Tuesday, September 5, 2023

WAJUMBE AGRF WATEMBELEA BWAWA LA SAMAKI BAGAMOYO.

 

Na Mwandishi wetu- Bagamoyo.


Baadhi ya wajumbe wanaoshiriki Mkutano wa kimataifa wa jukwaa la mifumo ya chakula barani Afrika (AGRF)  wametembelea bwawa la ufagaji Samaki la TANLAPIA lililopo Bagamoyo mkoa wa Pwani, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mafunzo na kuangalia fursa mbalimbali zilizopo nchini kwenye sekta ya ufugaji na uvuvi.


 Wakiongea mara baada ya kujionea ufugaji wa Samaki kwa njia za kisasa unaofanywa na Kampuni ya TANLAPIA wilayani Bagamoyo wajumbe hao wamesema Tanzania ni miongoni mataifa ulimwenguni ambayo yana Ardhi inayokubali uwekezaji wa aina mbalimbali ikiwemo kilimo na mifugo.


Wameongeza kwa kusema kuwa, kupitia ziara hiyo wameweza kufahamu fursa mbalimbali zilizopo Tanzania ikiwemo kilimo na ufugaji.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanlapia, Baraka Kalangahe amesema wanaishukuru serikaki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa wawekezaji hali inayopelekea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.


Kalangahe ameongeza kwa kusema kuwa, bado sekta ya ufugaji Samaki nchini inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa chakula cha samaki kwakuwa asilimia kubwa ya chakula hicho kinaagizwa nje ya nchi.


Aidha ameiomba Serikali kuendelea kuwashawishi wawekezaji waweze kuwekeza kwenye uzalishaji wa chakula cha samaki ili iwe rahisi kwa wafugaji wa samaki kuhudumia samaki wao na hatimae kuwavuna kwa wakati unaostahili ili kuepuka hasara za uendeshaji zinzosababishwa na usumbufu wa kupata chakula hicho cha Samaki.


Wajumbe hao waliotembelea Bwawa la Samaki la Kampuni ya TANLAPIA Bagamoyo ni miongoni mwa wajumbe zaidi ya 3,000 kutoka nchi 70 Duniani, wanaoshiriki katika Mkutano wa siku nne wa Mifumo ya chakula  Afrika (AGRF) ambao unafanyika katika Ukumbi wa Kimatifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Sar es Salaam kuanzia Tarehe 05 hadi 08 Septemba 2023.



















Picha zote na Herry Pesa.

MAGAZETI YA LEO JUMANNE TAREHE 05 SEPTEMBA 2023.

 



















SERIKALI KUFANYA MABADILIKO MAKUBWA YA SHERIA YA UTUMISHI ILI KUWAPA KIPAUMBELE WANAOJITOLEA- KIKWETE.

 


Serikali inaendelea kufanya mapitio ya sheria ya utumishi ili kupata muarobaini wale wote wanaojitolea katika taasisi mbalimbali za umma. 


Hayo yameelezwa leo Jumatatu Septemba 04, 2023 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akijibu swali la Mbunge wa Kiteto Edward Kisau na wabunge wengine waliotaka kujua mpango wa serikali kuwaangalia wanaojitolea na namna ya kuwapa kipaumbele katika ajira. 


"Serikali kwasasa inafanya mapitio ya sheria ya utumishi wa umma Sura no. 298, sera ya Menejimenti ya ajira ya umma toleo la pili la 2008, kanuni ya utumishi wa umma ya 2022 na miongozo yake inayohusu masuala ya ajira. Katika kufanya mapitio haya ikibainika kigezo cha kujitolea kinatakiwa kuingizwa kwenye marekebisho ya sheria ya utumishi wa umma basi serikali italeta marekebisho ya muswada wa sheria hiyo bungeni."


Kikwete amesema kumekuwa na miongozo mbalimbali katika suala la kujitolea na ndiyo maana sasa serikali inafanya mapitio ya sheria na miongozo hiyo kuhusu suala la kujitolea, na pindi ikikamilika itafikishwa Bungeni ili wabunge watoe maoni yao kabla ya kuwa sheria. 

DKT. BITEKO AIKABIDHI OFISI YA WIZARA YA MADINI KWA MAVUNDE

 

Mavunde aainishiwa Vipaumbele vya Wizara ya Madini 2023/24


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amemkabidhi Ofisi ya Wizara ya Madini kwa Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ili aanze rasmi kazi ya kuiongoza Wizara hiyo muhimu.


Makabidhiano hayo mafupi yamefanyika Septemba 4, 2023 katika ofisi za wizara jijini Dodoma ambapo Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kumkabidhi Waziri Mavunde vipaumbele vya Wizara ya Madini katika Mwaka wa Fedha 2023/2024.


Vipaumbele hivyo ni Kuimarisha ukusanyaji wa Maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, kuendeleza madini muhimu na madini Mkakati, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini na kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini.


Aidha, uanzishwaji wa minada na Maonesho ya madini ya vito, kuwaendeleza na kusogeza huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo na kuzijengea taasisi uwezo zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.


Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kuwashuru uongozi na Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kwa ushirikiano mkubwa waliomuonesha katika kipindi chote akiwa wizarani.


Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesisitiza atatoa ushirikiano kwa watumishi wa Wizara ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.


Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemshukuru Dkt. Biteko kwa ushirikiano aliompatia katika kipindi walichofanya kazi pamoja na kumtakia Kheri katika majukumu yake mapya.


Akizungumza kwa niaba ya watumishi wote Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amemuhakikishia Waziri Biteko kuwa watumishi watampatia ushirikiano wa kutosha Waziri Mavunde katika kutekeleza majukumu yake.


Viongozi wengine walioshiriki katika Makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Wakuu wa Taasisi za Wizara na Watumishi.