Thursday, August 17, 2023

MKUU WA CHUO IJA AWATAKA MAHAKIMU WAKAZI WAPYA KUWA WANYENYEKEVU


 Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewataka Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za mwanzo kuwa wanyenyekevu ili iwasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Kihwelo ameyasema hayo alipozungumza na Wahe. Mahakimu hao wanaoendelea kupatiwa Mafunzo Elekezi ya siku tano hapa IJA Lushoto mkoani Tanga.

Katika nasaha zake, Mhe. Jaji Kihwelo amesema: " Ushauri wangu kwenu nyote, be humble (kuweni wanyenyekevu), hii itawasaidia sana katika maisha yenu, msiwe watu wa kujikweza sana."


Vilevile, Mhe. Kihwelo amewataka Mahakimu hao kufanya kazi kwa kushirikiana miongoni mwao pamoja na Taasisi zingine zikiwemo za Serikali katika namna ambayo haitaathiri majukumu yao.


Kwa upande mwingine, Mhe. Dkt. Kihwelo amewashauri Mahakimu hao kila mmoja kumtegemea Mwenyezi Mungu kulingana na imani yake ili imsaidie katika utoaji wa maamuzi.


Aidha Mhe. Dkt Kihwelo ametoa wito kwa washiriki hao kujitahidi kusoma sana kwa minajili ya kujiongezea maarifa huku akibainisha kuwa maarifa ni nguvu.


Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA),


yalifunguliwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma mnamo Agosti 14, 2023 na yatamalizika Agosti 18, 2023

MAGAZETI YA LEO TAREHE 17 AGOSTI 2023.


























 

Wednesday, August 16, 2023

UKUSANYAJI MAPATO BAGAMOYO WAONGEZEKA.

 


Na Mwandishi wetu- Bagamoyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bi, Halima Okash ameipongeza Halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze kwa kuongeza ukusanyaji wa Mapato kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika kikao cha Ushauri Wilaya kilicho fanyika ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo leo tarehe 16 Agosti 2023.


Pamoja na pongezi hizo Mhe, Okash amewataka Viongozi wa Halmashauri kuwa wabunifu katika kuibua vyanzo vya mapato na kutengeneza mikakati kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani kwakuzingatia haki na usawa.


”Bila mapato hakuna Halmashauri tunategemea mapato katika kujenga Hospitali, Shule, Barabara, na kusambaza huduma nyingine za kijamii ikiwemo maji, umeme”.Alisema Mhe, Okash.


Pia amewataka Maafisa Tarafa, Kata na Vijiji kuvumbua vyanzo vya mapato vitakavyo saidia kukuza na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao, vilevile amewaomba Maafisa hao kuhakikisha wanatatua kero za Wananchi hivyo kuwafanya wananchi hao kuwa huru na kuweza kuendelea na shughuli zao za maendeleo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe, Mohamed Usinga, ameziomba taasisi zilizopo Wilaya ya Bagamoyo ikiwemo TANESCO na DAWASA kushirikiana na Halmashauri kutekeleza kwa vitendo katika kutengeneza na kuboresha Miradi inayoendelea.


”Naziomba Taasisi zote ziboreshe ushirikiano na Halmashauri ili tuweze kutekeleza miradi pomoja na shughuli zote za kijamii zinazoendelea katika Wilaya yetu kwa kufanya hivyo mambo yetu yatakwenda vizuri na kwa wakati ili tuweze kuendana na kasi ya Mhe.Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan”.







TFS YAPANDISHA HADHI MISITU 15 KUWA HIFADHI YA TAIFA KUTUMIKA KWENYE UTALII NA UWEKEZAJI

 


Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS), Prof.Dos Santos Silayo, akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari leo Agosti 16,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo na Mwelekeo wa utekelezaji  kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

...................

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAKALA wa Misitu Tanzania( TFS ) umefanikiwa kupandisha hadhi Misitu ya hifadhi 15 kuwa Misitu ya hifadhi ya Taifa na Misitu ya hifadhi za mazingira asilia mitano 5 yenye ukubwa wa hekta 58,216 katika kipindi Cha Mwaka 2022/2023 ambapo Upandishaji hadhi huo,utafanya Misitu hiyo kutumiwa kwa shughuli za utalii na uwekezaji.


Hayo yamesemwa leo Agosti 16,2023 jijini Dodoma na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS), Prof.Dos Santos Silayo,wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo na Mwelekeo wa utekelezaji  kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.


Prof. Dos Santos, ameitaja Misitu hiyo kuwa  ni; Kindoroko (Mwanga), Nou (Mbulu/Babati), Uvinza (Uvinza), East Matogoro (Songea) na Hassama Hill (Mbulu). 


