Thursday, January 2, 2020

WAZIRI BITEKO AKIFUNGA KIWANDA BUBU CHA UCHENJUAJI DHAHABU

 Waziri wa Madini Doto Biteko kushoto akimuelekeza jambo Mkuu wa jeshi la Polisi wa kituo cha Bugarama.
.................................


Na Tito Mselem, Kahama.

Waziri wa Madini Doto Biteko amekifunga kiwanda bubu cha kuchenjua madini ya dhahabu kilichofunguliwa kinyemela katika Kijiji cha Bunanga kata ya Bugarama Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama.


Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Simoni Shule kipo katikati ya makazi ya watu ambapo kinahatarisha maisha ya watu na kuharibu mazingira baada ya kutiririsha kemikali za sumu kwenye makazi ya watu.


Waziri Biteko alisema, licha ya serikali kuboresha Sekta ya Madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wa madini nchini, imebainika kuwa wapo ambao wamekuwa wakifanya shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu ikiwemo kuanzisha viwanda bubu kinyume na taratibu na kuikosesha  serikali mapato.


Hayo yalibainishwa Januari Mosi mwaka 2020 na Waziri Biteko baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kijiji cha Bunanga kata ya Bugarama Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama na kubaini kiwanda bubu cha kuchenjua madini ya dhahabu kilichopo katikati ya makazi ya watu.


“Kiwanda hiki kipo hapa katika nyumba hii kwa kipindi cha zaidi ya miezi 7 kikiendelea kufanya kazi bila kufuata Sheria na Taratibu zilizopo na kuipotezea Serikali mapato mengi, hivyo tutachukua hatua kali za kisheria kwa mmiliki wa mtambo huu ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia chafu kama hii,” alisema Biteko.


Aidha, Waziri Biteko aliwataka viongozi wa vijiji na mitaa wilayani humo kuhakikisha wanawafichua wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara haramu ya madini ambazo zinafanyika katika makazi ya watu kinyume na Sheria na kuikosesha Serikali mapato.


“Niwaagize viongozi wote wa ngazi zote Nchi nzima kuhakikisha mnasimamia na kuthibiti vitendo vya biashara haramu ya madini ambavyo vinaendelea kufanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu katika maeneo mbalimbali nchini, alisema Waziri Biteko.


Wakati huo huo, Waziri Biteko aliliagiza jeshi la polisi la Halmashauri ya Msalala kumkamata na kumuhoji Afisa Mtendaji wa kijiji cha Bunanga Kajanja Kajanja na Mke wa mwenye nyumba iliyobainika kuwa na mtambo wa kuchenjulia dhahabu unaomilikiwa na Simoni Shule

kuhusiana na kuhusishwa na tukio hilo.


Katika ziara hiyo mifuko zaidi ya 44 ya kemikali zinazotumika kuchenjulia madini ya dhahabu (Kaboni) imekamatwa katika kiwanda hicho inayodhaniwa kuwa na madini ya dhahabu, huku mashine hiyo yenye uwezo wa kubeba kilo 500 za Kaboni ikiwa tayari imewekewa

mzigo kwaajili ya kuanza kazi.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bunanga Januari Luhamba, alisema, baada ya kugundua shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho katikati ya makazi ya watu, alitoa taarifa kwa mamlaka za kisheria  ikiwemo polisi kuhusiana na uwepo wa kiwanda hicho katika eneo lake lakini hakuona hatua yoyote iliyochukuliwa kwa wahusika.


