Umasikini hasa wa kipato ili Kujiletea Maisha Bora

IMETOLEWA Na

OFISI YA MSTAHIKI MEYA 

MANISPAA YA UBUNGO

AFISA ANAYETUMIA CHEO KUOMBA RUSHWA YA NGONO AUMBUKA.


AFISA Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Valintine Mbai ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri hiyo ametakiwa kuacha tabia ya kutumia cheo chake kuomba rushwa ya ngono kwa Watendaji wa Vijiji katika Halmashauri hiyo na  kubadili mwenendo wake haraka iwezekanavyo.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 

Akizungumza na watumishi hao, Mary amesema, ni aibu kwa afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia maadili ya kiutumishi kutumia madaraka yake vibaya kwa kuomba rushwa ya ngono toka kwa Watendaji wa Vijiji jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya kiutendaji katika utumishi wa umma.

Amemtaka afisa huyo kuacha tabia hiyo na kujirekebisha maramoja ili awe mfano bora kwa watumishi anaowasimamia kimaadili.

Pia amemtaka, afisa huyo kuwa na heshima kwa wakuu wake wa kazi akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ili kutengeneza mazingira mazuri ya kiutendaji.

Aidha, Mary ametoa angalizo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Juma Abeid kutowatetea watumishi wasio waadilifu na badala yake awachukulie hatua za kinidhamu hata kama ni marafiki zake.
Mary Mwanjelwa ameendelea kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini akiwa wilayani Mkuranga na kutoa wito kwa watumishi wote wa umma kuhakikisha wazingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma.

MRADI WA SOKO LA KISASA MANISPAA YA MOROGORO WAMKUNA DKT. KIJAJI



 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo, wakati akikagua ujenzi wa Soko la Kisasa la Kimkakati la Manispaa ya Morogoro, ambalo ndilo la mfano katika miradi ya kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kujitegemea kimapato.

 Muonekano wa Soko la Kisasa la Kimkakati la Manispaa ya Morogoro, ambalo limekamilika kwa asilimia 30 na linatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali Septemba mwaka huu na kuhudumia wafanyabiashara zaidi ya 900.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa nne kushoto) akietendelea na ukaguzi wa ujenzi wa Soko la Kisasa la Kimkakati la Manispaa ya Morogoro  Mkoani Morogoro .

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

………………………..

Na Peter Haule, WFM, Morogoro

Halmashauri zote nchini zimetakiwa kujifunza kutekeleza miradi ya Kimakakati inayopatiwa ruzuku na Serikali, katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuwa thamani halisi ya mradi wa Soko la kisasa utakaogharimu Sh. bilioni 17 hadi kukamilika kwake inaonekana.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Soko la Kisasa katika Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro wenye lengo la kuzifanya Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kujitegemea kimapato.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Kama ipo halmashauri iliyopewa fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kuwekeana mkataba na Serikali na bado inashindwa kufuata makubaliano ya mkataba ijifunze kutoka Manispaa ya Morogoro.

“Ukilinganisha na miradi mingine ya kimkakati niliyoikagua katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huu ni wa mfano, zipo halmashauri ambazo zimepewa fedha halafu zinarudi tena kuangalia upya mikataba ambayo waliwekeana saini na Serikali jambo ambalo linatia mashaka, tuje tujifunze kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa nini ameweza kwenda na wakati ulio katika mkataba”alisema Dkt. Kijaji.

Alipongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 30 japo walitakiwa kufikia asilimia 40 katika kipindi hiki kutokana na changamoto ya kujaa maji na kuutaka uongozi wa Manispaa hiyo kukamilisha ujenzi ndani ya kipindi cha miezi mitano ili wafanyabiashara waanze kulitumia soko hilo.

“Mapato ya Soko hili yataongezeka kutoka Shilingi bilioni moja, kwa mwaka hadi Sh. bilioni 4 kwa kuwa idadi ya wafanyabiashara itaongezeka kutoka 400 kwa sasa hadi 900 na huduma zingine zitatolewa kama Benki” alieleza Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya kuanzisha miradi ya kimkakati kwa manufaa ya watanzania itatimia kupitia mradi wa Soko la Kisasa la Manispaa ya Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo, ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo Wilayani kwake, kwa kuwa soko lililokuwepo lilijengwa mwaka 1953 hivyo kuwa na miundombinu mibovu iliyosababisha wananchi kuwa na magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu, hivyo mradi huo si tu utaongeza mapato na kuweka mandhari nzuri, lakini pia utaimarisha afya za wananchi.

