Monday, October 29, 2018

RC GAMBO ATAKA UDHIBITI WA MATUKIO YA MIMBA SHULENI

 MKUU wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo
 ..............................

Na Ahmed Mahmoud Arusha.

MKUU wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo,ameziagiza halmashauri zote saba za mkoani  Arusha, kuhakikisha wanadhibiti matukio ya mimba kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi,  ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote waliowatia mimba wanafunzi hao.

Gambo,ametoa agizo hilo Oktoba 27 kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa,RCC, na kueleza kusikitishwa kwake na wanafunzi hao kukatishwa masomo kutokana na uja uzito.

Ameagiza kuhakikisha utoro shuleni unadhibitiwa sanjari na wazazi kuhakikisha wanachangia chakula shuleni ili kuwezesha wanafunzi kuwa na umakini kwenye masomo yao na hiyo pia ni njia ya kupunguza utoro.

Gambo,amempongeza ,mmiliki wa kiwanda cha Mount Meru Millers,ambae ameahidi kutoa chakula cha mchana kwa shule zote za msingi jijini Arusha,amekuwa akitoa chakula bure kwa wanafunzi 2000 wa shule za msingi jijini Arusha.

Akizungumzia ufaulu wa matokeo ya darasa la saba mwaka huu ambapo mkoa wa Arusha umeshika nafasi ya tatu kitaifa,Gambo,amesema mafanikio hayo yanatokana na mkakati wa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya elimu ikiwa ni pamoja na shule zote  kufanya mtihani mmoja wa pamoja.

Amesema kuwa  wamekubaliana na mkoa wa Dar es Salaam kuwa na mtihani wa pamoja, pia kushindanisha shule za msingi za mkoa wa Arusha na Dar es Salaam,

 Gambo,amesema hiyo ndio siri ya mafanikio kwa mkoa wa Dar es Salaam kuongoza kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu ingawa baadhi ya shule zimekuwa na madowa katika matokeo hayo ,lakini Arusha iko salama kutokana na kuwa na uadilifu

Amekiri kuwa matokeo yamekuwa na changamoto za ukosefu wa vyumba vya madarasa na kuahidi kuwa hadi January mwakani shule zitakapofunguliwa vyumba hivyo vitakuwa vimeshajengwa na kukamilika.

Hata hivyo serikali kuvifungia vyuo na shule zisizosajiliwa
SERIKALI imesisitiza msimamo wake wa kuzifungia shule za awali,msingi na vyuo ambavyo havijasajiliwa  ikiwa ni hatua ya kudhibiti elimu isitolewe kiholela bali kwenye maeneo maalumu yenye sifa.

.Kauli hiyo imetolewa Oktoba 27 na Naibu waziri wa Elimu, William ole Nasha, MB, alipokuwa akichangia kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Arusha,RCC, na kusisitiza kuwa taasisi zote za elimu lazima zisajiliwe vinginevyo hazitaruhusiwa kutoa huduma ya elimu nchini.

Nasha,ambae pia ni mbunge wa jimbo la Ngorongoro,mkoani Arusha,Kuhusu ufaulu wa darasa la saba mwaka huu,amepongezamkoa huo kwa ufaulu huo na kueleza kuwa siri ya kupata matokeo mazuri ni mkakati wa mkoa wa kuwa na mtihani mmoja kwa shule zote za msingi pia  usimamizi na ufuatiliaji .

Amesema ufaulu umepanda kutoka asilimia 72.7 mwaka jana hadi kufikia asilimia 77.7 huku wilaya ya Longido ambayo ilikuwa ikishika mkia kwa miaka iliyopita ufaulu wake umefikia asilimia 85 hivyo kuvuka lengo la kitaifa ambalo ni asilimia 77 na imekuwa ni wilaya ya tatu mkoani humo.

Kuhusu usimamizi wa miradi, Waziri, Nasha, amesema  lazima miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za serikali ikamilike kwa ubora uliowekwa na ndani ya muda ,akawataka wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha wanaisimamia ipasavyo.

