Friday, December 6, 2019

MAAFISA HABARI WAPONGEZWA KWA KUISEMEA VIZURI SERIKALI

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi  akitoa maelekezo kwa uongozi wa Chama cha Maafisa Habari Tanzania (TAGCO) wa kuendeleza mpango wa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa habari wa serikalini leo alipokuwa akifunga mafunzo ya maafisa hao yaliyokuwa yakifanyika jijini Dodoma kwa siku tano.
..........................................


Na Shamimu Nyaki – WHUSM,Dodoma

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo  Dkt.Ally Possi amewapongeza Maafisa Habari,Uhusiano na Mawasiliano Serikalini kwa kutangaza vizuri shuguli za Serikali ikiwemo miradi inayotekeleza ambayo itawaletea wananchi maendeleo.


Dkt.Possi ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya kimkakati ya Uandishi wa Habari za Serikali ya awamu ya pili kwa  Maafisa Habari,Uhusiano na Mawasiliano Serikalini ambapo amewataka kutumia elimu waliyopata kuendelea kuhabarisha umma kwa weledi na kwa usahihi habari zinazohusu Serikali.


“Maafisa Habari mnafanya vizuri katika kutangaza shughuli za Serikali kwa wananchi,naomba muendelee kufanya hivyo kwa kuwa kada yenu ni muhimu katika kufikisha ujumbe wa Serikali kwa wanachi na mtumie kalamu zenu vizuri ili kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu”alisema Dkt. Possi.


Aidha Dkt.Possi amewataka waandaaji wa mafunzo hayo kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na kutumia mifumo tofauti ya ndani na  nje ya nchi pamoja na kufanya tathmini ili kuona mabadiliko yaliyopatikana kutokana na mafunzo hayo.


Hata hivyo Dkt. Possi aliwashauri Maafisa Habari wote wa Serikali kujiunga na Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) ili kurahisisha mawasiliano miongoni mwao pamoja na kushirikiana katika kazi wanazofanya  ikiwemo kubadilishana uzoefu na kusaidiana kijamii na kitaaluma.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Habari –MAELEZO Bw.Rodney Thadeusi amesema kuwa jukumu la maafisa habari wa Serikali ni kutoa taarifa sahihi na  kwa wakati zinazohuzu Serikali kwa wananchi kutumia njia zote za mawasilano.


“Maafisa habari kazi yetu kubwa ni kuisemea Serikali tusiposema sisi wengine watasema na wengine wanaweza kusema ambayo sio sahihi na wakati mwingine kukosoa hata yale mazuri ambayo Serikali inatekeleza kwa wananchi wake hivyo tuendelee kutumia taaluma yetu kuitangaza vizuri  Serikali”alisema Bw.Rodney.


Naye  Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bibi.Sara Msika amesema lengo la  mafunzo hayo ni kuendelea kuboresha taaluma ya maafisa hao katika kipindi hiki ambacho dunia imekuwa na mabadiliko makubwa katika kada hii ya uandishi wa habari.


Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo  Afisa Habari kutoka TBC Bibi.Catherine Nyoni ameshukuru waandaaji wa mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa Maafisa Habari Serikalini ambayo yamesaidia  kuboresha taaluma yao pamoja na kubadilishana uzoefu.


Mafunzo hayo ya siku tano yalioandaliwa na Idara ya Habari –MAELEZO pamoja na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) yamekuwa na mada mbalimbali ikwemo namna ya kutumia mitandao ya kijamii kuhabarisha umma pamoja na uandishi mzuri wa habari za Serikali.


 

MAJAMBAZI YAIBA MILIONI 3 KIBAHA.

VICTOR MASANGU, PWANI.

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linawasaka watu sita wanaodhaniwa  kuwa ni  majambazi baada ya kuvamia katika kiwanda cha kutengenezea vifungashio kilichopo maeneo ya Picha ya ndege Wilayani Kibaha nakufanikiwa kuiba kiasi cha shilingi milino 3, simu nne za  mkononi, pamoja na kompyuta mpakato mbili.  


