Thursday, November 9, 2023

MAKONDA ATOA MAAGIZO KWA MAWAZIRI, KAGERA

 

Na Alodia Babara 


Bukoba. 



Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda,  ametoa maagizo mbalimbali kwa Mawaziri wa wizara nne hapa nchini ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuwapigia simu mawaziri hao na kutoa majibu ya changamoto na kutatua changamoto hizo.


Mawaziri waliopigiwa simu ni pamoja na waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa, Waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun, waziri wa uchukuzi Makame Mbarawa na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa.


Makonda ametoa maagizo hayo leo Novemba 9, 2023 wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara akiongea na wananchi mkoani Kagera uliofanyika uwanja wa mashujaa Mayunga.


Moja ya changamoyo zilizotajwa ni pamoja na ujenzi wa soko kuu, kingo za mto Kanoni, ujenzi wa stend kuu, uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Bukoba, tatizo la nida maeneo ya mipakani na ujenzi wa barabara za lami.


Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akijibu kuhusu changamoto za ujenzi wa soko kuu, stend kuu na kingo za mto Kanoni amesema kuwa maagizo ya katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa Makonda ameyapokea na kufanyia utekelezaji haraka, mwezi Desemba 2023 atafika mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua maeneo itakapotekelezwa miradi hiyo


Akijibia changamoto ya vitambulisho vya NIDA kwa upande wa wananchi waishio mipakani waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun amesema kuwa, swala la vitambukisho vya NIDA katika maeneo hayo wizara inalifanyia kazi ili kuharakisha zoezi na wale wenye haki ya kupata kadi za NIDA waweze kuzipata. 


Amesema wameanza mkakati wa kutembelea mikoa iliyopo maeneo ya mpakani kwa kuanza na mkoa wa Mara na baadaye watakwenda Kagera.


Makonda amewataka Askari wa usalama barabarani wote nchini kutowaonea waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na badala yake watumie sheria wanapowakamata na kuwakuta na makosa.

 



HALMASHAURI YA BAGAMOYO YAVUKA MALENGO UKUSANYAJI WA MAPATO

 

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imevunja rekodi ya kukusanya kiwango katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuaniza Julai mpaka Septemba 2023


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya Bagamoyo Mhe. Halima Okashi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo tarehe 09 Novemba 2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.



Akizungumza katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani Mkuu huyo wa Wilaya aliwapongeza Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuanzia Julai mpaka Septemba 2023. 



Katika kipindi hicho Halmashauri imekusanya zaidi ya shiling bilioni 1 sawa na asilimia 27.7 ambapo ni asilimia 2.7 zaidi ya malengo waliyojiwekea ya asilimia 25.



"Niwapongeze Madiwani wa Kata zote pamoja na Watumishi wa Halmashauri ya Bagamoyo kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato kwenye taarifa yenu inaonyesha mapato yaliyopatikana ni asilimia 27.7 ambapo malengo yalikuwa ni asilimia 25 hivyo hongereni sana kwa ongezeko hilo la asilimia 2.7" alisema Bi Halima Okashi


Aidha Mkuu wa Wilaya huyo aliwataka Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kuongeza ubunifu zaidi ili kuweza kupata wigo wa kuongeza mapato utakaopelekea uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo akipokea pongezi hizo kwa niaba ya Baraza la Madiwani Mhe. Mohamedi Usinga aliahidi kuendelea kuboresha vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuboresha mapato kwenye Halmashauri hiyo.





MAGAZETI YA LEO TAREHE 09 NOVEMBA 2023.

 


















Wednesday, November 8, 2023

WANUFAIKA MRADI WA KLIC WATAKIWA KUTUNZA VIFAA VYA TEHAMA-TET

 

Na Andrew Chale,Dar es Salaam.

Shule zote nchini zilizonufaika na vifaa vya mradi wa KOREAN E-LEARNING IMPROVEMENT COOPORATION(KLIC) ulio chini ya Ofisi ya Elimu ya Gwangju Metropolitan ya nchini Korea ya Kusini, wenye lengo la kuboresha elimu nchini katika eneo la TEHAMA, wametakiwa kuhakikisha wanatumia vizuri , kiusahihi na kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kunufaisha wanafunzi wengi zaidi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utafiti,Habari na Machapisho waTaasisi ya Elimu Tanzania(TET), Bw. Kwangu Masalu leo tarehe 8/11/2023 katika shule ya Sekondari Kimbiji iliyopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam katika ziara ya ujumbe wa watu kutoka korea ulipofika shuleni hapo kwa ajili ya kugawa vifaa vya TEHAMA vya kujifunzia masomo pamoja na kutoa mafunzo ya vitendo ya namna ya kuvitumia kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo .

