Saturday, October 19, 2019

TAKUKURU YAKAMATA 99 VIONGOZI WA AMCOS LINDI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI

TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (YAKUKURU) Mkoa wa Lindi ImeendeLea kuwakamata viongozi wa vyama vya Msingi (AMCOS) 99 kutoka 51, Wa awali ambao wamehusika katika kudhulumu fedha za Wakulima wa Ufuta wa Mkoa huo.

Ukamatwaji wa viongozi hao ni moja ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa oktoba 10 mwaka huu wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi, ambapo aliiagiza TAKUKURU pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuhakikisha vyama 10 vya Msingi (AMCOS) vinavyodaiwa na wakulima wa ufuta vinawalipa wakulima hao fedha zao kabla ya msimu mpya wa Korosho kuanza.


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Brigedia General John Mbungo alisema kuwa ongezeko la viongozi hao wa Vyama vya msingi limekuja baada ya taasisi yao kuendelea kufanya msako katika baadhi ya vyama vya Msingi (AMCOS) Mkoani humo

"ingawa Taarifa iliyokabidhiwa TAKUKURU na Naibu Waziri wa kilimo Mhe, Hussein Bashe ilikuwa inaonyesha wakulima wa ufuta wamedhulumiwa kiasi cha shilingi milioni 436,869, 982,00 na vyama 10 vya msingi (AMCOS) lakini uchunguzi na ufuatiliaji uliofanywa na TAKUKURU ulibaini kuwepo kwa vyama 31 vya Msingi (AMCOS) Kuwadhulumu wakulima wa ufuta kiasi cha shilingi Bilioni 1,236,363,075.00/=" alisema Mbungo.

Hata hivyo Mbungo alisema kuwa tokea zoezi hilo la kuwakamata viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) oktoba 16, mpaka oktoba 19 tayari kiasi cha shilingi milioni 255,598,194.00 zimerejeshwa katika Ofisi ya TAKUKURU na kwamba fedha hizo zitaanza kulipwa kwa wakulima hao kwa utaratibu utakaopangwa.


Mbungo pia alisema katika kuhakikisha wakulima wote waliodhulumiwa fedha zao wanapata haki zao Taasisi hiyo imeanza zoezi la kutambua, kupiga picha na kukamata Mali za viongozi hao wa AMCOS wanaodaiwa ili ziwe dhamana ya madeni wanayodaiwa na endapo watashindwa kulipa kwa muda waliokubaliana vitu hivyo vitauzwa ili kulipa madeni ya wakulima.


Aidha, alitoa rai kwa viongozi wote wa vyama vya ushirika Nchini vinavyodaiwa na wakulima walipe wakulima hao haraka iwezekanavyo kabla ya TAKUKURU haijawafikia kwani zoezi hilo litakuwa endelevu na kwamba hakutakuwa na chama chochote cha ushirika kinacho daiwa kitakachobaki salama

Friday, October 18, 2019

TAMASHA LA 38 LA KIMATIFA LA SANAA NA UTAMADUNI KUANZA KESHO BAGAMOYO.

TAMASHA  la 38 la Sanaa Bagamoyo linaanza rasmi kesho Oktoba 19-26 katika mji wa kihistoria Bagamoyo mkoani Pwani.


Mwaka huu tamasha hilo litaanza kwa mtindo wa tofauti na ilivyozoeleka, litaanza kwa kuzunguka mitaa mbalimbali ya wilaya hiyo, lengo likiwa ni hamasa kwa tukio hilo muhimu.


Wasanii wa kazi mbalimbali watazunguka mji huo kwa ngoma mbalimbali ili kuwachochea wadau kujitokeza katika ukumbi ulioko chuoni hapo.


Zoezi hilo la kuzunguka maeneo ya Bagamoyo, litaanza asubuhi likishirikisha wadau mbalimbali.


Bagamoyo ni mojawapo ya maeneo yenye urithi na utajiri mkubwa wa kiutamaduni Ulimwenguni, ambako Tamasha hilo la kimataifa, kwa mara nyingine tena litawakutanisha wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, ambao wataonesha kazi zao za sanaa na utamaduni.


Dk. Hebert Makoye, ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), ambao ni waandaaji wa tamasha hilo linalozidi kujizolea umaarufu kila mwaka, anasema lengo ni kuendeleza na kudumisha Utamaduni wa Mtanzania, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine kupitia warsha, kongamano na maonyesho mbalimbali.


Dk. Makoye, anasema tamasha la 38 linatarajiwa kushirikisha wasanii zaidi ya 100 ya hapa nchini na nje, likiwa na dhamira ya kubadilishana uzoefu katika sanaa, hivyo ni nafasi ya wadau mbalimbali wa sanaa kujitokeza na kushuhudia elimu kutoka kwa wasanii watakaopanda jukwaani.


Anasema, tamasha la mwaka huu litashirikisha vijana wa shule za Msingi na Sekondari kutoka Bagamoyo, Vyuo na Vyuo Vikuu.


