Thursday, February 1, 2024

DED BAGAMOYO AZINDUA HUDUMA KITUO CHA AFYA FUKAYOSI.

 

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw. Shauri Selenda Leo tarehe 1 Februari, 2024 amezindua rasmi utoaji wa huduma katika kituo Cha Afya Fukayosi.

Akizungumza na watumishi wa Afya pamoja na Kamati ya Maendeleo ya Kata Fukayosi (WARDC) Selenda, alisisitiza kufanya kazi Kwa weledi pamoja na  kunyenyekea wagonjwa kama sehemu ya miiko ya tasnia ya utoaji wa huduma za afya.

" Mgonjwa mpaka anafika hospitali maana yake anahitaji huduma hivyo haina budi kumpokea kwa unyenyekevu na kumsikiliza shida yake na kumpatia matibabu". Alisema Bwana Selenda.           

Kituo Cha Afya Fukayosi kimejengwa kwa kutumia fedha toka Serikali Kuu na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa lengo la kuimarisha huduma za afya ikiwemo Huduma ya Mama na Mtoto, Afya ya dharura na upasuaji wa wajawazito, Maabara, Jengo la Wagonjwa wa nje (OPD), Mionzi, na Jengo la kufulia.

Mkurugenzi Mtendaji alipanda miti kama ishara ya Uzinduzi wa huduma katika kituo hicho Cha Afya Fukayosi. Kituo Cha Afya Fukayosi kilianza Ujenzi Mwaka wa fedha 2021/2022 na kinategemea kuhudumia zaidi ya wakazi 17,000






DC. OKASH ATATUA KERO ZA BODABODA BAGAMOYO.

 

Na Daria Abdul, Hamisi Hamisi, Bagamoyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash, akishirikiana na  viongozi mbalimbali wa Halmashauri  ya Wilaya hiyo, amefanya kikao na madereva wa pikipiki zinazobeba abiria (BODABODA)  Januari 31,2024 katika ukumbi wa flexible hall Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA), kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi wao wa kila siku.

 Mhe.Okash, amewasisitiza bodaboda kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, pia wajiepushe na matukio ya uhalifu wa kupora mali za wateja wao.

”Ndugu zangu lazima tutii sheria za usalama barabarani kwani tunawategemea ninyi vijana kuwa ndio Taifa la kesho hizo rizki tunazozipata kuna watu wanatutegemea tusipotii sheria za usalama barabarani, kutakuwa na ajali za mara kwa mara zitakazopelekea kupoteza maisha na kuleta ulemavu.” Amesema Okash

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Usalama barabarani,  Wilaya ya Bagamoyo (DTO)  Azizi Zubeir, amewataka bodaboda kuhakikisha wanasajili vyombo vyao vya usafiri, leseni pamoja na bima ili wasikamatwe na vyombo vya usalama na kueleza Zaidi kuwa bima itasidia kupunguza gharama ya matengenezo ya vyombo hivyo na matibabu kwa dereva anapopata ajali.

"Ni waambie tu  bodaboda ili ufanye kazi kihalali lazima usajili vyombo vyetu, tuwe na leseni ya udereva pamoja na bima ya chombo husika ili itusaidie kupunguza gharama za matengenezo na matibabu inapotokea ajali.” Amesema Zubeir

Akitoa kero yake katika hafla hiyo Mwenyekit wa Bodaboda kata ya Dunda Ndug, James Mapunda, amesema kuwa wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya usalama barabarani na vyuo mbalimbali vikishirikiana na Jeshi la polisi Wilayani hapo na kuahidiwa kupatiwa leseni za udereva baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, badala yake hawapewi leseni zao licha ya kulipia fedha kwa ajili ya leseni hizo.

Kwa upande wake Waziri Mohammed (BODABODA), ameeleza kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na kukamatwa na Mgambo  kwa mabavu katika vituo vyao vya kazi (vijiwe) bila ya uwepo wa askari wa Jeshi la polisi kinyume na sheria hali inayopelekea kushindwa kufanya shughuli zao usafirishaji kwa amani.







WALENGWA WA TASAF WATAKIWA KUTUMIA FEDHA ZA TASAF KUJIENDELEZA KIMAISHA.

 

Mkurugenzi wa uratibu  wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Siajabu Suleiman Pandu akizumgumza na wanufaika wa mpango wa TASAF Manispaa ya Bukoba hawako pichani.

..........................................

Alodia Babara,

Bukoba.

