Wednesday, April 8, 2020

WADAU WAMKABIDHI WAZIRI MKUU SH. BIL 6.226 KUKABILI CORONA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 1,000,000,000/= kutoka kwa Mfanyabiashara, Rostam Aziz (wa tatu kushoto)  ukiwa ni mchango binafsi wa mfanyabiashara huyo  wa kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID – 19.   Makabidhiano hayo yalifanyika  kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 8, 2020.  

Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile,kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Makampuni ya Taifa, Abdulkarim Shah, wa pili ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Taifa Gas, Khamis Ramadhani na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Said Matamwe (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  wadau mbalimbali waliojitokeza kutoa michango kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serkali za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID – 19 kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 8, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
......................................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea kutoka kwa wadau msaada wa fedha pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 6.226.


Baada ya kupokea kupokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambapo hadi sasa kesi 24 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini na wagonjwa watano wamepona.


Waziri Mkuu amepokea msaada huo leo (Jumatano, Aprili 8, 2020) katika Ofisi Waziri Mkuu Mlimwa, jijini Dodoma. Amewataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.


Amesema hadi sasa jumla ya watu 396 wapo kwenye karatini katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa wakiwemo wageni wanaoingia nchini ambao wanafuatiliwa afya zao na baada ya siku 14 kama watakuwa hawana maambukizi wataruhusiwa kuungana na familia zao.


Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na kwa sasa imejiimarisha kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona.


“Serikali inatoa misitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.”


Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae kwa sababu hadi sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi wa corona nchini.


Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuvishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona pamoja na wasanii waliotunga nyimbo za kuuelimisha umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.


Miongoni mwa wadau waliotoa msaada huo ni kampuni ya Madini ya Twiga iliyotoa sh. bilioni nne, mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz ametoa sh. bilioni moja, kampuni ya Taifa Gesi imetoa sh. milioni 100 na kampuni ya mafuta ya Puma imetoa msaada wa mafuta lita 50,000 zitakazotumika katika magari yanayotoa huduma za kupambana na corona nchini yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa.


Wengine ni kampuni ya TEHAMA ya Huawei imetoa vifaa kuendeshea mikutano kwa njia ya video ambavyo ni cloudlink camera tatu, Cloudlink Mic tatu, Cloudlink TV terminal tatu, Cloudlink Platform pamoja na Thermal Imaging Temperature Measuring System moja vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 940, Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetoa sh. milioni 79.


Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.


Kuhusu wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa walio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.

Awali, mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Azizi alisema ametoa sh. bilioni moja ambayo ameielekeza katika kununua vitakasa mikono ambavyo vitatumiwa na wasafiri wa daladala wa Dar es Salaam na Zanzibar ili waweze kutumia kabla ya kupanda usafiri huo, hivyo kuweza kujikinga.


Pia, Mfanyabiashara huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kwa hekima na busara na kuwaepusha na taharuki kama ilivyotokea katika mataifa mengine.

Amempongeza Waziri Mkuu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa namna wanavyoshiriki katika kukabiliana na corona.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea lita 50,000 za mafuta kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya mafuta ya Puma Energy Tanzania, Dominic Dhanah ( wa pili Kushoto) na  Meneja Uzalishaji wa kampuni hiyo, Lameck Hiliyai (kulia) ukiwa ni mchango wa Kampuni hiyo wa kuunga mono mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID -19 nchini.

Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 8, 2020. Wa tatu Kushoto ni Waziri wa Madini, Doto Biteko, Wa pili Kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, ofisi ya Waziri Mkuu, Kanalı Said Matamwe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea mchango wa sh. 100, 000,000/= Kutoka kampuni ya Taifa Gas kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu – COVID-19. Pichani, Waziri Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Makampuni ya Taifa, Abdulkarim Shah (kulia) 
na Mkurugenzi Mtendaji wa Taifa Gas, Hamisi Ramadhani. Wa tatu kushoto ni Waziri wa Madini, Doto Biteko, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanalı Said Matemwe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WASIO CHUKUA TAHADHARI YA CORONA KUTOZWA FAINI

 Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akinawa mikono kabla ya kuingia katika Zahanati ya Saza itakayotumika kutibu endapo atapatikana mgonjwa wa Corona wilayani hapo wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipofanya ukaguzi wa utayari katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona kwa Wilaya ya Songwe.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia Opulukwa akinawa mikono kabla ya kuingia katika Zahanati ya Saza itakayotumika kutibu endapo atapatikana mgonjwa wa Corona wilayani hapo wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipofanya ukaguzi wa utayari katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona kwa Wilaya ya Songwe.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akizungumza na bodaboda wa kituo cha Stendi ya Mkwajuni Songwe ambapo amewaelekeza kukaa mbalimbali, kunawa kwa maji na sabuni ili kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona.
..........................................


Watu wote ambao hawachukui hatua za tahadhari za kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona kwa kutofuata maelekezo ya wataalamu wa Afya, watatozwa faini kwakuwa wana hatarisha maisha yao na ya wengine.


Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia Opulukwa amebainisha hayo jana mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Songwe kufanya ukaguzi wa utayari wa kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona katika Wilaya hiyo.


Opulukwa amesema, “Sasa tunaanza kutoza faini wote wasiofuata maelekezo ya wataalamu wa Afya kuhusiana na Corona, mfano tukipita dukani au sehemu ya biashara na hakuna maji na sabuni, tuta toza faini na kufunga kwa mda biashara hiyo mpaka mtu huyo azingatie maaelekezo hayo”.


Ameongeza kuwa lengo la Wilaya hiyo ni kuhakikisha kuwa mahali pa kufanyia biashara ni salama kwa wafanyabiashara na watumiaji wa huduma hizo huku akieleza kuwa wanawa fuatilia wageni wote wanao toka nje ya wilaya waliopo katika nyumba za kulala wageni na kuchukua maelezo yao kwa ajili ya tahadhari  endapo wana dalili za Ugonjwa wa Virusi vya Corona.


Opulukwa ameongeza kuwa elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi wote wa Wilaya ya Songwe hususani katika maeneo ya migodi ambapo kuna mikusanyiko ya watu wengi pia ameielekeza kamati inayohusika kutoa elimu ifanye ufuatiliaji wa kina endapo wananchi wanazingatia wanayo waelekeza.


Aidha amesema mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kufanya ukaguzi wa utayari wa Wilaya hiyo katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona, Kamati hiyo imebaini baadhi ya mapungufu ambayo kama wilaya itasimamia kuyarekebisha.


Amefafanua kuwa yote yaliyoonekana kama mapungufu yapo ndani ya uwezo wa Wilaya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha eneo la kuwatenga washukiwa wa Corona lina vitanda vya kutosha na kujenga kichomea taka katika Zahanati ya Saza ambayo itatumika kutibu wagonjwa wa Corona.


Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songwe Dkt Humphrey Masoke amesema wameshaagiza vifaa kinga na tiba vyote muhimu katika Bohari kuu ya Dawa ili kuongezea katika vifaa vichache walivyo navyo tayari.


Dkt. Masoke ameongeza kuwa wana endelea kutoa maelekezo na elimu kwa jamii  juu ya tahadhari ya ugonjwa wa Virusi vya Corona kwakuwa bado baadhi ya wananchi wanaamini ugonjwa wa Corona ni wa wazungu hivyo hauwahusu.


Estin Nyangito Mkazi wa Mkwajuni Songwe amesema wamesha pewa elimu ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na Virusi vya Corona na elimu hiyo wataisambaza kwa wananchi wengine ili nao waweze kuchukua tahadhari.


Kwa upande wake Jakson Mwampashi Mkazi wa Songwe amemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo kuweka utaratibu wa kutoa elimu mara kwa mara na kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia magari ya matangazo ya barabarani ili wananchi wote waweze kupata elimu ya Corona.