Mkuu
wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallaah (katikati) akizungumza na waandishi wahabari (hawapo pichani) kuhusu Tamashala la 40 Kimataifa la Sanaa na Utamaduni litakalofunguliwa rasmi siku ya Alhamisi tarehe 28 oktoba 2021, wa tatu kushoto ni
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Dkt. Herbert
Francis Makoye.
...................................................................
Mkuu wa
wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallaah, amewakaribisha wananchi ndani na nje ya
Bagamoyo kuhudhuria Tamasha la 40 la kimataifa la sanaa na Utamaduni litakalofanyika
katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) siku ya tarehe 28 Oktoba 2021 hadi 30 Oktoba 2021.
Akizungumza
na waandishi wa Habari katika Mkutano uliofanyika ukumbi wa TaSUBa, Mkuu huyo
wa wilaya ya Bagamoyo amesema Tamasha hilo la kimataifa la sanaa na utamaduni
ni fursa ya kipekee kwa wasanii kuonyesha kazi zao mbele ya wageni
watakaohudhuria hilo.
Alisema katika
Tamasha hilo zipo fursa nyingi kwa wasanii, wananchi wa kawaida pamoja na
serikali kwa ujumla.
Akifafanua zaidi
DC. Zainab alisema kwa wasanii ni fursa ya kuonyesha kazi zao kwa waliohudhuria
wakiwemo wageni kutoka nje ya nchi na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na
wadau wa sanaa na utamaduni.
Aidha alisema
wananchi wanaweza kutumia fursa hiyo ya Tamasha kujifunza namna sanaa inayoweza
kumuinua kijana wa kitanzania na kumfanya sio tu mtoa burudani kwa jamii lakini
pia ikampatia kipato kwaajili ya kuendesha maisha yake.
Aliongeza kwa
kusema kuwa, Serikali pia itatumia fursa hiyo ya Tamasha la sanaa kutangaza
vivutio vilivyopo Bagamoyo ambapo wageni watweza kujionea maeneo mbalimbali ya
kihistoria yaliyopo ndani ya Bagamoyo na hivyo watakapoweza kutembelea vivutio
hivyo serikali itaingiza mapato kupitia watalii hao.
Alisema
kutokana na umuhimu wa Tamasha hilo kwa wageni kutoka nje ya Bagamoyo na nje ya
Tanzania kutakuwa na punguzo maalum la bei katika hoteli zote za Bagamoyo ili
kuwarahisishia wageni kupata sehemu za kulala kwa gharama nafuu.
Mkuu huyo wa
wilaya amesema kutokana na mapambano dhidi ya ugonjwa Corona, kama wilaya
itatumika nafasi hiyo kuweka banda maalum lakupata chanjo ya uviko19, kwa wale
ambao bado hawajapa chanjo hiyo ili iwe rahisi kwao kuchanja huku wakiendelea na burudani kwa siku zote tatu za Tamasha hilo.
Wakati
huohuo, Mkuu huyo wa wilaya ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama wilaya, amewahakikishia wageni wote wilayani humo kuwa, wilaya ya
Bagamoyo ipo salama na kwamba wataweza kutembea maeneo mbalimbali ya wilaya
hiyo bila ya bghudha ya aina yoyote.
Alisema
wilaya ya Bagamoyo ni tulivu na haina vitendo vyovyote vya uhalifu na kwamba
ulinzi utaimarishwa zaidi siku za Tamasha.
Kwa upande wake
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Dkt. Herbert
Francis Makoye, alisema wanajinia kuendelea kuandaa matamasha kila mwaka ndani
ya chuo hicho tamasha la mwaka huu ni la 40.
Alisema yapo matamasha mengi yanaanzishwa hapa
nchini lakini hayana muendelezo kwa TaSUBa kuendelea kuandaa Tamasha kila mwaka
ni mafanikio makubwa ya kujivunia ndani ya chuo, kwa viongozi wa wilaya, wizara
na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Makoye alisema Tamasha la Kimataifa la Sanaa
na Utamaduni Bagamoyo hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) chini ya Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo
likiwa na malengo ya
· Kutunza
na kuenzi sanaa na utamaduni wa mtanzania.
· Kutengeneza
jukwaa ambalo wanafunzi wa TaSUBa wanalitumia kupima viwango vyao vya umahiri
katika sanaa kwa mwaka katikia fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi.
· Kukutanisha
watu wa tamaduni mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili kuonyesha
utajiri wao wa sanaa na utamaduni.
· Kutenegeneza
jukwaa ambalo ni kiungo cha kujenga mahusiano ya wasanii wa ndani na nje ya
nchi kupitia maonyesho ya sanaa.
· Kubadilishana
uzoefu na mawazo katika kuendeleza tasnia ya sanaa.
· Kutoa
burudani kwa watanzania na wageni kutoka nchi mbalimbali.
Tamasha la mwaka huu litapambwa na ngoma za
asili, muziki wa kizazi kipya, singeli, sarakasi, mazingaombwe, maigizo pamoja
na maonyesho na biashara ya sanaa na ufund.
Aidha, Dkt. Makoye aliongeza kuwa, katika Tamasha
hilo kutakuwa na warsha na semina zitakazohusu mambo mbalimbali katika Nyanja
za sanaa na utamaduni.
Alisema jumla ya vikundi ambavyo vimethibitisha
kushiriki ni 70 ambapo vikundi vya ndani ya nchi ni 60 na vikundi 10 kutoka nje
ya nchi.
Tamasha litafunguliwa rasmi siku ya Alhamisi
Tarehe 28 Oktoba 2021 likitanguliwa na mkesha siku ya Jumatano tarehe 27 Oktoba
2021 ambapo kila siku kutakuwa na mgeni mashuhuri na litafungwa rasmi siku ya
jumamosi tarehe 30 Oktoba 2021.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Dkt. Herbert
Francis Makoye, (aliyesimama) akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainab Abdallaah (wa tatu kulia).
Mkuu
wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallaah (wa nne kushoto) amkiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakufunzi na wageni waalikwa.