Mwakilishi wa walimu waliopo kwenye ziara hiyo kutoka nchini Korea Kusini, Bwana.Kim Chi Gon ameeleza kuwa , wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wanakuza utumiaji wa TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji hapa nchini na kwani kwa sasa ulimwengu umebadilika sana hasa katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Kwa upande wa Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kigamboni Bi. Twidike Ntima ameeleza kwamba shule hiyo kuwa moja ya shule za mfano wa kupata vifaa vya TEHAMA ni jambo kubwa ambapo imesaidia sana kwa walimu kuweza kufanya kazi kwa urahisi na kuwa endapo masuala ya TEHAMA yataendelea kusambaa nchi nzima basi wanafunzi nchini na walimu wataweza kupiga hatua katika masuala ya elimu.

Naye Mkuu wa shule hiyo Bi. Joyce Ndaona amesema kuwa kwa sasa walimu wa shule hiyo wamepata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa nchini Korea ya Kusini ambapo wameweza kupata ujuzi wa kurahisishiwa kazi hasa katika eneo la ufundishaji na kuwapa nafuu wanafunzi kutumia TEHAMA kwenye ujifunzaji tofauti na awali.

Hata hivyo ugeni huo wa walimu na wanafunzi ukiwa katika shule hiyo ya Kimbjiji, uliweza kujionea namna wanafunzi wanavyoonesha uelewa katika masomo yao ambapo waliweza kuonesha utaalamu wao kupitia masomo ya fikizia na Uchoraji na baadae wanafunzi hao kuweza kufanya mafunzo kwa vitendo.






WAFANYABIASHARA MKURANGA, KIBITI WAMSIFU SAMIA UHURU WA BIASHARA.

 

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

WAFANYABISHARA wilayani Mkuranga na Kibiti, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuliza dhorobu ya hali ya biashara nchini.

Wamesema kwenye wilaya hizo biashara zinafanyika kwa amani na utulivu bila usumbufu tofauti na miaka ya nyuma.

Wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti kwenye mkutano kati ya wafanyabishara wa wilaya hizo na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) inayoendelea mkoani Pwani yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wafanyabishara.

Mfanyabiashara Hassan Mbwana Kambangwa, amesema wafanyabiashara kwa asilimia kubwa wilayani humo wananufaidika sana tangu kuingia kwa utawala wa Rais Samia.

Amesema "Kimsingi namshuruku Rais Samia kwa kutuletea ugeni uliotupa fursa ya kuzungumza changamoto zinazotukabili, lakini sisi tangu kuingia kwa utawala huu wa Mama Samia tunafaidika nao kwa asilimia kubwa."

Mfanyabiasha huyo ametolea mfano wa mambo wanayofaidika nayo kuwa ni mikopo, uhusiano mazuri na halmashauri lakini pia taasisi mbalimbali za kifedha ziko huru kuwasaidia wafanyabiashara.

Amesema serikali imezingatia suala la amani na utulivu na kwa mikoa mingi ilikua inapata changamoto nyingi lakini hapa wilaya ya Mkuranga wafanyabiashara wako huru na wanafanyabiashara bila bugudha.

"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan tunafanyabiashara kwa amani lakini pia tunashukuru ujio huu wa leo umefanya tuweza kufunguka yale ambayo yako ndani ya moyo na tunaamini mtayafikisha," Kambangwa.

Naye mfanyabishara Wilaya ya Kibiti, Salim Juma, amempongeza Rais Samia kwa kuona sekta ya wafanyabishara ni sehemu ya uchumi wa Taifa na kuamua kuungana kwa pamoja kutatua kero zao.

"Ili kuwa na ustawi tumefanikiwa kumpa Rais Samia, ambaye ameona umuhimu wetu na kutambua mchango wetu ndio maana leo viongozi mpo hapa," amesema Juma.
Mwisho




BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA BAGAMOYO LAFANYA KIKAO CHAKE CHA KWANZA CHA ROBO MWAKA 2023

 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo leo tarehe 8 Novemba 2023 limekutana na kufanya Kikao chake cha kwanza katika mfululizo wa vikao viwili vya Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, vikao ambavyo vimepangwa kufanya tarehe 8-9 Novemba 2023.

Katika Kikoa hicho Baraza lilipokea Taarifa za Utendaji kwenye ngazi ya Kata kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023.

Akipokea taarifa hizo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Mohemed Usinga aliwapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Madiwani wa Kata zote kwa kazi nzuri walizozifanya katika kipindi hiki cha robo ya kwanza.

Aidha Mwenyekiti huyo aliagiza Madiwani pamoja na watendaji wa kata zote kutoanzisha miradi mipya ya maendeleo mpaka miradi iliyopo ikamilike, "Waheshimiwa Madiwani pamoja na Watendaji wa Kata hakikisheni mnamaliza miradi yote iliyokuwa haijakamilika kabla ya kuanzisha miradi mingine, tuhakikishe kwenye kata zetu tunamaliza viporo vyote vya miradi inayoendelea" alisema Mhe Usinga

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw. Majid Mhina alipokea maelekezo ya Baraza hilo na kwenda kuifanyia kazi. "Tumepokea maelekezo ya Baraza kwa ushirikiano wa Idara zetu na wataalamu tulio nao tunaenda kuyafanyia kazi" amesema Bw. Mhina 






ZAIDI YA WANAFUNZI 2,000 WANUFAIKA NA MRADI WA CAMFED CHALINZE.

