Saturday, November 3, 2018

SABA WAFARIKI AJALI YA GARI BARABARA YA DODOMA-MOROGORO

WATU saba ambao majina yao hayajafahamika mara moja wamefariki dunia na watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili ya serikali na lori moja, majira ya saa 6:30 usiku wa kuamkia leo Jumamosi, Novemba 3, 2018 katika Kijiji cha Mbande, Kata ya Sejeli, Tarafa na Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Katika ajali hiyo, gari lenye namba za usajili STL 6250 Toyota Land Cruiser mali ya ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikiendeshwa na Dickson Kitanda (42) Mgita, mkazi wa Dar es Salaam ikitokea Dodoma kuelekea Dar ikiwa na abiria sita iliigonga kwa nyuma gari namba T161 CBB/T152 CBB lori aina ya DAF mali ya Z.S Ally mkazi wa Dar iliyokuwa imeharibika barabarani.

Inaelezwa kuwa, baada ya ajali hiyo, STL 6250 iligongana uso kwa uso na gari lingine SU 41173 Toyota Land Cruiser mali ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (PSSSF) ikitokea Dar kuelekea Dodoma ikiendeshwa na Peter Elleson Masamu (35) Mchaga mkazi wa Dodoma ikiwa na abiria watatu ambao ni Elliad Eliyakunda Mdeme (40), Mwanasheria na mkazi wa Dodoma,  Vick Elisala Moshi (51) Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF na Abubakar Mjata Ndwaqta (42) Ofisa Takwimu wa PSSSF mkazi wa Kisasa, Dodoma.

Taarifa za awali zinasema waliofariki kwenye ajali hiyo iliyotokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Morogoro, ni ndugu sita wa Naibu CAG waliokuwa wakitoka kwenye msiba Chato mkoani Geita, kati yao wanawake wawili ambao ni abiria wa gari STL 6250 T/ Land Cruiser na dereva wa gari hilo la ofisi ya CAG huku majeruhi wakiwa watatu, abiria wa gari SU 41173 T/Land Cruiser.

Miili ya marehemu imepelekwa Hospitali ya Kongwa na majeruhi watatu wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Chanzo cha ajali bado kinachunguzwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, RPC Gilles Muroto amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.


WAZIRI MKUU ARIDHISHWA NA UJENZI RELI YA KISASA (SGR)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua utandikaji wa  Reli ya SGR katika eneo la Soga mkoani Pwani, Oktoba 3, 2018.   Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe.
...............................................


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa mfumo wa reli ya kisasa (SGR) inayojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi.

Amesema kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa km. 300 ambacho kilitakiwa kukamilika Julai 2019, wataalamu wamesema watakamilisha Aprili 2019.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 3, 2018) alipotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia eneo la Shaurimoyo Dar esSalaam hadi Soga,  Pwani.

“Nimeridhishwa na viwango na maendeleo ya ujenzi kwa sehemu ulivyofikia pamoja na ushiriki wa Watanzania wengi katika mradi huu, tunataka muendelee kujenga kwa kasi hii.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona malengo ya Rais Dkt. John Magufuli ya kutaka kuona SGR  inakamilika na kuanza kutumika nchini yanatimia.

Kuhusu suala la ajira, Waziri Mkuu amesema amefarijika kusikia asilimia 96 ya watu walioajiriwa katika mradi huo ni Watanzania, amewataka wawe mabalozi wazuri.

“Watanzania mnaofanya kazi katika mradi huu hakikisheni mnawajibika kwa kufanyakazi kwa bidii, uaminifu na muwe mabalozi wazuri ili wengine waweze wapate ajira.”

Awali,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya mradi huo wa reli  kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora unagharimu sh. trilioni 7.1.

Alisema mradi wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa km 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza umegawanyika katika vipande vitano, kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu km 300 na kitagharimu sh. trilioni 2.7.

