Tuesday, October 23, 2018

SAMIA SULUHU KUWASILI BAGAMOYO OKTOBA 24 KUANZA ZIARA MKOA WA PWANI.

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo (wa katikati) akizungumza kuhusu ujio wa makamu wa Rais mkoani humo, (wa kwanza kushoto) katibu tawala mkoa Theresia Mbando na wa kwanza kulia kaimu mkuu wa wilaya ya Kibaha Jokate Mwegelo.
.........................

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania ,Samia Suluhu anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi  Mkoani Pwani  octoba 24 ambapo atatembelea miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa  wa Pwani,  Mhandisi Evarist Ndikilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari .

Ndikilo alisema ,makamu wa Rais akiwa mkoani humo  atakagua miradi  mbalimbali   ya maendeleo katika Wilaya  nne za mkoa huo na ataanzia ziara kwa kukagua miradi ya maendeleo ya Wilayani Bagamoyo.

“Miradi hiyo ni pamoja na kutembelea   mradi mkubwa wa  Bandari mpya ya Mbegani wilayani Bagamoyo  yenye ubia  na nchi tatu za Tanzania,Oman na China,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa baada  ya kukagua miradi wilayani Bagamoyo atakwenda  Halmashauri ya wilaya ya Chalinze  ambako atakagua miradi ya maendeleo.
 “Baada ya hapo atakwenda , Wilaya ya Kisarawe, Mkuranga na atahitimisha ziara hiyo wilaya ya Kibaha”

Aidha mradi mwingine wa kitaifa ni atakaotembelea ni ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) kwenye karakana kubwa iliyoko Soga wilayani Kibaha.

“Mbali ya kutembelea miradi hiyo mikubwa pia atatembelea miradi mingine ikiwemo ya miradi ya  afya,  maji na elimu,”alisema Ndikilo.

Ndikilo alisema kuwa akiwa wilayani Kibaha Makamu wa Rais anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonyesho ya wiki ya viwanda itakayozinduliwa Oktoba 29 katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo  katika eneo la Picha ya Ndege.

Makamu wa Rais atakapoanza ziara hiyo  atapokea taarifa kutoka  Halmashauri zote  za mkoa huo pia atapata nafasi ya kuzungumza na  Wakurugenzi wa Halmashauri hizo.

KAMPUNI YA SAYONA YAKABIDHI VIFAATIBA VYA SHILINGI MILIONI TANO CHALINZE.


Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sayona,Bw Aboubakary Mlawa kulia akikabidhi vifaa hivyo kwa Diwani wa kata ya Talawanda.
....................................
 
Kampuni ya Sayona Fruits Limited ya Mboga Chalinze imekipatia Kijiji cha Magulumatali vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni Tano  kwa ajili ya Zahanati ya kijiji hicho.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Diwani wa kata ya Talawanda, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sayona,Bw Aboubakary Mlawa alisema msada huo unatokana na uhitaji wa huduma ya afya katika kijiji hicho.

Alisema baada ya kupata taarifa ya kumalizika kwa ujenzi wa zahanati hiyo ambao ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi alitembelea kijijini hapo na kukuta changamoto ya vifaa na hivyo kampuni yake kuamua kuwasaidia.

Bw Mlawa alisema vifaa hivyo vitasaidia sasa kuanza kwa huduma katoka zahanati hiyo ambayo ilishindwa kutoa huduma kutokana na kutokuwepo kwa vifaa .

Naye Diwani wa kata hiyo Bw Said Zikatimu akishukuru kwa niaba ya wananchi alisema licha ya kukamilika kwa ujenzi zahanati hiyo ilishindwa kuanza kutoa huduma kutokana na kukosekana kwa vifaa tiba.

Alisema Halmashauri iliwapangia Madaktari na wahudumu katika zahanati hiyo lakini hawakuweza kutoa huduma kutokana na kusubiri mchakato wa ununuzi wa vifaa.

"Kwa kweli tunawashukuru Sayona kwani sasa huduma zitaanza  kwa vifaa hivi lakini pia Halmashauri itaendelea na mchakato wake wa kuleta madawa"alisema Diwani huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Hlamaahauri ya Chalinze.

Vifaa vilivyotolewa na Sayona Fruit Limited Mboga ni pamoja na vifaa vya huduma kwa wagonjwa mchanganyiko sambamba na vifaa vya uzazi na huduma kwa watoto. 

Sayona imekuwa ikisaidia sekta mbalimbali katika huduma za jamii,sambamba na kuwasomesha watoto ambao wazazi wao hawana uwezo katika elimu ya sekondari katika Halmashauri ya Chalinze.
 

 Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sayona,Bw Aboubakary Mlawa kulia, akimkabidhi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu vifaa hivyo.

