Tuesday, September 24, 2019

JUMAA AKABIDHI MIONGOZO NA BOKSI ZA KARATASI ZA UCHAGUZI.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa (kushoto) akimkabidhi Raphael Maumba boksi za karatasi na miongozo kwa ajili ya chaguzi za viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, vilivyogharimu sh. Mil. 2.5. Picha na Omary Mngindo.

 ................................

Na Omary Mngindo, Mlandizi.

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, amemkabidhi Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Raphael Maumba, boksi za karatasi na miongozi mbalimbali zinazohusiana na chaguzi.

Karatasi na miongozo hiyo itakayotumika kwa ajili ya maandalizi ya chaguzi kuanzia ndani ya chama hicho, ni katika kuelekea kuchagua Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji, mchakato utakaoanzia kwenye ngazi za matawi ya chama hicho.


Akikabidhi vifaa hivyo kwa Maumba ambaye ni Katibu wa chama hicho wayani hapa, Jumaaa alisema kuwa boksi hizo za karatasi pamoja na miongozo vilivyogharimu kiasi cha shilingi milioni 2.5, vinalenga kuwaanda wanachama hao kuelekea kwenye uchaguzi unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.

"Nakukabidhi boksi za karatasi kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea kwenye chaguzi zinazokuja, sanjali na hayo pia, pokea miongozo inayotuelekeza nini cha kufanya wakati tunaelekea kwenye chaguzi hizo, hakikisha zinafika kwenye matawi," alisema Jumaa.

Aidha Jumaa aliwataka wana-CCM kila mmoja kutumia haki yake ya ndani ya chama hicho ikiwa ni pamoja na kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali, hivyo wajiandae na chaguzi hizo.

Kwa upande wake Maumba akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo, huku akisema kwamba umewafikia wakati mwafaka kwani katika kipindi hiki cha kuelekea chaguzi kunahitajika vitendeakazi kama hivyo.

"Nikuahidi Mbunge kwamba msaada huu umetufikia wakati mwafaka, na kwamba zitawafikia walengwa katika matawi yetu, ili wanachama wajifunze mambo mbalimbali yanayohusiana na chaguzi," alisema Maumba.

WEZI WAIBA KOMPYUTA SHULE YA MSINGI MSOGA, CHALINZE.

 
Kamanda wa Polisi, mkoa wa pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa,akiwaonyesha waandishi wa habari vifaa mbalimbali vilivyokamatwa kwenye msako unaondeleo mkoani humo.


NA MWAMVUA MWINYI, PWANI.

JESHI la polisi mkoani Pwani ,linawashikilia watu watatu wanaodaiwa kuiba kompyuta mpakato saba zenye thamani ya sh. milioni 4.2 mali ya shule ya msingi Msoga iliyopo Chalinze wilayani Bagamoyo.

Aidha Jeshi hilo, limewakamata watu 67 kwa tuhuma za kufanya uhalifu mbalimbali ,katika misako inayoendelea mkoani humo.

Kamanda wa Polisi, mkoa wa pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake, kuwa siku ya tukio watu wasiojulikana walivunja kwenye shule hiyo na kuiba vifaa hivyo.


Alieleza, tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo baada ya tukio hilo uongozi wa shule ulitoa taarifa polisi ambao walianza msako na walikamata watu hao wakiwa na kompyuta tatu.


“Tunaendelea na uchunguzi kwa watu wengine ambao watakuwa na hizo kompyuta nne zilizobakia ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,”alisema Wankyo.


Katika tukio lingine Said Athuman (32) Mkazi wa mkoa wa Tanga amekamatwa kwa tuhuma za kukutwa na matairi ya pikipiki 100 na 75 ya bajaji ambayo yanadhaniwa kuwa hayakulipiwa ushuru.


Alisema kuwa, tukio hilo lilitokea septemba 21 mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku eneo la Round About kata ya Dunda tarafa ya Mwambao wilaya ya Bagamoyo.