Naye Meya ya Manispaa ya Morogoro  Bw. Pascal Kihanga, alisema kuwa waliwaahidi wananachi kusimamia ujenzi wa Soko hilo jambo ambalo linatekelezwa kwa juhudi kubwa, hivyo kufikia mwezi Septemba mwaka huu mradi utakabidhiwa kwa Serikali na wafanyabiashara wote walioondolewa kupisha mradi na  wengine watarudi.

Mhandisi wa Mradi huo Antonio Mkinga, amesema kuwa mradi huo utakamilika katika muda uliopangwa, kwa kuwa mpaka sasa hakuna vikwazo ambavyo vinaweza kuzuia utekelezaji wake.

Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri 17 zilizokidhi vigezo vya kutekeleza jumla ya miradi 22 ya kimkakati nchini kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa gharama ya shilingi bilioni 147 ambapo Manispaa hiyo ilipata mradi huo wa soko la kisasa litakalogharimu shilingi bilioni 17.

KATIBU MKUU NISHATI ASIFU WATAALAMU TANESCO


KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua,(watatu kulia), akizungumza na vyombo vya habari mbele ya mashine (turbine) ya kufua umeme inayofanyiwa matengenezo makubwa ya kujilinda kwenye kituo cha kufua umeme wa gesi asilia cha Ubungo II, jijini Dar es Salaam.

KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, amewapongeza wataalamu wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha umeme unawafikia wateja licha ya changamoto ambazo zinawakabili

.

Dkt. Mwinyimvua ametoa pongezi hizo leo Februari 26, 2019 wakati alipotembelea vituo vya kufua umeme wa gesi  vya Ubungo I, Ubungo II, Songas lakini pia kuona kazi ya kufunga transfoma mpya kwenye kituo kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo.  Dkt. Mwinyimvua ambaye alifuatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amesema “Tunazitambua changamoto zinazowakabili, lakini niwapongeze kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wateja.” Alisema.

Akitoa taarifa ya Kituo cha kufua umeme utokanao na gesi asilia cha Ubungo II, Meneja wa kituo Mhandisi Lucas Busunge, alisema kituo hicho kina mashine tatu za kufua umeme kila moja ikizalisha Megawati 43 na hivyo kufanya jumla ya Megwati 129.

Adha kwa sasa kituo hicho kiko kwenye matengenezo makubwa ya kinga yaani (Preventive maintanence), kwa jina la kitaalamu matengenezo hayo huitwa Level C Inspection na hufanyika baada ya mitambo kutembea zaidi ya masaa 40,000 tangu kituo kianze kuzalisha umeme, alisema Mhandisi Busunge.

“Matengenezo haya yatahusisha mitambo yote mitatu na mtambo wa kwanza ulianza kutengenezwa Januari 9, 2019 katika mtambo namba mbili na yatafanyika kwa awamu kwa kuzima mtambo mmoja baada ya mwingine hadi yatakapokamilika na tunatarajia kazi hii ya kufanya matengenezo itakamilika Juni 5, 2019.” Alifafanua.

Matengenezo  hayo yanaambatana na marekebisho ya kufanya mitambo isizime kwa masaa 40 kila baada ya umeme wa Gridi ya Taifa kukatika kama ilivyo hivi sasa ambapo Gridi ya Taifa ikitoka basi mitambo ina block kwa masaa 40 kabla ya kurejea katika hali yake ya kawaida.

“Marekebisho hayo yataiwezesha mitambo kuweza kuanzisha Gridi kama ilivyo katika vituo vya Kidatu kuweza kurejesha umeme kwa haraka. Hivyo marekebisho haya yatawezesha mitambo kurejesha umeme kwa haraka jijini Dar es Salaam wakati umeme wa Gridi ya Taifa unapokatika.” Alibainisha Mhandisi Busunge.

Katika siku za hivi karibuni kunekuwepo na changamoto ya upatikanaji umeme kwa wakati wote baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ambapo imeelezwa kuwa sehemu kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani hutegemea Kituo Kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo ambacho kina transfoma mbili kubwa kila moja ina uwezo wa kusukuma Megawati 110 kila moja na kufanya jumla ya Megawati 220, lakini pia kuna Megawati zingine 300 kutoka vyanzo vingine vya Songas, Ubungo II na Tegeta na kufanya jumla ya Megawati 520 wakati mahitaji halisi ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani ni Megawati 570 na hapo kunakuwa na upungufu wa Megawati 50.