 

Zaidi ya wanafunzi 2,000 wasichana wamenufaika na Mradi wa Kampeni ya Elimu kwa mtoto wa kike (CAMFED) Halmashauri ya Chalinze kuanzia mwaka 2016 hadi sasa.


Mkuu wa Kitengo cha Shule ya Sekondari, Madam Salama Ndyetabura akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Timu na Watoto wa Kampeni ya Elimu kwa Wanawake (CAMFED), katika mada iliyowasilishwa leo Tarehe 08 Novemba 2023, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Chalinze.


Madam Ndyetabura wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa CAMFED, alifafanua historia ya CAMFED katika Halmashauri ya Chalinze, Wanafunzi wakisaidiwa na CAMFED, CAMA network, miradi ya CAMFED katika Halmashauri ya Chalinze, Serikali na Ushirikiano wa CAMFED kusaidia elimu ya wasichana Chalinze.


Madam Ndyetabura aliendelea kueleza kuwa CAMFED Tanzania ilitekeleza miradi mingi ya kusaidia elimu ya mtoto wa kike na wanawake vijana kama msaada wa elimu ya Msichana, mradi ambao ulianza 2016 hadi sasa na kusaidia jumla ya wanafunzi 2,347, Vijana wa kike, mradi huu ulianza 2019 ambapo 72 wanawake waliopata mafunzo,14 walifanikiwa kukamilisha makubaliano yao ya miezi 12, na  4 waliacha shule.


Hata hivyo serikali kwa kushirikiana na CAMFED ilisaidiana katika harakati za kumlinda na kumsaidia mtoto wa kike kupata elimu na kumaliza masomo yake.


Halmashauri imeanzisha na kuimarisha sheria mbalimbali kwa mfano kusisitiza sheria ya ulinzi wa mtoto kuanzia ngazi ya kijiji na kutumia mamlaka kwa maofisa watendaji wa vijiji (VEO) na maofisa watendaji wa kata (WEO) kushughulikia masuala yote yaliyoripotiwa yanayohusu ukatili dhidi ya watoto.





DC OKASH AIPONGEZA HALMASHAURI YA CHALINZE KWA UKUSANYAJI MAPATO

 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Mheshimiwa Halima Okash ametoa pongezi kwa Madiwani na wataalam wa halmashauri ya Chalinze kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika suala zima la ukusanyaji mapato ya ndani ya Halmashauri na kuvuka asilimia 27 ya malengo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024.


Mheshimiwa Okash ametoa Pongezi hizo leo Tarehe 08 Novemba 2023 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa robo ya kwanza uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.


Katika hotuba yake ya kutoa Salaam za Serikali amewataka madiwani na watendaji wa Halmashauri kuendelea na jitihada za ukusanyaji mapato ya ndani na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kufikia malengo ya ukusanyaji mapato ili kutoa huduma stahiki kwa Wananchi.


Okash Pia ametoa Pongezi kwa Halmashauri ya Chalinze katika suala zima la usimamizi wa mkataba wa lishe ulioiwezesha Halmashauri kushika nafasi nzuri kimkoa na kuwataka uongozi wa halmashauri kuifanya lishe kuwa ajenda ya kudumu kuanzia ngazi ya kitongoji mpaka wilaya.


Mkuu wa wilaya amewataka viongozi wa halmashauri kuzingatia utawala bora kwa kuhakikisha vikao vyote vya kisheria vinafanyika kwa wakati kuanzia Kitongoji,kijiji na Kata ili kuweza kubaini changamoto na kero mbalimbali zinazoweza kutokea katika jamii na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati pasipo kuchelewa.


Aidha Okash ametoa rai kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kuchukua tahadhali kutokana na mvua za Elinino zinazoendelea kunyesha katika mkoa wa Pwani hususan Chalinze, kwa kuondoka katika mabonde na kukaa maeneo yenye miinuko ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo.


Mkuu wa wilaya alimalizia hotuba yake kwa kuwataka viongozi wote katika Mamlaka za Serikali za mitaa kuendelea kuisemea Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa inayofanya katika kuboresha maisha ya watanzania kwa kujenga miundombinu mbalimbali katika sekta za afya,elimu,barabara na Maji ili watanzania wapate kufahamu yanayoendelea.


“Namshukuru Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuimarisha maisha ya watanzania,hususan wanachalinze kwa kuwaletea fedha zaidi ya Bilioni 2 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024 Mungu azidi kumtunza.” Okash alisema.