NA HADIJA OMARY, LINDI.
Ili kufikia azma ya Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati kupikia wakala wa umeme vijijini (REA) imekuja na program ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya Leo January 3, 2025 alipokuwa akimtambulisha mtoa huduma hiyo Katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi,
Amesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited kwa ajili ya kutekeleza mradi wa shilingi milioni 317.3 wa kusambaza majiko ya gesi 16,275 (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya 50% sawa na shilingi 19,500 kwa jiko katika maeneo ya vijijini ndani ya Mkoa huo
Amesema Katika program hiyo kwa Mkoa huo wa Lindi Jumla ya Kaya 16,275 Katika Maeneo tofauti ya vijijini linatarajiwa kunufaika huku akibainisha kuwa lengo la mradi huo ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za Nishati Safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti.
"Mradi huu unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya, pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza Mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi," alifafanua Mhandisi Yesaya.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa majiko ya ruzuku ambao utaongeza matumizi ya nishati safi kupikia hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujaza mitungi pale inapoishiwa gesi ili kuendelea kutumia huku akimuelekeza Mtoa huduma (Taifa Gas) kuhakikisha anakuwa na mawakala kwenye kila kata na vijiji ili kumrahishia mwananchi kubadilisha mtungi pale gesi inapomalizika.
"Ili kuwa na uendelevu wa matumizi ya gesi kupikia, natoa wito kwa Taifa Gas kuwa na mawakala ili kumrahishia mwananchi; tusikubali kumpoteza mtu kurudi kwenye kuni na mkaa kwa sababu ya kukosa mahala pa kubadili mtungi," alielekeza.
Kwa upande wake, Meneja mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Kusini, Hawa Omari amesema kuwa wanejipanga vyema kufika kwenye maeneo yote Mkoani hapo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi watakaonunua majiko hayo kabla ya kutumia.
No comments:
Post a Comment