Monday, August 4, 2025

TCRA YAWAFUNDA BLOGA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

 

Na Mwandishi Wetu

Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni, wameaswa kutotoa taarifa ambazo zitaleta taharuki na machafuko ndani ya nchi hasa katika kuelekea kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge  na Madiwani  utakao fanyika baadaye mwaka huu (2025).


Yamesemwa hayo jana tarehe 3, Agosti 2025 na Meneja Kitengo cha Huduma za Utangazaji,TCRA, Injinia Andrew Kisaka wakati  akiwasilisha makala (mada) katika mkutano ulioandaliwa na  wa  Tume Huru ya Uchaguzi nchini (INEC) kwa  watoa maudhui mtandaoni, amesema kuwa wakati wa uchaguzi kuna mazingira ya migawanyiko, mivutano ya kijamii, na upotoshaji wa hali ya juu hivyo ni muhimu  Mabloga waepuke  kuepuka kusambaza uvumi, kuripoti kwa umakini, kutopendelea upande wowote  na kukemea lugha za chuki.


Kisaka amewataka  bloga nchini kote  kuimarisha maadili yao na kuchukua jukumu muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani kwa kupandisha maudhui yenye tija na kama unaona maudhui yataleta taharuki  ni bora kuachana nayo.


Aidha Kisaka ametoa mfano wa  Historia ya machafuko ya uchaguzi yaliyotea katika nchi Kenya  Nigeria (2007) na Kenya (2011), amesema kuwa, katika machafuko hayo zaidi ya watu 800 walipoteza uhai nchini Nigeria mwaka 2011 wakati nchini Kenya zaidi ya watu 1,000 walipoteza uhai na wengine 600,000 kupoteza makazi.


Aidha amesema kuwa  katika mazingira magumu yenye shinikizo la juu la uchaguzi, vyombo vya habari vinaweza kujikuta vikichangia machafuko kwa kueneza uvumi au kuchochea upendeleo wa kisiasa.


Amesema ili kukabiliana na maafa wakati wa uchaguzi na baada kuna miongozo ya kuripoti ambayo inatatua changamoto hizo.


"Uvumi ndiyo chanzo kikuu cha vurugu hivyo  Vyombo vya habari vinapaswa kuchunguza kwa kina uvumi na kutoa taarifa sahihi haraka iwezekanavyo ili kuzuia mzunguko wa vurugu za kulipiza kisasi." amesema Mhandisi Kisaka.


Pia amehimiza Mabloga  kukataa lugha na vichwa vya Habari vya Kichochezi.


"Msiripoti kila kauli ya uchochezi kutoka kwa wanasiasa ,hata kama kauli hizo zinaonekana kuwa habari kwenu na zenye kuvutia msomaji acha kabisa ni muhimu kutokuzirudia kwenye vichwa vya habari, " amesema Mhandisi Kisaka na kuongeza kuwa lugha inayodhalilisha inaweza kuchochea wananchi kutenda vitendo vya kikatili.


Aidha amesema kuwa  katika kipindi hiki cha uchaguzi, ni  vyema Bloga kuchukua tahadhari binafsi  kutoa  matangazo ya moja kwa moja 'live'   ya mikutano ya kampeni za wagombea kwa sababu yanaweza leta  machafuko.


"Matangazo ya moja kwa moja 'live'  ya machafuko ya uchaguzi yanatakiwa kufanywa na Waandishi Waandamizi na  wenye  uzoefu na siyo 'One Man Show' kama ilivyo kwa Bloga .
Wanaohamasisha chuki na vurugu hawapaswi kupewa nafasi hewani," amesema Mhandisi Kisaka.

Aidha amesema kuwa  vyombo vya habari vinapaswa kuzuia kuonesha picha zinazochochea vurugu  na ikiwa  ni lazima, kusimamisha matangazo ya moja kwa moja ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.


Maafa na miongozo ya kuripoti
katika hali ambapo uchaguzi unafanyika wakati wa maafa, ni sehemu ya elimu zinazotolewa kwa   Mabloga katika kuhakikisha taifa linavuka salama katika uchaguzi wa mwaka 2025 kama ilivyokuwa katika chaguzi nyingine.