Kutokana na upungufu huo, Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini TANESCO imechukua hatua ya kununua Transfoma kubwa yenye uwezo wa kusukuma takribani Megawati 240 kutoka kwenye msongo wa kilovoti 220 kuelekea Msongo wa kilovoti 132 ili kuongezea nguvu umeme unaotumika katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani, ameongeza Meneja Miradi wa TANESCO Mhandisi Stephene Manda.

“Tunao umeme wa kutosha kilichokuwa kinasumbua ni namna ya kuushusha umeme huo wa msongo wa kilovoti 220 na kuushusha hadi msongo wa kilovolti 132 na ndiyo kazi tunayofanya hivi sasa ya kufunga transfoma mpya ambayo itatatua changamoto hiyo.” Alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Hamisi Mwinyimvua.

Pia Dkt. Mwinyimvua aliwapongeza TANESCO kwa ubunifu walioufanya wa kufanya marekebisho kwenye mitambo yake mitatu ya Kituo cha kufua umeme wa gesi asilia cha Ubungo II ambapo baada ya marekebisho hayo, umeme ukitoka kwenye Gridi ya Taifa, basi mitambo hiyo inaweza kuingilia kati na hivyo kulifanya jiji la Dar es Salaam na kuwa salama kwa maana ya kutoathirika kwa kutoka kwa Gridi ya Taifa.

 Dkt.Mwinyimvua (wapili kushoto), na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, (kulia), wakiongozwa na Meneja Miradi wa TANESCO, Mhandisi Stephene Manda, (kushoto), walipotembelea kuona transfoma hiyo.

 Hii ndiyo transfoma kubwa mpya yenye uwezo wa kusukuma umeme wa Megawati 240, ambayo inafungwa kwenye Kituo kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo na hivyo kufanya kituo hicho kuwa na transfoma tata.

 Wataalamu wakiwa kwenye chumba cha SCADA wakifuatilia mwenendo wa umeme kutoka vyanzo na vituo mbalimbali vya umeme nchini. Kituo hiki kiko Ungungo.



 Meneja wa Kituo cha kufua umeme utokanao na gesi asilia cha Ubungo II, Mhandisi Lucas Busunge, (kushoto), akifafanua jambo mbele ya Katibu Mkuu, Dkt. Mwinyimvua (wapili kulia) na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, (watatu kushoto).


Mhandisi wa TANESCO ambaye anahudumu kwenye chumba cha udhibiti (control room) cha kituo kikuu cha kupoza na kusambaza umeme cha Ubungo akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu na ujumbe wake, walipotembelea kituo hicho leo Februari 26, 2019.

Kuzaliwa Fatma Bint Muhammad (a.s) ndio siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani-Maulana Sheikh Jalala.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala (kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari katika kukumbuka kuzaliwa kwa Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Bi Fatma bint Muhammad (a.s), kuwa ndio Siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani, Jana Masjid Ghadir, Kigogo Post Jijini Dar es salaam


Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu Nyote.

Siku hii ya leo ambayo kwa tarekh ya Kiislamu tunaita ni Mwezi 9,ni siku ambayo wanazuoni wa Kiislamu wameitangaza kuwa ni Siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani, sababu kubwa ya Tangazo hilo nikutokana na kuzaliwa Bint ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae Bint huyu na Mama huyu na dada huyu ananafasi kubwa katika Dini ya Uislamu.


Mama huyu ambae tunakumbuka mazazi yake ambae Maulamaa wameitangaza kuwa ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani daraja lake mama huyu katika Uislamu ni kama vile daraja la Maryam bint Imran, Mama yake Nabii Issa (a.s). Lakini kwanini kukumbukwa mama huyu lakini vilevile kwani kutangzwa ni siku ya Mwanake wa Kiislamu Duniani.


 Sababu kubwa ni daraja la mwanamke na nafasi ya mwanamke katika jamii na katika Uislamu.Uislamu unamuangalia Mwanamke katika mambo yafuatayo, kwanza Uislamu unamuangalia Mwanamke kwamba ni mwanadamu wa Kawaida kama vile Mwanamume.kwa ibara nyingine nzuri Uislamu hautofautishi kati ya jinsia ya Kiume na jinsia ya Kike.


