Friday, July 19, 2019

WANAFUNZI WA SHULE YA VIPAJI YA KIBAHA SEKONDARI KUONDOKANA NA CHANGAMOTO YA UCHAKAVU WA MADARASA


Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita wanaosoma katika shule ya Kibaha sekondari  mkoani Pwani wakiwa darasani wakiendelea na masomo yao ya kawaida kwa ajili ya kujiandaa na mitihani yao mbali mbali ya majaribio na ule wa Taifa.
..................................


VICTOR MASANGU, PWANI 

SHULE kongwe ya wavulana ya vipaji maalumu  ya Kibaha sekondari iliyopo  Mkoani  Pwani licha ya  kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita kwa  mwaka wa 2018 na kushika nafasi ya sita kwa mwaka 2019  bado wanafunzi wake kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa walimu ya masomo ya sayansi, uhaba wa vitabu, uchakavu wa miundombinu ya madarasa, uhaba wa vitanda pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo.

Hayo yamebaishwa  na baadhi ya wanafunzi hao akiwemo Jonasi Baraka ambaye ni kaka mkuu wa serikali ya wanafunzi wa shule hiyo  pamoja na Kalani Mahila  ambapo wamedai kuwa serikali ya awamu ya tano inapaswa kulivalia njuga suala hilo kwa kuharakisha kufanya ukarabati wa majengo hayo ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Aidha  wanafunzi hao wamesema kwamba   lengo  kubwa ni kuhakikisha wanasoma  katika mazingira rafiki ambayo yatawafanya waongeze kiwango cha ufaulu, hivyo wameiomba serikali ya awamu ya tano kuwakarabatia majengo.

"vyoo vinavyotumika kwa sasa ni vinne tu, kwa idadi ya wanafunzi vyoo vingine vimefungwa kutokana na ubovu, na tuna uhaba wa maabara na walimu wa masomo ya sayansi

“Kwa sasa kwa kweli shule yetu ya Kibaha tunakabiliwa na changamoto mbali mbali lakini kitu kikubwa tunachohitaji kutoka kwa serikali ya awamu ya tano ni kutuboreshea  sekta ya elimu kwa kutufanyia ukarabati wa miundombinu ya majengo mbali mbali yakiwemo ya madarasani, vyoo, pamoja na mabweni ambayo kwa hali yake kwa sasa sio nzuri yamechakaa, na sisis nia yetu ni kushika nafasi ya kwanza kitaifa,”walisema wanafunzi hao.


Naye  mmoja wa wajumbe wa kamati ya wazazi ya maendeleo katika shule ya Kibaha Sekondari  Dk. Hamisi Likuli amekiri kuwepo kwa changamoto mbali mbali  zinazowakabili wanafunzi hao, ambapo alibainisha hatua ambazo  tayari wameshazichukua ni kuimarisha huduma ya afya, kuboresha miundombinu ya majengo na vyoo kujenga uzio pamoja na upatikanaji wa huduma ya maji kwa kuweka matanki pamoja na kuchimba kisima.


Katika kukabiliana na changamoto hizo Mkuu wa shule hiyo ya Kibaha Chrisdom Ambilikile ameamua kuja na mpango wa kuwakutanisha viongozi mbali mbali wa serikali pamoja, wabunge  pamoja na wadau wengine ambao wamesomea katika shule hiyo kwa  dhumuni la kufanya harambee ambayo inatarajia kufanyika Septemba 9 mwaka huu lengo likiwa ni kusaidia kutatua changamoto ambazo zinaikabili shule hiyo kwa kipindi cha miaka mingi.

Mkuu huyo alibainisha kuwa licha ya shule yake kushika nafasi ya sita kwa mwaka huu katika matokeo ya kidato cha sita kitaifa  lakini kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kimeongezeka  kwa daraja la kwanza kuwa na wanafunzi wapatao 143 waliopata divisheni 1.

“Kwa kweli ukizungumzia kitaalamu utaona sisi shule yetu kwa matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka huu wa 2019 tumeshika nafasi ya sita kitaifa lakini mwaka jana tulishika nafasi ya kwanza lakini kiwango cha daraja la kwanza kimeongezeka sana tumepata wanafunzi 143 kwa hivyo utaona tumefanya vizuri na kuwa na nafasi kubwa ya kuwapeleka wanafunzi wengi vyuoni,”alisema Mkuu huyo.


Pia mikakati yetu tuliyojiwekea ni kushirikiana bega kwa began na wazazi, pamoja na wadau wa maendeleo katika kuiboresha shule hiyo ambayo wanatarajia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya  mradi mkubwa wa ujenzi wa jengo kubwa la kisasa ambalo litakuwa likitumika kwa matumizi mbali ikiwemo maktaba,kompyuta pamoja na mambo mengine yanayohusiana na elimu.


