Wednesday, February 6, 2019

CCM PWANI WAMPONGEZA ZAYNABU MATITU VULU

Image may contain: 1 person, smiling, closeup
Na Omary Mngindo, Kibaha

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, kimempongeza Mbunge wa Viti Maalumu Zaynabu Matitu Vulu, kwa kuuliza swali kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Mafia Mbaraka Dau, kuhusiana na adha ya usafiri visiwani humo.


Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa (MNEC) Haji Abuu Jumaa, akizungumza na Waandishi wa habari mjini Kibaha, alisema hatua ya Vulu kusimama bungeni kuulizia mipango ya serikali juu ya usafiri kwa wana-Mafia, inaonesha ni namna gani wabunge mkoani humo walivyokuwa na ushirikiano.


"Mwishoni kwa wiki Pwani tulisherehekea madhimisho ya miaka 42 tangu kuzaliwa kwa chama chetu, baadhi ya wabunge na Mawaziri walihudhulia, wengine waliendelea na majukumu ya Bunge, katika kikao hicho Vulu aliuliza swali kwa niaba ya Mbaraka Dau, lililohusu usafiri wilayani Mafia" alisema Haji.


MNEC huyo alisema kuwa swali hilo lililoulizwa bungeni, limehusiana na changamoto ya usafiri na usafirishaji, linalowakabili wana-Mafia na Mkoa kwa ujumla wanaokwenda na kurudi kutoka visiwani humo, ambao wamekuwa na adha hiyo kwa muda mrefu.


Nae Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Mkoa Jackson Josian alieleza kwamba, kama Jumuia imefurahishwa kwa hatua hiyo, huku akieleza inatokana na mahusiano mazuri yaliyopo kwa wabunge mkoani humo. 


"Hii inaonesha ni namna gani wabunge wetu wanavyoshirikiana katika kuwakilisha matatizo ya wapigakura wetu, niwaombe utaratibu huu uwe endelevu, kwani wote ni wawakilishi wa wananchi kutokea katika chama kimoja cha CCM," alisema Josian.


Jumanne Feb 5 Vulu alimwakilisha Dau wa Mafia, kuiuliza Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, juu ya mipango wa kupeleka ndege visiwani humo, sanjali kuongeza ukubwa wa kiwanja cha ndege sanjali na kuimarisha usafiri wa majini.


Akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa Habari hizi kutokea mjini Dodoma, Vulu alisema swali lake la msingi kwa Wizara hiyo ni kutaka kufahamu hatua za serikali katika kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji visiwani humo, ambao kwa muda mrefu wanakabilia na adha hiyo.

SERIKALI YAAMUA KUINUA ZAO LA KAHAWA NCHINI.

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO 

DODOMA
 
Serikali imeamua kuanzisha minada ya kahawa kwenye maeneo ya uzalishaji kuanzia msimu wa 2019/2020 ili kuinua zao hilo la kimkakati nchini.


Hayo yamesemwa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo,  Omary Mgumba wakati akijibu swali Mhe. Bernadeta Mushashu kuhusu mpango wa Serikali wa kuinua zao la kahawa Mkoani Kagera ikiwemo kupandisha bei ili kumnufaisha mkulima.


Mgumba amesema kuwa lengo la utaratibu huo ni kuharakisha malipo na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa minada na kuwashirikisha wakulima wengi zaidi katika mikoa inayozalisha kahawa ikiwemo Mkoa wa Kagera.


Aidha, amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya biashara ya zao hilo, Serikali inadhibiti makato yasiyo ya tija kwa wakulima yanayokatwa kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi ili kubaki na makato yanayolenga kuendeleza zao la kahawa.


“Kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB), Serikali imewezesha vyama vya ushirika vya kahawa kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kufanikisha shughuli za ukusanyaji na uuzaji wa kahawa ya wakulima hivyo kumpunguzia mkulima mzigo wa riba uliokuwa unatozwa na mabenki ya kibiashara,” amefafanua Naibu Waziri Mgumba.


Hata hivyo,  Mgumba ameongeza kuwa, Serikali imefuta tozo na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinatozwa kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo zilizokuwa zinatozwa katika biashara ya kahawa pamoja na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinakusanywa na mkulima.


“Serikali pia  imepunguza kiwango cha ushuru wa mazao unaotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka asilimia tanohadi asilimia tatuya bei ya kahawa shambani,” amesema Mgumba


Wakati huo huo,  Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa akijibu swali la Mbunge wa Ziwani, Mhe. Nassoro Omar kuhusu mpango wa Serikali kuhamasisha kilimo cha viungo vya chakula nchini amesema kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa mazao hayo  kutokana na mchango wake katika kipato cha mkulima mmoja mmoja na pia katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni.


“Kutokana na umuhimu huo, Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi imeandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya viungo (Spice Sub-Sector Strategy-2014) ambao unalenga kuongeza uzalishaji na tija ukiwa na maeneo mahususi ya utoaji mafunzo ya kuongeza ujuzi katika uzalishaji kwa wataalamu wa wakulima, uanzishaji wa vituo vya kukusanyia mazao na kupanga madaraja na kuunda masoko ya pamoja ya wakulima,” amefafanua Naibu Waziri Bashungwa.


Ameongeza kuwa, Serikali imeandaa Mwongozo wa uzalishaji wa mazao ambao umeainisha maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo ya viungo ambao umalenga kuonesha fursa za uzalishaji wa mazao hayo.


Zao la kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati yanayoliingizia Taifa fedha zakigeni sambamba na korosho, pamba na chai. 

KAULI YA SERIKALI KUHUSU MAUAJI NA UTEKAJI WA WATOTO MKOANI NJOMBE.

