Tuesday, August 22, 2023

STAMICO YAWA MKOMBOZI KWA WAZALISHAJI WA CHUMVI NCHINI.


 


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza kushughulikia changamoto za wazalishaji wa chumvi nchini kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa chumvi nchini kuwa wa tija na manufaa.


Hayo amesema Meneja Uwezeshaji uchimbaji mdogo Tuna Bandoma wakati wa Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji akizungumza katika Kongamano la Wadau wa Chumvi lililofanyika Agosti 21, mkoani Lindi.


“Mikakati iliyopo ni mahususi kwa ajili ya kuja na suluhisho ili kutatua changamoto zilizopo ambayo tumehusisha wadau, tunakua na uelewa wa pamoja katika kushughulikia changamoto za wazalishaji wa chumvi nchini, “ amesema Bando.


Aidha, amesema STAMICO inaendelea na hatua mbalimbali ikiwemo hatua za haraka za kiwanda cha kusafisha chumvi katika wilaya ya Kilwa na tayari Mkoa umeonesha eneo kwa ajili ya utekelezaji wa kujenga kituo hicho.


Ameongeza kuwa, katika shamba darasa la STAMICO wazalishaji wa chumvi watafundishwa namna mbalimbali ya kuyafikia masoko kupitia ubora ili kuzalisha chumvi iliyo bora kufikia masoko ndani na nje ili kuvutia wawekezaji


Mafunzo hayo ni moja ya utekelezaji wa kalenda ya mafunzo kwa wachimbaji wadogo inayofanywa na STAMICO. 


Awali Kongamano hilo na mafunzo ya wazalishaji chumvi lilifunguliwa na Mhe. Naibu Waziri wa Madini Dkt.Stephen Kiruswa Kwenye Viwanja vya kilimahewa Wilaya Ruangwa Mkoani Lindi. 






MAKAMU WA RAIS AWATAKA MA RC. NA RAS. KUZINGATIA MAADILI SEHEMU ZA KAZI.

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa kuzingatia maadili na nidhamu katika maeneo ya kazi ili kuwa picha nzuri na ya mfano kwa wengine.

 

Makamu wa Rais amesema hayo leo Tarehe 22 Agosti 2023 wakati akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliopo Kibaha Mkoani Pwani. Amesema ni lazima wakati wote wa uongozi kutafuta njia bora ya kuwashirikisha wengine ili msingi wa uongozi na utendaji uwe chachu zaidi kuleta maendeleo kwa wananchi.

 

Pia Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mikoa kuongeza jitihada kuiwezesha sekta binafsi ili iweze kukua, kushamiri na kuzalisha ajira kwa kuweka vivutio na mazingira mazuri ya uwekezaji. Amesema sekta binafsi inapaswa kuwa mshirika muhimu katika shughuli zote za maendeleo katika mikoa.

 

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema maudhui ya mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo yanalenga kuondoa matukio mbalimbali yanayotokana na mapungufu katika uongozi ikiwemo kutokuzingatia mipaka ya kiutendaji kati ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wao hususan katika matumizi ya fedha pamoja na kushindwa kudhibiti uvujaji wa siri za Serikali hususan katika zama hizi za utandawazi na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

 

Pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala kuzingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira hususani kutunza vyanzo vya maji, kufuatilia fursa mbalimbali zitokanazo na shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na biashara ya Kaboni na Uchumi wa Buluu. Amewataka kuhakikisha kunakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuepuka migogoro mbalimbali ndani ya jamii na kuzingatia changamoto zozote zinazojitokeza katika jamii zinashughulikiwa mapema na kwa ukamilifu.

 

Makamu wa Rais amesema dhima ya mafunzo hayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020, ambayo inaelekeza umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika hali iliyo shirikishi na yenye ubora. Ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa mafunzo hayo muhimu kwa viongozi

 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Angellah Kairuki amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea viongozi hao uwezo wa kuongoza na kusimamia wananchi, fedha na rasilimali zingine muhimu za taifa. Pia amesema mafunzo hayo yatawawezesha viongozi kuwa na maamuzi ya kimkakati pamoja na kuwawezesha kuwa na uwezo katika masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao.

