Monday, February 4, 2019

WAKULIMA WA PAMBA WATARAJIE MABADILIKO MAKUBWA- WAZIRI HASUNGA.

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Katikati) akiongoza kikao kazi cha Wabunge wa maeneo yanayolima pamba nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Jijini, Dodoma leo Jumatatu tarehe 4 Februari, 2019. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Kulia) na Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumbwa. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
.................................... 


Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amewaambia Waheshimiwa Wabunge wa maeneo yanayolima pamba kuwa Wizara ya Kilimo imedhamiria kumkomboa Mkulima wa pamba na kwa kuanza imeanzisha zoezi la kuwasajili Wakulima wote nchini wakiwemo Wakulima wa pamba ambapo Serikali imetengeneza mfumo maalumu wa kuwatambua kwanza Wakulima, maeneo wanayotoka, mashamba yao yapo wapi na yana ukubwa gani.


Mhe. Hasunga ameyasema hayo wakati wa kikao maalumu na Waheshimiwa Wabunge hao katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Jijini, Dodoma leo Jumatatu tarehe 4 Februari, 2019.


Kikao hicho kilikuwa na lengo la kufanya maboresho kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa mauzo ya pamba ambao unatarajia kuanza Mwezi Aprili mwaka huu.


Mhe. Hasunga amesema moja ya mambo ambayo Wizara ya Kilimo itahakikisha inayashughulikia ipasavyo, sambamba na kuwatambua Wakulima wa pamba ni pamoja na kuupitia upya mfumo wa Ushirika katika ununuzi wa pamba, mfumo wa uagizaji na uingizaji wa viuatilifu vya pamba pamoja na masoko ya zao hilo.


Waziri Hasunga amesema katika kipindi hiki kifupi amekuwa akipata malalamiko mengi kutoka kwa Wakulima wa mazao mbalimbali kuhusu udhaifu wa mfumo wa uagizaji wa uingizaji wa pembejeo za kilimo yakiwemo madawa na mbegu hafifu.


“Napenda nikiri kuwa tuna tatizo katika mfumo wa uagizaji na uingizaji wa pembejeo za kilimo, bado haujakaa vizuri lakini baya zaidi ni viuatilifu hafifu. Serikali kamwe haiwezi kutazama Wakulima wakionewa na Wajanja wachache na huu ni uhujumu uchumi lazima wanaofanya mambo haya wachukuliwe hatua kali za kisheria”. Amekaririwa Waziri Hasunga.


Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya Wabunge wameshauri kuwa muda wa kupeleka pembejeo za kilimo kama mbegu bora na madawa uwe mapema zaidi kuliko ilivyo sasa. Mhe. Kiswaga Boniventura. 


Mbunge wa Magu ameishauri Serikali kuwa wakati wa zoezi la ununuzi wa pamba ghafi zoezi hilo liendane na zoezi la kuwapelekea Wakulima mbegu bora za pamba na kuongeza kuwa litaokoa fedha za Umma kwa kuwa fedha za usafirishaji itatumika mara moja tu.


Naye Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga amesema kuna haja kubwa ya kupitia mfumo mzima wa Vyama vya Ushirika vinavyonunua pamba, akitoa mfano katika msimu wa pamba uliopita wa mwaka 2018/2019 Wakulima wa pamba walikuwa wakikatwa shilingi 100 katika kila kilo moja kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa viuatilifu (Madawa ya pamba) katika msimu ujao wa kilimo.


Mhe. Njalu amesema kuna maeneo mengi ambayo Wakulima wengi wanafikisha zaidi ya kilo mia tano (500) na anapokatwa kiasi hicho cha fedha makusanyo yanakuwa makubwa hadi kufikia shilingi elfu hamsini (50,000/=) wakati thamani halisi ya pembejeo ambazo atapewa na Chama chake cha Ushirika hakizidi shilingi elfu kumi (10,000/=).


Mhe. Waziri Hasunga amekiri kuwa jambo hilo linaweza kuwepo na kuna haja ya kuufanya maboresho makubwa mfumo mzima ununuzi wa pamba kabla ya kuanza msimu mpya wa ununuzi wa pamba ambao unataraji kuanza mapema Mwezi Aprili, 2019

SERIKALI YANUNUA TANI 214,269.7 ZA KOROSHO GHAFI HADI KUFIKIA JANUARY 30.

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.

Hadi kufikia Januari 30 mwaka huu Serikali imenunua tani 214,269.7 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi  707,089,957,200.00 sawa na asilimia 89.3 ya lengo la uzalishaji wa msimu wa korosho wa mwaka 2018/2019.


Hayo yameelezwa leo Bungeni, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omari Mgumba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Mhe. Halima Mdee kuhusu tani ngapi zimenunuliwa na Serikali mpaka sasa na wakulima wangapi na vyama vingapi vya msingi vimelipwa na vingapi bado havijalipwa.


“Ununuzi wa korosho unafanywa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambapo malipo yaliyolipwa na kuingizwa kwenye akaunti za wakulima hadi tarehe 30 Januari, 2019 ni kiasi cha shilingi 424,849,405,110 zilizotokana na korosho za wakulima kiasi cha tani 134,535.9,” alisema Mhe. Mgumba.


Ameendelea kusema, jumla ya wakulima 390,466 wamelipwa hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2019. Aidha vyama vya msingi 603 vimelipwa kati ya vyama vya msingi 605 vilivyohakikiwa.


