Saturday, August 3, 2024

WANASHERIA WATATUA MIGOGORO ZIARA YA RAIS SAMIA MOROGORO

 


Na Mwandishi Wetu

TIMU ya wanasheria wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid imeambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake ya mkoani Morogoro kwaajili ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro iliyoanza tarehe mbili na inayotarajiwa kukamilika tarehe saba siku ya Jumatano mwezi huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo alisema wameambatana na Rais Samia ili kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria.

“Tutakuwa na Rais muda wote wa ziara hapa Morogoro na tupo na Waziri wetu mheshimiwa Pindi Chana na wasaidizi wa kisheria ngazi ya wilaya na mkoa, kila anapofika mheshimiwa Rais kama kuna mtu anachangamoto ya kisheria tunaichukua na kuifanyia kazi,” alisema

“Kupitia ziara hii tumeshatoa msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali na hata jamii ya wamasai tumekutana nao kwenye maeneo mbalimbali na tumewapa elimu ya sheria kuhusu migogoro yao ya mara kwa mara ya ardhi,” alisema Beatrice.

Alisema wakati wanasheria wengine wakiwa kwenye ziara  hiyo, Rais Samia ametuma wanasheria wengine kupitia Kampeni ya Mama Samia Legail Aid kutoa huduma za msaada wa kisheria kwenye maonyesho ya nane nane mkoani humo.

Beatrice alisema timu ya wanasheria hao iliwasili mkoani Morogoro juzi na inaendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi mbalimbali ambao wanamatatizo ya kisheia kwa kuwapa msaada wa kisheria.

Tangu wanasheria hao wawasili kwenye viwanja vya nane nane mkoani Korogoro wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la mama samia Legal Aid  katika  maonyesho hayoambapo wamekuwa wakipewa msaada wa kisheria.

Mama Samia yuko mkoani hapwa kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya za Mkoa wa Morogoro na mpaka sasa ameshatembelea Wilaya ya  Gairo, Kilosa, Mvomero,  na kesho Jumapili anatarajaiwa kuwasili wilaya ya Kilombero.

Mmoja wa wananchi aliyepata huduma ya msaada wa kisheria Jerome Kiangi,  alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kutatua matatizo yao ya kisheria.

“Kwa kweli nampongeza Rais Samia kwa upendo wake kwa watanzania amegundua kwamba wengi wetu tunahitaji msaada wa kisheria nimekuja hapa nimesikilizwa na wanasheria na wamesema tatizo langu la mgogoro wa nyumba litapatiwa ufumbuzi namshukuru sana,” alisema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine, John Lubeja alipongeza hatua ya rais Samia kutuma wanasheria kwenye maonyesho hayo kwani wamekuwa mkombozi kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria.

“Kupata wakili ni gharama sana kwa hiyo huduma kama hizi zinaposogezwa karibu na wananchi kama hapa kwenye maonyesho tena bure ni jambo la faraja sana na la kupongeza mno,” alisema Lubeja.










Sunday, July 28, 2024

SWEETBERT NKUBA AAHIDI KULETA MABADILIKO TLS.

 


Na Mwandishi Wetu

Mgombea wa urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Sweetbert Nkuba ameelezea namna ambavyo amejipanga kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo.


Moja ya mipango yake amesema ni kuboresha miundombinu ya TLS, uimarishaji wa miundombinu ya kisheria na kiteknolojia ili kuwezesha huduma bora kwa wanachama na jamii hususani kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ya kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kisheria na kuboresha ofisi za TLS katika mikoa mbalimbali kwa vifaa vya kisasa na miundombinu bora.


Jambo la pili anasema atasisitiza mafunzo endelevu kwa wanachama wa TLS ili kuhakikisha kuwa wanasheria wanakuwa na ujuzi wa kisasa na uwezo wa kushindana kimataifa ikijumuisha kuanzisha programu za mafunzo ya mara kwa mara kuhusu sheria mpya na mabadiliko ya sheria pamoja na kushirikiana na taasisi za kimataifa kwa mafunzo na kubadilishana uzoefu.


