Wednesday, October 9, 2019

MFUMUKO WA BEI WASHUKA HADI ASILIMIA 3.4 KITAIFA

Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana Oktoba 8, 2019 wakati akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba 2019 ambao umeshuka hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka unaoishia mwezi Agosti, 2019.
.....................................


Na Mwandishi Wetu


Mfumuko wa Bei  wa Taifa kwa mwezi septemba, 2019 umepungua  hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.


Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja wakati akitangaza mfumuko wa bei hapo jana Tarehe 08 Oktoba 209 Jijini Dodoma.


“Kushuka kwa mfumuko wa bei kunatokana na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwezi Septemba 2019 ikilinganishwa na bei za kipindi cha  Septemba,2018”. Alisisitiza Bi. Minja.


Akifafanua amesema kuwa baadhi ya bidhaa zilizopungua bei kwa mwezi Septemba ni mafuta ya taa asilimia 1.0, Petroli asilimia 3.3 ,majiko ya gesi asilimia 1.5, dawa za kuulia wadudu nyumbani asilimia 2.2 na mafuta ya nywele asilimia 1.3.


Aliongeza kuwa mfumuko wa Bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.


Akizungumzia nchi za Afrika Mashariki Bi. Minja amesema kuwa mfumuko wa Bei nchini Kenya  kwa mwezi Septemba umepungua hadi asilimia 3.83 kutoka 5.00 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.


Kwa upande wa nchi ya Uganda, mfumuko wa Bei kwa mwaka unaoishia mwezi Septemba 2019 umepungua hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka unaoishia mwezi Agosti, 2019.

RATIBA YA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA 2019.

HALMASHAURI ZATAKIWA KUWASAIDIA WATU WENYE ULEMAVU

Na Hadija Hassan, Lindi.

Halmashauri zimetakiwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu (walemavu) ambao wamepewa mikopo ya asilimia 2 inayotokana na asilimia 10 ya fedha za mapato ya Ndani katika Halmashauri zao kuwatafutia masoko ya uhakika ya bidhaa wanazozizalisha ili kuhakikisha fedha walizokopa wanarejesha kwa wakati.

Wito huo Umetolewa na kiongozi Wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally  alipotembelea na kuona kazi mbali mbali za mikono zinazofanywa na vikundi vya wajasiriamali wa Halmashauri ya wilaya ya Lindi ambavyo vimepewa mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri.

Ally, alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kundi, hilo ni kushindwa kutangaza bidhaa walizozizalisha ukilinganisha na makundi mengine kama ya vijana na Wanawake jambo ambalo huwafanya kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Alisema Serikali ilivyoamua kutoa mikopo hii ilikuwa na lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi pamoja na kuwawezesha kuondokana na umasikini hivyo ni wajibu wa Halmashauri kusaidia kundi hilo muhimu.

Awali afisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri hiyo ya Lindi Grace Mwambe alisema kuwa Halmashauri hiyo ipo msitari wa mbele katika kuwawezesha Wananchi kiuchumi hasa kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Alisema katika kutekeleza maagizo ya Serikali juu ya kukopesha makundi hayo kwa asilimia 10 za fedha zinazopatikana katika mapato ya ndani.

Halmashauri hiyo imeweza kutoa kiasi cha shilingi milioni 27 kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 kwa vikundi 17.

Aidha akiongeza kuwa kati ya vikundi hivyo 17 vilivyopewa mikopo hiyo , vikundi 7 vya vijana, vikundi 8 vya wanawake na 1 cha watu wenye ulemavu

WANAFUNZI 11 WAPATA MIMBA KIBITI

Na Omary Mngindo, Kibiti.

WANAFUNZI 11 wanaosoma katika shule ya sekondari ya Kata ya Mjawa wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, wamepata mimba katika kipindi cha miaka miwili, kwa kuanzia 2018/2019.


Hayo yamebainika katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Umoja wa Wanawake (UWT) mkoani hapa mwishoni mwa wiki, ikiwa ni siku moja kabla ya kuhitimishwa kwa wiki ya wanawake, ambayo kimkoa imefanyika wilayani Kibiti.


Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Yusufu Mkupi ameuambia msafara huo ulioongozwa na Arafa Kisera, Khatibu Chaurembo, Joyce Shauri, Josephine Gunda na Zaynabu Chitanda, kuwa kwa mwaka 2018 wamepatikana wanafunzi watano waliopata mimba.