 

Ameongeza kwamba katika siku sita za mafunzo jumla ya mada 20 zinatarajiwa kuwasilishwa kwa viongozi hao ambazo zitajikita katika masuala ya uongozi, usimamizi rasilimali, miongozo na taratibu mbalimbali za utendaji kazi serikalini, usimamizi miradi na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kukuza uchumi.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

20 Agosti 2023

Kibaha – Pwani.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka Saini katika kitabu cha wageni wakati alipowasili katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere – Kibaha Mkoani Pwani kufungua Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa leo tarehe 22 Agosti 2023.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere – Kibaha Mkoani Pwani. Tarehe 22 Agosti 2023.

 

BILIONI 19.5 KUTUMIKA KUBORESHA BANDARI YA BUKOBA.




 Na Alodia Babara- Bukoba. 

Bandari ya Bukoba inatarajia kutumia Sh19.5 bilioni kwa ajili ya kuiboresha na kuipanua kwa kujenga gati mpya, kuboresha magati yaliyokuwepo, ujenzi wa jengo la abiria na ujenzi wa maegesho ya magari.


Mkuu wa Bandari ya Bukoba Michael Palangyo akizungumza na waandishi wa habari jana Agosti 21,2023 amesema kuwa ujenzi huo umeanza toka Februari, 2023 ujenzi utakuwa wa mwaka mmoja na nusu hadi sasa ni miezi sita.


Alisema tayari mkandarasi ameishafanya kazi takribani asilimia 13, na ujenzi utakamilika Julai 2024 ma utagharimu Sh19.5 bilioni hadi kukamilika kwake.


"Ujenzi huu umeanza toka Februari, 2023 utachukua mwaka mmoja na nusu,  hadi sasa ni miezi sita, mkandarasi ameishafanya kazi takribani asilimia 13 na ujenzi utakamilika Julai 2024 hadi kukamilika kwake utagharimu Sh19.5 bilioni" amesema Palangyo 


Palangyo amesema, upanuzi na uboreshaji wa Bandari unahusisha ujenzi wa gati jipya na kuboresha yaliyopo, ujenzi wa jengo la abiria, ujenzi wa miundombinu ya umeme na maji ya mvua na maegesho ya magari.


Ameeleza kwamba, ujenzi wa Bandari hiyo si tu ni kwa ajili ya kupokea meli kubwa ya Mv Mwanza hapa kazi tu bali ni sehemu ya kuboresha mazingira kwani yamebadilika.


Aliongeza kwa kusema kuwa, toka ilipojengwa Bandari hiyo mwaka 1945 kumekuwa na maboresho madogo madogo lakini kwa sasa hayo ni maboresho makubwa na ni sehemu ya kuboresha huduma kwa wananchi.


Aidha wajumbe wa bodi ya Wakala wa huduma za meli TASAC wametembelea Bandari ya Bukoba, Kemondo na kiwanda cha kuchakata minofu ya sangara kilichopo Bukoba, huku mjumbe wa bodi hiyo King Chiragi akieleza lengo la ziara hiyo kuwa ni kubaini changamoto zinazokabili usafiri wa majini na kuzitafutia ufumbuzi na mwisho wa siku usafiri wa majini uwe salama na Bandari na mialo zifanye kazi zao kwa ufanisi.


Mmoja wa wananchi Adelina Kubalyenda amesena uboreshaji wa Bandari hiyo utasaidia abiria kupata jengo la kupumzika na kuondoa changamoto hiyo na upanuzi utasaidia kuwepo mzunguko wa fedha baada ya kuongezeka meli na vyombo vingine vya majini.




Pichani ni shughuli za ukarabati na upanuzi wa Bandari ya Bukoba zikiendelea.


BAGAMOYO: WANANCHI KWA USHIRIKIANO NA HALMASHAURI YA KIJIJI WAKABIDHI MADAWATI SHULE YA MSINGI KIDOMOLE.