La tatu anasema atahakikisha TLS inakuwa na sauti yenye nguvu katika masuala ya kitaifa na kimataifa yanayohusu sheria na haki ikiwamo kuanzisha mikakati ya ushawishi kwa serikali na bunge ili kuboresha mfumo wa sheria nchini na kutoa msaada wa kisheria kwa jamii, hususani makundi yenye uhitaji maalum.


Nkuba anasema jambo la nne atasimamia kwa uwazi na uwajibikaji katika shughuli zote za TLS ili kujenga imani kwa wanachama na wadau wengine ikiwamo kuboresha mifumo ya ukaguzi wa ndani na nje ili kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali yake, kuanzisha utaratibu wa kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wanachama kuhusu shughuli na matumizi ya fedha za taasisi hiyo.


Pia, anasema jambo la tano atajenga na kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali, ikiwamo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na taasisi za kimataifa pamoja na kuanzisha na kudumisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa ya kisheria kwa manufaa ya wanachama wa TLS na kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika kutoa elimu ya sheria na mafunzo ya vitendo.


Jambo la sita anasema ni kuhakikisha wanachama wa TLS wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na uongozi wa chama ikiwamo kuanzisha mifumo ya ushirikishwaji wa wanachama katika maamuzi muhimu pamoja na kutoa fursa kwa wanachama wote hususani wanawake na vijana, kushiriki katika nafasi za uongozi.


"Kwa sera na mtazamo huu, ninaamini nitafanikiwa kuiboresha TLS na kuifanya kuwa chama imara na chenye ushawishi mkubwa katika sekta ya sheria nchini Tanzania,"anasema Nkuba.


"Naomba support yenu na kura zenu ili kujenga TLS moja, imara na huru ili kuhakikisha tunaondoa matabaka miongoni mwetu pamoja na kusimamia madhumuni ya TLS kama yalivyoainishwa kwenye kifungu cha 4 cha Sheria ya TLS, madhumuni na shabaha mbalimbali zilizopo kwenye mpango mkakati."


Kadhalika, Nkuba anasema akichaguliwa kuwa rais wa TLS, ataanzisha mfuko wa malipo ya ada ya Mwaka kwa unafuu,
kuanzisha na kusimamia vituo vya malezi kwa mawakili wapya, pamoja na upatikanaji wa bima ya afya kwa utaratibu wa kulipa kidogo kidogo.


Nyingine anasema atasimamia kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa bima ya maisha kupitia makundi, utakaosaidia familia ya wakili atakayefariki kulipwa sio chini ya Sh.milioni 100,000,000 ili kuondoa utaratibu wa kizamani ambapo familia hulipwa Sh.milioni 6,000,000 tu.


Nkuba anasema atahamasisha kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa lengo likiwa kuweka msingi wa kuanzisha taasisi kubwa ya fedha ya mawakili ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa inawakopesha mawakili.


Pia, anasema atahakikisha mahusiano yenye afya na wadau wote, serikali, mahakama, Polisi na vyombo vyote, jamii na mawakili yanadumishwa na ⁠kuendeleza vita dhidi ya vishoka wa aina zote.


Nyingine anasema atashinikiza mabadiliko ya sheria zinazowanyima mawakili kazi na kuhakikisha suala la "local content" kwa kazi za sheria linazingatiwa katika mikataba yote ya uwekezaji, kutungwa kwa sera ya jinsia itakayotoa dira katika ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika uongozi wa TLS na nafasi za ajira na kuilinda na kuitetea taaluma hiyo na kuhakikisha inakuwa msemaji wa mawakili.

Katika uchaguzi huo wagombea wa nafasi hiyo ya Urais wa TLS, sita ambao ni Boniface Mwabukusi,  Emmanuel Muga, Ibrahim Bendera,  Paul Kaunda, Revocatus Kuuli na Sweetbert Nkuba.