“Mwaka huu, tamasha linatarajiwa kuhudhuriwa na jumla ya watazamaji 60,000 kutoka maeneo ya Bagamoyo, Dar es Salaam na sehemu zingine za Tanzania pamoja na nje ya nchi,” anasema Dk. Makoye na kuongeza.


Kusudi la Tamasha hili ni kutoa fursa kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi, pamoja na watazamaji kukutana na kuuenzi utajiri wa utamaduni wao unaowatofautisha na mataifa mengine, ambao unaonyesha utofauti wao katika muktadha wa maadili na mshikamano, pamoja na ubunifu.


Malengo maalum ya Tamasha
Dk. Makoye, anasema ni jukwaa kwa wanafunzi wa TaSUBa na wa kutoka taasisi zingine za mafunzo, kuonesha kazi zao na stadi walizopata katika mafunzo yao ya sanaa na utamaduni.


Anasema, pia ni kukuza na kubadilishana tamaduni kati ya wasanii wa ndani na wa kimataifa, ni jukwaa la wasanii wachanga kuonesha vipaji na ustadi wao kwenye sanaa na utamaduni, kuongeza uhamasishaji miongoni mwa vijana na wasanii juu ya masuala yanayohusu sanaa, michezo na utamaduni wa Kitanzania.


Dk. Makoye, anasema Kauli mbiu ya Tamasha la mwaka huu ni ‘Sanaa na Utamaduni Ajira Yangu’.


Aidha, anasema katika tamasha la mwaka huu, kutakuwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali za sanaa na za kiutamaduni, vyakula mbalimbali kama vile nyama choma, samaki, pamoja na vyakula vya baharini.
Pia, anasema wageni watapata fursa ya kutembelea mji wa kihistoria wa Bagamoyo.


TaSUBa, Clouds Plus kuboresha tamasha
Mapema mwaka huu, TaSUBa imeingia makubaliano na Kampuni ya Clouds Plus Production yenye lengo la kushirikiana katika kusaka rasilimali za uendeshaji wa Tamasha hilo la Kimataifa la 38.


Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano iliyofanyika ukumbi mkubwa wa maonesho wa TaSUBa, Dk. Makoye, anasema lengo kuu la makubaliano hayo ni kutafuta rasilimali zitazowezesha kuendesha tamasha hilo lenye lengo la kuenzi, kudumisha na kutunza utamaduni wa Mtanzania.


Anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1982, tamasha limekuwa likifanyika kila mwaka bila kukosa mbali na kukumbwa na uhaba wa fedha, lakini anaamini kwa kushirikiana na kampuni kubwa ya biashara ya Clouds Plus Production, tamasha linaweza kuvutia wawekezaji mbalimbali.


Naye Mkurugenzi Uendeshaji wa Clouds Plus Production, Ramadhani Bukini, anasema kampuni yake inayomiliki runinga na redio, itatumia mbinu mbalimbali kulitangaza tamasha hilo Duniani ili kufanya lifikie malengo yake ya kuenzi na kudumisha utamaduni wa Mtanzania na pia  kuvutia wawekezaji wengi.

Ratiba mahsusi

Dk. Makoye, anasema katika wiki ya tamasha zipo siku zitakuwa maalum kwa ajili ya ratiba mahsusi, ambako Jumatatu itakuwa ni ‘Usiku wa Filamu’, Jumatano ‘Usiku wa Muziki wa Dansi’ na Jumapili ‘Usiku wa Taarabu’.


Wasanii wanaotarajiwa kupanda jukwaani
Wasanii wanaotarajiwa kupanda jukwaani mwaka huu ni Khamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, Juma Kassim ‘Juma Nature’, Barnaba Elias ‘Barnaba’, Dullah Makabila, Gigy Money na Vitalis Maembe.


Wengine ni Mashauzi Classic, Malkia Khadija Kopa, Thabit Abdul, Bendi ya Msondo Ngoma, John Kitime na bendi yake, Sisi Tambala, Sinaubi Zawose, Shada Acrobatics na Baldreda kutoka Marekani.


Dk. Makoye, anabainisha kuwa pia makundi ya hapa nchini yatashiriki, ambapo Bagamoyo itatoa 37, Dar es Salaam 28, Zanzibar mawili huku mikoa  ya Mwanza, Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro, Njombe yatatoa kundi moja moja, Arusha mawili na Dodoma 10.


Makundi kutoka nje ya Tanzania, Marekani yatakuwa mawili, Botswana, Korea Kusini, Zimbabwe, Uganda, Zambia na Finland kundi moja moja huku kutoka Kenya yakiwa nane.


Mgeni rasmi ufunguzi/ufungaji

Dk. Makoye, anaweka wazi mgeni rasmi wakati wa ufunguzi katika tamasha la mwaka huu, anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe huku wakati wa kufunga atakuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza.

WANAFUNZI WAMUOMBA SONGE KUFIKISHA SALAMU ZAO KWA RAIS DKT MAGUFULI.

