Thursday, September 7, 2023

VIFAA VYA KUJIPIMA UKIMWI MILIONI 1.6 VIMESAMBAZWA NCHINI

 

Na. WAF - Dodoma


Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI hadi sasa imeweza kusambaza vifaa vya mtu kujipima mwenyewe maambukizi ya Virusi vya UKIMWI zaidi ya Mil. 1.6 kuanzia Mwaka 2021 nchini Tanzania. 


Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo kwenye kilele cha Mdahalo wa Kitaifa wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambapo Mgeni rasmi alikua ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.


Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuongeza nguvu za kusambaza vifaa hivyo vya watu kujipima wenyewe Virusi vya UKIMWI ili kuweza kutambua hali zao wenyewe na kwa haraka kuhusu ugonjwa huo.


Waziri Ummy amebainisha kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanua wigo wa vituo vya kupima na kutoa huduma za matunzo (CTC) kwa watu wenye UKIMWI ambapo hadi sasa tuna vituo 8,529.


“Nitoe rai kwa watu wote wanaoishi na VVU kuzingatia matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI ili kuweza kujilinda wao wenyewe lakini pia kuwalinda wengine” amesisitiza Waziri Ummy.


Pia, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa huduma za kupima, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU hapa nchini ili vituo vyote vinavyotoa huduma za Afya viwe pia vituo vya kupima na kutoa matunzo (CTC) kwa 95% ifikapo Mwaka 2025.


Aidha, Waziri Ummy amesema chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia, Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vitendanishi kwaajili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na kuendelea kufuatilia taarifa zote kuhusu uwepo wa dawa mpya ambazo ni bora zaidi.


Mwisho, Waziri Ummy amelipongeza Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA) kwa kuanzaa mdahalo wa kuadhimisha Miaka 20, “Sekta ya Afya inatambua mchango wao mkubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI”. Amesema Waziri Ummy.






USHIRIKIANO TANZANIA, MAREKANI KUIMARISHA SEKTA YA MADINI

 

Marekani kuipa Kipaumbele Sekta ya Madini nchini


Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amekutana na kuzungumza na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Marekani nchini katika ziara iliyolenga kuzungumzia masuala mbalimbali katika shughuli za uchimbaji na maendeleo ya Sekta ya Madini, Mji wa Serikali jijini Dodoma.


Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Septemba 7, 2023, Katibu Mkuu Mahimbali amesisitiza kuimarisha ushirikiano katika uchimbaji wa madini hususan ya kimkakati, kujengewa uwezo wataalam mbalimbali wa Sekta ya Madini ili mnyororo mzima wa shughuli za madini unufaike.


Amesema kuwa Wizara ya Madini imeweka vipaumbele katika maeneo manne ili kuimarisha zaidi Sekta hiyo, maeneo hayo ni pamoja na Utafiti wa kina, maendeleo ya rasilimali watu, ushirikiano sambamba na KanziData ya Madini.


Aidha, amesisitiza kuwa milango ya uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini ipo wazi kwa nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye kipaumbele ili nchi zote zinufaike na uwepo wa madini hayo.


Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Kiuchumi kutoka Ubalozi wa Marekani nchini, Jonathan Howard amesisitiza kuwa, nchi yake itashirikiana na Tanzania katika shughuli za Sekta ya Madini hususan katika kujengeana uwezo na ujuzi, fedha na teknolojia.


Vile vile, Howard ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya kumteua na kumuapishwa Mhe. Antony Mavunde kuwa Waziri wa Madini. Wamesema nchi yao itampatia ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake kuiongoza Sekta ya Madini.


Ameongeza kuwa wanatarajia kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Madini linalotarajiwa kufanyika Oktoba 25 na 26, 2023 jijini Dar es Salaam.


Pia, amepongeza juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuvutia wawekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi inayochochea maendeleo na uchumi kwa ujumla.

 





SWALA LA MAFUTA, WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA NAIBU WAZIRI MKUU

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko aendelee kushughulikia suala la changamoto ya upatikanaji wa nishati ya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini.