WALENGWA wa mpango wa kunusuru kaya maskini nchini, TASAF wametakiwa kuzitumia fedha za mpango huo kama sehemu ya ukombozi, kuimarisha ndoa na familia zao kwa lengo la kuondoa umaskini.

Hayo yamesema Januari 31, mwaka huu 2024, na Mkurugenzi wa uratibu wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais Zanzibar Siajabu Pandu wakati wadau mbalimbali wa mpango huo walipotembelea walengwa katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa lengo la kukusanya maoni na changamoto zinazowakabili walengwa, ambazo baada ya kuzibaini zitawawezesha wadau hao kuboresha mpango unaofuata.

“Serikali tunaamini fedha hii iwe ni sehemu ya ukombozi, kwa hiyo ninawaomba muishi katika ndoa njema, familia nzuri ni sehemu ya ukombozi, fedha ni matokezeo tu sasa tuzitumie hizi fedha kuimarisha ndoa zetu, ndoa si chochote ni subira, tunapaswa kuvumiliana kuhakikisha kwamba tunaishi na watoto wetu kwa pamoja na familia zetu ili kuondoa hali hii ya umaskini” amesema Pandu

Katika ukusanyaji maoni na kusikiliza changamoto za walengwa wadau hao wamegundua kuwa, baadhi ya kaya za walengwa wametelekeza familia zao na kumuacha mzazi mmoja wapo, baba/mama, akiangalia majukumu ya kulea watoto peke yake.

Aidha baadhi ya walengwa wa mpango huo katika mtaa wa Kabale ka Ngaiza manispaa ya Bukoba wakati wakitoa hadithi zao mbele ya wadau hao imeonekana kuwa kuna baadhi ya walengwa ambao ni watoto walishindwa kuendelea katika mpango baada ya wazazi wawili mke na mme kutengana na hivyo watoto kuhamishwa eneo la mtaa husika bila kuwepo mawasiliano na mratibu wa mpango na hivyo kusababisha watoto kuondolewa katika mpango.

Esther Peter mkazi wa mtaa wa Kabale Ka Ngaiza mwenye wategemezi sita, watoto wake wanne na wadogo zake wawili amesema kuwa, yeye anakabiliwa na changamoto mbili mtaji wake kuwa mdogo tofauti na mahitaji yake pamoja na sehemu ya kuishi kwani anaishi kwenye nyumba za kupanga.

Amesema kutokana na changamoto za ndoa watoto waliingizwa kwenye mpango baadaye baba yao akawachukua kuishi nao eneo jingine na hivyo kutokana na kwamba hakuwa na mawasiliano naye watoto waliondolewa kwenye mpango na sasa baada ya kuanza kuishi nao tena anafanya utaratibu wa kuwarudisha kwenye mpango.

“Nashukuru mpango huu wa TASAF na namshukuru Rais wa nchi yetu mama Samia Suluhu Hassan mimi kabla sijaingia  katika mpango huu nilikuwa naishi kwa kuomba omba chakula na nguo kwa watu lakini baada ya kuingia kwenye mpango huu kwa sasa naweza kumudu chakula milo mitatu naweza kuvaa nguo nzuri na kuwanunulia wanangu pia na nimepata mtaji kidogo nafanya biashara ya kuuza samaki” amesema Peter

Amesema, kipindi hicho alikuwa na mdogo wake yuko kidato cha pili lakini kwa sasa amemaliza chuo cha maendeleo ya jamii ingawa bado hajapata ajira na mdogo wake yuko chuo kikuu anasomea sheria.

Aidha walengwa hao wameiomba serikali waendelee kuwa walengwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini kwani wapo baadhi yao wamekumbwa na changamoto mbalimbali na hivyo kusababisha kutoinuka kiuchumi na kubaki wakiwa maskini.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kabale ka Ngaiza Longino Goerge ametoa maombi kadhaa kwa wadau hao kuwa, ni pamoja na TASAF kuunda dawati la usuluhishi kwa wanandoa, kuwaingiza wazee kwenye mpango na kutoa ajira kwa vijana waliotokana na mpango.

Akijibu maswali ya mwenyekiti Kaimu mkurugenzi wa mifumo , mawasiliano na ufuatiliaji TASAF makao makuu Peter Lwanda amesema kuwa, wanaendelea kutengeneza mpango mwingine ambao utaendelea.

Kuhusu ajira ameeleza kuwa, TASAF ilikuwa inafuatilia wale wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne  ambao hawaendelei ofisi ya waziri mkuu inawapeleka vyuo vya ufundi na kuwa serikali bado inaangalia matatizo ya ajira na kuyafanyia kazi.