Aidha amesema, zoezi la operesheni korosho linaenda vizuri na linatarajia kukamilika ifikapo tarehe 15 Februari mwaka huu.


Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ni taasisi ya kibiashara yenye lengo la kupata faida na mtaji wake unatokana na ruzuku kutoka Serikalini na mikopo kutoka taasisi za Fedha kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo – TADB, NMB na CRDB.


Mnamo Novemba, 2018 Serikali iliungana na msimamo wa wakuliwa wa kukataa bei zilizotolewa na kampuni za ununuzi wa korosho, ambapo zilitangaza kununua korosho kwa bei ya kati ya shilingi 2,717 na shilingi 1,900  kwa kilo ikiwa imeshuka kutoka zaidi ya shilingi 3,600 ya msimu uliopita.


Aidha, Mhe. Rais Dkt. Magufuli alitangaza Serikali kununua korosho hizo kwa shilingi 3,300 badala ya shilingi 3,000.

MFUKO WA MISITU LINDI WATAKIWA KUREJESHA KWA WAKATI FEDHA ZA UPANDAJI MITI

Na Hadija Hassan, Lindi

Halmashauri ya Wilaya ya Lindi mkoani humo imewashauri Mfuko wa Misitu Tanzania (Tanzania Forest Fund)  kurejesha kwa wakati fedha za upandaji Miti ili kuendelea kupambana na Mabadiliko ya Tabia Nchi


Wito huo umetolewa na afisa  Aridhi na Maliasili wa Wilaya hiyo Victor Shau  leo  alipokuwa anazungumza na Bagamoyo kwanza ofisini kwake


Amesema ni vema fedha hizo zikalejeshwa kwa wakati  ili ziweze kusaidia katika miradi midogomidogo hasa kwa kuanzisha vitalu vya upandaji wa miti


Alisema fedha hizo kwa kiasi kikubwa zinatokana na makusanyo yao kama Halmashauri katika mavuno ya Mazao ya misitu


Kwa upande wake Afisa Maliasili wa Wilaya hiyo   Chares Mwaipopo alisema kuwa katika kipindi cha mwezi may 2017 hadi mwezi june 2018 Halmashauri hiyo iliweza kukusanya kiasi cha milioni 29.178191 ambapo walitakiwa kurejeshewa kiasi cha shilingi milioni 78468.50


Hata hivyo BAGAMOYO KWANZA BLOG ilipomtafuta afisa Misitu wa  wakala wa misitu TFS Wilaya ya Lindi,  Oswald Laswai  alikili wilaya hiyo kucheleweshewa  mrejesho wa Fedha zao za mavuno ya mazao ya misitu  ambapo amesema kuwa ucheleweshwaji wa fedha hizo kwa kiasi kikubwa unatokana na wahusika kuchelewa kupeleka madai katika mfuko huo


KUPUNGUZA UJAZO TUMESAIDIA WAKULIMA- SADALA

Na Omary Mngindo,  Chalinze


SERIKALI imesema kuwa, hatua ya kudhibiti upakizi wa lasirimali za misitu kutoka ujazo wa kilo 110 mpaka 50, inalenga kulinda wakulima, ambao walikuwa wanapunjwa na wafanyabiashara.


Hayo yameelezwa na Sadala Ally Afisa Misitu (DFO) Idara ya Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Chalinze Bagamoyo Pwani, akitolea ufafanuzi wa swali la Madiwani waliotaka kufahamu sababu za kupunguzwa ushuru kutoka shilingi 24,000 mpaka kiwango kinachotozwa hivi sasa.


"Kabla ya mabadiliko ya sheria ile, kulikuwa na utozwaji wa kati ya sh.  24,000 ikaja 16,000 baada ya mabadiliko ikaja sh. 12,000, hatua hii inalenga kuwanusuru wakulima waliokuwa wanadhulumiwa na wafanyabiashara," alisema Sadala.


Ameongeza kuwa kupitia mabadiliko ya pesa ya mwaka jana, serikalu ikatoa maelekezo kupitia gn namba 46 ikatoa maelekezo kwamba halmashauri zitoze asilimia 5 kinachouzwa kutoka kunakozalishwa.


Katika Baraza hilo Madiwani walielekeza malalamiko katika idara ya Ardhi ambayo imedaiwa kushindwa kumaliza migogoro kati ya vijiji na vijiji hali na mingine inayowahusu wananchi wa kawaida, ambapo baadhi yao inahatarisha usalama katika halmashauri hiyo.


Madiwani Malota Kwaga, Rehema Mwene na Lucas Lufunga kila mmoja alielezea masikitiko yake kuhusiana na migogoro ya ardhi, huku Lufunga akilalamikia hati za viwanja vilivyopimwa katika eneo la Kibiki Kata ya Bwilingu Mamlaka ya Mji Mdogo wa Chalinze.


Mkuu wa wilaya hiyo Zaynabu Kawawa alitoa siku tatu kwa maofisa wa ardhi kuwasilisha vielelezo kwa maandishi kuelezea namna walivyoshughulikia migogoro hiyo.


Afisa Ardhi Mteule Zefania Sabo aliliambia baraza hilo kwwamba aliliwasilisha suala la viwanja katika eneo la Kibiki katika Kamati ya fedha, huku akitaka iwasilishwe kwenye baraza lijalo.