“...Watanzania wapate hii huduma, upatikanaji huu ni muhimu kuhusisha taasisi zote za mafuta na wanunuaji mafuta kwa pamoja ‘bulk’ wakae pamoja na Wizara zinazohusika ikiwemo Wizara ya Fedha na Idara ya Ofisi ya Uratibu Ofisi ya Waziri Mkuu waone namna ya upatikanaji wa mafuta.”


Ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Septemba 7, 2023) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha Taifa linakuwa na mafuta ya kutosha.


“Lakini pia tupanue wigo wa waagizaji wa mafuta ili tuwe na mafuta mengi nchini kwa usalama wa Taifa letu. Na kama hili litafanyika ndani ya wiki moja tutakuwa tumeshapata majibu na kuwapa taarifa Watanzania.Tutahakikisha nishati hii ya mafuta inapatikana na Naibu Waziri Mkuu atashughulikia hilo.”


Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI iendelee na utaratibu wa kubaini maboma yote kwenye sekta ya afya na elimu ambayo waliyajenga na hayakukamilika, wahakikishe wanaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuyakamilisha kwa sababu yametokana na bajeti zao.


Waziri Mkuu amesema suala la ujenzi wa miradi ya elimu au afya ambayo inahusisha majengo ni mkakati ulioelekezwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia fedha zinazopelekwa kutoka Serikali Kuu ambazo zinapelekwa kujenga majengo hayo kwa thamani ya jengo kutokana na makadirio waliyoyatoa, hivyo wanatakiwa wasimame ujenzi ukamilike kama ilivyokusudiwa.


Aidha, Waziri Mkuu amesema chanzo kingine ni fedha inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri zenyewe ambapo wao hupanga mipango ya maendeo yao kupitia bajeti yao na kwenda kujenga, maboma mengi yanatokana na mipango yao, hivyo wayakamilishe.


“Uzoefu tulioupata wakati wa ukaguzi wa miradi hii, majengo ambayo yametekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu yamekwenda kama yalivyo na pale ambapo hayakukamilika hatua kali zimechukuliwa. Sasa kwa kuwa maboma mengi yanatokana na mipango yao na kushindwa kuyaendeleza, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha maboma yote yanakamilika.“


Ametumia fursa hiyo kuziagiza zifanye tathmini ya miradi yake ione maeneo gani ambayo walianza miradi na wameshindwa kukamilisha na yamebaki maboma ili wapange bajeti ya kila mwaka kuhakikisha maboma hayo yanakamilika. “Halmashauri haziwezi kushindwa kupata shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati.“


Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mwaifunga aliyetaka kujua ni nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha inakamilisha maboma ya kutolea huduma za elimu na afya nchini, miradi iliyoanzishwa na Serikali na nguvu za wananchi ili wananchi hao waweze kuona thamani ya nguvu yao na ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika maeneo yao.

JAJI MKUU AZINDUA KITABU CHA MKUSANYIKO WA MASHAURI YA UNYANYASAJI WA KINGONO KWA MTOTO.

 

NA MWANDISHI YETU


Mhe. Prof. Ibrahim H. Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania amezindua Kitabu cha Mkusanyiko wa Mashauri ya Ukatili wa Kingono kwa Mtoto wa Tanzania na Ireland na kutoa wito kwa wadau kufanyia kazi yale yote yaliyomo ndani ya kitabu hicho.



Uzinduzi huo umefanyika tarehe 05/09/2023 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, na umeratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Irish Rule of Law International (IRLI) kupitia ufadhili wa ubalozi wa Ireland hapa nchini Tanzania.



“Kitabu hiki kitakuwa hakina maana kama hatutakwenda hatua nyingine kutekeleza mapendekezo yaliyomo kwenye kitabu hiki,” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.



Mhe. Jaji Mkuu ameongeza kuwa kitabu hicho kimekuja wakati muafaka ambapo Tume ya Rais ya maboresho ya haki jinai imewasilisha ripoti yake ambayo ina baadhi ya masuala ambayo yanashabihiana na yaliyomo kwenye kitabu hicho.