 Wananchi kwa kushikiriana na Halmshauri ya Kijiji cha Kidomole wilayani Bagamoyo wamejitolea kutengeneza Madawati thelasini na tano (35) na kukabidhi kwa Shule ya Msingi Kidomole.


Akikabidhi madawati hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Afisa Elimu Awali na Msingi Bi Wema Kajigiri aliwashukuru wananchi hao kwa msaada huo kwani changamoto ya madawati imekuwa ikiikabili shule hiyo kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidomole Bw. Mrisho Saidi Some amewashukuru wananachi wake kwa kufanikisha upatikanaji wa madawati hayo.




MAGAZETI YA LEO JUMANNE TAREHE 22 AGOSTI 2023.

 

























𝗕𝗔𝗕𝗔 𝗔𝗦𝗞𝗢𝗙𝗨 𝗦𝗛𝗢𝗢 𝗔𝗠𝗘𝗧𝗨𝗙𝗨𝗡𝗨𝗟𝗜𝗔 𝗞𝗜𝗧𝗨 𝗙𝗨𝗟𝗔𝗡𝗜 𝗞𝗨𝗛𝗨𝗦𝗨 𝗗𝗣 𝗪𝗢𝗥𝗟𝗗

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo kutoka Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Fredrick Shoo ikiwa ni kwa ajili ya jitihada zake za kuleta Maendeleo nchini wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 ya  Kanisa hilo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Mfuko wa Wastaafu Mkoani Arusha tarehe 21 Agosti, 2023

..........................

Na Abbas Mwalimu

Jumatatu tarehe 21 Agosti 2023

Miongoni mwa mambo yaliyosubiriwa kwa hamu kubwa katika siku ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) ni hotuba ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo.

Hotuba ya Baba Askofu Shoo ilijaa hekima, maarifa na falsafa kubwa kiasi kwamba ilihitaji utulivu wa hali ya juu kuweza kumuelewa.

Baba Askofu alisema na hapa ninamnukuu:

"Lipo hili la DP World Mheshimiwa. Kwanza naomba tu ieleweke wazi kwamba kanisa linaunga mkono uwekezaji. Hatupingi uwekezaji Mheshimiwa Rais, na tunajua, wewe, kwenye nia yako unataka wawekezaji.

Hata hivyo, jambo hili limekuwa na maoni mbalimbali ya wananchi na vyombo vya habari, viongozi wa dini zote, kwenye vyombo vya habari, kwenye mitandao n.k tumeona maoni mbalimbali.

Lakini Mheshimiwa Rais unatambua kwamba sisi viongozi wa dini zote, kwa uwakilishi, tuliomba kuja kukuona. Pale mwanzoni kabisa mwa jambo hili, na kwa uungwana wako, na kwa unyenyekevu ulio nao, utayari wa kusikiliza, Mheshimiwa Rais ulitupokea na tulikuletea maoni yetu kama taasisi na viongozi wakuu wa dini katika nchi yetu ya Tanzania.

Madhehebu yote ya kikristo, tukiwa CCT, tukiwa TEC, tukiwa Bakwata.

Mimi nakumbuka jinsi ulivyotupokea, ukatusikiliza, ukapokea maoni yetu na ushauri wetu viongozi wa dini na ukaahidi kuwa maoni na ushauri huo utayapeleka kwa wataalamu na kufanyiwa kazi kwa uzito unaostahili kwa maslahi mapana ya taifa.

Tuna imani na wewe Mheshimiwa Rais. Tunakuamini Mheshimiwa Rais na tunaamini kwamba ukisema, taasisi zako na vyombo vyako vitafanyia kazi jambo hili, unamaanisha hivyo.

Sasa najua, katika jambo hili tunaelekea mahali ambapo tunataka kugawanyika kabisa, na wengine wanatumia sababu za kidini, wengine maslahi yao ya kisiasa, na wengine kiuchumi.

Tunashukuru Mungu amekujaalia hekima katika hili, kama mama na kiongozi, umekaa kimya. Na kimya chako hiki Mheshimiwa Rais siyo kwamba hulifanyii kazi.

