Saturday, June 1, 2024

NMB YATOA MSAADA VIFAA TIBA VYA MILIONI 10 HOSPITALI YA BAGAMOYO

 

Benki ya NMB yatoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo ikiwa ni kutekeleza majukumu yao ya kusaidia wananchi katika kuimarisha afya zao.


Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Meneja wa kanda ya Dar es salaam, Ferdinand Mpona, amesema NMB imetekeleza msaada huo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali chini ya uongozi wake Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda, amesema wanaishukuru Benki ya NMB kwa kutoa vifaa hivyo kwani vitasaidia katika matibabu ya afya za wananchi.


Amesema serikali imetenga fedha za kujenga na kukarabati majengo mbalimbali ya Hospitali ya Bagamoyo hivyo inapokea taasisi binafsi zikajitolea kusaidia vifaatiba inasaidia kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.


Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Vitanda vitano vya kujifungulia kinamama wajawazito, pamoja na magodoro yake, na viti vya magurudumu (wheelchairs) ishirini kwaajili ya kubebea wagonjwa ambavyo vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 10.







Friday, May 31, 2024

DED BAGAMOYO AFUNGUA MAFUNZO KUHUSU MABORESHO YA MITAALA YA ELIMU YA AWALI, MSINGI, SEKONDARI NA UALIMU KATIKA SHULE YA SEKONDARI BAGAMOYO MKOANI PWANI.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw Shauri Selenda tarehe 30 Mei 2024 amefungua mafunzo kuhusu maboresho ya mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo Mkoani Pwani.


Mafunzo hayo, yamelenga kuwapitisha washiriki katika muundo wa Elimu, Maboresho Elimu Msingi na Sekondari pamoja na Ualimu.


" Ndugu zangu nyinyi mliopo hapa ni asilimia ndogo sana ya washiriki wanaohitajika kupata mafunzo haya, hivyo nawaomba muwe makini kutumia muda Ili muweze kupata Yale yaliyotarajiwa kutoka kwa wawezeshaji wetu ". Alisema Bw Selenda.


Mafunzo haya ya siku mbili yanajumuisha Walimu Wakuu 78 toka Shule za Msingi za Serikali na binafsi Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Ofisi ya Raisi- TAMISEMI






Thursday, May 30, 2024

WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO 2024

SOMA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA KATI KWA MWAKA 2024.

UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA KATI, 2024



CHAGUA MKOA ULIKOSOMA


MKOA WA KAGERA KUANZISHA MASHAMBA YA KAHAWA ZAIDI YA HEKTA 4,000

 

Na Alodia Dominick,

Bukoba.

Mkoa wa Kagera unatarajia kuanzisha mashamba ya pamoja ya kahawa zaidi ya hekta 4,000 lengo likiwa ni kuondoa umaskini kwa wananchi wa mkoa huo.


Hayo yamebainika katika mkutano wa wadau wa kahawa uliofanyika Mei 29, mwaka huu katika ukumbi wa mkuu wa mkoa huo.


Akifungua mkutano huo mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa, amesema kuwa, kuanzishwa kwa mashamba ya pamoja ya  kahawa ni agizo la Wizara ya kilimo ililolitoa hivi karibuni kwa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) kuhakikisha inatoa matrekta na Wizara itatoa miche ya mibuni zaidi ya milioni 5.


"Dhamira ya serikali ni kupanua kilimo cha kahawa, sote tunayo kumbukumbu kahawa ilivyokosa bei wakulima wengi walikata miche ya kahawa hivyo mashamba mengi yana miche michache ya kahawa na tunao uwezo wa kuzalisha mara mbili ya kahawa  tuliyo nayo katika mkoa wetu wa Kagera"


"Tukifanya hivyo hata ile ya kutajwa tajwa eti sisi ni wa pili kutoka mwisho kwa umaskini itaisha tutakuwa tunashikilia namba 10 bora za uchumi Tanzania, sisi kama mkoa tukishirikiana na wizara ya kilimo tumeamua kufungua mashamba ya pamoja ya kahawa kwa mwaka huu tunaenda kuanzisha hekta 4,000 wilaya za Karagwe na Muleba ili kufikia mwaka 2030 mkoa wa Kagera umaskini usiwepo tena" amesema Mwassa.


Aidha amesema kuwa, baada ya kuanzishwa kwa mashamba hayo watakuwa wanakata hekali mbili wanagawia wakulima na wale watakaohitaji hekali zaidi watapatiwa.


Katibu Tawala mkoa wa Kagera (RAS) Steven Ndaki amesema kuwa, mkoa wa Kagera ndiyo mkoa wa kwanza Tanzania kwa uzalishaji wa zao la kahawa kwa mwaka huzalisha tani 60,000 hadi tani 80,000 ingawa uzalishaji huo unakumbwa na changamoto mbalimbali.