WAZALISHAJI WA MAUDHUI MTANDAONI WAHIMIZWA KUHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU 2025

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutanio wa Tume na Wazalishaji Maudhui Mtandaoni kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 03 , 2025.

 

Baadhi ya wawakilishi wa serikali waliohudhuria mkutano huo.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg.Kailima Ramadhani akitoa mada wakati wa ufunguzim wa mkutanio wa Tume na Wazalishaji Maudhui Mtandaoni kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 03 , 2025.

Picha ya pamoja ya washiriki 


NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM.


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele, amewahimiza wazalishaji wa maudhui mtandaoni kutumia majukwaa yao ya kidijitali kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


Akizungumza leo tarehe 03 Agosti, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni, Mhe. Mwambegele amewapongeza wazalishaji hao kwa ushirikiano walioutoa kwa Tume katika hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi.


Mhe. Mwambegele amewasihi wazalishaji hao wa maudhui kuendelea kuwa daraja muhimu kati ya Tume na wananchi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.


“Tuna imani kuwa tutazidi kushirikiana nanyi kwa karibu zaidi, na mtatumia nafasi zenu kuwapatia wananchi taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu kwa kupiga kura,” amesema Mhe. Mwambegele.


Amebainisha kuwa Tume inatambua mchango wa wazalishaji wa maudhui mtandaoni katika njia mbili kuu. Kwanza, kama daraja la mawasiliano kati ya Tume na wadau, na pili, kama wadau wa moja kwa moja wa mchakato wa uchaguzi.


“Tume inathamini kazi yenu ya kuandaa, kuchapisha na kusambaza taarifa kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali kama mitandao ya kijamii, blogu, tovuti na majukwaa ya video kama YouTube,” ameongeza.


Akizungumzia nafasi ya vijana katika uchaguzi, Mhe. Mwambegele amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya kidijitali kwa kundi hilo, akiwahimiza wazalishaji hao wa maudhui kutumia ubunifu wao kwa kutumia michoro, video na ujumbe wenye mvuto ili kuwafikia wapiga kura kwa njia rahisi na ya kuvutia.


Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujadili hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya uchaguzi, kubadilishana mawazo, na kusikiliza changamoto zinazowakabili wazalishaji wa maudhui mtandaoni ili kutafuta suluhisho kwa wakati.


“Mkutano huu si wa upande mmoja; ni jukwaa la mawasiliano ya pande mbili ambalo linawapa fursa ya kueleza changamoto zenu na kusaidia kuboresha utekelezaji wa shughuli za uchaguzi,” ameeleza Mhe. Mwambegele.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani, amehimiza waandaaji wa maudhui mtandaoni kutumia majukwaa yao kutoa habari sahihi, na zilizothibitishwa na kufanyiwa utafiti.


Ameongeza kuwa majukwaa hayo ya kidijitali yanasaidia kurahisisha upokeaji wa taarifa za Tume na kuwafikia wananchi kwa haraka.


Aidha, Bw. Kailima amewahimiza wazalishaji wa maudhui mtandaoni kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, ikiwa ni pamoja na kuitumia kauli mbiu ya uchaguzi “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura” ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba, 2025.


Mkutano kati ya Tume na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni ni mfululizo wa mikutano ya Tume na wadau wa uchaguzi ambayo ilianza tarehe 27 Julai, 2025. Mikutano hiyo inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 04 Agosti, 2025 kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari kupatiwa mafunzo.







Picha mbalimbali za washiriki wa Mkutano huo.


Tuesday, July 8, 2025

DIRA 2050 INA KINGA YA BUNGE -PROF MKUMBO

 

Na Mwandishi wetu 


SERIKALI imewatoa hofu Watanzania kuhusu hoja ya kuwa utekelezaji Dira 2050 unaweza kukumbwa na changamoto ya uhalali wa kisheria na hivyo mpango huo muhimu kwa taifa ukawa na ombwe la kiufanisi hapo baadae 


Akiongea katika kikao maalum na Wahariri kutoka jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Waziri wa nchi ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaii Profesa Kitila Mkumbo amesema Dira ya taifa 2050 imewekewa ulinzi kwa kupelekwa bungeni na kwamba hakuna Rais atakayeweza kwenda kinyume na uamuzi huo


Profesa Mkumbo amesema Dira 2050 itatekelezwa na Marais watatu,na kwa atakaetaka kuibadilisha atatakiwa kupeleka bungeni na kwamba Dira hii imekuwa tofauti kwa kuwa ya 2025 iliishia hatua ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri tu.


