Tuesday, January 30, 2024

TAKUKURU KAGERA YAWANOA WAANDISHI KUELEKEA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA.

 

Na Alodia Babara

Bukoba

Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera amewasihi waandishi wa habari mkoani humo kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo katika kuelimisha jamii na kufichua vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.


Mkuu huyo Pilly Mwakasege aliyasema hayo Januari 30, mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani Kagera ambapo amesema kuwa, wanawategemea waandishi wa habari kuwapa ushirikiano katika kuwapatia taarifa mbalimbali zinazohusu vitendo vya rushwa kwa sababu ni watu muhimu katika jamii na wanauwezo wa kufika kokote na wanaaminiwa sana na jamii.



Amesema kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri vitaleta mabadiliko kwa jamii kwani watapatikana  viongozi bora na si bora viongozi ambao watasimamia vizuri miradi ya maendeleo na kukemea viashiria vya rushwa.


Amewasisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika mema yaliyofanywa na Serikali kuliko kuitumia tofauti kwani itakuja kuleta athari za rushwa na akaomba kupitia semina hiyo ili wakawe mabalozi na watoe ushirikiano kwa taasisi hiyo.


Aidha amesema  elimu ambayo itatolewa na Takukuru kupitia vyombo vya habari na kuwafikia wananchi itasaidia kujua kwamba  wanapaswa kuchagua kiongozi wa eneo lao ambao wanazitambua changamoto zilizopo kwa undani na watasimamia vizuri maendeleo yao.


Amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa wanapopigiwa kura ile nafasi waliyoipata siyo eneo la kutafuta fursa au mtaji bali ni sehemu ya kwenda kushirikiana na wananchi wao kuwaletea maendeleo. 


“Kiongozi anayetoa rushwa ni yule ambaye hajiamini na hakujiandaa kwa wananchi wake, mkoa wa Kagera tunataka uchaguzi utakapofanyika wachaguliwe viongozi wenye maadili mema watakaosimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi” amesema Mwakasege.


Kwa upande wake  mkuu wa dawati la elimu kwa Umma TAKUKURU mkoa  Esther Mkokota amesema kuwa, rushwa ni adui wa haki na kuwa inaminya haki za watu kuchagua au kuchaguliwa hivyo akasema waandishi wa habari waelimishe watu juu ya kuacha tamaa ambayo ni kisababishi kikubwa cha rushwa.


Amesema kuwa kuna watu wanapowaona wenzao wana mali wanazitamani mali hizo bila kujiuliza mali hizo walizipata kwa njia ipi na hivyo kusababisha wajihusishe na rushwa jambo ambalo litasababisha mtu kama huyo kuchukuliwa hatua za kisheria.


Mkokota ameeleza kuwa, jamii ijue kuwa rushwa ni njia ya mkato ambayo inatumika kufikia lengo na endapo watachagua viongozi kwa kupewa rushwa wajue watakuwa wamepata viongozi wasiokuwa na sifa, rushwa inazorotesha maendeleo ya nchi na miradi inajengwa chini ya kiwango kutokana na kusimamiwa na kiongozi asiye na maadili mema.


Ameongeza kuwa, wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wachague viongozi bora wenye maadili watakaosimamia miradi ya maendeleo




No comments:

Post a Comment