KATIBU MKUU CCM, DKT NCHIMBI AZURU KABURI LA HAYATI MKAPA.

 














CCM YATOA MILIONI 10 KUBORESHA MAJENGO YA SHULE LUPASO

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ametembelea kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya 3, hayati Benjamin William Mkapa katika Kijiji cha Lupaso mkoani Mtwara, leo Julai 28, 2024, kuhani familia na kuzungumza na wananchi wa Lupaso.

Balozi Nchimbi amesema “naomba nikiri kuwa mimi ni mwanafunzi wa hayati na nimekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), katika kipindi chake, ndiye alinilipia ada ya kusoma chuo kikuu na alikuwa mfuatiliaji sana na alitulea vizuri, sio sisi tu, bali Watanzania wote aliwalea pia.


Alikuwa mzalendo kwa nchi, alifanya mabadiliko makubwa kwa nchi yake na kwa Chama chake, lakini yote CCM chini ya Dkt Samia tutaendelea kuyaenzi yale yote aliyoyoacha hayati Benjamin Mkapa. 


Pamoja hayo nimeambiwa kero za hapa na tumezichukua. CCM inatoa shilingi milioni 10 kuanza kukarabati shule ya hapa Lupaso.”

Katika ziara hii Dk Nchimbi ameambatana na Katibu wa NEC-Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndg. Amosi Makalla, Katibu wa NEC-Organaizesheni Ndg. Issa Ussi Haji (Gavu) pamoja na Katibu wa NEC- Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ndg. Rabia Abdallah Hamid.

NANI KUUKWAA URAIS WA TLS UCHAGUZI WA IJUMAA?

 

Na Mwandishi Wetu


KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambao unatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa wiki hii zinaendelea kupamba  moto ambapo wagombea wanaendelea kunadi sera wakitaka kufanya mabadiliko kwenye taasisi hiyo.


Mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Sweetbert Nkuba, alisema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa anataka nafasi hiyo ili akapambane na mawakili ambao hawana sifa ya kufanyakazi hiyo.


TLS ni taasisi muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mfumo wa sheria na haki nchini Tanzania na kwa mwaka huu wagombea wa nafasi ya urais kwenye uchaguzi huo watakuwa sita, ambao ni Boniface Mwabukusi,  Emmanuel Muga, Ibrahim Bendera,  Paul Kaunda, Revocatus Kuuli na Sweetbert Nkuba.


Nkuba alisema anauzoefu wa muda mrefu wa uongozi katika ngazi mbalimbali na kuomba achaguliwe kwenye nafasi hiyo ili afanikishe vipaumbele vitano ikiwemo kuwaunganisha wanachama wa TLS na kuhakikisha maslahi ya kiuchumi ya wanachana wa chama hicho yanazingatiwa.


“Nikichaguliwa nitahakikisha wanachama  wote wa TLS wanakuwa na bima ya afya, bima ya maisha, nitaaanzisha kituo cha malezi kwa wanachama wanaochipukia, kuimarisha uhusiano baina ya wanachama wa TLS, Serikali, mahakama na jamii kwa ujumla,” alisema Nkuba


Mgombea mwingine Wakili Paul Kaunda amejinadi kuwa yeye si mgeni kwenye uongozi kwani amefanyakazi kwa miaka 10 katika maeneo mbalimbali ya sheria hasa sheria za jinai na madai na ni mdau mkubwa sana kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda yaani akili bandia (AI).


Alisema kwamba yeye pia siyo mgeni wa kuongoza taasisi kama TLS kwani  2019 -2020  alipata bahati ya kutumika kama Mjumbe wa Baraza la Uongozi na Mjumbe wa Kamati ya Sheria  na Katiba ya TLS kwa miaka mitano.