Waziri huyo amesema mchakato wa kutengeneza Dira 2050 umepitia hatua 13 ambazo ni kuandaa na kuidhinisha miongozo ya Dira.


Mkakati wa kuandika Dira ulianza Aprili mwaka 2023, kwa kuunda vyombo vya kutathimini mchakato wa Dira na kufanya tathimini ya utekelezaji wa Dira 2025.


Pia kukusanya maoni ya wananchi na wadau juu ya maudhui gani yaingie kwenye Dira, kujifunza kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Asia na Marekani kwa hatua zilizopigwa.


Alizitaja baadhi ya nchi walizojifunza ni Botswana, Moroco, Mauritius, Afrika Kusini na Kenya.


Kwa Asia wamejifunza Kusini mwa Asia za China, Indonesia, Korea Kusini, Singapore na India, na kwamba kwa Ulaya wamejifunza kidogo kutokana na kwamba historia yao si ya muda mrefu kama nchi zenye historia 1,000.


Hatua nyingine ni uchambuzi, uandishi na uhariri wa taarifa na kutoa Rasimu ya kwanza ya Dira 2050.


Pia kulinda rasmu ya kwanza ya Dira 2050 iliyozinduliwa Desemba 2024,na kuchukua Rasimu kupeleka tena kwa wadau ili kupata maoni ya kihariri.


"Tulikutana na wadau mbalimbali kama waandishi wa habari na vyama vya siasa ili kupata makubaliano ya pamoja.


Tulivyokutana na vyama vya siasa tulikubaliana tusibishane juu ya tunakwenda wapi ila tukubaliane tuende huku, Ilani zetu ziakisi tunaenda wapi, "amesema.


Hatua nyingine, ni kutoa rasimu ya pili ya Dira ya Taifa na kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Juni 2025 iliidhinishwa na Baraza la Mawaziri na kufuatiwa na Bunge.


Aidha, amesema hatua ya mwisho ni kuutaarifu umma kuwa mchakato wa Dira umekamilika na itajulikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza Dira  2050 Tanzania Tuitakayo, na hatua ya mwisho ni Rais Samia Suluhu Hassan kuizindua Julai 17, mwaka huu.

Friday, June 13, 2025

ANUSURIKA KIFO BAADA YA KUPIGWA NA WAFUGAJI.

 

Na Omary Mngindo,u


ELIAS Madinga mkazi wa Kitongoji cha Mlelani, Kijiji cha Visezi Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na Wafugaji.


Mkazi huyo akiwa na mkewe katika nyumba ya bosi wake Kitongojini hapo, siku ya tukio akipulizia dawa mazao aliona makundi ya ng'ombe yaliyogawanyika mara tatu yakiingia ndani ya shamba hilo.


Alisema kuwa alipoona hivyo alianza kuiswaga ili itoke shambani, wakati huo akiwepo kijana mdogo jamii ya Wafugaji na kwamba wakati akiendelea na zoezi ilo ghafla yule kijana alitoweka.


"Kwakuwa nilikuwa na zoezi la kupulizia dawa, nikachukua baskeli nikaenda kisimani kuchota maji, wakati narudi nikamuona mke wangu amembeba mtoto wetu wa miezi mitatu wamemzingirwa na Wafugaji hao", alisema Madinga.


Aliongeza kuwa"Nikiwa nakaribia aliniambia nisifike kwani ameshashambuliwa na Wafugaji hao, sikumuelewa wakati nikaribia nikajikuta mimezingrwa na kundi la Wafugaji wakaanza kunishambuliwa kwa silaha mbalimbali za jadi," alisema.


Alieleza kuwa wakati wanamshambulia mke wake aliwaomba wamwachie akamvalishe mtoto nguo, akatumia nafasi hiyo kukimbilia kijijini kutoa taarifa kwa Mwenyekiti, ambapo alifika Askari Mgambo akamchukua wakamkimbiza Zahanati.