Lwanda akijibia swala la wazee kuingizwa kwenye mpango ameeleza kuwa, watalichukua na kulifanyia kazi mpango ujao.

Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera una walengwa wa TASAF wapatao 80,563 ambapo tangu mpango ulipoanza mwaka 2015 hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 57.2 zimeishatolewa kwa walengwa hao.





Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masiki mtaa wa Kabale Ka Ngaiza

Tuesday, January 30, 2024

BARAZA LA MADIWANI LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 38.9 KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25

 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo limepokea na kupitisha bajeti ya shilingi Bilioni 38,982,000,000.00 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huku shilingi Bilioni 6,482,058,127.00 ikitarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani na shilingi 32,496,016,000.00 ruzuku kutoka Serikali kuu.


Bajeti hiyo imepitishwa Tarehe 30 Januari 2024 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.


Akiwasilisha bajeti hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, ambae pia ni Diwani wa Kata ya Nianjema, Abdul Pyallah amesema ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji isimamie kikamilifu mikakati ya ukusanyaji mapato.


Akizungumza katika Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Mhe. Mohamed Usinga, amemtaka Mkurugemzi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wakuu wa idara ambao watakamilisha miradi huku ikiwa na madeni.


Usinga alisema ipo tabia ya baadhi ya wakuu wa idara kutekeleza Miradi huku wakiwa wanakopa kwa wazabuni na kuisababishia Halmashauri kuwa na madeni yasiyo ya lazima.


Alisema ni Mkuu wa idara atekeleze Mradi wake kwa mujibu wa bajeti ilivyo na si vinginevyo.


Alisisitiza kwa kisema kuwa, Mkuu wa idara atakasababisha deni kwenye Mradi achukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka.


Nae Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo amesema atahakikisha anasimamia bajeti hiyo ili kufikia malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji pamoja na utekelezaji wa Miradi mbalimbali.



TAKUKURU KAGERA YAWANOA WAANDISHI KUELEKEA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA.

 

Na Alodia Babara

Bukoba

Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera amewasihi waandishi wa habari mkoani humo kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo katika kuelimisha jamii na kufichua vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.


Mkuu huyo Pilly Mwakasege aliyasema hayo Januari 30, mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani Kagera ambapo amesema kuwa, wanawategemea waandishi wa habari kuwapa ushirikiano katika kuwapatia taarifa mbalimbali zinazohusu vitendo vya rushwa kwa sababu ni watu muhimu katika jamii na wanauwezo wa kufika kokote na wanaaminiwa sana na jamii.



Amesema kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri vitaleta mabadiliko kwa jamii kwani watapatikana  viongozi bora na si bora viongozi ambao watasimamia vizuri miradi ya maendeleo na kukemea viashiria vya rushwa.


Amewasisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika mema yaliyofanywa na Serikali kuliko kuitumia tofauti kwani itakuja kuleta athari za rushwa na akaomba kupitia semina hiyo ili wakawe mabalozi na watoe ushirikiano kwa taasisi hiyo.


Aidha amesema  elimu ambayo itatolewa na Takukuru kupitia vyombo vya habari na kuwafikia wananchi itasaidia kujua kwamba  wanapaswa kuchagua kiongozi wa eneo lao ambao wanazitambua changamoto zilizopo kwa undani na watasimamia vizuri maendeleo yao.


Amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa wanapopigiwa kura ile nafasi waliyoipata siyo eneo la kutafuta fursa au mtaji bali ni sehemu ya kwenda kushirikiana na wananchi wao kuwaletea maendeleo. 


“Kiongozi anayetoa rushwa ni yule ambaye hajiamini na hakujiandaa kwa wananchi wake, mkoa wa Kagera tunataka uchaguzi utakapofanyika wachaguliwe viongozi wenye maadili mema watakaosimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi” amesema Mwakasege.


Kwa upande wake  mkuu wa dawati la elimu kwa Umma TAKUKURU mkoa  Esther Mkokota amesema kuwa, rushwa ni adui wa haki na kuwa inaminya haki za watu kuchagua au kuchaguliwa hivyo akasema waandishi wa habari waelimishe watu juu ya kuacha tamaa ambayo ni kisababishi kikubwa cha rushwa.


Amesema kuwa kuna watu wanapowaona wenzao wana mali wanazitamani mali hizo bila kujiuliza mali hizo walizipata kwa njia ipi na hivyo kusababisha wajihusishe na rushwa jambo ambalo litasababisha mtu kama huyo kuchukuliwa hatua za kisheria.