 Kuhusu upungufu wa walimu wa sayansi,hisabati amesema serikali mwakani itaajiri walimu wengi lengo ni kutosheleza mahitaji na walimu wanaoajiriwa wanagawanywa kwenye shule kulingana na uwiano  na mwaka huu serikali imeajiri walimu 7000

Amesema bado  kuna upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi,hisabati na Tehama ni mkubwa na serikali itaendelea kuwaajiri ili kukabiliana na upungufu huo.. 

Kwa upande mwingine
SERIKALI imetoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa hospital mbili za wilaya za Longido na Ngorongoro mwaka huu 2018,ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma ya afya na kusogeza huduma hiyo kwa wananchi.

Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Arusha,Dakta Omari Chande, ameyasema hayo Oktoba 27wakati akiwasilisha taarifa ya huduma ya afya kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa RCC, na kusema kuwa kila wilaya imepewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa hospital hizo za  wilaya.

Dakta,Chande,amesema kuwa mkoa umefanikiwa kutoa chanjo  ya mlango wa kizazi kwa wasichana asilimia 80% na chanjo ya pili  itatolewa Novemba mwaka huu Kuhusu upatikanaji wa dawa amesema kiwango cha upatikanaji wa dawa ni asilimia 94%  .

KKuhusu watumishi,Dakta Chande, amesema   mkoa una upungufu  wa watumishi  wa afya wa kada mbalimbali, hivyo halmashauri zinapaswa kuomba Wizara ya Utumishi watumishi hao kwa kuzingatia kada zao .

Akiwasilisha taarifa ya elimu, afisa elimu mkoa wa Arusha,Gifty Kyando,amesema Mkoa  una upungufu wa vyumba 413 vya sekonbdari huku jiji la Arusha likiongoza kwa upungufu wa vyumba 192, ArushaDC vyumba 109, Meru vyumba 37 Monduli vyumba 32 Longido vyumba 29 na Ngorongoro vyumba 33 isipokuwa wilaya ya Karatu ndio pekee isiyokuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,ambapo jiji la Arusha linaongoza kwa wanaunzi kupata mimba .

Jumla ya wanafunzi 38293 walisajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, na waliofanya mtihani ni 37,820 ,waliofaulu ni 33035 sawa na asilimia 87.30 huku jiji la Arusha likiongoza kwa kufaulisha ambapo mkoa umekuwa wa tatu katikitaifa katika kufaulisha wanafunzi mwaka 2018.

MWAKYEMBE AAGIZA WAMILIKI NA WAHARIRI WA TANZANITE KUJIELEZA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb), amesema habari iliyochapishwa na gazeti la kila siku la Tanzanite la leo Jumatatu tarehe 29 Oktoba, 2018 lenye habari zenye tuhuma za kisiasa dhidi ya Viongozi kadhaa, haziakisi msimamo wa Serikali na ameagiza mmiliki na Bodi ya uhariri ya gazeti hilo waitwe mara moja Idara ya Habari (MAELEZO) kujieleza kuhusu msingi wa habari hiyo.

Dkt. Mwakyembe ametoa ufafanuzi huo leo mchana, mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuelezea kushtushwa kwake na mwenendo wa gazeti hilo kuchapisha habari zinazoibua tuhuma za kisiasa dhidi ya baadhi ya Viongozi nchini, wakiwemo Wabunge na kusababisha taharuki kubwa katika jamii.

Gazeti la Tanzanite linatolewa na kampuni ya CZ Information and Media Consultant LTD ya Dar es Salaam na leo katika toleo lake Na. 254 limeandika katika ukurasa wake wa mbele  habari yenye kichwa kinachosomeka “Vigogo 14 hatari kwa nchi watajwa” ambayo inawataja viongozi kadhaa wa kisiasa na wafanyabiashara.

KAMATI YA HUDUMA ZA JAMII YA HALMASHAURI YA CHALINZE YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO.


Kamati ya Elimu,Afya na Maji ya Halmashauri imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2018/2019.