"Nilipoteza fahamu niliposhtuka nikajikuta niko Zahanati natibiwa, nilipochukuliwa pale nyumbani sikujitambua, pamoja na kwamba nilikimbilia ndani lakini waliingia wakaendeleza mashambulizi," aliongeza Mhanga huyo.


Aliongeza kwamba "Baada ya kupelekwa kesi Polisi Chalinze walimfuata wakataka kumpatia kiasi cha shilingi laki tatu nikakataa, nafuatilia ili suala ili niende Mahakamani," alimalizia mkazi hiyo.


Swala la wafugaji kudharau mashamba ya wakulima wilayani Bagamoyo limekuwa ni jambo la kawaida hali inayotishia usalama wa wakulima.


Wananchi walioongoe na BAGAMOYO KWANZA BLOG wameiomba Serikali kuchukua hatua dhidi ya wafugaji ili kukomesha vitenda vya dharau na unyanyasaji wanavyofanyiwa wakulima.


Thursday, March 20, 2025

TCRA KUSHIRIKIANA NA TBN KUSADIA KUZALISHA MAUDHUI YENYE TIJA

 


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeahidi kufanyakazi na Mtandao wa Wana Blogu Tanzania (TBN), pamoja na vyama vingine vya waandishi wa habari ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe  19.Machi 2025 Jijini Dar es Salaam na Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alipokutana na ujumbe wa TBN ofisini kwake, katika kikao cha kujadiliana changamoto mbalimbali zinazowakabili Bloga nchini.

“Sisi huwa tunapenda kufanya kazi na vyama ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao, badala ya kufanyakazi na mwaandishi mmoja mmoja…tunafurahi sana kufanyakazi na waandishi kupitia vyama vyao,” amesema Mhandisi Kisaka.

Mhandisi Kisaka amesema kuwa TCRA imefurahi kukutana na TBN kwa kuwa wanafahamu kuwa Bloga wanasehemu kubwa sana kwenye maudhui ya ndani, na hata kwenye usajili wa TCRA Bloga wanachukua nafasi kubwa sana katika maudhui ya mtandaoni.

“Kwa hiyo TBN mtakuwa silaha moja wapo nzuri sana yakutuwezesha sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano nchini, tunao simamia utangazaji pamoja na maudhui ya mtandaoni kuwa karibu na nyinyi na kuhakikisha maudhui ya mtandaoni yanaleta tija na maendeleo kwa wananchi,” amesema Mhandisi Kisaka.

Monday, March 17, 2025

MFUMO WA USAJILI WAANDISHI WA HABARI KIDIJITALI UPO MBIONI KUKAMILIKA- MSIGWA

 


Na Mwandishi Wetu, 

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao (e-GA) inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi wa mfumo wa Usajili na utoaji wa vitambulisho vya kidigitali kwa Waandishi wa Habari nchi nzima - Journalists Accreditation & Registrations System (JARS).


Mfumo huo unaotengenezwa na chini ya Idara ya Habari (Maelezo) na Wataalamu wa Mifumo wa e- GA, unalenga kurahisisha, kuongeza uwazi na kuimarisha utendaji kazi wa waandishi wa Habari kwa kuwapatia huduma ya usajili na utoaji wa vitambulisho vya kazi katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri kwenda Dodoma au Dar es salaam kupata huduma hiyo.


Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo miradi iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita wakati wa mkutano na waandishi wa habari tarehe 16 Machi, 2025 katika Bandari Kavu ya Kwala, mkoani Pwani.


Amebainisha kuwa Mfumo huo pamoja na mambo mengine utakuwa na uwezo wa kusajili, kuhakiki na kuhifadhi taarifa za waandishi wa habari wote nchini


"Mwandishi wa habari atakuwa na uwezo wa kujaza taarifa na kuweka mambo muhimu kama vile picha, mahali anapofanya kazi, taarifa za uraia wake n.k, na Mfumo utatoa alama za usalama ambazo mtu hawezi kughushi," amesema Bw. Msigwa na kuongeza;


"Kupitia mfumo huu Mwandishi wa Habari atakua na uwezo wa kuomba na kupata kitambulisho chake (physical ID). Mfumo una uwezo wa kuonesha taarifa kwenye ukurasa wa nyuma back-end ambazo zitahakikiwa na kutumiwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB kutoa kitambulisho (Press Card) kwa njia ya mtandao".