Akizungumza na waandishi wa habari Ofisni kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamisshna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa, amesema kwamba tukio hilo limetokea usiku wa kumakia leo  majira ya tisa usiku ambapo pia waliwashambulia wamiliki wa kiwanda hicho  wakiwa na silaha mbali mbali za jadi ikiwemo marunga, mapanga, na nondo na kukimbilia pasipojulikana na kwamba walinzi wa kiwanda hicho wanashikiliwa.


Katika hatua nyingine Kamanda Wankyo  amebainisha kuwa Polisi mkoani humo imewakamata  watu nane  akiwemo daktari wa idara ya mifugo kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa mifugo aina ya mbuzi na kondoo  pamoja na kuuza nyama ya ng’ombe kilo 405 isiyokaguliwa katika eneo la halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani ambapo watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani.

Thursday, December 5, 2019

WANANCHI BUZA WAMIMINIKA KUPATA HUDUMA TRA.

Na Shushu Joel. 

WANANCHI wa Buza jijini Dar es Salaam wamejitokeza kwa wingi kwenye banda la utoaji wa huduma na Elimu kwa mlipa kodi.

Wakizungumza kwa wakati tofauti mara baada ya kuhudumiwa na kukabidhiwa kwa vyeti vyenye Namba ya Utambulisho wa Mlipakodiza, wameipongeza mamlaka hiyo kwa kuwapelekea huduma milangoni mwao.

Gift Bosco (47)ni mkazi wa buza ninaipongeza mamlaka ya mapato Tanzania kwa utoaji wake wa elimu kwa kutufuata wakazi wa buza.

"Nimefanikiwa kupata TIN ninaamini huu ni mwanzo wa kuwa miongoni mwa walipa kodi wazuri"

Aliongeza kuwa wananchi wengi hawana uelewa juu ya umuhimu wa kulipa kodi hivyo wawe wanaangalia vipindi vya TRA kwenye TV kwani vinaelimisha sana kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

Aidha amewataka mamlaka ya mapato kuendelea kuwatembelea na kuwaelimisha kwani uelewa unaongezeka siku hadi siku.

Naye Muhammad Ally ni mmoja wa wakazi wa Buza na ni mfanyabiashara wa duka amesema kuwa miaka ya nyuma ukiwaona watu wa mamlaka ya mapato Tanzania wanakuja basi unaenda kufunga duka na wewe kwenda kujificha lakini kutokana na elimu pana inayotolewa na mamlaka hiyo wengi wamekuwa waelewa juu ya ulipaji wa kodi.

Aidha, Ally amesifu utendaji wa kazi wa TRA kwa kuwafikia wateja wake tena majumbani kabisa.

Kwa upande wake Meneja wa Elimu kwa mlipa kodi Diana Masalla kutoka TRA alisema kuwa zoezi la utoaji wa elimu linaendelea kila mahali kwa lengo la kuwaelimisha wananchi zaidi.

Hivyo amewapongeza wananchi wa buza kwa namna walivyojitokeza kusikiliza na kuelimishwa umuhumi wa kuwa na TIN na kulipia kodi ya majengo.

Aidha Masalla aliongeza kuwa TRA itaendelea kutoa elimu kwa kila mwananchi ili aweze kunufaika na biashara yake anayoifanya kwani wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifeli kutokana na ukosaji wa elimu.

"TRA imetambua thamani yenu na ndio maana tumeamua kuwafuata karibu na biashara zenu ili msifunge na kutufuata mbali sasa tunakufuata mlangoni kwako ili tukuhudumie"

DC, MSHAMA ATAKA WANAFUNZI WASICHANA WANAOPATA MIMBA WACHUKULIWE HATUA.

NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA

MKUU wa wilaya ya Kibaha ,mkoani Pwani ,Assumpter Mshama ameeleza iko haja ya kuwa na usawa wa kijinsia kwa watoto wa kike na wa kiume pindi mwanafunzi wa kike anapopata mimba akiwa shuleni, ili iwe fundisho kwa wanafunzi wengine .