Na tunaamini kakika Uislamu ya kwamba jinsia hizi mbili zote zipo sawasawa, jinsia ya Kike na Jinsia ya Kiume. Kwahiyo siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani ni siku ya kufuta maneno yanayowezwa kusemwa ya kwamba mwanamume ni bora kuliko mwanamke, hapana ni jinsia mbili ambazo zipo sawasawa kama ni mapungufu basi yapo kwa wanaume na yapo vilevile kwa wanawake.


Jambo la pili ni jambo la haki, mwanamume anahaki kwenye mambo mengi na mambo kadhaa haki hizo vilevile zipo kwa mwanamke, kwa mfano mwanamke anayohaki ya kufanya kazi? Je katika Uislamu mwanamke anayohaki  ya kufanya kazi? Jawabu ndio. Haki hiyo vilevile anayo mwanamke katika Uislamu.


Mwanamume anayohaki ya kuendesha gari, Je mwanamke anaruhusiwa kuendesha gari? Ndio mwanamke vilevile anayohaki ya kuendesha gari katika uislamu. Mwanamume anayohaki ya Elimu, mwanamume anayohaki ya Kusoma mpaka kufikia ngazi za juu, je haki hiyo mwanamke anayo katika uislamu? Ndio mwanamke vilevile anayohaki ya kusoma na kusomeshwa mpaka ngazi za juu.


Katika siku hii ya kumkumbuka mwanamke duniani, katika sikun hii ya kumkumbuka mwanamke wa Kiislamu Duniani moja ya jambo la kuliangazia ni jambo la Elimu ya kwamba wazazi watambue kama walivyokuwa na haki kumsomesha kijana wa kiume na mototo wa kiume vilevile ni haki yao kumsomesha binti wa kike na kijana wa kike na kumsomesha hakuna kiziwizi maalumu ikiwa na maana asomeshwa mpaka ngazi Fulani kasha basi.


Kulikuwa na fikra ambazo zinapatikana kwenye baadhi ya maandiko ambayo maandiko hayo tunayasema ni maandiko ya Kimakosa kwa mfano kuna baadhi ya fikra zinaona Mwanamke ndie aliefanya makosa alipokuwa kule Peponi na ikawa ndio sababu ya kufukuzwa adam na hawa kwamba sababu ilikuwa ni mwanamke.


 Hapana dini ya Uislamu inaangalia yakwamba makosa yaliyofanya ndani ya pepo hayana mahusiano na Mwanamke na kwamba mwanamke ni kiumbe kama vile viumbe wengine wa kawaida. Mwanamume anayokarama anayoheshima, je heshima hii ipo kwa mwanamke?


Mwenyezi Mungu ndani ya Quran anaitaja waziwazi hawa wanaadamu wote wanakarma wanaheshima, kama vilevile mwanamume anatakikana aheshimiwe na vilevile mwanamke anatakikana aheshimiwe, kama vile mwanamume anadaraja kubwa mbele za mwenyezi Mungu kwasababu ni kumbe ambacho kinaroho ya Mungu, daraja hili vilevile analo mwanamke kwasababu nae ni kumbe cha mwenyezi Mungu.


Tunapojaribu kuisoma Quran na kuiangalia Quran iliyowazungumza wanawake na daraja iliyowapa, tutaona ya kwamba daraja hilo halina tofauti na daraja la mwanaume, kwa mfano Quran imewataja wanawake ambao ni wanawake watakatifu kama ilivyowataja wanaume, Quran imemtaja Maryam (a.s) ambae ni mama yake Nabii Issa (a.s) yakwamba ni mwanamke mtakatifu.


Kama ambavyo imemtaja Fatma Zahraa (a.s) ambae leo tunakumbuka mazazi yake katika aya tofauti, kama ambavyo imemtaja mlezi wa Nabii Mussa (a.s) au Mke wa Firaun, Quran imemtaja mwanamke kwa kiwango hicho na kwa daraja hilo na kwa heshima hiyo kama vile ambavyo imemtaja mwanaume kwa heshima na kwa daraja tofauti alilokuwanalo.