“Kitabu hiki kimekuja wakati muafaka wakati ambapo Tume ya Rais ya maboresho ya Haki jinai ikiwa imetoa ripoti yake na imebainisha maeneo kadhaa muhimu ambayo yanafana na mapendekezo mengine yaliyomo kwenye kitabu hiki,” amesema Mhe. Jaji Mkuu.



Kitabu hiki kimeandaliwa kwa Ushirikiano kati ya IRLI na IJA na ni moja ya maeneo ya Makubaliano ya Mashirikiano (MoU) baina ya taasisi hizo mbili uliosainiwa Machi 2022, kwa lengo la kuendeleza uhusiano kwenye eneo la haki ya mtoto.



Naye Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema kuwa ili kuhakikisha kitabu hicho kinaleta tija, watatoa mafunzo kwa baadhi ya Majaji na Mahakimu ambao watakwenda kuwafundisha maafisa wengine wanaohusika na masuala ya usimamizi wa haki.



“Baada ya kutengeneza kitabu hiki, tutakwenda kwa hatua ya pili kwa kutoa mafunzo kama vile mafunzo kwa ajili ya wakufunzi ambayo yatafanyika kwa Majaji na Mahakimu 15, baada ya hapo tutakwenda kwenye kanda saba kutoa mafunzo kwa kuwatumia hao wakufunzi kutoa elimu kwa maafisa wa Mahakama,” amesema Mhe. Jaji Dkt. Kihwelo.









MAGAZETI YA LEO TAREHE 07 SEPTEMBA 2023.

 




















Tuesday, September 5, 2023

WASTAAFU WAOMBA KUKUTANA NA DKT. MPANGO.

 

Rais wa REAT nchini Mwalimu Dauda Bilikesi akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba hawapo pichani akimuomba makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philip Isdor Mpango kukaa na wastaafu ili kutatua changamoto zao.

Na Alodia Babara- Bukoba


UMOJA wa wastaafu Tanzania (REAT) wamemuomba makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isidor Mpango kukutana nao sambamba na kuwakutanisha na viongozi,watendaji wa Serikali (waajiri)na mifuko ya Hifadhi ya jamii ili waweze kujadili hoja 13 walizowasilisha kwa Serikali.


Akizungumza na Waandishi wa habari leo mjini Bukoba Rais wa REAT nchini Mwalimu Dauda Bilikesi amesema mwezi Januari mwaka huu umoja huo ulituma maombi kupitia Wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake,watoto na makundi maalum na kuwasilisha hoja zao 13 mojawapo ikiwa ni kuboresha kima cha chini cha pensheni ambapo kwa mujibu wa sheria kima cha chini cha pensheni inapaswa isiwe chini ya asilimia 40 ya mshahara wa watumishi wa Umma.


"Wapo wastaafu wengi wanaolipwa kiasi cha shilingi 45,000 hadi 75,000 pungufu 100,000 kama pensheni ya mwezi,ndio hao wasio na huduma ya bima ya Afya chini ya mfuko wa NHIF kutokana na udogo wa pesheni zao huku umri wao mkubwa unasababisha kukabiliwa na maradhi ya mara kwa mara na ugumu wa maisha ya sasa, hivyo, kupitia hadhara hii tunamuomba mhe. makamu wa Rais Dkt. Mpango atupatie nafasi ya kukutana naye nakutusaidia kufikia muafa wa kutatatua changamoto zetu"amesema Bilikesi. 


Amesema maombi yao yanakuja baada ya taarifa ya Naibu waziri ofisi ya Waziri mkuu, ajira, kazi na Vijana Patrobasi Katambi aliyoitoa bungeni Septemba mosi mwaka huu ya kuwa Serikali imeboresha kima cha chini cha pensheni cha wastaafu wote kifikia shl 100,000 huku wengine wakiwa bado.

 

WANANCHI BUMBWINI WAFUNGUKA MAZITO MBELE YA RC AYUB, ATATUA KERO ZAO KWA VITENDO

 

Na Andrew Chale, Kusini Unguja, Zanzibar.


