Saturday, May 11, 2019

HALMASHAURI ZIJIANDAE KUKABILIANA NA UGONJWA WA PUMU.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati wa maadhimsho ya siku ya Pumu Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.
...................................


Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amezitaka halmashauri kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya visanduku vya huduma ya kwanza kwa ugonjwa wa pumu katika shule zote za msingi na sekondari.
 
Pia amesema ni lazima wakurugenzi katika halmashauri zote kuwa na visanduku huduma ya kwanza kwa ugonjwa wa pumu na mengineyo katika ofisi zao jambo ambalo litawasaidia wafanyakazi wenye matatizo hayo kupewa huduma ya kwanza kabla ya kufika hospitalini.
 
Jafo alitoa maagizo hayo jijini Dodoma baada ya maandamano ya kuadhimisha Siku ya Pumu Duniani ambayo huadhimishwa Mei 7 kila mwaka.
 
Alisema tatizo la pumu ni kubwa na takwimu zinaonesha kuwa nusu ya watu wenye pumu ni watoto ambao wengi wapo mashuleni na hawana uwezo wa kujisaidia.
 
“ Ukiangalia takwimu za Shirika la afya zinasema vifo vinavyotokana na pumu hapa nchini ni zaidi ya 2,000, sasa kama nusu ya hao ni watoto hii inamaanisha tunapoteza shule mbili nzima, yaani wanafunzi wa shule iliyokamili kutoka Darasa la Kwanza hadi la Saba. 

Hii inaonesha tatizo hili ni kubwa na kwamba ipo haja ya kutathimini kama taifa.”
 
Kutokana na hali hiyo, Jafo aliagiza halmashauri katika bajeti ya mwaka 2020/2021, halmashauri zitenge fedha kiasi cha Shilingi laki moja, 100,000 kwa kila shule katika eneo lake ili kununua visanduku viwili vya huduma ya kwanza kwa ugonjwa wa pumu.
 
“ Ghamara ya first aid kit moja ya huduma ya kwanza kwa ugonjwa wa pumu ni Sh 50,000 hivyo kila shule ikitengewa kits mbili haitakuwa fedha kubwa, Hivyo kwa shule zote zaidi ya 17,000 kutenga Sh bilioni 1.7 kwa hili sio fedha nyingi. 

Maadamu bajeti imeshipita, tutakapoanza maandalizi ya bajeti nyingine, halimashauri iliingize hili.”
 
Jafo alisema jamii kubwa ya Watanzania haina ufahamu wa tatizo la ugonjwa wa pumu, dalili na namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa wa aina hii hivyo ametaka maadhimisho hayo kupewa kipaumbele kwa Waganga wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo yao kuadhimisha siku hii kwa kutoa elimu katika jamii na mashuleni.
 
Pia ametumia nafasi hiyo kuziagiza halmashauri na mipango miji kutenga maeneo kwa ajili ya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukizo, akiutaka mkoa wa Dodoma kuangalia namna ya kutenga siku moja kwa mwezi kwa walimu na wanafunzi kushiriki katika mazoezi.
 
Jafo pia alisema kwa kushikiana na wizara nyingine wataangalia namna ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhudumia magonjwa yasiyoambukiza na kuangalia namna ya magonjwa haya kuingizwa kwenye mitaala ya elimu ili wanafunzi wapate elimu ya awali kama ilivyo kwa HIV.
 
Aidha, Jafo aliwapongeza waandaaji wa maadhimisho hayo kwa kazi ya kuwafundisha walimu 40 ambao wamepewa mafunzo ya namna ya kutoa huduma kwa wananfunzi wenye ugonjwa wa pumu na kushauri kutoa mafunzi kwa walimu wa walimu na kushauri wigo wa kufundisha walimu hao kuongezwa.
 
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Magonjwa ya Mfumo wa Hewa (TARD) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukuza (Tancida), Dk Digina Riwa alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha dunia inawagonjwa zaidi ya milioni 3 huku nusu ya wagonjwa hao ni watoto.
 
Alisema kwa Tanzania tawkimu hizo zinaoneshwa kuwa vifo 2,491 vinatokana na ugonjwa wa pumu na kuwa kutokana na makadirio ya kuwa wagonjwa wa pumu wanaweza kuongezeka kwa asilimia 30, Shirikisho hilo likajikita katika kutoa elimu.
 
Akizungumzia sababu ya maadhimisho hayo jijini Dodoma, Riwa alisema ni baada ya kubanika kuwapo kwa tatizo hilo na kutoa takwimu kuwa kwa mwaka jana 2018 pekee wilaya ya Mpwapwa ilikuwa na wagonjwa 1,223, Kongwa ni 1,101, Chemba ni 1,459 na Chamwino wagonjwa 1512.
 