Mkokota ameeleza kuwa, jamii ijue kuwa rushwa ni njia ya mkato ambayo inatumika kufikia lengo na endapo watachagua viongozi kwa kupewa rushwa wajue watakuwa wamepata viongozi wasiokuwa na sifa, rushwa inazorotesha maendeleo ya nchi na miradi inajengwa chini ya kiwango kutokana na kusimamiwa na kiongozi asiye na maadili mema.


Ameongeza kuwa, wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wachague viongozi bora wenye maadili watakaosimamia miradi ya maendeleo




Sunday, January 28, 2024

KILIMO SHADIDI CHA MPUNGA CHAANZA KUCHANGAMKIWA.


Na Mwandishi wetu- Mbeya.

Wakulima wa zao la mpunga wameeleza kufurahishwa na Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga, chenye kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mfumo wa kuongeza mpunga (SRI) ambao unapunguza  gharama za uzalishaji huku tija ikiwa inaongezeka  mara dufu ya kilimo cha kawaida.


Hayo yameelezwa  katika kikao Cha mwaka cha Wadau wa Kilimo shadidi kilichofanyika Januari 24-27 Jijini Mbeya katika viunga vya Kituo Cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI Uyole.


Akielezea hili, Mkulima wa Skimu ya Mkula Wilaya ya kilombero Mkoani Morogoro Filbert Kadebe, amesema katika Kilimo cha kawaida alikuwa akipanda mbegu kilogramu 30 kwa hekari moja lakini kwa kutumia  Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga  wenye kanuni ya kutumia kitalu mkeka anapanda mbegu kilogramu 2 hadi 3 kwa hekari moja.


Pia, Kadebe alisema upandaji wa mche mmoja katika kilimo shadidi unatoa machipukizi mengi ambayo hupelekea kuongezeka kwa mavuno ukilinganisha na upandaji wa Kilimo cha kawaida.


Kilimo shadidi cha mpunga  kinachojulikana kitaalamu  (System of rice Intesification- RSI) ni mchanganyiko wa teknolojia za kilimo cha mpunga wa umwagiliaji kwa kubadilisha mfumo wa uratibu wa mimea, udongo, matumizi ya maji na virutubisho kwa lengo la kuongeza tija.


Nchini Tanzania, Kilimo Shadidi Katika zao la mpunga ni matokeo ya utekelezaji wa mradi  wa mifumo ya uzalishaji mpunga inayokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na rasilimali kwa ufanisi.


Mradi huo unatekelezwa na  TARI kwa kushirikiana na taasisi ya Utafiti ya Norway- Norwegian Institute  of Bioeconomy research (NIBIO) na taasisi ya Utafiti ya Swamination (MSSRF) ya nchini India.


Akielezea Mradi huo, Mratibu  wa  mradi ambaye pia ni Mtafiti Mkuu Kituo Cha Utafiti TARI Uyole, Dkt. Atugutonza Bilaro amesema kilimo  hicho kinatekelezwa katika Halmashauri tano ambazo ni Kilombero, Chalinze, Iringa Vijijini, Mbarali na Bunda.


Dkt. Bilaro amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tayari wamewafikia Wakulima mia tisa lengo ikiwa ni Katika kipindi Cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mradi wafikie Wakulima 4,500.


Naye kiongozi mwenza wa mradi kutoka taasisi ya (NIBIO) Prof. Udaya Sekhar anaeleza lengo la kukutana ni kujadili maendeleo ya mradi, na kuweka mipango ya kutekeleza katika kipindi cha mwaka wa pili.


kwa upande wake  Mtafiti, taasisi ya MSSRF Dkt. Ramasamy Rajkumar ameeleza kufurahishwa namna ambavyo wakulima na Wadau wengine wameanza kutumia elimu wanayofikishiwa na wataalamu.




Friday, January 26, 2024

BARAZA LA WAFANYAKAZI BAGAMOYO, LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 38.9 

 

Na Hamisi Hamisi, Zuhura Kassimu.Bagamoyo

Baraza la wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo limepitisha bajeti ya Shilingi Bilioni 38,978,074,127.00 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huku shilingi bilioni 6,482,058,127.00 ikitarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi Bilioni 32,496,016,000.00 ruzuku kutoka serikali kuu.


Bajeti hiyo imepitishwa januari 25,2024 katika kikao maalum cha kamati tendaji ya Baraza la wafanyakazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.