TUNAFUATILIA KERO YA MAJI MIMI NA RIHIWANI- DKT. KAWAMBWA.

MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa, na Mbunge mwenzake wa Jimbo la Chalinze, Mwanasheria Ridhiwani Kikwete wakisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati Rais Magufuli alipowasili wialayani Bagamoyo katika moja ya ziara alizowahi kufanya wilayani humo pembeni kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.
................................................................ 

Na Omary Mngindo, Mwavi

MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa, amesema kuwa yeye akishirikiana na Mbunge mwenzake wa jimbo la Chalinze Mwanasheria Ridhiwani Kikwete wanaendelea kupambana na suala la maji kwa wapigakura wao.

Dkt. Kawambwa ametoa kauli hiyo katika Kitongoji cha Vigwaza, Kijiji cha Mwavi Kata ya Fukayosi jimboni hapa, alipokuwa anazungumza na wapigakura wake inayolenga kupokea chabgamoto zao ili aziwasilishe kwenye bunge lijalo.

Alisema kwamba mradi wa maji unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) awali ulianza ukiwa na vijiji 9, sasa kina vijiji zaidi ya mia, ongezeko ambalo limeuzidi uwezo mradi huo.

"Mimi na Mbunge mwenzangu Ridhiwani Kikwete upande wa Chalinze kwa pamoja tupo katika harakati za kupambana na tatizo la maji ambalo limekuwa linawasumbua kwa muda mrefu, niwaombe mtambue hivyo," alisema Dkt. Kawambwa.

Aliongeza kwamba awali Serikali iliingia Mkataba na Kampuni moja ambayo kutokana na kushindwa kutekeleza kazi zake imemfutia mkataba, hivi sasa iko katika mpango wa kumpata Mkandarasi mwingine atayeuendeleza mradi huo.

Kwa upande wake mkazi Nuhu Ally alimweleza Dkt. Kawambwa kuwa, wanatumia muda mwingi kutafuta maji katika visima hali, inayowapunguzia muda wa kufanya shughuli za kimaendeleo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwavi Shabani Mkumbi alisema kuwa changamoto ya maji kitongojini hapo ni ya muda mrefu, huku akieleza kuwa wakati wakisibiri mipango ya muda ntefu, ni vizuri kukapatikana visima vitavyowapunguzia adha hiyo wakazi hao.

Akizungumzia ombi la kisima, Dkt. Kawambwa amewaambia wana-Vigwaza hao kuwa tayari kuna mmoja wa marafiki zake wapo tauati kuchimba kisima kwenye eneo hilo.

KITAME FC WALILIA KAWAMBWA CUP

Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa, akikabidhi Jezi kwa moja ya timu zilizowahi kushiriki mashindano ya Kawambwa Cup katika jimbo hilo.
.....................................................

Na Omary Mngindo, Kitame- Oktoba 23

TIMU ya soka ya Kitame Fc ya Kijiji cha Kitame, Kata ya Makurunge Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani imemtaka Mbunge wao Dkt. Shukuru Kawambwa kurejesha michuano ya soka ya Kawambwa Cup.

Wakizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na mbunge wao, nahodha wa timu hiyo Daniel Joseph na Mwenyekiti Salehe Ismail wamesema kuwa kusimama kwa mashindani hayo yamewakosesha vijana kuonesja uwezo wao, hivyo kudumaza vipaji.

Nae Ismail alisema kuwa michuako hiyo iliyokuwa inachezeshwa kwa miaka kumi mfululizo, yakishirikisha timu mbalimbali kwa kiasi kikubwa ilisaidia kuibua vipaji vya vijana ambapo baadhibyao wanefanikiwa kucheza ligi mbalimbali.

"Mbunge tunakuomba ufanye juu chini uturudishie mashindano ya Kawambwa Cup, katika kipindi chote cha miaka kumi timu zetu zililuwa zinashiriki michuano hiyo kuanzia ngazi za Vijiji, Kata hatimae hatua ya Kawambwa Cup," alisema Mwenyekiti hiyo.

Akijibia maombi hayo, Dkt. Kawambwa alisema kuwa yupo katika mikakati ya kuhakikisha kuanzia mwanzoni kwa mwaka ujao wa 2019 yaanze kama ilivyokuwa hapo awali.

"Ni kweli michuano ya Kawambwa Cup iliyochezwa kwa miaka kumi mfululizo yalikuwa na hamasa mkubwa, vijana walipata fursa ya kuonesha vipaji vyao, Niko mbioni kuona no namna gani yaweze kuchezwa kuanzia mwakani," alisema Kawambwa.

Alisema kuwa kukosekana kwa michuano hiyo katika kipindi kifupi hata kwake hakijamfurahisha na lwba imetokana na kutokuwa katika mazingira mazuri ya kifedha.