"Mwaka 2018 wanafunzi watano waliacha shule kwa ajili ya mimba, mwaka huu 2019 mwezi wa pili wanafunzi wengine watano wamebainika wana ujauzito, na mwezi wa nne tulipowapima amepatikana mwingine, hivyo kufanya wanafunzi 11 kukatisha masomi kwa mimba katika miaka hii miwili," alisema Mkupi.


Mkupi aliongeza kuwa sababu kubwa ya kushamiri kwa matukio hayo ni uhuru wanaopatiwa wanafunzi hao, ambao wanaangalia video kwenye mabanda mpaka saa 5 au 6 usiku, na wanaporejea majumbani hakuna mzazi anayemuuliza mtoto wake.


Akizungumza na wanafunzi hao, Arafa Kisera amesikitishwa na hali hiyo, ambapo aliwaambia kuwa matukio hayo ni ya aibu, na hasara kwao, huku akiwanyooshea kidole wanafunzi wa kiume wanaojihusisha na vitendo vya kuingilia kinyume cha maumbile.


"Siku hizi kumezuka tabia ya watoto wa kiume kuvaa nguo zao mlegezo, jiangalieni msijihusishe na kuingiliana kinyume cha maumbile, vitendo hivyo ni hasara kwenu hata mkija kuoa hamtakuwa na uwezo wa kuzalisha," alisema Kisera.


Kwa upande wake Khatibu Chaurembo ambaye ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibiti, amewataka walimu hao kumpatia majina ya wanafunzi wote walioacha shule kwa ajili ya mimba, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.


"Hili ndio kwanza nimelisikia hapa, walimu nipeni majina ya wanafunzi wote waliopata mimba, tutakwenda kukaa na Kamati husika pamoja na viongozi mbalimbali, ili kuhakikisha tunachukua hatua stahiki kwa walengwa," alisema Chaurembo.


Nae Joyce Shauri, amewataka wanafunzi hao kutoona aibu kuwataja wanaojihusisha na vitendo hivyo, huku akiwaambia kwamba kwa sasa mwanafunzi atakayebainika kushika mimba yeye na aliyehusika wote wanashitakiwa.

WANANCHI ELFU 83 BUKOBA WATARAJIWA KUJIANDIKISHA KWAAJILI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Aliyevaa suti nyeusi ni mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti akikagua vituo vya kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura serikali za mitaa.   Mkoa wa Kagera unatarajia kuandikisha wananchi milioni moja laki mbili na elfu themanini huku vituo vikiwa ni 3,738.
...............................


Na Alodia Dominick, Bukoba

Wananchi wa manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wanaokadiliwa kuwa elfu themanini na tatu (83,000) wameanza kujiandikisha katika mitaa Yao kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa.

Msimamizi wa uchaguzi katika manispaa ya Bukoba Richardi Mihayo amesema kuwa, manispaa ya Bukoba inavyo vituo vya kujiandikisha vipatavyo 66 na wanatarajia wananchi 83,000 watajiandikisha katika zoezi hilo ambalo limeanza Octoba 08 na litaisha octoba 14 mwaka huu.

Akikagua baadhi ya vituo mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti akiwa kituo cha Kabangamilembe kata ya Hamugembe manispaa ya Bukoba ametoa wito kwa wasimamizi wa vituo mbalimbali mkoani Kagera kuhakikisha wanaandikisha wananchi wa mitaa husika na siyo kufanya hujuma kwa kuwaandikisha wananchi ambao wanatoka vitongoji jirani.

Brigedia Gaguti ameongeza kuwa, sheria lazima ichukuliwe kwa wale watakaobainika wanajiandikisha kwenye vitongoji ambavyo siyo wakazi husika na kuwa wananchi wa mkoa wa Kagera wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye vitongoji vyao ili waweze kuwachagua viongozi wanaofaa katika uchaguzi huo unaotarajia kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Kabangamilembe kata ya Hamugembe manispaa ya Bukoba Zainabu Mugusha amesema katika kitongoji chake wananchi wanaendelea kufika kwenye kituo kujiandikisha ingawa wanakuja kwa kasi ndogo.

Mmoja wa waliokuja kujiandikisha katika kituo hicho Masoud Ibrahim amesema, zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura za serikali za mitaa baadhi ya wananchi wanalichangaya na zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupata kitambulisho cha mpiga kura katika uchaguzi mkuu mwaka kesho hivyo serikali inapaswa kutoa elimu kwa jamii ili wananchi watofautishe mazoezi hayo mawili.