 Aidha, shilingi Bilioni 6,486,058,127.00 kutoka mapato ya ndani kati ya fedha hizo mapato huru ni Bilioni 3,417,946,627.00 na mapato fungiwa ni Bilioni 3,068,111,500.00 na makadirio hayo ni ongezeko la shilingi milioni 593,528,127.00 kutoka kiasi cha shilingi Bilioni 5,892,530,000.04 kilichoidhinishwa kutumika mwaka wa fedha 2023-2024 sawa na ongezeko la asilimia 10% 

 

Akiwasilisha bajeti hiyo, Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya Bagamoyo, Bi Huruma Eugene, amesema vipaumbele vimewekwa kupitia fedha za mapato ya ndani ikiwa ni Pamoja na kuongeza ukusanyaji kwa kuanzisha vyanzo vipya, kuimarisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira katika ngazi zote,kujenga uwezo wa jamii katika masuala ya jamii na kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa wajasiliamali wadogo, wanawake ,vijana na walemavu,kuboresha ubora wa elimu kwa kujenga miundombinu katika shule za msingi na sekondari na kuboresha huduma za afya kwa kujenga miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya.


Akizungumza katika Baraza hilo mmoja wa wajumbe ameiomba Halmashauri kuwa na utaratibu wa kupandisha madaraja kwa watumishi wa kada mbalilimbali Pamoja na kuwalipa stahiki zao kwa wakati. “Naiomba Halmashauri kupitia ongezeko la mapato ya ndani  kuhakikisha wanawapandisha watumishi wa kada mbalimbali madaraja pamoja na kuwalipa stahiki zao ili kuongeza weledi katika utendaji kazi’’


Sambamba na hayo wajumbe wamemchagua  Ndg .Faraja Mponele kuwa katibu mkuu wa Baraza la wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Pamoja na wajumbe Sita watakaounda kamati tendaji  iliyopo chini ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Bagamoyo Mhe.Shauri Selenda.


Thursday, January 11, 2024

DC OKASH KUWACHUKULIA HATUA WAZAZI WASIOWAPELEKA WATOTO SHULE

 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash amesema atawachukulia hatua Kali wazazi wote watakashindwa kuwapeleka watoto shule ifikapo Jumatatu tarehe  15 January,2024.

Akizungumza Kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya upokeaji wanafunzi katika Shule mbalimbali Halmashauri ya Bagamoyo alisema kuwa msako mkali utafanyika Kwa wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto shule.

" Niwaambie tu  ndugu zangu tutawashughulikia wazazi wote watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao Shule ifikapo Mwisho wa Wiki hii, na Jumatatu tutaanza msako mkali ". Alisema Mhe. Okash



DC OKASH AKEMEA UNYANYASAJI WA KIJINSIA BAGAMOYO.

 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe.Halima Okash amekemea vikali vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia unaendelea katika Wilaya ya Bagamoyo.

Akizungumza na wazazi pamoja na waalimu alipotembelea Shule ya Sekondari Nianjema Leo tarehe 10 Januari, 2024 alisema kuwa, kuna ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia katika maeneo mengi ya Bagamoyo ikiongozwa na Kata ya Mapinga pamoja na Nianjema.

"Niwaambie tuu kuwa, Mimi kama Mkuu nasikitishwa sana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea katika maeneo yetu hivyo hatutasita kuwachukulia hatua wahusika wote watakaobanika kujihusisha na vitendo hivyo.

Nawaomba wazazi muwe mstari wa mbele kuwalinda watoto wenu".Alisema Mhe. Okash.

Aidha Mhe. Okash aliwaomba wazazi kuwapeleka Shule watoto wote waliojiandikisha kuanza madarasa ya awali,la kwanza na kidato Cha Kwanza Kwa Sasa hakuna shida ya watoto kuripoti shuleni kwani Serikali Kwa makusudi imeondoa ada Ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata Elimu.

Aliwashauri walimu na wazazi washirikiane kuhakikisha kuwa watoto wanapata chakula shuleni Ili kuboresha Elimu.

" Natoa rai kwa walimu na wazazi  kushirikiana Kwa pamoja kupitia vikao vyenu kupanga Mipango ya kuwapatia watoto Chakula".Alisisitiza.

Ziara hiyo ya Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ni sehemu ya kukagua maendeleo ya  kuwapokea wanafunzi wa Shule za awali, msingi na kidato Cha Kwanza katika Kata mbalimbali ndani ya  Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.







