Friday, January 18, 2019

MFUMO WA TTMS KUONGEZA UWAZI NA MAPATO SERIKALINI: DKT. MAGUFULI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia katika  hafla ya makabidhiano ya Mfumo wa Kudhibiti Mawasiliano ya Ndani na Nje ya Nchi (TTMS) iliyofanyika makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es salaam leo Januari 18, 2019
......................................

Rais Dkt John Pombe Magufuli ametaka mfumo mpya wa usimamizi na udhibiti wa  sekta ya mawasiliano nchini TTMS kutumiwa vizuri ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya mtandao pamoja na kuongeza pato la Taifa.


Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya mfumo huo kati ya Mamalaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya SGS/GVG, Rais Magufuli amesema kuwa sekta ya mawasiliano ni sekta nyeti na ni muhimu kwa ujenzi wa taifa na kwa sasa inakuwa kwa kasi kubwa duniani kote.


“Sekta ya Mawasiliano ni sekta iliyonyeti na ni muhimu kwa watu wote duniani na kwa sasa inakua kwa kasi kubwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni 5 wanatumia simu za mkononi duniani kote huku watu bilioni 3.9 wakiwa wanatumia vifurushi (data), lakini kwetu Tanzania watu 42,961,000 kwa sasa wanatumia simu huku 22,995,000 wakitumia kifurushi”, alisema Rais Magufuli.


Rais Magufuli alisema kuwa katika ukuaji wa kasi ya ajabu kwa matumizi hayo ya simu idadi ya upashanaji habari nao umeongezeka duniani kote huku mifumo ya uapatikanaji wa habari hizo ikiwa wazi kwa kila mtu kwa jambo lolote litakalotokea duniani lisipo ripotiwa kwenye Redio na Televisheni basi ni kwa njia ya mawasiliano kama Facebook, Whatsapp, Twitter na Instagram.


Akizungumzia faida za sekta ya Mawasiliano nchini Rais Magufuli alisema kuwa sekta ya mawasiliano ni kichocheo kikubwa cha uchumi kwa jamii kwani kwa sasa kinaongeza uzalishaji viwandani na duniani kote kwani teknolojia ya viwanda sasa inaendeshwa na sekta hii hasa kwa biashara za rejareja za mitandao yaani (E-Commerce).


“Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2017 biashara za rejareja zilizofanyika kwa njia ya mtandao yaani E-commerce zilikuwa na thamani ya trilioni 2.3 na hivyo kuzipita biashara za madukani na kwenye super market kwa hiyo watanzania mfumo huu mpya utaiongeza uwazi kwa biashara hiyo”, alisisitiza Rais Magufuli.


Katika mfumo huu wa mawasiliano huduma mbalimbali kama vile afya na elimu zinapatikana kwa njia ya mtandao yaani E-education na E- health, huduma za usafiri yaani Uber na taxify, lakini pia kupitia uwazi wa mfumo huu watu waliojisajili kwenye huduma za kifedha kwa sasa wanafikia watu milioni 20.85, kitu kilichochangia kwa Tanzania kuwa kinara wa uchumi jumuishi kwa nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika.


Rais Magufuli alitaja sehemu za  mfumo huo ambao utaleta uwazi mkubwa kwa mawasiliano nchini katika Serikali ya Awamu ya Tano kuwa utakuwa ni mfumo wa kusimamia ubora wa mawasiliano Tanzania, kutoa takwimu za mawasiliano kwa njia ya sauti, matumizi ya  vifurushi vya simu na jumbe fupi na kubaini mawasilino ya simu za kimataifa zinazofanyika kwa njia ya udanganyifu.


Mifumo mingine iliyoko kwenye TTMS ni kufuatilia miamala ya kifedha inayofanyika kwa njia ya mtandano, kutambua namba tambulishi (IMEI) ya simu za kiganjani na kuhakiki kuwa vifaa vilivyounganishwa kwa watoa huduma zinakidhi kiwango cha kimataifa na mfumo wa mwisho TTMS ni ule wa kuhakiki mapato yatokanayo na simu/mtandao.


Aidha Rais Magufuli alieleza jinsi matumizi ya mfumo huo ulivyoleta faida tangu uanze kutumika ambazo ni kufahamu idadi kamili ya watumiaji wa simu na vifurushi, TTMS umepunguza kiwango cha udanganyifu kutoka asilimia 65 mpaka asilimia 10 sasa.


Katika kuweka bayana uwazi wa mawasiliano kupitia TTMS  Serikali imevuna fedha za kitanzania shilingi bilioni 93.665  huku shilingi bilioni 82.258 zikienda hazina na shilingi bilioni 11.407 zikipelekwa COSTECH, kwa hiyo kuongezeka kwa uwazi katika mawasiliano kwa kutumia TTMS imeweza kuongeza mapato kwa Serikali.


Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe alisema kuwa uwazi kwa kutumia mfumo wa TTMS umewezesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kwani kwa sasa sekta hii imekuwa pana zaidi nchini hasa kwa wamiliki wa laini za simu.


“Mfumo huu TTMS utaweka uwazi zaidi na kuchangia mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa taifa tangu kuanzishwa kwake 2017 kwani watumiaji wa simu za mkononi walionekena wakiongezeka kwa kasi kutoka 39,808,419  mwaka 2015 mpaka 42,661,449 mwaka 2018 hii inaonesha kuwa mfumo huu utakuza sekta ya mawasiliano kwa kasi zaidi kwa miaka ijayo hapa nchini”, Waziri Isack Kamwelwe.

WAZALENDO KISARAWE WAKABIDHI VIFAA VYA MIL. 6


Na Omary Mngindo, Kisarawe 

JUKWAA la Wazalendo wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, Jumamosi ya Jan 13 limekabidhi Mashine ya Kudurufu moja sanjali na Kompyuta vyenye thamani ya sh. Mil. 6.


Vifaa hivyo vinavyolenga kutumika kuchapishia mithihani kwenye shule za sekondari na msingi zilizomo Tarafa ya Marumbo, lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa nzuri ya kushiriki masomo, yatayowawezesha kufanya vizuri kwenye mithihani yao.


Katika hafla hiyo iliyoambatana na Mkutano Mkuu wa mwaka kwa wana-Jukwaa hilo, uliofanyika Kijiji cha Malumbo Kata ya Mfulu Tarafa ya Manerumango wilayani hapa, umehudhuliwa na mamia ya wana- Kisarawe, wakiongozwa na mgeni rasmi Mhandisi Wakati Mwaruka.


Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mhandisi Mwaruko alisema kuwa lengo la kukabishi vifaa ni kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa wilaya humo, inayolenga kutokomeza ziro ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali wilayani humo inayodhamilia kuinua kiwango cha elimu.


"Jukwaa la Wazalendo linaundwa na wana- Kisarawe na wapenda maendeleo wengine kutoka maeneo mbalinbali hapa nchini ambai kwa umoja wetu tumeanzisha Group la Wazalendo Kisarawe, ambao kwa umoja wetu tunajitoa katika shughuli za kimaendeleo, ikiweno shida mbalimbali kwa wana-Jukwaa," alisema Mhandisi Mwaruko.


Mwaruko alisema kwamba vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa shule ya Sekondari ya Kibuta na ya msingi Mfuru, vinalenga kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu, kwenda kupata huduma ya kuchapa mitihani yao, hali ambayo kwa namna moja au nyingine ilikuwa inachangia kukwamisha juhudi za upatikanaji wa elimu.


Akitoa neno la kushukuru kwa wana-Jukwaa la Wazalendo Kisarawe, Afisa elimu Kata ya Marumbo, Harrison Ukwai alisema kwamba msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwenye Kata hizo na kuongeza ufaulu.


"Msaada huu ni mkubwa, wana-Jukwaa wameonesha ni namna gani wanavyogushwa na changamoto nyingi ikiwemo ya elimu, ambayo kimsingi ndio sekta muhimu inayozalisha viongozi katika maeneo yote hapa nchini na duniani kwa ujumla," alisema Ukwai.

WAKWEPA KODI CHALINZE WATAKIWA KUJISALIMISHA KWA MKURUGENZI.