Changamoto hizo ni pamoja na utoroshaji wa kahawa ambapo baadhi ya wananchi wanalazimika kuivuna kahawa kabla ya wakati na kusababisha ubora wa kahawa kushuka.


Ametaja  lengo la kikao hicho kuwa ni kujadili fursa, mafanikio na changamoto na mwisho watoke na mkakati utakaowezesha kudhibiti ubora, kuongeza tija na kuimarisha mfumo wa masoko wa zao hilo.


Baada ya wadau wa kahawa kujadili kwa undani wametoka na maazimio ambayo ni kila halmashauri kuweka mikakati ya kuzuia biashara ya magendo ya kahawa bila kutumia nguvu ili kulinda mapato ya wakulima pamoja na serikali, halmashauri za Karagwe na Muleba zitenge maeneo kwa ajili ya kilimo cha kahawa.


Maazimio mengine ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya uvunaji wa kahawa mbichi na utoroshaji wa kahawa, msimu wa ununuzi wa kahawa ufunguliwe mapema mwezi Aprili ili kuwezesha ununuzi wa kahawa aina ya arabica na kuzuia magendo, kuongeza tija na ubora wa kahawa.


Amcos ziwezeshwe kuweka mikakati ya kuwakopesha wakulima mapema kabla ya kuvuna ili kudhibiti biashara ya kahawa changa ikiwa bado shambani (obutura), mikutano ya wadau wa kahawa ngazi ya mkoa ihuishwe na wajumbe wote kutoka maeneo ya uzalishaji washirikishwe.


Serikali iwekeze kikamilifu kwenye mialo,  beria na mikapani kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti utoroshaji wa kahawa.


MWENGE WA UHURU WAZINDUA KLABU YA WAPINGA RUSHWA NA DAWA ZA KULEVYA  GREAT MINDS SCHOOL 

 

NA HADIJA OMARY, LINDI

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 Godfrey mnzava amezindua klabu ya Wapinga Rushwa na Dawa za kulevya ya shule ya Great minds primary school iliyopo Halmashauri ya manispaa ya Lindi Mkoani Lindi .


Uzinduzi huo ulioenda sambamba kwa Shule hiyo kukabidhiwa  cheti cha ufunguzi,  uzinduzi rasm wa klabu hiyo ulifanyika jana   katika viwanja vya shule ya msingi Mnazi Mmoja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambako mkesha wa mwenge huo wa uhuru ulifanyika.


Akizungumza na wanafunzi, walimu , viongozi alioambapatana nao pamoja na wananchi waliojitokeza katika viwanja hivyo Mnzava  aliwataka wanafunzi na wana klabu hiyo kuendelea kujifunza vizuri maswala hayo ya Rushwa na mapambano dhidi ya Dawa za kulevya ili wawe mabalozi wazuri kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.


Awali akisoma risala kwa kiongozi huyo, Anjela Lukanga mwanafunzi wa shule ya Great minds, amesema klabu hiyo ina jumla ya wananchama 33 ambapo kati yao wasichana 12 na wavulana 21na inalengo la kuwajenga kimaadili pamoja na kushirikishwa kwenye mapambano dhidi ya Rushwa na Dawa za kulevya.


" Tunashukuru kwa kutuwezesha kutambua nafasi na wajibu wetu kwa kushiriki kuzuia na kupambana  na Dawa za kulevya  hapa Nchini sambamba na kutujengea uwelewa juu ya madhara na kuchukia Rushwa na dawa za kulevya katika maisha yetu hali tungali bado mashuleni.


Kwa upande wake salome mbonile kutoka ofisi ya mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya amesema ili kuhakikisha Elimu ya kuendeleza mapambano dhidi ya Dawa za kulevya inawafikia watu wengi  mamlaka hiyo imeanza kushirikiana na taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU kwa kuziongezea majukumu klabu za kupinga Rushwa zijifunze na kuzungumzia maswala hayo ya Dawa za kulevya.


" katika Mkoa wa Lindi tayari kama mamlaka tumesha ziongezea majukumu hayo shule  zipatazo 22 za Sekondari , 86 za msingi na vyuo klabu mbili " alisema Bi.Salome.


Ujumbe wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 kuhusu Dawa za kulevya ni " Epuka matumizi ya Dawa za kulevya zingatia utu. Boresha huduma za kinga na tiba









Wednesday, May 29, 2024

TAWI LA UDSM KUJENGWA KAGERA.

 

Na Alodia Babara,

Bukoba

Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa ametaja manufaa manne yatakayopatikana baada ya kukamilika ujenzi wa tawi la chuo kikuu cha Dar es Salaam ikiwemo kupanua mji, kukuza uchumi, kuongeza fursa kwa vijana wa Kagera na kuongeza urafiki.