WANANCHI wa Bumbwini wa Shehia tatu za Misufini, Mangapwani na Kidazini wamefunguka mazito mbele ya mkutano wa wazi wa Wananchi kutoa kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe Ayoub Mohammed Mahmoud huku baadhi ya kero hizo akizitatua papo kwa papo.


Katika mkutano huo wa ziara yake ya siku ya kwanza jana mchana, Septemba 4, 2023 iliyofanyika kwenye uwanja wa Vidimni, Mhe RC Ayoub ameweza kupokea kero mbalimbali za Wananchi huku kero kubwa ikiwemo ukosefu wa maji, Umeme sambamba na suala la malalamiko ya watu kutolipwa fidia katika maeneo ambayo miradi ya Kiserikali iliopita maeneo yao huku suala kubwa wananchi hao wakilalamikia moja ya Mgahawa wa mwekezaji wa ndani uliopo kwenye fukwe Shehia ya Mwangapwani kujihusisha na vitendo vya uvunjivu wa maadili wakitaka ufungwe.


Ambapo katika kutatua kero hizo, RC Ayoub ameweza kuwapigia Wakuu wa Idara pamoja na Watendaji wakuu wa mamlaka husika zikiwemo Maji, Umeme na wengine wengi ambao waliweza kujibu moja kwa moja kero hizo ambazo zingine waliahidi kuzifanyia kazi kwa haraka.


Nae Bi. Salma Thabit Abdalah amesema kuwa wamefuatilia suala la Umeme kwa muda mrefu lakini wamekosq majibu hivyo amemuomba Mkuu wa Mkoa kutatua kero hiyo ili waweze kupata umeme sambamba na maji katika maeno yao.


Kwa upande wake, Khamis Athuman, kero yake kubwa shamba lake la mihogo kutolipwa fidia,ambalo ulipita mradi wa Serikali. 


"Wakazi bwimbwini' wataka Beach Kidimbwi ifungwee


"Viongozi Zanzibar wanafirigisa mambo kuonekana Rais hafai. Tumsaidie Rais kwa kuja kuchukua kero za huku chini, tunakupongeza Mkuu wa mkoa kwa kuja huku chini kutusikiliza" amesema Mwananchi huyo kufuatia mkutano huo


Hata hivyo akijibu baadhi ya kero, RC Ayoub amesema:


"Ipo tabia kwa baadhi ya watumishi wa sekta, kufanya kazi bila kutoa taarifa popote. Naomba nitoe maelekezo kwa viongozi wote waliopo kwenye maeneo yangu, wananchi kama wamekuja hawana taarifa muwafukuze.


Mtu akija kufanya kazi hizo zozote, kama hakuna taarifa mumfukuze 'Nikiwa kama mimi mkuu wa mkoa ni marufuku, lazima taratibu zifuate."Amesema RC Ayoub 


Akitolea ufafanuzi suala la eneo la mwekezaji wa ndani ambaye amejenga eneo la Bar na kulaza wageni pamoja na kupiga muziki,ambapo wananchi wamelipa eneo hilo kama 'Beach Kidimbwi ' ambapo amesema Serikali haikutoa kibali kufanya Bar ya kuuza vileo eneo hilo, bali Serikali ilitoa kibali 2022, kwa jina la 'Nice One beach resort' ikiwa kibali cha Mgahawa.


"Yanayotokea sasa kupiga muziki Bar, Nice one beach resort, naifunga rasmi,




Tumepata kero nyingi kwa wananchi vikao vya ndani na mkutano wa wazi, Kuuza madawa ya kulevya kama Unga, vilevi, biashara ya ukahaba mambo mengine huku ni kuvunja maadili, naenda kuufunga usiku jioni hii nikitoka hapa lengo kulinda maadili na kufuata misingi ya kisheria." Amesema RC Ayoub. 


Ziara hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo katika Shehia mbalimbali za Mkoa wa Kaskazini Unguja.