Sunday, January 28, 2024

KILIMO SHADIDI CHA MPUNGA CHAANZA KUCHANGAMKIWA.


Na Mwandishi wetu- Mbeya.

Wakulima wa zao la mpunga wameeleza kufurahishwa na Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga, chenye kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mfumo wa kuongeza mpunga (SRI) ambao unapunguza  gharama za uzalishaji huku tija ikiwa inaongezeka  mara dufu ya kilimo cha kawaida.


Hayo yameelezwa  katika kikao Cha mwaka cha Wadau wa Kilimo shadidi kilichofanyika Januari 24-27 Jijini Mbeya katika viunga vya Kituo Cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI Uyole.


Akielezea hili, Mkulima wa Skimu ya Mkula Wilaya ya kilombero Mkoani Morogoro Filbert Kadebe, amesema katika Kilimo cha kawaida alikuwa akipanda mbegu kilogramu 30 kwa hekari moja lakini kwa kutumia  Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga  wenye kanuni ya kutumia kitalu mkeka anapanda mbegu kilogramu 2 hadi 3 kwa hekari moja.


Pia, Kadebe alisema upandaji wa mche mmoja katika kilimo shadidi unatoa machipukizi mengi ambayo hupelekea kuongezeka kwa mavuno ukilinganisha na upandaji wa Kilimo cha kawaida.


Kilimo shadidi cha mpunga  kinachojulikana kitaalamu  (System of rice Intesification- RSI) ni mchanganyiko wa teknolojia za kilimo cha mpunga wa umwagiliaji kwa kubadilisha mfumo wa uratibu wa mimea, udongo, matumizi ya maji na virutubisho kwa lengo la kuongeza tija.


Nchini Tanzania, Kilimo Shadidi Katika zao la mpunga ni matokeo ya utekelezaji wa mradi  wa mifumo ya uzalishaji mpunga inayokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na rasilimali kwa ufanisi.


Mradi huo unatekelezwa na  TARI kwa kushirikiana na taasisi ya Utafiti ya Norway- Norwegian Institute  of Bioeconomy research (NIBIO) na taasisi ya Utafiti ya Swamination (MSSRF) ya nchini India.


Akielezea Mradi huo, Mratibu  wa  mradi ambaye pia ni Mtafiti Mkuu Kituo Cha Utafiti TARI Uyole, Dkt. Atugutonza Bilaro amesema kilimo  hicho kinatekelezwa katika Halmashauri tano ambazo ni Kilombero, Chalinze, Iringa Vijijini, Mbarali na Bunda.


Dkt. Bilaro amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tayari wamewafikia Wakulima mia tisa lengo ikiwa ni Katika kipindi Cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mradi wafikie Wakulima 4,500.


Naye kiongozi mwenza wa mradi kutoka taasisi ya (NIBIO) Prof. Udaya Sekhar anaeleza lengo la kukutana ni kujadili maendeleo ya mradi, na kuweka mipango ya kutekeleza katika kipindi cha mwaka wa pili.


kwa upande wake  Mtafiti, taasisi ya MSSRF Dkt. Ramasamy Rajkumar ameeleza kufurahishwa namna ambavyo wakulima na Wadau wengine wameanza kutumia elimu wanayofikishiwa na wataalamu.




No comments:

Post a Comment