 Na Shushu Joel

WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya kijereshi iliyoko katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu wamemuomba mjumbe wa kamati ya siasa mkoani Simiyu Simon Songe kufikisha salamu zao za dhati kwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kitendo cha kufanya watoto wa masikini kusoma.

Wakitoa salamu hizo wanafunzi hao katika mahafali ya kidato cha nne walisema kuwa wazazi jambo la Rais Dkt Magufuli kuwafutia ada imekuwa ni faraja kubwa kwao na familia zao.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Pula John alisema kuwa wanafunzi wengi ndoto zao ni kuja kulisaidia taifa lakini wengi wao zilizima kutokana na familia nyingi ni masikini.

"Tunakuomba Simon Songe kufikisha salamu zetu kwa Rais kwani wewe ni kiongozi mkubwa katika mkoa wetu wa simiyu hivyo salamu zetu zitafika"

Aliongeza kuwa wanampongeza Songe kwa kuthamini sherehe ya wanafunzi hao ingawa majukumu yake ni mengi lakini amefika na kutatua baadhi ya changamoto za shuleni hapo.

Aidha katika mahafari hayo Songe ameweza kusaidia vitu mbalimbali kwa ujenzi wa miundombinu ya shule, jezi za michezo kwa wavulana na wasichana, mipira na pesa taslimu.

Naye mkuu wa shule hiyo Zakaria Miyeye amempongeza Simon Songe kwa hotuba yake ya kuwataka wanafunzi waliopo mashuleni kutumia fursa iliyotangazwa na serikali ya awamu ya tano ya kusoma bure.

Songe ni kijana mwenye busara na ushauri mzuri kwa vijana hivyo watu kama hawa ni hazina ya pekee katika taifa.

Kwa upande wake Mgeni rasmi Simon Songe amewahakikishia wanafunzi wa shule hiyo kuwa salama hizo zitamfikia mh Rais Magufuli bila wasiwasi.

"Nadhani mmeona jinsi wadogo zenu wa darasa la saba walivyoutangaza mkoa wa simiyu Kwa kuwa kumi bora"Alisema.

Hivyo amewataka wanafunzi wote wa kidato cha nne katika mkoa wa simiyu kutumia vizuri ubunifu wa hali ya juu unaofanywa na mkuu wa mkoa Antony Mtaka kwa kuanzisha makambi kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani.

WAZEE TUNU YA TAIFA,TUWATUNZE- KIKWETE.

Na Shushu Joel

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Mh. Ridhiwani Kikwete amewataka vijana nchini kuwalinda, kuwatunza na kuwajali Wazee ambao ndiyo Walezi wa Jamii yetu.

Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na baadhi ya Wazee wa kata ya Bwilingu katika halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

"Wazee wamelipigania taifa hili , na sasa ni Muda muafaka wa sisi kupambana ili kulinda maslahi yao, wazee hawa walipambana sana kutufikisha tulipo, leo amani tunayoiona na maendeleo haya ni kazi waliyo asisi na hivyo juhudi zao zimetufanya sisi kuwa na amani kubwa na kuwa Mfano wa kuigwa na baadhi ya mataifa"Alisema Kikwete.

Aliongeza kuwa serikali ya Tanzania imejipanga ili kuhakikisha wazee wanaenziwa na kunufaika na nchi yao kutokana na kile walichokifanya wakati wa ujana wao.

Wamekuwa mstari wa mbele kushauri hivyo amewataka vijana kuongea na wazee mara kwa mara kwani wanaushauri mzuri juu ya mwenendo wa maisha yetu kama vijana.

"Vijana wengi tumeshindwa kujua na kutambua historia ya wazee wetu kutokana na kutokuwa karibu nao ili kujua jinsi wao walivyokuwa wakiishi na hivyo kujifunza toka kwao", Alisema.

Kwa upande wake Mzee Said Bwilingu (87) alisema kuwa amempongeza Mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete Kwa jinsi anavyowajali wazee Kwa kuwatembelea kila wakati na kuwajulia hali zao.

"Hivyo wazee tumefarijika sana kutembelewa na mjukuu wetu, sisi tuliishi na Wazee wake na hivyo Analolifanya mbunge ni kufuata mwenendo ulioasisiwa na wazee wake." Aliongeza kuwa amani ya nchi yetu inatokana na jinsi tulivyokuwa na umoja na mshikamano wenye nia ya kujenga taifa letu la Tanzania.


Wazee musiwatenge, Watembeleeni ili muweze kufaidika na mawazo yao japo vijana mnaona wa kizamani, alisema mzee huyo.

Aidha mzee huyo alisema kuwa anafarijika kuona jimbo la chalinze linavyozidi kupata maendeleo makubwa ambayo kipindi hicho ilikuwa ni historia lakini kwa sasa mambo mengi yanafanyika na kuleta neema kwa wananchi.

Pia amempongeza mbunge Ridhiwani Kikwete kwa ufanisi wake katika kuwatumikia wananchi wa jimbo lake kwani wakati wetu maji, umeme, huduma za afya na miundombinu vilikuwa ni changamoto kubwa.