Watu 29 wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya utekaji na mauaji ya watoto Mkoani Njombe.

Akiwasilisha bungeni leo Jijini Dodoma taarifa ya Serikali kuhusu mauaji hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola amesema Serikali imeshachukua hatua mbalimbali katika kutatua na kuzuia matukio hayo sanjari na kutoa maelekezo ya hatua za kupambana na uhalifu huo ikiwemo kuwatia mbaroni watuhumiwa.


“Mpaka sasa hatua zilizochukuliwa na Serikali zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 29 kwa ajili ya uchunguzi na mahojiano zaidi na kazi bado inaendelea” ameongeza Waziri Lugola.


Mhe. Lugola amebainisha kuwa,  hivi karibuni kumejitokeza matukio yasiyo  ya kawaida ya utekaji na mauaji ya watoto yaliyokuwa yakihusishwa na imani potofu za kishirikina katika Mkoa wa Njombe.


“Kufuatia matukio hayo hadi sasa watoto saba wa umri chini ha miaka 16 wameripotiwa kuuawa, mmoja kujeruhiwa na wawili kupotea na badae kuonekana, matukio haya yametokea  katika maeneo ya Ikando, Matembwe, Mjimwema, Msitu wa Sekondari ya Njombe, Lukosa, Sido na Mfekere,” ameeleza Waziri Lugola.


Akifafanua zaidi, Lugola amesema kuwa, mbali na juhudi za Serikali, Jeshi la Polisi kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe imechukua hatua mbalimbali kuzuia aina hiyo ya uhalifu kwa kutumia timu ya wataalamu wa upelelezi kuvisaidia vyombo vya dola kuchunguza matukio hayo.


Pia kutumia falsafa ya ulinzi shirikishi wa jamii kwa kutoa elimu mashuleni kwa walimu ili kuweza kuwaelimisha wanafunzi kuongeza umakini katika mienendo yao, kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa wazazi na wananchi kwa ujumla juu ya elimu ya ulinzi na usalama, vikao na waganga wa kienyeji, viongozi wa dini, Wazee wa Mila, Viongozi wa Kata pamoja na kufanga doria na misako kwenye maeneo mbalimbali ya misitu na nyumba za kulala wageni zilizopo pembezoni, ni mbinu zilizotumika kuzuia vitendo hivyo.


Hata hivyo, Mhe. Lugola ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na matukio hayo na itikadi za kisiasa, imani za kidini au shughuli za kibiashara.


Aidha, amebainisha kuwa Serikali itachukua hatua kwa wale watakaojihusisha na vitendo vya usambazaji wa taarifa za kichochezi mitandaoni hivyo amewaasa Watanzania kuacha kusambaza taarifa za uzushi mitandaoni  kwa nia yoyote ile kwani ni takwa la Sheria ya Mtandao.


Mbali na hayo amesema kuwa, Serikali itahakikisha wote waliohusika na mauaji wanaendelea kusakwa, kuhojiwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria bila kujali nafasi zao katika jamii.


Hivi karibuni yamajitokeza matukio ya utekaji na mauaji ya watoto wadogo Mkoani Njombe, jambo ambalo limezua taharuki mkoani humo na nchini kote kwa ujumla.

WAUGUZI WANNE KITUO CHA AFYA WASIMAMISHWA KAZI KUTOKANA NA KUTOA LUGHA CHAFU KWA MGONJWA.

NA MWAMVUA MWINYI, BAGAMOYO

SERIKALI mkoani Pwani pamoja na idara ya afya mkoani humo,imewasimamisha kazi wauguzi wanne katika kituo cha afya kiitwacho Mkoani ,baada ya kudaiwa kutoa lugha chafu kwa mama aliyempeleka mtoto wake aliyekuwa amekwamwa na chaki kooni.

Aidha mkoa huo imeelekeza fedha kiasi cha sh. milioni 400-500 zinazopelekwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya zitumike vizuri bila ubabaishaji.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo aliyasema hayo, wakati alipotembelea kituo cha afya cha Matimbwa kata ya Yombo, Bagamoyo kuangalia ujenzi unavyoendelea,na kusema wauguzi hao ni wale waliokuwa zamu siku ya tukio .

Alisema, wauguzi hao wamewasimamisha wiki iliyopita na tayari wameandika barua za kujieleza ,ambapo vimeundwa vyombo vya uchunguzi kujua chanzo na ukweli wa jambo hilo.

Ndikilo alisema, endapo wakibainika kuhusika na kitendo hicho hatua itachukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine .

“Baada ya kufikishiwa malalamiko hayo kutoka kwa mama wa mtoto, nilikutana na mganga mkuu wa mkoa, katibu afya, mkurugenzi wa halmashauri na muuguzi mkuu kujadili suala hilo na kuchukua hatua za awali “

“Wahusika wameandika barua za kujieleza, na kati ya hao wengine tumegundua mafaili yao yanaonyesha kupewa onyo mara kadhaa kutokana na tabia hiyo hiyo. “alifafanua Ndikilo.

Mkuu huyo wa mkoa, alieleza serikali inaelekeza nguvu zake kuboresha huduma za afya kwa kutoa mabilioni ya fedha, hivyo vituo vya afya vyote viendane na utoaji wa huduma bora.

Nae mganga mkuu wa mkoa wa Pwani, dokta Gunini Kamba alisema inadaiwa mama huyo alipoona karushiwa maneno makali na wauguzi hao aliondoka kwenda hospital nyingine na baadae aliamua kwenda kutoa malalamiko hayo ambayo yameanza kuchukuliwa hatua hizo.

Alitoa onyo kwa watumishi na wauguzi wa afya ambao wanakiuka taratibu na maadili waliyopatiwa.