Friday, April 5, 2019

JESHI LASHIRIKIANA NA TFS KUPANDA MITI.

Image may contain: 1 person, outdoor and nature
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikina na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam wamepanda miti kando kando ya mto Tegeta.


Katika zoezi hilo lililofanyika asubuhi ya leo Aprili 05, 2019, Katibu wa chuo hicho Kanali Furahisha Ntahena aliwaongoza wanafunzi hao wanajeshi kupanda miti.


Kanali Ntahena amesema wamefikia uamuzi huo kwa lengo la kukabiliana na athari za mazingira ambazo zimeanza kuonekana kutokana na uharibifu uliofanyika.


Alisema jeshi limeona ipo haja ya kushiriki kwenye kampeni ya upandaji miti  kwa kuwa athari za mazingira zinapotokea zinaikumba jamii nzima.


“ Athari za mazingira zikitokea hazichagui, sasa kutokana na uharibifu ambao wote tumeuona tuna kila sababu ya kushiriki kwenye kampeni hii ya upandaji miti,”

“Tunapanda kando kando ya mto Tegeta lakini hatuishii hapa tutapanda pia kwenye maeneo yetu na vilevile tutawapa miti mingine wanajeshi wakapande kwenye makazi yao,” Alisema Kanali Ntahena.


Katika zoezi hilo jumla ya miti 2,000 ilipandwa kwenye mto huo ambao umeathiriwa na shughuli za kibinadamu.


Kwa upande wake Meneja wa TFS wilaya ya Kinondoni Dotto Ndumbikwa ameziomba taasisi na watu binafsi kushiriki kwenye kampeni ya upandaji miti ili kutunza mazingira.


“Ikitokea la kutoa kutokana na athari za uharibifu wa mazingira tutakaoathirika ni wote, hivyo ni muhimu kila mmoja kwenye nafasi yake akatunza mazingira,”

Ndumbikwa ameeleza kuwa katika wilaya yake ya Kinondoni uharibifu wa mazingira ni mkubwa na unachangiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo uvamizi katika maeneo ya mito.
Image may contain: one or more people and outdoorImage may contain: one or more people, people standing, tree and outdoor

POLISI LINDI WAKAMATA DAWA ZA KULEVYA NA GONGO.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Pudensiana  Protasi, akiwaonyesha waandishi wa habari mizigo iliyosheheni dawa za kulevya iliyokamatwa kufuatia doria za polisi mkoani humo kupambana na dawa za kulevya.
.................................
 
NA HADIJA HASSAN- LINDI.

JESHI la Polisi Mkoa wa Lindi limefanikiwa kukamata Dawa za kulevya aina ya Bangi  kilo162 ,Heroine  Gram 9.49 pombe ya moshi (Gongo) lita 177 pamoja na kuvuna shamba la  Bhangi lenye ukubwa wa hekari 6.  


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Pudensiana  Protasi,  alisema kuwa  madawa hayo yamekamatwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia January-march 2019


Kamanda Protasi alisema madawa hayo yamekamatwa kupitia Doria mbali mbali zilizofanywa na Jeshi hilo ikiwa ni moja ya kupambana na Madawa ya kulevya katika Mkoa huo.


Alisema katika Msako huo Wilaya ya Kilwa ndio iliyoongoza kwa kukamata madawa ya kulevya ambapo jumla ya Gram 3.4 , bangi kg 113.975 zilikamatwa  pamoja na kuvuna Shamba la Bangi lenye ukubwa wa hekali 6 ambapo pia katika tukio hilo watuhumiwa 11 walikamatwa


"Wilaya inayofuata ni Lindi ambapo tulikamata madawa ya kulevya aina ya Heroine jumla ya Gram 1.3 pamoja na Bangi kg 48.53 na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 8 wa kiume na wakike 1" alieleza Kamanda Protas.


"Vile vile tulikamata Dawa za kulevya aina ya Heroine Gram 4.79 na huku watuhumiwa 6 wanaume wakikamatwa na wa kike 1 na kufanya jumla ya watu 7,  pia kwa pombe ya Moshi (Gongo) jumla ya Lita 177 pamoja na watuhumiwa wa kiume 25 wa kike 8." Alifafanua Kamanda  Protas


Aidha, Kamanda huyo wa Mkoa Acp Protas  alisema  Washitakiwa wote  wa matukio hayo wameshafikishwa Mahakamani na hatua nyingine za kisheria zinaendelea huku akisisitiza kuwa Jeshi la polisi Mkoani humo litaendelea kufanya doria na misako ya aina hiyo mara kwa mara ili kukabiliana na wahalifu wa aina hiyo
  

Hata hivyo  ACP Protas alitoa Wito kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kuendelea kutoa Taarifa wanapokuwa na mashaka/ wasiwasi juu ya kitu au Mtu yeyote.
 
Mabegi yenye Dawa za kulevya aina ya Bangi  kilo162 ,Heroine  Gram 9.49 ambayo yamekamatwa Mkoani Lindi kufuatia msako uliofanyika ili kupambana na madawa ya kulevya mkoani humo.

MKUTANO WA KUPITISHA KATIBA MPYA TASWA KUFANYIKA APRILI 12 UWANJA WA TAIFA

KAMATI ya Marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imekamilisha hatua zote muhimu kuhusu marekebisho ya katiba hiyo na sasa imeitisha mkutano wa wadau wote Aprili 12 mwaka huu kwa ajili ya kuijadili na kuipitisha rasimu hiyo.


Mkutano huo unatarajiwa kufanyika ukumbi wa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Kamati ya Katiba ya TASWA inaamini mkutano huo utakuwa na tija katika kuboresha rasimu hiyo ili taratibu zingine ziendelee ikiwa ni pamoja na kupanga tarehe ya uchaguzi wa TASWA.