“Kipande kingine ni kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa km. 422 ambacho kitagharimu sh. trilioni 4.4, Makutupora hadi Tabora km. 376.5, Tabora hadi Isaka km 162.5 na Isaka hadi Mwanza km. 311.25.”

Mkurugenzi huyo alisema kukamilika kwa reli hiyo ya kisasa kutachochea mipango ya Serikali katika kutekeleza sera ya viwanda na kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Pia reli hiyo itachochea mapinduzi ya kiuchumi kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususan kwa nchi zisizopakana na bahari kwani watasafirisha mizigo yao kwa haraka na uhakika.

Akizungumzia mradi huo kwa ujumla, Kadogosa alisema maendeleo ya mradi huo ni asilimia 32 kwa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro na asilimia 3. 31 kwa kipande cha Morogoro-Makutupora.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua utandikaji wa  Reli ya kisasa ya  SGR katika eneo la Soga mkoani Pwani, Oktoba 3, 2018.   Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe na kulia kwa Waziri Mkuu ni Mkurugenzi Mkuu wa Shiraki la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa


DKT ABBASI ASEMA SERIKALI IMEBORESHA SEKTA YA AFYA

 Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbas

Na Grace Semfuko-MAELEZO

Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbas amesema  Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli imeongeza kasi ya ujenzi wa  Hospitali za Wilaya na vituo vya afya nchini ambapo kwa miaka mitatu pekee jumla ya vituo hivyo 67 vimejengwa ukilinganisha na 77 vilivyojengwa miaka 53 iliyopita tangu uhuru.

Dkt Abbasi amesema hatua hiyo ya Serikali ya ujenzi wa kasi wa hospitali na vituo vya afya inalenga kuimarisha afya za watanzania ambapo hivi sasa idadi kubwa ya watanzania inatumia huduma za bima ya afya ya Taifa NHIF idadi ambayo awali ilikuwa milioni 9.9 mwaka 2015 mpaka kufikia zaidi ya milioni 16 Mwaka huu wa 2018.

Akizungumza nkatika semina ya Waandishi wa Klabu ya waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar Es Salaam (DDCPC) iliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF iliyokuwa na lengo la kujengeana uwezo ili umma wa watanzania waweze kunufaika zaidi katika huduma za Afya Nchini, Dkt Abbasi amesema ipo haja kwa waandishi wa habari hao kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.

“Unajua hata sisi waandishi wa habari tunayo haki ya kupongeza,pale unapoandika changamoto na zikafanyiwa kazi ni muhimu kupongeza pia sio kukosoa tu, juhudi za Serikali ya awamu ya tano kwa kipindi kifupi tu makubwa yamefanyika ukilinganisha na kipindi kingine chochote” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa Serikali.

Aidha Dkt Abbasi amewataka waandishi wa Habari Nchini kutumia kalamu zao katika kuandika  mafanikio makubwa ya miaka mitatu yanayofanywa na rais Dkt John Pombe Magufuli.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF Bw. Mbarouk Magawa amesema idadi hiyo ya wanachama iliyoongezeka inaufanya mfuko huo kuzidi kujiimarisha na kuhudumia wanachama wengi zaidi.

Mbarouk amesema kuongezeka kwa idadi hiyo ya wanachama kunaifanya  Juhudi za Serikali ya awamu ya tano kufikia malengo yake ya kuhakikisha huduma za afya nafuu zinapatikana nchini kote.

“Mfuko wa Taifa wa Bima za Afya lengo letu ni kuhudumia wanachama wengi zaidi na kwa awamu hii chini Uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli wanachama wengi zaidi wameongezeka tangu kuanzishwa kwa mfuko huu mwaka 2001” alisema Magawa Mkurugenzi wa Huduma za wanachama wa NHIF.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya ulianzishwa kwa Sheria namba 8 ya Bunge ya mwaka 1999 na mfuko huo ulianza kufanyakazi rasmi  mwaka 2001,hadi sasa mfuko huo una wanachama zaidi ya milioni 16 kutoka Milioni 9.9 waliokuwepo hapo awali.