 “Nimedhamiria kuleta heshima kwa TLS na nyote ni mashahidi kwamba heshima ya chama hiki imeshuka sana kwa hiyo nitakwenda kurejesha heshima hasa sisi mawakili tunapowawakilisha wateja wetu wakiwa polisi, magereza na mahakamani,” alisema


Naye Ibrahim Bendera alisema amefanyakazi ya uwakili kwa miaka 18  upande wa Tanzania Bara na miaka 19 kwa upande wa  Zanzibar hivyo amejipima na kuona anatosha kuongoza chama hicho hasa wakati huu ambapo Rais wa chama hicho ataongoza kwa miaka mitatu badala ya mwaka mmoja.


“Zamani Rais alikuwa anahudumu kwa mwaka mmoja sasa kwa mwaka mmoja siyo rahisi kuleta mabadiliko kwa hiyo baada ya mabadiliko na kuweka ukomo wa miaka mitatu nimeona nitapata nafasi ya kulieleza Baraza la Uongozi maoni yangu na mpango mkakati wa TLS unaisha mwaka huu kwa hiyo nitaweka msukumo wa kutengeneza mkakati mpya,” alisema


Alisema kwa mwaka TLS  yenye wanachama 12,000 inapata wastani wa bilioni 1.2 na  inalipa mishahara inayofikia shilingi milioni 80  kwa mwezi hivyo akichaguliwa atahakikisha anapunguza gharama za matumizi na kuwawekea mazingira mazuri mawakili vijana waweze kupata uzoefu.


Revocatus  Kuuli yeye alisema yeye amekuwa wakili kwa miaka 13 Tanzania Bara na wakili Zanzibar kwa miaka minne na kwamba katika mawakili 13 waliosajiliwa na Mahakama ya Afrika iliyopo mkoani Arusha yeye ni miongoni mwao.


Alisema anafanyakazi pia kwenye Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya IRMCT yenye Makao yake Makuu Geneva Uswis na Arusha Tanzania na kwamba ametumikia nafasi mbalimbali serikali na ngazi yake ya mwisho serikalini alikuwa ofisa  Wizara ya Katiba na Sheria.


Naye Wakili Emmanuel Muga alisema amekuwa wakili kwa miaka 12 hivyo amejipima na kuona kuwa anaweza kumudu majukumu ya kuwasimamia mawakili wenzake kama atachaguliwa kushika nafasi hiyo kwenye uchaguzi ujao.


Alisema amekuwa mwenyekiti wa TLS mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili akianzia 2019 mpaka 2021 na kwamba fursa hiyo ndiyo ilimpa nafasi ya kuwafahamu mawakili na mahitaji yao na nini kifanyike ili chama hicho kiweze kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.


 “Nikiwa mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Dar es Salaam nilifanikiwa kuunda kamati nane na zilileta mageuzi makubwa sana tunayoyaona kwa Chapter ya chama chetu hapa Dar es Salaam kwa hiyo mafanikio haya ndiyo yamenifanya nione ninaweza kuongoza chama hiki kwa ubora,” alisema


Boniface Mwabukuzi alisema anataka nafasi hiyo ili kuleta mageuzi ambayo kwa muda mrefu yameshindikana ikiwemo kupambana na mafisadi kwenye chama hicho na nje ya chama.


Alisema TLS kwa muda mrefu imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kusaidia wanachama kutokana na watu wanaochaguliwa kuiogopa serikali hali ambayo iliwafanya washindwe kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa TLS.




Thursday, July 25, 2024

SHAHIDI AELEZA MUME WAKE ALIVYOPIGWA NA NATHWANI MPAKA KUZIMIA.

 

Na Mwandishi Wetu


 SHAHIDI Kiran Lalit Ratilal (52), ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jinsi mume wake alivyopigwa na mshtakiwa Bharat Nathwan (57) hadi kupoteza fahamu kutokana na ugomvi ambao ulikuwa unaendelea wa baina yao kuhusu ujenzi uliyokuwa unaendelea katika eneo la makazi yao.


 


Nathwan pamoja na mke wake Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


 


Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, Kiran alidai kuwa anakumbuka Julai 21, 2023 alikuwa nje ya akiendelea na majukumu yake nanpia shughuli za mapambo zilikuwa zinaendelea nyumbani kwake mafundi wakiweka vigae.