Kwa vile Kamati imekamilisha jukumu ililopewa la kuandaa rasimu hiyo, hivyo kilichobaki ni ushirikiano kutoa kwa wadau ili kumaliza jambo hilo.


Pamoja na mambo mengine rasimu hiyo imeandaliwa kwa kuangalia Katiba za vyama mbalimbali duniani vinavyohusiana na waandishi wa habari za michezo na pia kupitia muongozo kutoka Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS), ambacho TASWA ni mwanachama.


Pia Kamati imechambua Katiba ya sasa ya TASWA na kupokea maoni kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kuhusu maeneo yenye upungufu kwa nia ya kuiboresha.


Maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi  katika rasimu hiyo baadhi yakiwa ni sifa ya mwanachama, wajibu wa mwanachama, muundo wa uongozi, sifa za viongozi na pia ukomo wa uongozi, pia kuna mapendekezo katika rasimu hiyo ya kuanzishwa kamati mbalimbali kwa nia ya kuisaidia Kamati ya Utendaji.


Kamati ya Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyelitaka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) lisitishe uchaguzi wa TASWA uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana na badala yake BMT ikutane na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.


Kamati ya Katiba inayoongozwa na Mwenyeketi wa zamani wa TASWA, Boniface Wambura ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), viongozi wengine ni Katibu wa Kamati Amir Mhando ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TASWA na mwanahabari, Gift Macha ambaye ni Katibu Msaidizi wa Kamati. 


Wajumbe ni Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Abdul Mohammed, Mhazini wa zamani wa TASWA, Nasongelya Kilyinga na wanahabari Thabit Zacharia na Devotha Kihwelu.

KIKWETE APONGEZWA CHALINZE.

Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, akijenga ukuta wa madarasa  katika shule ya msingi Kibindu, iliyopo kata ya Kibindu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo hii ilikuwa mwezi Machi 2018
Picha kutoka Maktaba yetu.
.............................................


Na Shushu Joel,Chalinze.

WANANCHI wa kata za Kibindu na miono, wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wamempongeza mbunge wa jimbo la chalinze Ridhiwani Kikwete kwa jinsi anavyojitolea katika ufanikishaji wa miradi ya maendeleo kwenye Nyanja za Elimu,Afya na maji.


Pongezi hizo zimetolewa na diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi  wakati  alipokuwa akikagua bweni la wanafunzi wa kike na majengo mawili ya madarasa  ya shule za msingi unaoendelea katika kata hiyo.


Alisema kuwa awali maeneo hayo yalikuwa na changamoto kubwa ya uhaba wa  miundombinu ya elimu, hasa upungufu wa vyumba vya madarasa amabavyo kutokana na kuwepo kwa miaka mingi vimekuwa na nyufa kubwa hivyo kuhatarisha maisha ya wanafunzi na hata walimu.


Mpwimbwi aliongeza kuwa alimuomba mbunge wake Ridhiwani Kikwete waweze kuona namna jinsi wanavyoweza kupata wafadhili au hata kupitia mfuko wa jimbo ili kuwasaidia watoto waliokuwa wakisoma katika shule hiyo ili wasomee kwenye vyumba vilivyo na ubora kama ilivyo kwa wengine jimboni humo.


Kufuatia ombi hilo, Mpwimbwi alisema alifanikiwa kupata fedha kutoka kwa Mbunge huyo ili kuhakikisha wanafanikisha ujenzi huo wa vyumba vya madarsa na bweni la watoto wa kike ili kuwanusuru na vijana wasio na nia njema kwa watoto wa kike.


Naye Halma Iddi mkazi wa kata hiyo ametoa pongezi zake kwa mbunge huyo na kumtaka kuendelea kuwa na moyo huo katika kuwasaidia ili watoto waweze kupata elimu wakiwa katika mazingira mazuri kama ilivyo katika shule zingine.


Aliongeza kuwa awali wanafunzi hao walikuwa na changamoto kubwa ya kusomea katika mazingira magumu  kutokana na majengo yaliyo mengi kuwa na nyufa.


Aidha  aliendelea kusema kuwa, wanampongeza mbunge huyo kwa wepesi wa kushughulikia jambo lolote lile mara tu anapoambiwa na wananchi wake.


Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG kwa njia ya simu mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ni majukumu yake kuhakikisha anaishawishi serikali ili kufanikisha miradi ya maendeleo kwa wananchi wake wa chalinze.


Alisema kuwa wakati anaomba ridhaa ya kuwatumikia aliwahakikishia kuwa yeye atakuwa ni mbunge wa maendeleo na sasa wananchi hao wanayaona wao wenyewe kwani awali tulikuwa na wakati mgumu lakini kwa sasa kila jambo linalohusu maendeleo katika jimbo la chalinze kila kitu kinaenda vizuri.


Hivyo Kikwete amewataka wananchi hao kuendelea kuilinda miradi hiyo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu kwa kutumiwa na kizazi na kizazi cha chalinze.


Aidha alisema kuwa kuna miradi mingi inakuja chalinze hivyo wananchi wanatakiwa kuchangamkia fursa zitakazokuwa zinajitokeza kwa kuomba ajira katika viwanda, na kwamba kitu cha kujivunia malighafi zipo za kutosha chalinze na kuongeza kwa kusema kuwa, tunazidi kuwaomba wawekezaji wazidi kufika kwa wingi jimboni humo ili kuanzisha viwanda vya aina mbalimbali
 
MBUNGE wa jimbo la Chalinze,wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani  Kikwete (mwenye kofia ya CCM) akiwa katika jimbo lake kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.