Shule  hiyo kongwe ya Kibaha sekondari yanye wanafunzi 669 na walimu 56 ilianzishwa mwaka 1965  ambapo viongozi mbali mbali wa serikali na wabunge wameweza kusomea hapo akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Spika wa Bunge Job Ndugai sambamba na Free Man Mbowe Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) pamoja na Razaro Nyarandu.
Mkuu wa shule  ya  Kibaha Sekondari  Chrisdom Ambilikile akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake  kuhusiana na mikakati mbali mbali  aliyojiwekea katika kuhakikisha anapandisha zaidi kiwango cha elimu, pamoja na mpango wa kufanya harambee kubwa ya kuwakutanisha viongozi wa serikali na wabunge waliosomea katika shule hiyo ili kuzitatua changamoto zilizopo katika sekta ya ellimu.

Mkuu wa shule  ya  Kibaha Sekondari  Chrisdom Ambilikile akiwaonyesha baadhi ya waandishi wa habari hawapo pichani chumba cha maabara ambacho kimefanyiwa ukarabati na serikali kwa lengo la kuweza kuwapa fursa wanafunzi kujifunza zaidi kwa vitendo.
Kaka mkuu wa serikali ya wanafunzi wa shule  ya Kibaha Sekondari  Jonasi Baraka  akizungumzia changamoto mbali mbali zinazowakabili katika shule hiyo pamoja na mipango waliyojiwekea katika kuongeza kiwango  cha ufaulu katika matokeo yajayo ya kidato cha sita.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya wazazi ya maendeleo katika shule ya Kibaha Sekondari  Dk. Hamisi Likuli akifafanua jambo kuhusiana na hatua mbali mbali ambazo tayari wameshazichukua katika kuhakikisha wanashirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya elimu katika shule hiyo.

(PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU).

Thursday, July 18, 2019

Tanzania Yang’ara Umoja Wa Mataifa Utekelezaji SDGs


Na Saidina Msangi, WFM, New York, Marekani.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) amewasilisha ripoti ya Tanzania kwa mara ya kwanza ya Mapitio ya Hiyari ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika Mikutano ya Jukwaa la Juu la Kisiasa la Ngazi za Mawaziri chini ya Umoja wa Mataifa inayofanyika New York nchini Marekani.

Akiwasilisha ripoti hiyo Waziri Mpango ameeleza kuwa Tanzania imefanikiwa katika utekelezaji wa malengo 17 yaliyoamuliwa kutekelezwa na nchi zote ulimwenguni ili kuondokana na umasikini na kuharakisha maendeleo katika nyanja zote.

Akizungumzia lengo namba nne lenye kuangazia elimu jumuishi na bora kwa wote, Dkt. Mpango ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza ambao wana mwaka mmoja wa elimu ya awali kwa asilimia 95.6 mwaka 2018 ambayo ni juu ya makadirio ya asilimia 87.5 ifikapo mwaka 2020.

Aidha, wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wameongezeka kwa asilimia 17.4 ikiwa ni kutokana na mafanikio ya elimu bure chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Pia Dkt. Mpango aliongeza kuwa Tanzania imefanikiwa katika maeneo ya utoaji huduma bora za afya, uongozi bora na amani ya nchi kwa ujumla.

Ripoti hiyo imepokelewa vizuri  katika Jukwaa hilo la Umoja wa Mataifa ambapo nchi zilizotoa maoni kuhusu ripoti hiyo ikiwemo Kenya zimepongeza juhudi zilizofikiwa na Tanzania katika utekelezaji wa malengo endelevu.

“Malengo haya ndio dira ya maendeleo na yanaunganika na mipango yetu ya maendeleo kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanaendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, na MKUZA kwa upande wa Zanzibar hivyo ni lazima tutekeleze malengo haya kwa bidii,” alisema Waziri Mpango.

Dkt. Mpango ametoa wito kwa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa na nchi zenye utaalamu kuisaidia Tanzania katika matumizi ya teknolojia ili kuweza kufikia azma ya malengo endelevu upande wa utunzaji wa mazingira.

Waziri Mpango amewashukuru wadau wote, sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kwa ushiriki wao katika kuandaa ripoti hiyo kwa kiwango kizuri. Aidha ametoa wito kwa taasisi na sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa rasilimali fedha na utaalamu zitumike kwa ajili ya kushughulikia utekelezaji wa malengo endelevu.

Tanzania imeungana na nchi zote duniani katika utekelezaji wa malengo 17 yaliyoazimishwa  miaka minne iliyopita  ikiwa ni mkakati wa kufikia  ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.

Mikutano hiyo yenye kauli mbiu uwezeshaji wa watu na kuhakikisha ujumuishwaji na usawa imekutanisha nchi mbalimbali ambazo zimetuma wawakilishi kutoka Serikalini na Sekta binafsi, inatoa fursa kwa nchi kuweza kutathmini mafanikio, changanoto na mambo ya kujifunza katika kuelekea utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.