Alisema katika kuadhimisha mwaka huu wameamua kufanya upimaji katika shule za msingi na sekondari ambapo wameweza kuwapata wale ambao wanajitambua kuwa na ugonjwa, lakini idadi kubwa ya wanafunzi walikuwa hawajitambui.
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mwanahamisi Mukunda aliahidi kuwa mkoa utaendeleza mkakati wa kutambua na kubaini watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa pumu.
 
“ Kwetu sisi mmetusaidia kubaini ukubwa wa tatizo, tumekuwa hatufanyi vizuri kwenye ufaulu kwenye mitihani ya taifa na tulikuwa tunatafuta mchawi, kumbe mmoja wa mchawi ni tatizo la pumu ambalo linachangia wanafunzi kukosa masomo.”alisema

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akiongoza matembezi ya pamoja katika kuadhimisha siku ya Pumu Duniani iliyofanyika Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Chama cha Magonjwa ya Mfumo wa Hewa (TARD) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukuzia(Tancida), Dk Digina Riwa akitoa taarifa ya hali ya ugonjwa kwa pumu Nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya Pumu Duniani iliyofanyika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma
Naibu Katibu Mkuu(E) Tixon Nzunda akihitimisha maadhimisho ya ya Pumu Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma
 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akimvisha Medali mshindi wa mashindano ya Uchoraji wa viashairia vya ugonjwa wa Pumu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi wakati wa maadhimsho ya siku ya Pumu Duniani

 
Wanafunzi wa Shule za Wilaya ya Dodoma akimskiliza mgeni rasmi wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Pumu Duniani iliyofanyika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

Katika ya Pamoja ni Viongozi wa OR-TAMISEMI, waandaaji wa maadhimisho ya siku ya pumu pamoja na Walimu wakufunzi wa Ugonjwa wa Pumu baada ya maadhimisho ya siku ya Pumu iliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

KATIBU WA CCM ATOA TAMKO RUFIJI.

Na Shushu Joel, Ikwiriri.


KATIBU wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Omary Mtuwa ametoa onyo kali viongozi na wanachama wa chama hicho wenye tabia ya kujifanya CCM mchana na huku usiku ni wapinzani.


Akitoa onyo hilo Mtuwa alisema kuwa kuna taarifa kuwa baadhi ya viongozi na wanachama CCM wamekuwa na tabia za kukisaliti chama kwa kuwafanyia wapinzani kampeni kipindi cha usiku na kuwapatia taarifa juu ya kile kinachopangwa kwenye vikao vya CCM kuhusu mwelekeo wa ushindi.


Onyo hilo  amelitoa jana wakati wa mkutano na viongozi wote wa kata, matawi na mashina uliokuwa na lengo la kupeana mikakati ya ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu nchi nzima.


"Sasa nawatahadharisha mapema kuwa mtu yeyote yule tutakaye mbaini na tabia hiyo cha moto lazima akione juu yake na lazima ajutie jambo hilo"Alisema.


Aliongeza kuwa Rufiji ilikuwa ngome ya Cuf lakini tangu kuanza kwake kazi wamekuwa na kazi ya kupokea wanachama wa upinzani toka maeneo mbalimbali ya wilaya.


Aidha amewataka viongozi hao kuhamasisha wanachama kulipia ada zao ili utambulisho wao uendelee kuwepo ndani ya chama hicho.


Pia katibu huyo amewataka wana CCM wa Rufiji kutembea kifua mbele kutokana na jinsi hali ya machafuko ilivyokuwa kipindi cha nyuma lakini Mwenyekiti wa CCM Taifa Comred Dkt John Pombe Magufuli amelimaliza na sasa kila jambo ni shwali katika wilaya yetu.


Aliongeza kuwa kutokana na jinsi gani Mwenyekiti wetu wa taifa alivyojitolea kulimaliza jambo hilo sie kama wanarufiji tunampatia Zawadi ya ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa asilimia 95 kama pongezi kwetu juu ya jambo alilotufanyia.


Kwa upande wake katibu mwenezi wa kata ya mgomba Fatma Mohamed amempongeza katibu huyo kwa kuwakutanisha viongozi na baadhi ya wanachama kwa lengo la kujadili mustakabali wa chama Chao na hasa wale wenye tabia ya kuwa wasaliti wa chama hicho.


Aidha amewataka viongozi wenzake kutembea kifua mbele kwani ni makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano hivyo ushindi ni lazima upatikanaji kwa kishindo.


Naye Mbunge wa jimbo hilo Mohamed Mchengelwa amewapongeza viongozi hao kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo na hii ni ishara kubwa hakuna kizingiti cha aina yeyote ile katika uchaguzi wa serikali za Mitaa.


Pia amewataka viongozi hao wa ccm kuyasemea yale yote yanayofanywa na Rais Magufuli katika jimbo hilo kwani ni mengi sana.


Aidha amewahakiishia wananchi kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli ipo makini katika kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanafanyika kwa haraka ili wananchi waweze kunufaika na miradi yao.