Ameeleza, inapaswa mtoto wa kike nae achukuliwe hatua sawa na mtoto wa kiume kwani ujauzito hautokani na upande mmoja bali ni ushirika wa watu wawili wa jinsia mbili tofauti.


Akizungumza katika  mahafali ya wanafunzi wa chuo cha ufundi stadi VETA Pwani, pamoja na mambo mengine, Mshama alisema ifikie hatua kila mwanafunzi apate adhabu sawa baada ya kupeana mimba ili kukomesha tabia hiyo.


“Kwa wilaya hii wote mtapata adhabu, haiwezekani mtoto wa kike aendelee kutamba wakati muda mwingine unakuta mtoto huyo ndio alikuwa chanzo cha kumtongoza mwalimu au mwanafunzi mwenzie, hamjawahi kuona hilo!,  Alihoji Mkuu huyo wa wilaya.


Aidha Mshama alishauri Vijana hao waliomaliza chuo cha ufundi stadi VETA,   kujiajiri kwa kufungua  viwanda vidogo vidogo na kutengeneza vifaa vyenye ubora ili waweze kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira.


Mapema wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi wanachuo ZAHARA ABDUL na IDD ATHUMANI waliiomba serikali ya mkoa huo, kutoa kipaumbele cha ajira na fursa mbalimbali zilizoko ndani ya mkoa.

Nae kaimu mkuu wa chuo hicho, Karim aliainisha changamoto kubwa inayoikabili chuo ni upungufu wa mabweni.

ZAIDI YA WATOTO 14,000 BAGAMOYO KUPATIWA VYETI VYA KUZALIWA.

Image may contain: 4 people, people smiling, people sitting
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Fatuma O. Latu, amefungua rasmi mafunzo kwa wataalamu watakaoendesha zoezi maalumu la uandikishaji na usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili wapatiwe vyeti vya kuzaliwa bure.

Mafunzo kwa Wataalamu wasajili hao yamelenga kuwajengea uwezo ili kutekeleza mpango wa usajili wa watoto kwa kasi inayotakiwa na kwa ufanisi mkubwa.

“Ni wajibu wenu kuhakikisha zoezi hili mnalitekeleza kwa weledi mkubwa, ili muisaidie Serikali kupata takwimu sahihi zitakazoisaidia kupanga shughuli za maendeleo katika Halmashauri yetu ya Bagamoyo, hivyo umakini mkubwa unatakiwa wakati wa mafunzo ili kupata uelewa sahihi wa kutekeleza zoezi” Amesema Bi. Fatuma Latu


Anaongeza “Kila mtoto ana haki ya kusajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa kwani cheti hiki kina umuhimu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kumtambulisha mtoto wakati wa kupata huduma muhimu za kijamii, mfano; wakati wa kuandikishwa shule, kuingia chuo kikuu, wakati wa kujiandikisha ili kupata kitambulisho cha Taifa, kuomba pasipoti ya kusafiria na matumizi mengine mengi muhimu, hivyo ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anatumia fursa hii kuhakikisha mtoto wake anasajiliwa na kupatiwa cheti cha kuzaliwa”


Jumla ya watoto 14,565 wanatarajiwa kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia mpango huu maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ambapo zoezi la usajili wa watoto ili kupatiwa vyeti vya kuzaliwa linatarajiwa kuanza siku ya tarehe 06/12/2019 na litaendelea hadi tarehe 19/12/2019.


Usajili huu wa watoto utafanyika katika Ofisi za Kata zote 11 za Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, pia katika Vituo vya kutolea huduma za Afya, ambavyo ni Zahanati zote, Vituo vya Afya na katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, ambapo Mzazi anatakiwa kufika katika Vituo hivyo vya usajili akiwa na nakala (copy) ya kadi ya kliniki au tangazo la mtoto kuzaliwa ili kufanya usajili huo.

Mpango wa usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Pwani, unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya watu wa Canada, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) pamoja na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).