Amesisitiza kuwa Mfumo utakuwa na uwezo wa kumpatia mwandishi wa habari taarifa kabla ya muda wa kuisha matumizi ya kitambulisho chake (alert when the ID is about to expire) pia utamtumia ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi


Bw. Msigwa amesema kupitia mfumo huo Mwandishi anapoomba kitambulisho atapatiwa namba ya malipo “control Number” ya kulipia mtandaoni na akishalipia malipo yake yataonekana na kupitishwa na mamlaka husika (approved) na kwamba utakuwa na mwonekano wa aina mbili (madirisha) kwa ajili ya waandishi wa ndani na wa nje (International). 


"Mfumo utamwezesha Mwandishi wa Habari kupakia nyaraka muhimu kama vile vyeti vya taaluma kwa ajili ya uhakiki (VERIFICATION) na pia mfumo utapokea maombi ya waandishi wa nje ya nchi na wao kama ilivyo kwa wale wa ndani utawataka kupakia (Requirements) wakiwa wamekidhi vigezo ndipo hatua nyingine itafuata," amesema.


Mfumo utakuwa na uwezo wa kuhakiki taarifa za waandishi kwa kuunganishwa na mifumo mingine ya serikali kama GePG, NIDA, NECTA, Uhamiaji n.k kwa ajili ya malipo, uhakiki wa vyeti na taarifa (Verification).


Aidha, Bw. Msigwa amesema mfumo utakuwa na uwezo wa kuondoa wale wote waliokosa sifa/wasiohuisha taarifa zao pale wanapotakiwa kufanya hivyo, utamwezesha mtumiaji kuweka saini mahali panapohusika (Digital signature) pamoja na kuruhusu taarifa za kitaaluma na eneo la kazi kupatikana kwa njia ya msimbo papo (QR CODE).


"Huduma hii ya kupata vitambulisho vya kidigitali itapatikana kwa Waandishi wa habari wote watakaokuwa wamekidhi vigezo vya kitaaluma (Taaluma ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma),"










Monday, February 24, 2025

WAZIRI KIKWETE KUFANYA ZIARA YA SIKU TATU MKOANI SONGWE.

 

Anatarajiwa kukagua na Kuzindua Miradi ya Maendeleo  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu -Mhe. Ridhiwani Kikwete Februari 23, 2025 amewasili mkoani Songwe kwa lengo la ziara ya  kukagua miradi ya Maendeleo ikiwemo ya sekta  ya Elimu, Afya na Miundombinu   kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya wananchi .


Mhe. Waziri Kikwete anatarajiwa kukagua na kuweka Mawe ya msingi katika miradi hiyo ambayo inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 700 katika Halmashauri zote za mkoa huo.


Mara baada ya kuwasili katika  mkoa huo , Waziri Kikwete alipokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Ndg. Daniel Chongolo ambaye alimpa hali ya maendeleo ya Mkoa huo na maandalizi ambayo yameshafikiwa kwa ajili ya ziara hiyo.


Vile vile Mhe.  Kikwete anatarajiwa pia kukagua Maendeleo ya Kituo cha Vijana cha Sasanda wilayani   Songwe ambapo atakagua  mradi wa Shamba la vijana lililopo kituo hicho.


 Mhe Waziri Kikwete ameambatana  na watendaji mbalimbali ambapo amemhakikishia Mkuu wa mkoa huo  kuwa timu yake ipo tayari kwa ajili ya kazi iliyowaleta.







Saturday, January 4, 2025

MRADI WA MAJIKO YA GESI YA RUZUKU WATUA LINDI

 







NA HADIJA OMARY,  LINDI.