Kamanda Wankyo, alifafanua ,mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia gari aina ya Mazda Pick Up yenye namba T 135 DPU ambapo gari hilo lilikamatwa wakati polisi wakiwa doria na inadhaniwa mali hizo zilipitia kwenye bandari bubu zilizopo Bagamoyo.


Pia mkazi wa Lugoba Mtupe Abdala (45) anashikiliwa kwa tuhuma za kusafirishama mbao ngumu 60 kwa kutumia gari lake aina ya Howo lenye namba za usajili T 693 CEH/T 672 DSK bila ya kuwa na kibali.


Hata hivyo, Kamanda Wankyo, alisema polisi walimkamata mtuhumiwa septemba 20 eneo la Chalinze Mzee tarafa ya Chalinze wilaya ya Kipolisi Chalinze katika msako unaoendelea wa usiku na mchana wa kukamata wahalifu.

Sunday, September 22, 2019

TAMASHA LA JINSIA 2019: TGNP WAMTAJA MAMA GETRUDE MONGELA KUWA MGENI RASMI




Mkurugenzi Mtendaji TGNP akifafanua jambo kwa waandishi wa habari

Na Selemani Magali, Dar es Salaam.

Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kufanyika kwa Tamasha la 14 la jinsia, TGNP Mtandao limemtaja Balozi Mama Getrude Mongela kuwa mgeni rasmi katika tamasha la 14 linalotarajiwa kuanza September 24 hadi  27,  2019.
Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Lilian Liundi wakati akizungumza na  waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Akifafanua sababu za kumpa heshima Mama Mongela kuwa Mgeni Rasmi katika Tamasha hilo la 14, Liundi amesema kuna sababu nyingi za kufanya hivyo lakini kubwa ni harakati zake alizozifanya hadi kufikia hatua za kuleta mageuzi ya jinsia hapa Nchini.
“Amesema kuwa kipekee Tanzania itakumbukwa katika historia  kwa kuweka misingi ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake kwani katika mkutano wa Beijing Balozi Getrude mongela aliibuka kidedea katika mkutano huo” alisema Mkurugenzi.
Katika hatua nyingi, Mkurugenzi amebainisha kuwa zaidi ya watu 1000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki Tamasha la mwaka huu.
 
Tamasha hilo litakaloongozwa na kauli mbiu inayosema  'Wanaharakati wa Jinsia Mbioni Kubadilisha Dunia' limeandaliwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za wanawake na usawa wa kijinsia na wanaharakati binafsi.

Lilian Liundi amesema washiriki wa tamasha hilo watakuwa ni pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka ndani na nje ya nchi,viongozi mbalimbali kutoka ngazi ya halmashauri na serikali kuu,wanaharakati na wananchi.

"Tunatarajia tamasha la Jinsia la Mwaka huu litakuwa la kipekee kwani kitaifa na kidunia tumeanza kusherehekea maadhimisho ya miaka 25 ya Azimio na Mpango kazi wa Beijing ambapo kilele chake ni mwaka 2020”

Kwa njia moja au nyingin maandalizi ya mkutano wa Beijing yalikuwa chachu kubwa ya kuanzishwa na kuimarishwa kwa asasi nyingi zinazotetea haki za wanawake ",alisema.

"TGNP ni mojawapo ya asasi iliyoleta chachu kubwa ya kuunganisha wadau mbalimbali kutoka vikundi vya wanawake,wanazuoni na mitandao ya wanawake kupata sauti ya pamoja katika ushiriki wa mkutano wa Beijing,hivyo TGNP inaendelea kusherehekea uwepo wake kwa zaidi ya miaka 25 sambamba na maadhimisho ya mkutano wa Beijing",alieleza Liundi.

Alisema Tamasha hilo linatoa fursa kwa asasi za kiraia zilizoshiriki katika mchakato wa Beijing kutakafari na kusherehekea uwepo wa asasi hizo kwa zaidi ya miaka 25 ambapo azimio na mpango kazi Beijing ndiyo iliyoweka misingii ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake kidunia.
 