Kamati hiyo ikiongozwa na Bi Rehema Mno ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo imeanza kwa kukagua kikundi cha Wapole Bodaboda Msata,kilichopewa milioni 4, na kununua pikipiki 2 Mwenyekiti wa kikundi Omari salum Mfikilwa ameieleza kamati kuwa kikundi kinaendelea vizuri na kitarejesha mkopo kwa wakati.

Kamati pia imetembelea Shule ya Sekondari kikaro mahali ambapo panajengwa mabweni ya wasichana kwa ufadhili wa mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Mamlaka ya Elimu Tanzania ilitoa Fedha za kitanzania Milioni 150 ambapo zitajenga mabweni mawili yenye kubeba wanafunzi 80.

Kwa mujibu wa Mwalimu wa Fedha,Naftali Sanga alieleza mbele ya kamati kuwa mpaka sasa ujenzi unaendelea na vifaa vya ujenzi vipo vyote na kuihakikishia kamati kuwa Mabweni haya yatakamilika lakini pia na nguvu za wananchi zitahitajika katika ukamilishaji wa mradi huu na hatimaye kuondoa tatizo la malazi kwa watoto wa kike katika Shule hii.

Kamati ilienda moja kwa moja katika jiko la Shule ya Sekondari kikaro la kisasa ambalo limejengwa kwa msaada wa Mapato ya ndani ya halmashauri kiasi cha shilingi Milioni 40,kutokana na Fedha hizo waliweza kujenga pia choo cha jikoni.

Mradi mwingine ulitembelewa na kukaguliwa na kamati ni mradi wa ujenzi wa madarasa mawili shule ya msingi kikaro mradi unaotekelezwa kutokana na Fedha iliyotolewa na serikali jumla ya Fedha za kitanzania Milioni 16.4,lakini kutokana na nguvu za wananchi kutumika serikali ya kijiji iliamua kuongezea chumba kimoja na kufikia vyumba vitatu.

Kamati ya huduma za Jamii imeweza kufika pia Shule tarajali ya Komkomba ambayo imejengwa na ina madarasa manne lakini haijapata usajili kutokana na kutokidhi vigezo kwa maana kwamba bado inaupungufu wa madarasa mawili,kamati imejionea ujenzi wa darasa moja lenye thamani ya Fedha za kitanzania Milioni 20.

Kwa upande wa sekta ya afya kamati ya huduma za Jamii imefika katika kijiji cha kibaoni kata ya Mandera na kuona ujenzi wa zahanati ya kijiji unaoendelea,katika ujenzi wa zahanati hii halmashauri imechangia kiasi ya Fedha za kitanzania Milioni 30,

Kamati ya huduma za Jamii ilikamilisha kazi yake kwa kutembelea na kuona ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Mwetemo,kata ya Kiwangwa, ujenzi huu unatekelezwa kutokana na Fedha zilitolewa na halmashauri kutokana na Mapato ya ndani ya halmashauri jumla ya Fedha za kitanzania Milioni 8.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati ya huduma za Jamii, Mheshimiwa Rehema Mno aliwashukuru wasimamizi wa miradi katika sekta mbalimbali kwa kuonyesha moyo wa uzalendo katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka watendaji wa halmashauri kuipitia Mara kwa Mara miradi inayotekelezwa vijijini kwa ufanisi zaidi.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI, MAWASILIANO NA UHUSIANO
HALMASHAURI YA CHALINZE

RAIS MAGUFULI ATOA MSIMAMO KUHUSU BEI YA KOROSHO.

MAGAZETI YA LEO OKTOBA 29 2018

Sunday, October 28, 2018

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA WANUNUZI WA KOROSHO ATOA MSIMAMO WA SERIKALI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wanunuzi wa zao la Korosho katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kutoa msimamo wa Serikali kuhusu bei ya Korosho kuwa isipungue shilingi 3000 kwa kilo moja.
 

Wadau na Wanunuzi wa Korosho wakiwa wanasikiliza Maelekezo ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati alipokutana nao na kuzungumza nao jijini Dar es Salaam.

PICHA NA IKULU.