“Kiwanda hiki kipo katika nyumba hii kwa muda mrefu sasa, kuna vijana wageni wengi wamekuja kufanya kazi ya kuchenjua dhahabu katika kiwanda hiki, viongozi wote wa eneo hili wanajua tumelalamika sana kuhusiana na kumwagwa ovyo kwa maji yenye kemikali kwenye makazi yetu,” alisema.Luhambo.
 Maafisa wa Madini wa Wilaya ya Kahama wakiweka sildi katika mlango wa kiwanda bubu cha kuchenjulia madini ya dhahabu.
Waziri wa Madini Doto Biteko kulia akimuelekeza mwenyekiti wa Kijiji cha Bunanga January Luhamba sehemu ya kusaini.
 Waziri wa Madini Doto Biteko kushoto akichungulia chumba kilichosimikwa mtambo wa kuchenjulia madini ya dhahabu, kulia ni mwenyekiti wa Kijiji cha Bunanga Luhamba.
Baaadhi ya mifuko iliyojazwa kemikali za kuchenjulia dhahabu. (kaboni)
 Waziri wa Madini Doto Biteko kulia akiwa amebeba furushi la kemikali za kuchenjulia madini ya dhahabu (kaboni) kushoto ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Bunanga Kajanja Kajanja.



BRELA YAONGEZA MUDA WA KUHUISHA TAARIFA ZA MAKAMPUNI NA MAJINA YA BIASHARA

Wednesday, January 1, 2020

BIL. 5 ZAJENGA TENKI LA MAJI HOSPITALI MKURANGA


Na Omary Mngindo, Mkuranga

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatumia kiasi cha shilingi bilioni 5 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji unaojengwa mwenye hospitali ya wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Mradi huo unaotarajiwa kuondoa adha kwa wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu, hususani akina mama wanaojifungua, utakapokamilika utakuwa mkombozi hospitalini hapo, kwani ni muda mrefu sasa wagonjwa wanakwenda na ndoo za maji.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja, akitoa taarifa ya ujenzi huo mbele ya Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jafo, akiwa na mwenyeji wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akiambatana na Mbunge wa Viti Maalum Zaynab Vulu.

Luhemeja alisema kuwa mradi huo mkubwa unaotekelezwa kwa fedha za ndani kutokana na makusanyo ya bili za wateja wake, ni utekelezaji wa dhamira ya serikali inayoongozwa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Magufuli.

"Kipekee kabisa niishukuru serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Magufuli, jana (juzi) tumezindua mradi mwingine mkubwa wa maji pale Kisarawe, maji yanayotokea katika chanzo cha Mto Ruvu yanayokwenda kupunguza kama sio kumaliza changamoto hiyo,"alisema Mhandisi Luhemeja.

Kwa upande wake Waziri Jafo alilipongeza shirika hilo kwa ufanisi wake mkubwa katika kusambaza maji maeneo mbalimbali, huku akisema hatua hiyo inafuatia dhamira kubwa na njema ya Rais Magufuli ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo ya maji.

"Sote tu mashahidi, tangu serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu kipenzi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, miradi mingi ya kimaendeleo imekuwa ikitekelezwa katika wilaya na mikoa mbalimbali, nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati ya moyo wangu," alisema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Ulega nae hakusita kuishukuru serikali kwa hatua hiyo kubwa, huku akieleza kwamba mradi huo unaojengwa hospitalini hapo, mbali ya kutoa huduma eneo hilo, pia maji hayo yatavinufaisha vijiji mbalimbali.

"Nikuombe ndugu yangu Jafo utufikishie salamu zetu za shukrani kwa Rais wetu John Magufuli, hakika anatupenda sana wana-Mkuranga, leo tunashuhudia ujenzi huo mkubwa wa tenki la maji linalolenga kuondoa changamoto husika," alisema Ulega.

Mbunge wa Viti Maalumu Zaynab Vulu aliishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuyafikisha maji hospitalini hapo, huku akisema huduma ya maji pamoja na umuhimu kwa binadamu wote, lakini wanawake ni watumiaji wakubwa wa maji.

"Tunaishukuru serikali yetu kupitia DAWASA kwa mradi huo mkubwa Jambao leo tunaushuhudia hapa, utakuwa mkombozi katika eneo hili la hospitali, pia kama tulivyoelezwa na Mkurugenzi Luhemeja kwamba maji haya yatafika mpaka maeneo ya vijiji vyetu," alisema Vulu.