Kamishna huyo ameeleza kuwa kufuatia juhudi za serikali ikiwemo ubunifu wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuandaa filamu ya “Tanzania the Royal Tour” ambayo imeitangaza Tanzania  ndani na nje ya nchi kwa kiasi kikubwa, TFS imejipanga kutumia fursa hiyo kuongeza tija katika uhifadhi, utalii na ukusanyaji maduhuli.


“Juhudi  hizo zimesaidia  kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia ambapo hadi kufikia Juni 2023 jumla ya watalii 242,824 walitembelea vivutio hivyo,”alisema


“Idadi hii ni ongezeko la asilimia 60.8 ukilinganisha na watalii 152,002 waliotembelea vivutio hivyo kwa kipindi hicho kwa mwaka 2021. Jumla ya sh.bilioni  1.3  zilikusanywa ikilinganishwa na sh.milioni 603.3 zilizokusanywa mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la Asilimia 126.9.”


Amebainisha  kuwa :”Katika kipindi cha miaka miwili TFS imeanzisha shamba jipya moja la Makere Kasulu-Kigoma, na kufanya upanuzi wa mashamba mawili,


Katika hatua nyingine, profesa Silayo amesema katika mwaka wa fedha uliopita, TFS ilizalisha jumla ya tani 25.9 za mbegu za miti na kuotesha miche  milioni 32.7 ya aina mbalimbali ambayo ilipandwa katika mashamba 24 ya serikali na mingine kugawiwa kwa watu binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kupandwa katika maeneo yao.

Amesema  kuwa hadi sasa, TFS imepanda miti katika hekta 6,909 na kurudishia miti iliyokufa kwenye hekta 2,434 pamoja na kuendeleza mashamba ya miti kwa kupalilia hekta 31,197, kupogolea hekta 8,353 na kupunguzia miti kwenye hekta 2,785.

”Wakala umeandaa mkakati wa usimamizi na uendelezaji wa mashamba ya miti ya serikali wa miaka 30 kuanzia 2021 – 2050  ambao umelenga kupanua wigo wa aina ya miti ikiwemo ile ya madawa kama vile Prunus africana na mpira . 


Miti hii imeanza kupandwa katika mashamba ya Mbizi, Wino, Rongai, Saohill, Iyondo Mswima, Meru na Shume,”ameeleza




DC. BAGAMOYO AHIMIZA WATENDAJI KUIMARISHA UTALII.

 


Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya ushauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Halima Okash, amewaagiza Watendaji wa Idara na taasisi mbalimbali zilizopo kwenye wilaya hiyo kuweka mkazo kwenye suala la utalii ndani ya wilaya hiyo.


Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya kilichofanyika leo tarehe 16 Agosti 2023 katika ukumbi wa Halmshauri ya Wilaya ya Bagamoyo na kuwahusisha Wenyeviti, Wakurugenzi na Watumishi wa idara mbalimbali katika halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze, Bi. Halima amewataka wajumbe wa kikao hicho kuwa mabalozi wa utalii katika idara zao na taasisi wanazotoka.


"Hili ni agizo nawaomba wakuu wa idara kuandaa utaratibu kwa watumishi waliopo kwenye idara zenu kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika halmshauri zetu" ameagiza, Bi. Halima.


Amewasisitiza maafisa elimu kuhakikisha kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanatembelea na kuvielewa vivutio mbalimbali vya utalii vilivyomo katika wilaya ya Bagamoyo.


"Niwaombe Maafisa Elimu kuandaa utaratibu mzuri kwa wanafunzi wa shule zetu zilizopo wilaya ya Bagamoyo kutembelea vivutio vyetu vya utalii kwa kufanya hivyo tutaongeza ufahamu na kuvitangaza kirahisi hivyo kuwa na ongezeko la watalii litakalopelekea kukua kwa mapato kupitia sekta hii" aliongeza Bi. Halima.


Wilaya ya Bagamoyo imekuwa na vivutio mbalimbali vya utalii kama vile Mbunga ya Saadan ambayo ni mbuga pekee nchini inayopakana na fukwe za bahari, mji mkongwe wa kaole, fukwe tulivu zenye mandhari ya kuvutia za bahari ya hindi, na soko la watumwa.


Aidha Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati mbalimbali ya kukuza utalii hapa nchini kwakua utalii ni sekta inayoingiza fedha nyingi zinazosaidia kujengwa kwa miradi mbalimbali kwenye jamii.






MAKAMU WA RAIS, DKT. MPANGO AWASILI NCHINI ANGOLA.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 16 Agosti 2023 amewasili Jijini Luanda nchini Angola ambapo anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 17 Agosti 2023.



Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Umuhimu wa Rasilimali Fedha na Rasilimali Watu katika kuendeleza Viwanda na Uchumi” utajadili masuala mbalimbali yahusuyo Jumuiya hiyo.



Aidha, Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali umetanguliwa na mkutano wa Kamati ya Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 13–14 Agosti 2023.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango tarehe 16 Agosti 2023 akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa 4 De Fevereiro Jijini Luanda nchini Angola ambapo anatarajia kumwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 17 Agosti 2023.





DKT. BITEKO AWATAKA WAFANYABIASHARA WA MADINI KUREJESHA FEDHA ZA KIGENI BAADA YA MAUZO


 

Wauza Nje Madini ya Thamani ya Shilingi Trilioni 2.24

Katibu Mkuu Mahimbali Aunda Timu ya Wataalam 9 Kutathmini Biashara ya Madini Nje

Dodoma

Wafanyabiashara wa Madini wametakiwa kuhakikisha wanarejesha nchini fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya madini nje ya nchi ili zisaidie kuimarisha uchumi wa nchi.


Hayo yamebainishwa Agosti 16, 2023 jijini Dodoma na Waziri wa Madini Dkt.Doto Biteko wakati wa kikao chake na wafanyabiashara hao kutoka nchi nzima na kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi wa Wizara na Taasisi zake, Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Maafisa Madini Wakazi kutoka mikoa mbalimbali nchini.


Ameongeza kwamba, Sekta ya madini nchini imetawaliwa na uwekezaji wa mitaji kutoka nje ya nchi ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 5.1 cha Sera ya madini kinasisitiza ustawi wa masuala ya kiuchumi ikiwemo ustawi wa huduma za benki nchini ili kuleta manufaa kwa Serikali na sekta binafsi.


Amesema kutokana na kifungu hicho, wizara ingependa kuona fedha za mauzo ya madini zinarejeshwa nchini kama Sheria inavyoelekeza kupitia mifumo ya kibenki na kwa kuzingatia sheria zote za nchi na kuongeza kwamba, hayo yote yanalenga kuboresha shughuli za madini nchini kutokana na umuhimu wa Sekta hiyo kiuchumi.


Pia, Dkt. Biteko ametumia jukwaa hilo kuwapongeza wafanyabiashara hao kwa mchango wao mkubwa ulioiwezesha Sekta ya Madini kuwa kinara katika kuliingizia taifa fedha za kigeni na kueleza kuwa, mwaka 2022 madini yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 3,395.3 yaliuzwa nje ya nchi sawa na asilimia 56 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi. ‘’ Mauzo hayo ni ongezeko la asilimia 9 ikilinganishwa na mauzo ya Dola za Marekani milioni 3,116.40 mwaka 2021,’’ amesema Biteko.


Vilevile, Dkt. Biteko ametambua mchango wa wafanyabiashara hao kupitia Masoko ya Madini na kusema, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/23 Julai 2022 hadi Juni 2023, waliweza kuuza madini nje ya nchi yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.24.


‘’Katika kipindi hicho, Serikali ilikusanya kiasi cha Shilingi bilioni 157.44 kama malipo ya mrabaha na ada ya ukaguzi, sawa na asilimia 25 ya mrabaha uliokusanywa kwa madini yote. Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa mchango wenu huo,’’ amesema Dkt. Biteko.


Amesema pamoja na mafanikio hayo, kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara wa madini kuuza madini yao nje ya nchi bila kurejesha fedha za mauzo kwenye benki za hapa nchini na kueleza kwamba, Mwaka wa Fedha wa 2022/23 wafanyabiashara wa madini kupitia kampuni zao walisafirisha nje ya nchi jumla ya madini yenye thamani ya Dola za Marekani 952,926,784.


Amefafanua kwamba, bado kiwango cha fedha za kigeni kinachoingia hakilingani na thamani ya madini yanayouzwa na kuwataka kutumia kikao hicho kujitathmini na kueleza wizara kuwa, inataka kuongeza mchango wa fedha za kigeni unaotokana na Sekta ya Madini.


‘’Wizara ya Madini imeandaa mpango mkakati wa kuongeza mauzo ya madini nje ya nchi. Mpango huo utahakikisha kuwa Sekta ya Madini inaendelea kuwa ni miongoni mwa Sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika kuingiza fedha za kigeni nchini. Tunataka mlete fedha za kigeni, hakuna mtu atakayechukua hela yako tunachotaka Sekta ya Madini iwezeshe kununua bidhaa nyingine muhimu, tupate fedha za kigeni za kutosha kukuza uchumi wetu,’’ amesisitiza Biteko.