Ili kufikia azma ya Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati kupikia wakala wa  umeme  vijijini (REA) imekuja na program ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku


Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya Leo January 3, 2025 alipokuwa akimtambulisha mtoa huduma hiyo Katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, 


Amesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited kwa ajili ya kutekeleza mradi wa shilingi milioni 317.3 wa kusambaza majiko ya gesi 16,275 (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya 50% sawa na shilingi 19,500 kwa jiko katika maeneo ya vijijini ndani ya Mkoa huo


Amesema Katika program hiyo kwa Mkoa huo wa Lindi Jumla ya Kaya 16,275 Katika Maeneo tofauti ya vijijini linatarajiwa kunufaika huku akibainisha  kuwa lengo la mradi huo ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za Nishati Safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti. 


"Mradi huu unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya, pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza Mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi," alifafanua Mhandisi Yesaya.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa majiko ya ruzuku ambao  utaongeza matumizi ya nishati safi kupikia hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini. 


Pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujaza mitungi pale inapoishiwa gesi ili kuendelea kutumia huku akimuelekeza Mtoa huduma (Taifa Gas) kuhakikisha anakuwa na mawakala kwenye kila kata na vijiji ili kumrahishia mwananchi kubadilisha mtungi pale gesi inapomalizika.


"Ili kuwa na uendelevu wa matumizi ya gesi kupikia, natoa wito kwa Taifa Gas kuwa na mawakala ili kumrahishia mwananchi; tusikubali kumpoteza mtu kurudi kwenye kuni na mkaa kwa sababu ya kukosa mahala pa kubadili mtungi," alielekeza. 


Kwa upande wake, Meneja   mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Kusini, Hawa Omari amesema kuwa wanejipanga vyema kufika kwenye maeneo yote Mkoani hapo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi watakaonunua majiko hayo kabla ya kutumia.


Wednesday, January 1, 2025

NANI ATAKUWA MRITHI WA KINANA CCM?

 

Na Mwandishi Wetu.



NANI atakuwa makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara?


Ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na makada wa CCM na hata wafuatiliaji wa karibu wa siasa nchini, hasa mwaka huu ambao Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu Rais, Wabunge na Madiwani.


Jibu la swali hilo linatarajiwa kupatikana kupitia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwezi huu, lakini kitendawili cha nani atakuwa Makamu Mwenyekiti atakitegua Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Makamu mwenyekiti anayetakiwa kwa wakati huu ni yule ambaye atakuja kufanya kazi ya kuivusha salama CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Anahitajika Makamu Mwenyekiti mwenye uwezo wa kukabili jukwaa na hadhira yake. Makamu Mwenyekiti asiye bubu wala mbabe, asiye mwenye ‘makando kando’, asiyekuwa mbinafsi, mchoyo na ambaye akisema atasikilizwa na kuaminiwa na wanachama na viongozi wenzake wa chama hicho tawala.


Pamoja na majukumu mengine, makamu mwenyekiti atasimamia maadili ndani ya CCM. Ilivyokuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa dola, suala la wanachama kuzingatia maadili ni jambo la msingi kabisa maana ulegevu wowote katika hili ni kupata wagombea ambao hawana maadili. 


Kwa jinsi mambo yana vyokwenda CCM, inahitaji makamu mwenyekiti mwenye ushawishi kwa umma, mwenye nguvu na mvuto ambaye hatoyumbishwa kwa namna yoyote ile iwe Abdallah Bulembo ndani ya CCM au hata nje ya chama hicho.


Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, katika hotuba aliyotoa mwa ka 2005 Chimwaga mkoani Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuteua wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, alitaja sifa 13 anazostahili kuwa nazo mtu anayetaka kushika nafasi hiyo.


Pamoja na nyingine nyingi, Mkapa aliwataka wanaCCM wasichague mtu kwa kumpenda, bali achaguliwe kwa sifa. 


Mkapa akatoa mfano wa bangili akisema hata ikiwa nzuri kiasi gani, kama inabana kwenye mkono haifai.


Je, hao wanaotajwa au kujitaja kuwa wanaweza kushika wadhifa wa makamu mwenyekiti CCM Bara sifa yao ni kama bangili yenye kubana mkononi au isiyo bana? 


Kwa vyovyote vile, mtu anayefaa kwa nafasi hiyo asiwe mgeni ndani ya CCM, bali awe mwenye kuvifahamu vikao vya chama, katiba, kanuni na miongozo huku akizingatia sera na hali ya kisiasa.


