Saturday, January 11, 2020

MABULA AKABIDHI HATI MIA MOJA ZA KIMILA KWA WAKULIMA WADOGO KIJIJI CHA LITOA RUVUMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Kimila Bibi Dafrosa Komba wakati wa zoezi la kutoa hati kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Litoa katika wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma jana. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Songea Pololeti Mgema.
......................................


Na Munir Shemweta, WANMM SONGEA.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekabidhi hati mia moja za Kimila kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Litoa kilichopo katika jimbo la Peramiho wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma na kuwataka wamiliki wake kuzitunza na kuzitumia hati hizo kujiletea maendeleo.


Akizungumza wakati wa kuwakabidhi hati hizo katika kijiji cha Litoa wilaya ya Songea vijijini akiwa kwenye shughuli za kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi ya ujenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa katika mikoa ya kusini jana, Naibu Waziri Mabula aliwataka wakulima waliokabidhiwa hati kutouza ardhi zao kwa nia ya kupata fedha za haraka.


‘’Mmepiwa msikimbilie kuuza ardhi bila kufuata taratibu kwa tamaa ya kupata fedha za haraka maana mkiuza mnaweza kupunjwa fedha’’ alisema Dkt Mabula.


Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji ili kuwa na salama za miliki za ardhi zilizoainisha maeneo ya shule, soko, maeneo ya kuabudia, viwanja vya michezo pamoja na maeneo ya uwekezaji.


Dkt Mabula alizitaka pia halmashauri kuandaa maeneo ya uwekezaji sambamba na kuhaulisha maeneo ili kuwa rahisi kwa Mwekezaji atakayekuja kuwekeza katika sekta mbalimbali na kusisitiza kuwa ili kuwaendeleza wananchi kiuchumi ni lazima ardhi ipimwe na kufanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Vijijini Pololeti Mgema aliupongeza Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa juhudi kubwa iliyofanya kufanikisha wakulima wadogo kupata hati miliki za kimila na kubainisha kuwa wilaya yake imejifunza bila kushirikisha wadau zoezi la kuwapatia hati wakulima wadogo lingechukua muda mrefu.


 Naye Mratibu wa MVIWATA katika mkoa wa Ruvuma Laila Haji alisema Asasi yake iliona umuhimu wa wakulima wadogo kuwa na salama za miliki za mashamba yao na ndiyo maana ikafanya juhudi kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Songea ili kuwapatia hati wakulima wa kijiji cha Litoa.


Hata hivyo, alisema changamoto kubwa iliyopo kwa wakulima na wananchi kwa ujumla katika suala la hati miliki za ardhi ni elimu ndogo kuhusiana na masuala hati za ardhi, mfumo dume kwa wanawake kumiliki ardhi pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji.


Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alitembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi na nyumba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) uliopo Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma. 

Mradi huo pamoja na miradi mingine ya ujenzi wa nyumba na ofisi za TFS katika maeneo mbalimbali nchini unajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiangalia nondo zinazotumika kwenye ujenzi wa mradi wa nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  katika eneo la Mpepo wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma jana wakati akikagua mradi huo. Kulia ni  mhandisi wa Mradi kutoka NHC Omar Chitawala

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akifafanua jambo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa nyumba na Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwenye shamba la miti la Mpepo lililopo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma jana. Kushoto ni Meneja Mawasiliano wa NHC Muungano Saguya na aliyekunja mikono ni Mhandisi wa Mradi kutoka Omar Chitawala.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi waliokabidhiwa Hati za Kimila wakati wa zoezi la kutoa hati katika kijiji cha Litoa wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Songea Pololeti Mgema. 


MAHAKAMA YAJENGA MAJENGO 42 NDANI YA MIAKA MINNE


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Kilwa.
................................

Na Magreth Kinabo-Mahakama



Mahakama ya Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kukamilisha miradi 42 ya ujenzi na ukarabati wa majengo yake katika ngazi zote kuanzia Mahakama Kuu mpaka Mahakama za Mwanzo.

Miradi hiyo ya ujenzi imetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutatua changamoto iliyopo ya upungufu na uchakavu wa majengo ya Mahakama na kutekeleza azma ya Serikali  ya kuboresha na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru amesema kutokana na ukamilishwaji wa miradi hiyo, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuzindua majengo ya Mahakama za Wilaya za Ruangwa na Kilwa.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa litazinduliwa Januari 14, 2020 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa. Wakati Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma atazindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kilwa Januari 15, 2020.

‘Tunajenga majengo haya kwa kuzingatia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kurahisisha shughuli za utoaji haki kwa wakati,’ alisema Kabunduguru.