Awali, akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema kikao hicho kimelenga kujadili mwenendo mzima wa biashara ya madini.


Vilevile, amesema Wizara imepunguza idadi ya leseni za wafanyabiashara wa madini kutoka 700 hadi 150 ili kubaki na wafanyabiashara wachache wanaokidhi vigezo.


Aidha, akihitimisha kikao hicho, Katibu Mkuu ameitaja timu ya wataalamu 9 kutoka upande wa Serikali ikiwemo Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Wizara ya Fedha, Benki Kuu Tanzania, na Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) kwa ajili ya kutathmini mwenendo wa biashara ya madini nje ya nchi.


Kwa upande wake, Katibu wa TAMIDA Leopold Kimaro ameishauri Serikali kuangalia masuala mbalimbali ikiwemo utoaji leseni kwa wafanyabiashara wa madini na kuongeza kwamba, chama hicho kiko tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha suala hilo la mwenendo wa biashara ya madini yanayouzwa nchi ya nchi linafanyiwa kazi.








HAWAKUKAMATWA KWA KUKOSOA MKATABA WA BANDARI" WAZIRI NAPE

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Balozi Mstaafu Dkt. Willibrod Slaa, Mpaluka Nyangali maarufu Mdude na wakili Boniface Mwabukusi wamekamatwa kwa tuhuma za uhaini na sio kutokana na wao kukosoa mkataba wa uwekezaji bandarini kama inavyopotoshwa.


Kupitia taarifa aliyoitoa katika ukurasa wake wa mtandao wa twitter, Waziri Nape amesema, hakuna mtu yeyote ambaye amekamatwa wala hatakamatwa kwa kukosoa tu mkataba wa bandari au mradi, mpango, mpango au sera yoyote ya serikali.


Vilevile amesema, kauli kuhusu kukamatwa kwa watu hao zimechanganya mambo mawili tofauti ambayo ni mjadala wa kitaifa unaoendelea kwa uwazi kwa sasa nchini Tanzania kuhusu mapendekezo ya uwekezaji wa bandari kwa upande mmoja, na suala la sheria kwa upande mwingine.


Akielezea uhalisia wa kukamatwa kwa watatu hao Waziri Nape amesema,


"Watu hao watatu walikamatwa na polisi kwa kutoa vitisho vya uhalifu hadharani, ambavyo ni pamoja na kutaka kupinduliwa kwa nguvu kwa serikali. Watuhumiwa hao ambao baadhi yao walitaka hadharani kuhamasisha wananchi kubeba silaha dhidi ya jeshi la polisi Tanzania, walikamatwa ili kutuma ujumbe mahususi wa kuwazuia wahalifu wengine kufanya makosa ya jinai"


Kufuatia hilo Waziri Nape amebainisha kuwa,


Kukamatwa kwao hakuzuii kwa vyovyote vile uhuru wa kujieleza nchini Tanzania, bali ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ili kuzuia machafuko ya kijamii yanayoweza kutokea kutokana na wito wa uasi dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.


Akizungumzia moja ya kauli za Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu kuhusu sakata la kukamatwa kwa watu hao, Waziri Nape ameeleza.


"Moja ya kauli za hivi majuzi zaidi kutoka kwa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu limeamua kupotosha ukweli kwa nia mbaya kwa kudai kimakosa kwamba washukiwa walikamatwa kwa kukosoa tu mpango wa bandari kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)" alisema Waziri Nape na kuongeza kuwa.


"Watu binafsi, makundi, asasi za kiraia, wanataaluma, vyombo vya habari, viongozi wa dini, vyama vya siasa na taasisi wanaendelea kujadili kwa uhuru masuala ya kitaifa na kukosoa msimamo wa Serikali bila vitisho wala kukamatwa. Hivi sasa vyama vya upinzani vinafanya mikutano ya hadhara kwa uhuru nchini kote kukosoa mkataba wa bandari na sera nyingine za Serikali jambo ambalo hawakuweza kulifanya miaka michache iliyopita kabla ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani"


Tangu kukamatwa kwa Balozi Dkt. Wilbrod, Mdude Nyagali na Wakili Boniface Mwabukusi watu mbalimbali wamekoa wakitoa maoni yao kuhusu sakata la kukamatwa kwao, miongoni mwao ni wadau wa haki za binadamu ambao wamelitaka jeshi la polisi kuwaachia kwa kile kilichodaiwa kuhusianishwa na ukosoaji wao katika mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA).

JUKWAA LA WAHARIRI LALAANI KUSHABULIWA WAANDISHI WA HABARI NGORONGORO