Tawi hilo la chuo kikuu litajengwa katika kijiji cha Itahwa kata ya Kalabagaine halmashauri ya Bukoba na eneo la chuo hicho ni hekali 315 ambazo zilitolewa na wananchi wa vijiji viwili vya Kangabusharo na Itahwa na hafla  ya kukabidhi eneo la ujenzi kwa mkandarasi imefanyika Mei 29,mwaka huu.


Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika eneo litakapojengwa tawi la chuo kikuu cha Dar es Salaam amewashukuru  wananchi kwa kutoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na kutoa manufaa manne yatakayopatikana baada ya kukamilika kwake.


"Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutukumbuka wanakagera kutuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu, wanakagera walitamani kuwa na chuo kikuu miaka mingi iliyopita kwani wanahistoria ya kupenda kusoma" amesema Mwassa


Ameongeza kuwa, wanatambua chuo hicho ni kwa ajili ya watanzania wote na raia wa nchi nyingine lakini watatumia fursa hiyo vizuri.


Amesema kuwa, uwepo wa mradi huo utaleta fursa mbalimbali kwa wakazi wa mkoa wa Kagera ikiwemo fursa ya elimu kwa wakazi wa Kagera kwani kitakuwepo kituo cha mafunzo ya ujasiriamali hata kama mtu hajamaliza kidato cha sita, kupanua mji, kukuza uchumi, na kuongeza urafiki.


Aidha ametoa rai kwa wanafunzi wanaosoma shule za sekondari zinazozunguka eneo la chuo kikuu kuongeza bidii katika masomo ili watakapohitimu kidato cha sita waweze kuendelea na masomo ya juu katika chuo hicho.


Pia amemtaka mkandarasi wa ujenzi katika chuo hicho kumaliza kwa wakati ujenzi huo.

Kwa upande wake Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia taaluma Prof. Beneventura Rutinwa amesema mpango wa ujenzi wa tawi la chuo hicho ulianza mwaka 2019 na kwa kipindi cha kwanza cha ujenzi zitatumika shilingi bilioni 20.

Amesema ujenzi ulianza Mei 17,2024 utakamilika Octoba mwaka kesho utachukua muda wa miezi 18.

Aidha mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema, wilaya ipo tayari kutoa ushirikiano kipindi chote cha utekelezaji wa ujenzi huo.


KLABU ZA WAPINGA RUSHWA MASHULENI ZINASAIDIA KUENDELEZA  MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

 

Na Hadija Omary, Lindi.


Imeelezwa kuwa Kuanzishwa kwa klabu za wapinga rushwa mashuleni ni chachu ya kuimarisha na kuhamasisha wanafunzi kupenda kushiriki kwenye vitendo vya kuzuia, kupinga na kupambana na rushwa katika jamii.


Hayo yameelezwa na  Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024,  Godfrey  Mnzava alipotembelea Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Sekondari Hawa Mchopa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi. Kwa lengo la kuimarisha klabu hiyo.


Mnzava  amesema kuwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya KUZUIA RUSHWA NIJUKUMU LAKO NA LANGU, TUTIMIZE WAJIBU WETU,  jamii inapaswa kuendelea kutoa msisitizo na kuwekeza zaidi katika kuelimisha wanafunzi ambao ndio viongozi wa kesho ili waweze kujua madhara ya Rushwa kwa jamii.


"Tuweke nguvu zaidi katika kuunda klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni ili kuwaandaa hawa viongozi wetu wa kesho kujua madhara ya rushwa na kuichukua rushwa ili tuweze kujenga taifa la watu wanaoichukia rushwa na kutoa haki vile inavyopaswa" ameeleza.


Awali akitoa taarifa ya Klabu ya Kuzuia na Kupinga Rushwa, Katibu wa Klabu hiyo Noshard Christopher ameeleza kuwa kupitia Klabu hiyo wanafunzi wamepata fursa ya kutambua madhara na viashiria vya rushwa pamoja na kuelimisha wanajamii kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia nyimbo, ngonjera, uchoraji wa katuni na uandishi wa insha.


"Tuna imani kwamba uwepo wa vilabu vya kupinga Rushwa mashuleni na vyuoni vinasaidia jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Rushwa na hivyo kujenga Tanzania imara isiyokuwa na Rushwa.


Vilevile, tunawahamasisha wananchi kufichua na kukemea vitendo vya Rushwa katika maeneo yao kwa kutoa taarifa ofisi ya TAKUKURU kwa njia ya simu namba ya  bure 113" ameongeza Noshard.


Amesema klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Hawa Mchopa ilianzishwa miaka 7 na hadi sasa jumla ya wanachama hai 122, kati yao wavulana ni 71 na wasichana 51.




SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI.

 

Wizara ya Ujenzi imeanza utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi kwa utaratibu wa ubia (PPP)katika kutekeleza miradi ya miundombinu.


Haya yamebainishwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25, Bungeni jijini Dodoma leo, Mei 29, 2024


Amesema ni katika kuipunguzia Serikali gharama kubwa za utekelezaji wa miradi ya miundombinu hasa barabara na madaraja ambayo Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha.


“Lengo la kutumia utaratibu huu ni kujenga miundombinu na kuitekeleza kwa wakati.”


Aliitaja iradi inayotekelezwa kwa utaratibu huo kuwa ujenzi wa barabara ya Kibaha-Chalinze-Morogoro-Dodoma (Expressway) yenye urefu wa kilometa 423.8 kwa mfumo wa kulipia.


Tuesday, May 28, 2024

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA 2024 AWAPA HEKO MTAMA KWA KUANZISHA KITUO CHA REDIO

 

Na HADIJA OMARY, LINDI


kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 Godfrey Mnzava ameipongeza halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi kwa uibuaji wa mradi wa  kituo cha kurusha matangazo cha Redio Mtama.


Mradi huo wa ujenzi wa studio za redio jamii Mtama FM(106.3) uliibuliwa mwaka 2023 chini ya ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliopo chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.



Akizungumza na wananchi mara baada ya mwenge wa uhuru kutembelea katika Redio hiyo iliyopo katika Mtaa wa majengo katika halmashauri hiyo  kiongozi huyo amesema mradi huo ni mzuri na kwamba utawezesha halmashauri kufikisha Taarifa kwa wananchi kwa uharaka.



Hata hivyo Mnzava ameitaka  jamii kutumia kituo hicho ili kiweze kuleta tija kwao na kutoa wito kwa uongozi wa halmashauri kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kwa hatua zilizobaki ili kiweze kuanza kutumika kwa wakati.


Aidha Mnzava ametumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa vyombo vya habari na kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 ambayo inasisitiza juu ya Umuhimu wa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Utunzaji wa Mazingira.


Akitoa taarifa kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge Mhandisi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF ) Mhandisi Baraka Elieza amesema mradi huo  unatekelezwa na makandarasi ElsewedyElectric East Africa Ltd P.O BOX 9213 DSM ukiwa na gharama kiasi cha Tsh. Milioni 972 huku gharama zote zikilipwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote yaani UCSAF.



Mhandisi Elieza ametaja wanufaika wa mradi huo kuwa ni wananchi wote kutokana na redio hiyo kusikika kwenye kata zote 20 za Halmashauri ya Mtama, kutumia redio katika kuelimisha jamii kupitia vipindi mbalimbali, kutumia redio kama chanzo cha mapato ya halmashauri kutokana na kurusha matangazo ya wateja mbalimbali.





UPOTOSHAJI WA VIVUKO KIGAMBONI UNA MASLAHI BINAFSI: WAZIRI BASHUNGWA

 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewatoa hofu Wananchi wa mkoa wa Dar es salaam wanaotumia usafiri wa vivuko eneo la Kigamboni -Magogoni juu ya taharuki kuhusu huduma inayotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nakueleza kuwa imetengenezwa na watu wenye maslahi binafsi.


Ameyasema hayo leo Mei 28, 2024 wakati alipokuwa akifanya mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.


"Niwatoe wasiwasi Wananchi wa Dar es salaam pamoja na kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa hakukuwa na sababu ya kutengenezwa. Lakini sisi tunaofahamu yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki" Amekaririwa Bashungwa


Ameeleza kuwa sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwa ajili yakupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.


Aidha, Bashungwa amesema kuwa tayari ameikutanisha TEMESA na Kampuni ya AZAM Marine na kujadili namna bora yakushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni - Kigamboni.


"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaboresha vivuko na tutaweka machaguo kwa abiria ambapo watakuwa na chaguo. Ukitaka kutumia kivuko cha TEMESA sawa au ukitaka cha AZAM muda mchache kuvuka kwasababu zile ni ndogo siyo kama kivuko kikubwa ambacho unasubiri kupakia magari na abiria ili muweze kuondoka pamoja" Amesisitiza.


Bashungwa amesema Wizara inatambua changamoto ya wananchi ni huduma bora ya vivuko nakusema kuwa kuanzia mwezi Agosti mwaka huu wataanza kutekeleza mpango huo utakaotoa wigo kwa wananchi kuchagua huduma wanayotaka kutumia.


"Wapo wanaotaka kushinikiza ili utaratibu na mwelekeo uende kama wanavyotaka wao, sisi hatuendi hivyo"amesema Bashungwa huku akisema kuwataja watu hao ni kuwapa sifa.