Mimi nasema jambo hili linahitaji hekima kubwa ya kuliendea na sisi kama tulivyosema tunaendelea kukuombea kwa Mungu ili hekima yote itumike katika kuweza kuleta muafaka wa jambo hili pasipo kuwagawanya au wananchi kugawanyika na kutumika kama kitu cha kuchochea wananchi kwa watu wenye malengo yao mengine. Mheshimiwa Rais, kanisa liko pamoja nawe." Mwisho wa kunukuu.

Baada ya kumaliza kusoma hotuba yake Askofu Mkuu Dkt. Fredrick Shoo alimkaribisha Mgeni Rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhutubia wahudhuriaji.

Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais alisema na hapa ninamnukuu:

"Ndugu zangu na hasa kaka yangu, Baba Askofu Shoo, nimeyasikia yote uliyosema kuhusu usalama, amani, umoja na muendelezo wa taifa letu.

Niliamua kunyamaza kimya na naendelea kunyamaza kimya.

Ninachotaka kuwahakikishia, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa taifa hili.

Hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuuza taifa hili.

Hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye taifa hili.

Sasa hayo itoshe kuwa ni ujumbe wangu kwenu. Asanteni sana!" Mwisho wa kunukuu.

Hotuba hizi mbili, ile ya kwanza ya Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Fredrick Shoo na ile ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan zinabainishia mambo yafuatayo:

(i) Kwamba, KKKT inaunga mkono uwekezaji ukiwemo wa DP World. Lakini ni muhimu kwa serikali kuzingatia ushauri na maoni yanayotolewa na wadau mbalimbali juu ya uendeshaji wa bandari hiyo.

(ii) Kwamba, viongozi wa madhehebu yote ya dini nchini walikwenda Ikulu na kukutana na Mheshimiwa Rais na kutoa maoni na ushauri wao juu ya uendeshaji wa bandari na serikali ikayapokea na kuwaeleza viongozi hao kuwa yatafanyiwa kazi.

(iii) Kwamba, Mheshimiwa Rais ameyapokea maoni na ushauri uliotolewa na viongozi wa dini na amewapa wataalamu kuchakata maoni na ushauri huo ndiyo maana amekaa kimya akisubiri wataalamu wamalize wampe mapendekezo awaite viongozi wa dini awape mrejesho.

(iv) Kwamba, wapo watu wanaotumia suala la DP World kwa mrengo wa kidini, wengine wakitumia hilo kama kete ya kisiasa ya kupata uungwaji mkono na wengine kujiunufaisha kiuchumi pasina kujali athari zinazoweza kutokea kwenye nchi.

(v) Kwamba, wapo watu wanaotumia suala la DP World, si kwa maslahi ya taifa bali kwa lengo la kuvuruga amani na kuleta machafuko nchini ndiyo maana Mheshimiwa Rais alionya kwamba, hakuna mwenye ubavu wa kuligawa taifa wala kuharibu amani na usalama uliopo au kuliuza taifa kwa gharama yoyote ile.

Aidha, hotuba hizi mbili, ya Askofu Shoo na ya Mheshimiwa Rais Samia zinatupa maswali kadhaa ya kujiuliza kutokana na Tamko la TEC lililotolewa Ijumaa Agosti 18 2023.

(a) Kama viongozi wa TEC walikuwa miongoni mwa viongozi wa dini walioenda Ikulu kutoa maoni na ushauri, kwa nini wasingesubiri kuona kama maoni na ushauri wao umefanyiwa kazi au lah kabla ya kutoa Tamko?

(b) Kama TEC waliamua kutoa Tamko, ina maana kuwa hawamuamini Mheshimiwa Rais kuwa atafanyia kazi maoni na ushauri waliotoa? Tukumbuke Baba Askofu Dkt. Shoo yeye alisisitiza kuwa KKKT lina imani na Rais hivyo wanaamini atayafanyia kazi maoni na ushauri waliotoa, vipi kwa TEC?

(c) Tamko la TEC lilieleza kwamba TEC imefuatilia kwa umakini mijadala, maoni, mapendekezo na vilio vya wananchi walio wengi ambao ni wamiliki wa bandari na rasilimali zote na wametambua kuwa wananchi walio wengi hawautaki Mkataba wa DP World, je maoni waliyotoa kwa Rais hayakuwa na tija?