 Je, mwanamke anamiliki? Katika Uislamu, mwanamke anayohaki ya kufanya kazi na kumuliki kama anavyomiliki mwanamume? Mwenyezi Mungu anatangaza waziwazi ya kwamba kama alivyokuwa mwanamume anayohaki ya kumiliki vilevile mwanamke anayohaki ya kumiliki, mwanamke anayohaki ya kurithi? Ndio mwanamke hata baada ya kuolewa vilevile anayohaki ya kurithi kama alivyokuwa mwanamume anayohaki ya kurithi.


Kwa ufupi yote tuliyoyasema ni katika kuzungumza daraja na nafsi ya mwanamke katika dini ya Uislamu katika siku hii ambayo tunakumbuka mazazi ya bint ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) bi Fatma bint Muhammad (a.s), katika siku amabyo wanachuoni wameitangaza hii ni siku ya mwanamke duniani.


Kwamba mwanamke ni kiumbe kama kiumbe kingine cha kawaida, jinsia zao ziko sawa, mapungufu kama yapo yapo kwa mwanaume na yapo kwa mwanamke, wana haki sawa kama mwanamume anahaki na vilevile mwanamke anahaki sawa.


Asanteni sana, Hongereni kwa siku hii nzito ya kuzaliwa ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) bi Fatma Zahra bint Muhammad (a.s) na siku ya Mwanamke Duniani.

Imetolewa na 

Maulana Sheikh Hemed Jalala 

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania.     Tare : 26.02.2019, Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.

SERIKALI YA AWAMU YA TANO ITAENDELEA KULINDA NA KUKUZA HAKI ZA BINADAMU -PROF KABUDI ALIAMBIA BARAZA LA HAKI ZA BINADAMU LA UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
 ..................................


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu na ustawi wa jamii kama kipaumbele chake na  itaendelea kushirikiana na Baraza hilo kuhakikisha haki za binadamu nchini na duniani kote zinadumishwa.


Prof. Kabudi amesema hayo alipolihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.


Prof. Kabudi amesema Serikali ya Tanzania imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha haki za binadamu, utawala bora na utii wa sheria nchini na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.


“Serikali imelenga kuimarisha haki za binadamu, utawala bora, utii wa sheria na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, kwa sasa tunatekeleza mpango mkakati wa kitaifa wa kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22, lengo likiwa ni kulinda na kudumisha haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu,” alisema Prof. Kabudi.


Amesema Serikali pia inazingatia suala la kuwapatia haki kwa haraka wananchi wasio na uwezo kwa kutolea maamuzi kwa haraka mashauri yanayowahusu watu wasio na uwezo na kuwapatia msaada wa kisheria kupitia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 ili wananchi hao waweze kupata haki zao kwa wakati.


Aidha, Prof. Kabudi amelihakikishia Baraza hilo kuwa Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari nchini na imeendelea kuhakikisha uhuru wa vyombo hivyo unalindwa huku jumla ya vituo vya redio 152, televisheni 34, magazeti 172  nchini kote yamesajiliwa na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira stahiki yatakayowezesha vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru.


Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuleta ustawi wa jamii kwa kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na kunadi kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote.


“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote na kuongeza kuwa Serikali inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 23 kwa mwezi kutoa elimu pasipo malipo na hivyo kuongeza udahili wa watoto wanaojiunga darasa la kwanza kwa asilimia 35.2 na asilimia 20.1 kwa wanaojiunga na kidato cha kwanza,” alisema.


Prof. Kabudi pia amesema Serikali imedhamiria kufikisha huduma za afya karibu na watanzania wote ambapo imeongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni 269 mwaka 2017/2018 na kuongeza kuwa Serikali inatekeleza mikakati ya kujenga vituo vya afya ambapo hadi sasa imejenga vituo 304, na nyumba za watumishi wa afya 578 zimejengwa nchini kote.


Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kukuza na kulinda haki za binadamu duniani kote na kushughulikia uvunjwaji wa haki za binadamu unaotokea katika nchi wanachama wa umoja huo na kushauri hatua za kuchukuliwa ili kuboresha haki za binadamu duniani.


Baraza hilo pamoja na mambo mengine linatarajia kupokea taarifa mbalimbali kuhusu haki za binadamu duniani na kutoa nafasi kwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa maelezo yao kuhusu utekeelezaji wa wajibu wao wa kulinda na kukuza haki za biandamu katika nchi zao.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maofisa wa Tanzania mara baada ya kuhutubia kikao hicho cha Baraza la Haki za Binadamu jijini Geneva Uswissi.