Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya
sh. 1,000,000,000/= kutoka kwa Mfanyabiashara, Rostam Aziz (wa tatu kushoto) ukiwa
ni mchango binafsi wa mfanyabiashara huyo wa kuunga mkono mapambano dhidi
ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID – 19. Makabidhiano hayo
yalifanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini
Dodoma, Aprili 8, 2020.
Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile,kulia ni Makamu
Mwenyekiti wa Makampuni ya Taifa, Abdulkarim Shah, wa pili ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Taifa Gas, Khamis Ramadhani na kushoto ni Mkurugenzi wa
Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Said Matamwe (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na
wadau mbalimbali waliojitokeza kutoa michango kwa ajili ya kuunga mkono
juhudi za serkali za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID – 19
kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 8, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
......................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea
kutoka kwa wadau msaada wa fedha pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya
kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya
corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 6.226.
Baada ya kupokea kupokea msaada huo,
Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika
mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambapo hadi sasa kesi 24 zimeripotiwa
tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini na wagonjwa watano wamepona.
Waziri Mkuu amepokea msaada huo leo
(Jumatano, Aprili 8, 2020) katika Ofisi Waziri Mkuu Mlimwa, jijini Dodoma.
Amewataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika kuchukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Amesema hadi sasa jumla ya watu 396
wapo kwenye karatini katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa wakiwemo wageni
wanaoingia nchini ambao wanafuatiliwa afya zao na baada ya siku 14 kama
watakuwa hawana maambukizi wataruhusiwa kuungana na familia zao.
Waziri Mkuu amesema Serikali kwa
upande wake imeendelea kuchukua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa
COVID-19 na kwa sasa imejiimarisha kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya
namna ya kujikinga na virusi vya corona.
“Serikali inatoa misitizo kwa
wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya
virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na
kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka
wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa
huo ili kuzuia usisambae kwa sababu hadi sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na
wagonjwa zaidi wa corona nchini.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuvishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa katika
kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona pamoja na wasanii
waliotunga nyimbo za kuuelimisha umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Miongoni mwa wadau waliotoa msaada
huo ni kampuni ya Madini ya Twiga iliyotoa sh. bilioni nne, mfanyabiashara
maarufu nchini Rostam Aziz ametoa sh. bilioni moja, kampuni ya Taifa Gesi
imetoa sh. milioni 100 na kampuni ya mafuta ya Puma imetoa msaada wa mafuta lita
50,000 zitakazotumika katika magari yanayotoa huduma za kupambana na corona
nchini yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa.
Wengine ni kampuni ya TEHAMA ya
Huawei imetoa vifaa kuendeshea mikutano kwa njia ya video ambavyo ni cloudlink
camera tatu, Cloudlink Mic tatu, Cloudlink TV terminal tatu, Cloudlink Platform
pamoja na Thermal Imaging Temperature Measuring System moja vyote vikiwa na
thamani ya sh. milioni 940, Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetoa sh. milioni 79.
Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri
Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali
walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha
walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Kuhusu wadau wengine wanaohitaji
kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa walio nje ya
nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na:
9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.
Awali, mfanyabiashara maarufu
nchini, Rostam Azizi alisema ametoa sh. bilioni moja ambayo ameielekeza katika
kununua vitakasa mikono ambavyo vitatumiwa na wasafiri wa daladala wa Dar es
Salaam na Zanzibar ili waweze kutumia kabla ya kupanda usafiri huo, hivyo
kuweza kujikinga.
Pia, Mfanyabiashara huyo ametumia
fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kwa
hekima na busara na kuwaepusha na taharuki kama ilivyotokea katika mataifa
mengine.
Amempongeza Waziri Mkuu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto kwa namna wanavyoshiriki katika kukabiliana na corona.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea lita
50,000 za mafuta kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya mafuta ya Puma Energy
Tanzania, Dominic Dhanah ( wa pili Kushoto) na Meneja Uzalishaji wa
kampuni hiyo, Lameck Hiliyai (kulia) ukiwa ni mchango wa Kampuni hiyo wa kuunga
mono mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID -19 nchini.
Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa
jijini Dodoma, Aprili 8, 2020. Wa tatu Kushoto ni Waziri wa Madini, Doto
Biteko, Wa pili Kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya
Maafa, ofisi ya Waziri Mkuu, Kanalı Said Matamwe. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea mchango wa sh. 100, 000,000/= Kutoka kampuni ya
Taifa Gas kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na ugonjwa
wa homa kali ya mapafu – COVID-19. Pichani, Waziri Mkuu akiwa katika picha ya
pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Makampuni ya Taifa, Abdulkarim Shah
(kulia)
na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taifa Gas, Hamisi Ramadhani. Wa tatu kushoto ni Waziri
wa Madini, Doto Biteko, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile na kushoto ni Mkurugenzi
wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanalı Said Matemwe. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment