Wednesday, April 24, 2019

SERIKALI KUWEKA BEI ELEKEZI YA PEMBEJEO ZA KILIMO-MHE MGUMBA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 24 Aprili 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma


Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo za kilimo (mbegu, mbolea, viuatilifu na zana za kilimo) zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu.


Hatua hizo ni pamoja na uagizaji wa pamoja, ruzuku, kufuta au kupunguza tozo na kodi zinazochangia kuongezeka kwa bei ya pembejeo na kufanya tafiti katika mnyororo wa thamani wa mazao.


Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 24 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ndanda Mhe Cecil David Mwambe aliyetaka kufahamu kwanini Pembejeo za kilimo ni ghali sana, hivyo wakulima wengi hushindwa kununua na kusababisha kupata mavuno haba na kama Serikali ipo tayari kupunguza au kuweka bei elekezi iliyo nafuu kwa mkulima ili aweze kupata pembejeo za madawa, mbolea na zana za kilimo.


Alisema kuwa Serikali ina utaratibu wa kuweka bei elekezi ya mbolea kupitia Mfumo wa Ununuzi wa pamoja nchini kwa mbolea za kupandia aina ya DAP na kukuzia aina ya Urea. Utaratibu huu unalenga
kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu.


Mhe Mgumba aliongeza kuwa katika jitihada za
kuongeza uzalishaji na kipato cha mkulima, Serikali hununua  na kusimamia uthibiti na usambazaji wa viuatilifu vya kupambana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea kama vile kweleakwelea, viwavijeshi, viwavijeshi vamizi, panya, nzige wekundu na nzi wa matunda.


Kadhalika, ili kumpunguzia mkulima harubu katika
uzalishaji na uongezaji thamani ya mazao, Serikali imeendelea kutoa mikopo nafuu ya zana za kilimo kupitia Mfuko wa Taifa wa Pambejeo za Kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Shirika la Maendeleo la Taifa.


Kwa upande wa mbegu na viuatilifu, Mhe Mgumba alisema kuwa serikali inafanya utafiti wa kubaini gharama za uzalishaji wa mbegu kwa kulinganisha na bei za mbegu zilizopo sasa ambao utaiwezesha Serikali kuamua endapo kuna ulazima wa kuweka bei elekezi.


Aidha, Mhe Mgumba pamoja na hatua hizo, Serikali
inahamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, viuatilifu, zana za kilimo na uwekezaji katika mashamba ya mbegu ili kupunguza gharama za pembejeo hizo.

MARIAM KUHAMISHIWA HOSPITALI YA SARATANI OCEAN ROAD

Mariam Rajab Juma (25) akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako ameanza kupatiwa matibabu ya kidonda kinachomsumbua mgongoni sehemu ya bega la kulia. Wataalam wamesema atahamishwa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Mariam akiwa wodini leo wakati waandishi wa habari wakimhoji kuhusu maendeleo ya afya yake.
............................


Baada ya Mariam Rajab Juma (25), mkazi wa Singinda kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa unaomsumbua, wataalam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wameshauri ahamishiwe Hospitali ya Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.


Wiki iliyopita Mariam alifikishwa Muhimbili akitokea mkoani Singida na kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa unaomsumbua katika kidonda kilichopo sehemu ya bega la mkono wake wa kulia.


Akizungumza leo na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Muhimbili, Dkt. Ibrahim Mkoma amesema Mariam ataanza matibabu rasmi katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na kwamba baada ya kumaliza matibabu atarejeshwa Muhimbili kuendelea matibabu zaidi.


Dkt. Mkoma amefafanua Mariam atahamishiwa Hospitali ya Saratani ya Ocean kwa kuwa kuna baadhi huduma za matibabu ambazo anapaswa kupatiwa katika hospitali hiyo kutokana na ugonjwa unaomsumbua.


Daktari alipoulizwa kuhusu ugonjwa unaomsumbua Mariam, Dkt. Mkoma amesema suala la ugonjwa ni siri ya mgonjwa na wataalam wa hospitali na kwamba taratibu za hazimruhusu kuweka wazi  aina ya ugonjwa unaomsumbua mgonjwa.


Naye Mariam amesema amefurahishwa na huduma nzuri ya matibabu aliyopatiwa na walaam wa Muhimbili kwani tangu alipofikishwa hapa amekuwa akihudumiwa vizuri.


“Hivi sasa naendelea vizuri, tangu nimekuja Muhimbili naendelea vizuri. Kabla sijafika Muhimbili nilikuwa siwezi kutembea vizuri lakini sasa naweza kutembea vizuri,” amesema Mariam.


Mariam alifanyiwa vipimo vya CT-scan ya kifua na kichwa, Ultrasound pamoja na vipimo mbalimbali vya damu ambavyo vimesaidia kubaini ugonjwa unaomsumbua Mariam.


Dkt. Mkoma amesema kidonda kilichopo sehemu ya mgongo wa Mariam ni kidonda sugu ambacho kilihitaji kufanyiwa vipimo mbalimbali kubaini ugonjwa unaomsumbua.


Awali, Mariam amesema aliwahi kuugua moto akiwa na umri wa miaka mitano ambapo alitibiwa na kupona ingawa alibaki na kovu kubwa kuanzia sehemu ya mgongo wake hadi kwenye kisogo.


Amesema mwezi wa nane mwaka jana alipata kipele kwenye kovu na baadae kipele hicho kugeuka kuwa jipu. Alipotumbua jipu lilitoa usaha na kisha kuanza kuota kidonda kilichoendelea kuongezeka siku hadi siku.


 “Nilienda kutibiwa katika Hospitali ya Makiungu iliyopo Manispaa ya Singida, lakini pia kutokana na wazazi wangu kutokua na uwezo wa kifedha niliacha kwenda hospitalini na kuanza kusafisha kidonda mwenyewe, huku nikiwaomba marafiki zangu niliosoma nao sekondari wanichangie fedha ili niweze kununua dawa,” amesema Mariam.