"Katika kuendelea kuenzi na kuthamini mchango wa Mama Getrude Mongella,TGNP na Tapo la Ukombozi,tumeamua kumchagua Balozi Mhe. Dr. Getrude Mongella aliyeongoza mchakato wa Beijing na pia mchakato wa 'Kuileta Beijing Nyumbani' kuwa mgeni rasmi wa Tamasha la Jinsia mwaka huu",alifafanua Liundi. 

Hata hivyo Liundi alisema mgeni maalum kutoka serikalini atakuwa Naibu Waziri- Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Mhe. Dr Faustine Ndugulile.

Alibainisha kuwa tamasha hilo litahusisha mawasilisho,mijadala ya pamoja,maonesho na warsha,kusherekea mchango wa mashujaa wanawake katika kufikia haki na usawa wa kijinsia.

Saturday, September 21, 2019

Serikali yaja na muarobaini wa kupunguza foleni Dar

 


Serikali imeanzisha miradi ya kupunguza foleni jijini Dar es Salaam ili kupambana na sumu inayozalishwa kutokana na tatizo hilo.

Akizungumza leo Jumamosi Septemba 21, 2019 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene wakati akizindua kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani, Simbachawene amesema Serikali ina miradi mbalimbali ya kupunguza gesi ukaa nchini.

Ameitaja baadhi ya miradi hiyo ni wa mabasi yaendayo kasi  lengo likiwa ni kupunguza foleni na idadi ya magari barabarani.

Mingine ni miradi ya ujenzi wa barabara za juu itakayosaidia kupunguza muda wa kukaa barabarani.

“Ile hali iliyoko Dar es Salaam ya kukaa muda mrefu kwenye foleni inazalisha hewa ukaa nyingi. Na hivyo kwa mtu aliyeko Dar es Salaam anakula sumu kwa kiasi kikubwa sana kuliko aliyeko Dodoma kwa sasa au kijijini,” amesema.

Amesema wanaoishi Dar es Salaam hukaa husimama katika foleni kwa saa saba bila kufika anakokwenda, kubainisha kuwa ni maisha hatari kwa binadamu kuliko ya mtu anayeishi miji isiyo na changamoto hiyo.

RC MAKONDA KUWAWEKA KIKAANGONI WATENDAJI WALIOSABABISHA MIRADI YA KIMKAKATI KUTOTEKELEZWA KWA WAKATI



Mkuu wa Mkoa wa Dar ea salaam *Mhe. Paul Makonda* amehitisha *kikao* baina yake na watendaji wa Mkoa huo wakiwemo *Wakuu wa Wilaya, Mamea, Wakurugenzi wa Manispaa, Makatibu tawala na wakuu wa Idara* ili wamueleze ni kitu gani kinachowafanya *miradi ya kimkakati* ikiwemo Machinjio ya *Vingunguti* na Ufukwe wa *Coco* imechelewa kutekelezwa licha ya *Rais Dkt. John Magufuli* kutoa fedha za miradi hiyo lakini *fedha hizo zimeishia kukaa kwenye Akaunti* pasipo utekelezaji.

*RC Makonda* amesema katika mkutano huo utakaofanyika Jumatano ya *September 25* Ukumbi wa Karimjee *mtendaji atakaebainika kusababisha uzembe huo atawajibisha*  hapohapo kwa mujibu wa sheria na wengine *watazuiwa mishahara yao.*

Aidha *RC Makonda* ametoa wito kwa *Wizara ya Utumishi na TAMISEMI* kutafuta *njia bora ya kuwapata wakuu wa Idara wenye uwezo wa kuleta matokeo Chanya* tofauti na sasa ambapo *wengi wao wamepanda na kuwa wakuu wa idara kwa kigezo cha kukaa kazini Muda mrefu.*

Hayo yote yamejiri leo wakati wa hafla ya *kutoa zawadi kwa walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika taaluma na Michezo.*