 


Alidai kuwa, mshtakiwa Sangita alitoka ndani akaanza kupaza sauti akitaka atoe malighafi (material) yote yaliyokuwepo kwenye kibaraza hicho, wakati yote yapo upande wa Kiran Lalit Ratilal na sio upande wake.


 


"Aliendelea kupaza sauti mimi nikamjibu kwamba nitaondoa baada ya mafundi kumaliza kazi, nilipomjibu akaanza kutumia lugha chafu akidai hataki kusikia chochote na kwamba niondoe uchafu wangu,"


 


"Nilijaribu kumuelewesha, lakini hakunielewa ndipo nilipompigia simu mume wangu akakuchukua dakika tano aafika pale, wakati anafika na mume wa mshtakiwa Sangita nae akafika kwa maana ya Bharat,"alidai Kiran


 


Kiran alidai kuwa baada ya waume zao kufika kwa pamoja, akajaribu kumuelewesha  Bharat kutokana na aliyoyasema mke wake (Sangita), lakini hakumulewa  na pia mume wake alijaribu kuwaelewesha nankuwataka wakayazunguze lakini hawakuelewa.


 


"Sangita alianza kutumia maneno machafu tena, na nilipomuelewesha mume wake kuhusu maneno machafu ya mke wake alikaa kimya, mume wangu akaniambia kama hawajamuelewa awaache,"alidai


 


Alidai kuwa baada ya kumalizia hiyo sentensi, Bharat alimrukia mume wake na kuanza kumpiga kwa kumkandamiza kifuani na kumpiga mateke.


 


"Aliendelea kumpiga mume wangu nilipoenda kuamulia Bharat alinishika kichwa changu na kukitumbukiza kwenye ndoo ambayo ilikuwa na mchanganyiko wa saruji na kisha akaendelea kumpiga mateke,"


 


" Watu wote waliyokuwepo kwenye eneo hilo wakaanza kumsukuma Bharat ndipo alipoanicha mimi na kumfuata tena mume wangu akaanza kumpiga akadondoka chini akapoteza fahamu, muda huo uso wangu, macho na masikio yalikuwa yamejaa saruji ila nilikimbia kumsaidia ila hakuweza kuamka,"alidai Kiran


 


Kiran alidai kuwa alimuita mtu wa ofisini ili aweze kumsaidia ndipo alipompa simu yake akaanza kuchukua picha, mshtakiwa Sangita baada ya kuona hivyo alichukua simu hiyo ili aitupe wakati hayo yote yanaendelea mume wake alikuwa amelala chini.


 


"Nilifikiria njia ya kumsaidia mume wangu, mafundi walimbeba hadi sakafu ya pili ndipo akaanza kuzinduka akapewa maji, wakamkimbiza hospitali kwa ajili ya kupata huduma ya kwanza. Niliondoa saruji baada ya mume wangu kuzinduka, aliulizia simu yake akaanza kupiga simu,"


 


"Niliona wanaume wawili wakiwa wamevaa nguo za polisi, taratibu macho yangu yakaanza kupoteza uono kwa sababu ya ule mchanganyiko. Waliniambia natakiwa niende Kituo cha Polisi Kati kuripoti wakanishauri niite gari la wagonjwa kwa sababu nilikuwa siwezi kutembea vizuri,"alidai


 


Alidai alifanikiwa kuita gari hilo, wakati hayo yote yakiendelea Bharat aliendelea kutoa maneno machafu na za kitishio ya maisha, gari hilo lilimpeleka hadi kituoni hapo akapewa fomu moja akiwa na mume wake akampelekwa Hospitali ya Mnanzi Mmoja kwa matibabu.


 


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 6,2024, baada ya Wakili wa washtakiwa hao Edward Chuwa kuomba ahirisho kwa sababu alikuwa anakwenda kwenye shauri lingine mahakama ya juu, siku atamuuliza maswali ya dodoso shahidi.