Alisema miradi ya ujenzi iliyokamilika inajumuisha majengo manne ya Mahakama Kuu ambapo imejenga  majengo mapya katika mikoa ya Kigoma na Musoma na kuanzisha huduma za Mahakama Kuu pamoja na kuyafanyia ukarabati mkubwa majengo ya Mahakama Kuu kanda za Mbeya na Tanga.

Aidha, Mahakama ya Tanzania imekamilisha ujenzi wa majengo matano ya Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Pwani, Manyara, Geita, Njombe na Simiyu.

Katika kipindi cha miaka minne Mahakama imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa majengo 16 ya Mahakama za wilaya ambazo ni Bagamoyo, Kigamboni, Mkuranga, Ilala, Kibaha, Babati na Bariadi. Majengo mengine ni pamoja na Mahakama za wilaya za Chato, Geita, Bukombe, Ruangwa, Kilwa Masoko, Bariadi, Kondoa, Longido, Chunya na Kasulu.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Mahakama za Mwanzo, Mahakama  imefanikiwa kujenga majengo mapya ya Mahakama  za Mwanzo Kawe (Dar es salaam),Mkunya (Newala), Msanzi (Sumbawanga), Mtowisa (Sumbawanga), Uyole (Mbeya), na Ngerengere (Morogoro).

Mahakama imekamilisha miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo iliyokuwa imesimama katika maeneo ya Iguguno (Singida), Bereko (Kondoa), Wasso (Loliondo), Old Korogwe na Magoma (Korogwe). Maeneo mengine ni Mvomero (Morogoro), Karatu (Arusha), Robanda (Serengeti), Itinje (Simiyu), Totowe na Mlowo (Songwe). 

Mahakama inaendelea na ujenzi wa majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Katavi na Lindi pamoja na Mahakama za wilaya za Rungwe, Kilindi, Sikonge, Wanging’ombe, Makete na Bunda.

Aidha ujenzi wa Majengo ya Mahakama za Mwanzo Mtae (Tanga), Laela (Sumbawanga), Lugarawa (Ludewa), Mang’ula na Mlimba (Morogoro) unaendelea. Kwa upande wa ukarabati, Mahakama inaendelea na ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga. Miradi hii yote inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 2020.

Alisema Mahakama inaendelea na kasi ya uboreshaji wa miundombinu yake ambapo leo imeingia Mkataba na Wakandarasi kujenga majengo sita ya Mahakama Kuu maarufu kama vituo vya utoaji wa Haki Jumuishi (Intergrated Justice Centre) katika mikoa ya Morogoro, Dar Es Salaam (Kinondoni na Temeke), Dodoma, Mwanza na Arusha.

Katika mwaka huu wa fedha Mahakama inakusudia kujenga majengo mengine 33 katika maeneo mbalimbali nchini. Ujenzi wa majengo haya unaenda sambamba na uwekaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA.

Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na uanzishwaji wa Mfuko wa Mahakama chini ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Mfuko huu unawezesha upatikanaji wa fedha za Maendeleo na Uendeshaji wa shughuli nyingine za Mahakama kwa haraka na uhakika.
 

HALMASHAURI ZA WILAYA ZATAKIWA KUTENGA BAJETI KUPANGA MATUMIZI BORA YA ARDHI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Halmashauri na Wilaya za hapa Nchini zimetakiwa kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kupanga matumizi bora ya Ardhi katika maeneo yao.

Agizo hilo limetolewa na Naibu waziri wa Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Angelina Mabula alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Lindi.

Wakati wa ziara hiyo Mabula alibaini kuwa zaidi ya asilimia 66% ya vijiji vya Mkoa wa Lindi havijapangiwa matumizi bora ya Ardhi.

Mabula alisema ili kunusuru migogoro mbalimbali ya ardhi inayoweza kujitokeza katika maeneo hayo ni kuhakikisha Halmashauri zinakuwa na mpango wa matumizi bora ya Ardhi katika maeneo yote.

Aliongeza kuwa migogoro mingi ya ardhi hasa ile ya wakulima na wafugaji hutokea pale ambapo Halmashauri husika hazikuweka mpango shirikishi wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji au maeneo yao.

"Huku tunaowakulima wengi lakini pia tunayo pia maeneo mengi ya uwekezaji sasa tusipopanga matumizi bora ya ardhi yetu tutajikuta hatuko tayari sana kupokea wawekezaji hivyo tunachoweza kufanya katika hili ni kuongeza kasi ya upangaji" alisema Mabula.

Awali katibu tawala uchumi na uzalishaji Majid muyao akitoa taarifa ya Mkoa huo kwa niaba ya Katibu tawala Mkoa wa Lindi alisema kuwa Mkoa huo una jumla ya vijiji 524 ambapo ni vijiji 176 sawa na (34%) ndivyo vyenye mpango shirikishi wa matumizi bora ya Ardhi