Friday, December 15, 2023

RMO KAGERA ATENGULIWA KWA KUZUILIWA MWILI WA MTOTO MCHANGA KWA MADAI YA DENI LA MATIBABU HOSPITALINI.

 


Na Alodia Babara

Bukoba.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amemwagiza katibu mkuu wa TAMISEMI nchini kutengua nafasi ya mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Issesanda Kaniki baada ya hospitali ya rufaa ya Bukoba ya mkoa huo kuzuia mwili wa mtoto mchanga kwa muda wa siku mbili kutoruhusiwa kwenda kuzikwa wakati wakijua watoto wanatibiwa bure.


Maagizo mengine ameyatoa kwa viongozi wa serikali, siasa na watumishi mbalimbali nchini.


Waziri Mchengerwa ametoa maagizo hayo  Desemba 15, mwaka huu wa 2023, wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kagera katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani kinachokarabatiwa ambapo pia alishuhudia utiaji wa saini ya mikataba ya usanifu miradi ya uboreshaji wa miundomninu ya miji Tanzania (TACTIC) kwa miji 15 ya kundi la pili.


Ameagiza katibu mkuu TAMISEMI kwa kushirikiana na sekta ya afya kufanyika mapitio ya menejimenti nzima ya hospitali hiyo na kutoa maamuzi kwani alipata malalamiko kuwa wapo baadhi ya watumishi wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa.


Amesema,  muda wa kubembelezana haupo tena kwa nyakati hizi watu wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea sasa hatuwezi kuendelea na watumishi wa namna hiyo kwa sababu wananchi wana imani na serikali yao.


Wakati huo huo waziri Mchengerwa alisema mtu yoyote au kiongozi yoyote awe wa kisiasa au mtendaji yeyote wa serikali atakaye jaribu kufanya ubadhilifu au kukwamisha miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika manispaa ya Bukoba ikiwemo stend kuu, soko kuu, barabara ya kilomita saba na kingo za mto Kanoni na kufunga taa za barabani
hatofumbiwa macho atachukulia hatua kali za kisheria.


"Tunataka  tubadilishe muonekano wa Kagera mhe. Rais alizitafuta fedha hizi maeneo mbalimbali anataka kuibadilisha Kagera hivyo, kiongozi yoyote awe wa kisiasa au serikali atakayejaribu kuingiza mkono bila kujali nafasi yake nitashugulika naye ikiwemo kumfukuza kazi, hatutaki ubabaishaji katika miradi hii"amesema Mchengerwa.


Aidha amesema, kama kuna viongozi wa siasa ndani ya manispaa ya Bukoba au mkoa wa Kagera wanaokwamisha miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ni kiu ya wanakagera kwa muda mrefu atasimamisha baraza la madiwani mpaka miradi hiyo ikamilike.


"Maagizo yangu ujenzi wa soko uzingatie wale wafanyabiashara  wa zamani waliondolewa kinyume na taratibu wapate vibanda ndipo wapya wapewe mabanda na wale waliko nje ya soko wote wapate nafasi hii pia tukikamilisha hatutaki kuona wafanyabiasha wakiendesha shughuli zao nje ya soko hili ambalo Dk.Samia anakwenda kulijenga katika maeneo haya kiongozi yoyote atakaye kaidi maagizo, ujeuri na kiburi aliyeko kwenye mamlaka yangu nitamfukuza kazi na walioko kwenye mamlaka za juu nitawafikisha kwa Rais awafukuze kazi”alisema.


Pia waziri aliwaagiza  wakurugenzi wote nchini kuendana na kasi ya Ras Samia ambapo kila mkurugenzi anatakiwa kuanzisha vyanzo viwili vya kuingiza mapato atakayeshindwa kufanya hivyo atahovumiliwa.


Mratibu wa miradi ya ushirikiano na benki ya dunia TACTIC  mhandisi Humphrey  Kanyenye alisema miradi hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa miezi nane ikiwezekana mwezi Machi mwakani ujenzi uanze mara moja.


Ujenzi wa kituo cha mabasi Bukoba na soko kuu kimekuwa kitendawili cha muda mrefu baada ya kukwama kujengwa takribani miaka 15 iliyopita baada ya kutokea mgongano wa masrahi ya kisiasa.


Miradi hii ya uboreshaji wa miundombinu ya miji Tanzania TACTIC  kwa miji 15 ya kundi la pili (Tier) ambapo Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji itakayonufaika na miradi hiyo zilitengwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi huo kati ya sh moja trilioni ya miradi yote.