(d) Kwa nini TEC hawakukutana na viongozi wenzao wa dini kama awali na kuwaeleza kubadilika kwa msimamo wao kama ambavyo walikutana hapo awali na kwenda kwa Rais kutoa maoni na ushauri wao?

(e) Tamko la TEC limeweka msimamo kuwa wao hawaungi mkono Mkataba wa DP World ilhali KKKT wameweka wazi kuwa wanaunga mkono uwekezaji ukiwemo wa DP World kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa dini. Je, itakuwaje kama Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na viongozi hao wakiwemo wa TEC na makubaliano kuendelea hatua nyingine?

Mtazamo wangu usio na tija:

Suala si bandari, suala ni uchaguzi wa 2025.

Dini zinatumiwa kama mwamvuli na baadhi ya wanasiasa kutafutia huruma (appealing to sympathy/pity).

Nyoka aliye ndani ya nyumba anahitaji hekima kubwa kama aliyosema Baba Askofu Dkt. Shoo kumtoa la sivyo utavunja vyombo na kupata hasara au atakugonga au kukurushia mate ya sumu.

Kuna nyoka pahala. Lipo tatizo pahala. Umakini , weledi na hekima vinahitajika.

Asanteni:

Wenu:

Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse|LinkedIn|Threads)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp).


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya Wazee waanzilishi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwenye Maadhimisho ya miaka 60 ya  Kanisa hilo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Mfuko wa Wastaafu Mkoani Arusha tarehe 21 Agosti, 2023. Kushoto Mzee Johansen Rutabingwa, na wa pili kulia Mchungaji Elirehema Philip Mwanga



Monday, August 21, 2023

TANZANIA KUWA KITOVU CHA UCHAKATAJI MADINI BARANI AFRIKA - DKT. KIRUSWA

 

Dkt. Kiruswa Afungua Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Lindi


Ruangwa - Lindi


Imeelezwa kuwa, Serikali inaandaa Mkakati wa kuwezesha uongezaji thamani madini kwa lengo la kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na madini utakaopelekea Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa wakati akifungua rasmi Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji yanayokwenda sanjari na Kongamano la Wadau wa Madini ya Chumvi Mkoani Lindi leo Agosti 21, 2023


"Serikali inaendelea kuhimiza uongezaji thamani madini nchini ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na madini. Katika kuhakikisha kuwa kusudio hilo linafikiwa, nawaomba wawekezaji kuendelea kuwekeza katika viwanda vya uongezaji thamani madini," amesema Dkt. Kiruswa

 

Aidha amesema, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini ili kuvutia mitaji kutoka ndani na nje ya nchi, amesema katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kufanya mapitio ya Sera mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji, Viwanda na Biashara nchini.


"Ninapenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wadau wote wakiwemo washirika wetu wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi, napenda pia kuwashukuru washiriki wote mliotoka sehemu mbalimbali mliojumuika na wananchi wa Mkoa wa Lindi hii leo, hakika uwepo wenu unadhihirisha umuhimu wa maonesho haya kwamba sio tu kwa watu wa Lindi bali ni dhamira ya Serikali yetu ambayo ina nia kubwa ya kuendelea kuona Mkoa wa Lindi na Mikoa mingine ya Ukanda huu wa Kusini inafunguliwa kiuchumi," amesema Dkt. Kiruswa


Vile vile, Serikali itaendeleza jitihada za kujenga na kuimarisha misingi thabiti ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na ujenzi wa viwanda kama ilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainabu Telack amesema kuwa kupitia maonesho haya wawekezaji wanajionea fursa mbalimbali za rasilimali madini ikiwa pamoja na kutangaza fursa nyingine za kiuchumi zinazopatikana mkoani Lindi.


Kaulimbiu ya maonesho hayo ni *"Wekeza Lindi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Maendeleo ya Jamii"*. Maonesho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini waliopo ndani na nje ya nchi yanayoendelea hadi Agosti 26 mkoani Lindi.