Hadi sasa kuna watu kadhaa wanatajwa na ku zungumzwa kuwa huenda wana sifa za kuwa makamu mwenyekiti wa CCM Bara kurithi ‘viatu’ vya Komredi Abdulrahman Kinana aliye jiuzulu wadhifa huo mwaka jana.


Miongoni mwa wanaota jwa ni William Lukuvi, Abdulrahman Juma, Mizengo Pinda, Abdallah Bulembo, Paul Kimiti, Dk Asha–Rose Migiro, Anne Makinda, na Stephen Wassira.


Makala haya yanaangazia wagombea hao ambao na wengine wanaotajwa kuwa na sifa za kumrithi Komredi Kinana aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.


Wa kwanza kumuangazia ni kada wa siku nyingi, Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo.

 

Kwa wasiomfahamu Bulembo ni kuwa, kada huyo ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM. Amewahi kuwa Mbunge, Mjumbe wa NEC, Kamati Kuu na kwa sasa ni Mshauri wa Rais Mambo ya Siasa na Jamii.


Mwaka 2015, Bulembo alizunguka nchi nzima kumnadi aliyekuwa Mgombea Urais wa wakati huo, Dk John Magufuli akiwa Meneja wa Kampeni. 

Bulembo ni kada wa CCM mwenye msimamo thabiti, asiyekubali kuburuzwa na hababaishwi na jambo. 


Ilihitaji moyo na ustahamilivu kuweza kuwa meneja wa kampeni wa mwanasiasa aina ya Magufuli, lakini kwa busara zake na uwezo wake wa kisiasa, Bulembo aliweza kumnadi vyema Rais Magufuli na kufanikisha ushindi wa kishindo wa CCM.


Mbali na uzoefu wa kisiasa na utumishi ndani ya CCM, Bulembo anaonekana kuwa na sifa nyingine ambayo pengine wengine hawana. 


Sifa kimsingi, ndiyo inayomfanya awe anatajwa na makada wa CCM kuweza kumrithi Komredi Kinana.


Sifa ya ziada ya Bulembo ni kuwa mwanasiasa anayewakilisha mawazo ya rika tofauti ya wazee, kizazi kipya, umri wa kati na mtu anayeweza kuwa kiungo cha wanasiasa wazee na vijana ndani ya CCM na hata katika vyama vingine vya siasa.


 Je, ni hulka yake ya kujichanganya na watu wa rika tofauti? Ni haiba yake ya utu uzima, busara mpenda watu na aliye tayari kujitolea ikibidi hata vitu vyake binafsi?


Ni upeo wake mkubwa wa kuona mambo? Ni hoja zake za kisasa? Ni uzalendo wake? Ni upungufu walionayo wanasiasa wengine wanaotajwa kufaa katika nafasi hiyo? Ni kitu gani hasa? Wana CCM wanapaswa kuyatafutia jawabu maswali haya.


Bulembo mwenye umri wa miaka 63, bado anabeba matumaini ya zama za sasa.


Hajapitwa na wakati. Ikiwa zama za leo ni za vijana na watu wa umri wa kati. Wapigakura wengi ni vijana na hadhira ya kisiasa imebadilika sana, hivyo anahitajika makamu mwenyekiti wa CCM anayeweza kuyanadi matarajio ya vijana katika ulingo wa kisiasa na zaidi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Bulembo ni muumini wa dhati kabisa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mapinduzi ya Zanzibar, ni mzalendo na ni mwanasiasa mwenye siasa za kati.


Anaonekana pia kuwa mwanafalsafa ambaye amegeuka kuwa tumaini la mabadiliko chanya ndani ya CCM. Anao uwezo wa kusaidia CCM kukabili changamoto za kisiasa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.


Changamoto kubwa inayomkabili Bulembo ni misimamo yake isiyoyumba kwani ni mtu ambaye habadiliki kama kinyonga katika jambo mlilokubaliana. 


Kwa matamshi mengine, Bulembo si kigeugeu, si ndumi lakuwili, bali ni mwenye msimamo thabiti kwa matendo na maneno.



Wiki ijayo tutaendelea kuwachambua makada wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara. Itaendelea