Image may contain: one or more people, people standing, sky, outdoor and nature
Kamati ya fedha,utawala na mipango ya halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo imeanza ziara ya kukagua na kuona vyanzo vya mapato vinavyotokana na madini ya kokoto katika makampuni ya Z&A, Lavender Infrastructure, China Gold,Nyanza Road Works, Jiwe Project, Mhingara Company Ltd na Grand tech.


Kamati hiyo imeanza kufanya ziara hiyo kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2018/2019, katika ziara hiyo wajumbe wamehoji kutaka kujua makampuni ya uchimbaji madini yanalipa kodi ya huduma na ushuru wa mapato yatokanayo na kokoto.


Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze Mheshimiwa Said Omari Zikatimu na kamati ya fedha alitaka kujua kama makampuni hayo yanalipa ushuru na kodi kwa mujibu wa sheria ya fedha namba 9 ya serikali za mitaa ya mwaka 1982.

"Lengo la halmashauri yetu ni kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100 Ili kuvuka malengo ya bajeti yetu na kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi na shuru mbalimbali. " alisema Zikatimu.


Hata hivyo kamati ya fedha ilipokuwa ikikagua shughuli za uchimbaji wa kokoto iliweza kubaini baadhi ya makampuni kuendesha shughuli zake pasipo kuwa na nyaraka mbalimbali za kisheria kama leseni ya kuchimba madini, leseni ya biashara na nyaraka zingine kwa mujibu wa sheria.


Kamati ilipobaini mapungufu hayo ilitoa maagizo kwa wamiliki wa kampuni hizo kuwasilisha nyaraka husika ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halamsahauri haraka iwezekanavyo vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya makampuni tajwa kwa kukiuka sheria za uwekezaji.

WASTAAFU DAWASA WAMPONGEZA MAGUFULI

Na Omary Mngindo, Mlandizi

WASTAAFU wa Shirika la Maji (DAWASA) Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, wamempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kusikiliza kilio cha Wastaafu, huku wakimuomba atupie jicho shirika hilo, ili wapate mafao yao stahiki.

Wakizungumza na Waandishi wa habari, baadhi ya Wastaafu hao kwa niaba ya wenzao walianza kupongeza Rais Magufuli, huku wakiomba kuangaliwa Mkataba wao wa hali bora kazini ambao viongozi wao waligoma kuusaini.

"Kiukweli Rais John Magufuli ameonesha ni kiongozi bora anayejali maslahi ya wananchi, nasi Wastaafu tuliolitumikia Shirika la Maji Dar es Salaam (DAWASA) tunamuomba atupie jicho, tunadai Mkataba wa hali bora kazini, viongozi waligoma kuusaini," alisema Suleiman Sule.

Nae Elidrick Chichwa akizungumza kwa niaba ya wenzake ambao hawakupenda kutaja majina yao, alisema kuwa wanamuomba Waziri wa Maji awasaidie wapate haki yao ya mafao ya kustaafu kupitia Mkataba huo.

"Tunaimani kubwa na Serikali iliyopo Madarakani inayojali wanyonge, kupitia Waandishi wa Habari tunaimani kwamba kilio au ombi letu litapokelewa na viongozi husika, kisha kufanyiwakazi," alisema Chichwa.

Mstaafu mwingine alisema kwamba yeye alifanyakazi Shirika la Maji Dar es Salaam (DAWASA), City Water na DAWASCO na kwamba wakati wakiwa kazini kuna Mkataba wao wa hali bora ambao uliandikwa ambao hata hivyo haukusainiwa na viongozi wao.

"Nimefanyakazi kwa miaka 26, cha kishangaza nimestaafu mwezi wa nane mwaka 2018 nikaambulia sh. Mil. 11 tu, kama Mkataba wa hali bora kazini ningepokea kiasi cha sh. Mil. 80, kwa sasa naishi maisha magumu sana," alisema Mstaafu huyo.

Wamemalizia kwa kumuomba Waziri mwenye dhamana wa Wizara hiyo kuangalia mkataba huo, ili wastaafu hao nao wanufaike na miaka waliyosaidia ujenzi wa nchi kwa kipindi chote.


MAGAZETI YA LEO JANUARI 18, 2019.