Friday, May 4, 2018

NAIBU WAZIRI WA NISHATI AWASHA UMEME VIJIJI VYA CHALINZE,

  
Naibu waziri wa Nishati Mh. Subira Hamisi Mgalu akiwa kijiji cha saleni Halmashauri ya Chalinze kwaajili kuwasha umeme Mradi wa Umeme Vijijini Kwa kupitia Ujazilizi Densification ulioanza kutekelezwa April 2017 na kukamilika Sasa.Wananchi wameanza kuunganishiwa umeme Kwa gharama ya 27000 tu.
 Image may contain: 6 people, including Subira Mgalu, people smiling, people sitting
Naibu waziri wa Nishati, Mh. Subira Mgalu amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Dkt. John Magufuli imedhamiria kufikisha umeme kila kijiji ili kuwaondolea adha wananchi walikosa huduma ya umeme kwa muda mrefu.

Naibu waziri huyo wa Nishati ambae pia ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani aliyasema hayo katika ziara yake Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo ambapo aliweza kuzindua miradi ya umeme vijijini REA kwa kuwasha umeme katika vijiji kadhaa vya Halmashauri hiyo.

Aidha, alisema ni fusa kwa wananchi sasa kujitokeza kuchukua fomu na kulipa gharama ya shilimngi 27,000 kwaajili ya kuunganishiwa.

Alisema uzinduzi wa miradi hiyo ya umeme ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na serikali ya awamu ya tano katika kampeni za uchaguzi na kwamba kilichobaki sasa ni utekelezaji tu.

katika hatua nyingine Naibu waziri huyo amewashukuru wadau wa Elimu katika Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mrs Barbara na Wentworth Africa Foundation kwa msaada wao walotoa katika Sekondari ya wasichana Mandela ambapo waliweza kukabidhi taulo maalum kwaijili ya matumizi ya wasichana na kila msichana amepata Taulo Za kutumia Mwaka Mzima Kwa Wasichana Mia Tano Hamsini.
Wakati huo huo Naibu waziri huyo wa Nishati aligawa Taa za sola kwa Zahanati ambazo hazijafikiwa na umeme ili kuwarahishia kina mama wakati wa kujifungua.

Image may contain: 4 people, people smiling, people standing, outdoor and nature
Naibu waziri wa Nishati Mh. Subira Hamisi Mgalu akiwa ziara katika vijiji vya Chalinze ambapo aliweza kuwasha umeme katika vijiji vya Hondogo na Saleni pmoa na kugawa Taa za sola katika Zahanati ya Mihuga.
 Naibu waziri wa Nishati Mh. Subira Hamisi Mgalu ambae pia ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani akikabidhi Taulo maalum kwaijili ya matumizi ya wasichana Kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mandela ambapo kila msichana amepata Taulo Za kutumia Mwaka Mzima Kwa Wasichana Mia Tano Hamsini, Msaada huo umetolewa na Mrs Barbara na Wentworth Africa Foundation, Wadau hao wa Elimu Pia wameahidi kufadhili ujenzi wa Maktaba.
 Image may contain: 4 people, people smiling, people standing, crowd and outdoor 
Mh. Subira Mgalu amekabidhi, Mabox ya Vitabu Kwa Maendeleo ya Shule.
Image may contain: 4 people, including Subira Mgalu, people sitting
Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa katika zoezi la kugawa Taa za solar Kwa ajili ya Wadi za kuzalishia Kina Mama Kwa ajili ya Zahanati za Mihuga , Masimbani na Kweikonje Maeneo ambayo hayana MiundoMbinu ya Umeme.
Image may contain: 1 person, crowd, tree, sky and outdoor 
Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa kijiji cha Hondogo kata ya Miono Halamshauri ya Chalinze ambapo aliweza kuzindua mradi wa umeme viijini REA ambapo kijiji hicho sasa kimepata umeme.

Wednesday, May 2, 2018

DKT. ABBAS AKUTANA NA WAANDISHI, WASOMI WA MAWASILIANO YA UMMA MKOANI MWANZA

Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania Abubakar Karsan akimuonesha  Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi bango lenye kuonesha majukumu ya klabu za waandishi wa habari nchini,Jana 1/05/2018 mkoani Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania Abubakar Karsan akikabishi  Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi kalenda ya chama hicho,Jana 1/05/2018 mkoani Mwanza.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi  akiongea na wasomi wa Mawasiliano ya Umma wa Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza kuhusu Maadili ya Uandishi wa Habari na umuhimu wa uandishi katika kufuata weledi, Jana 1/05/2018 mkoani Mwanza.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akishiriki kipindi cha TUJADILIANE kinachoendeshwa na Doto Bullendu chenye lengo la kuhamasisha maendeleo katika nchi kwa kutumia vyombo vya Habari, Jana 1/05/2018 mkoani Mwanza
Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania Abubakar Karsan akiongea wakati wa kumkaribisha Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Dkt. Hassan Abbasi kabla hajashiriki kipindi cha TUJADILIANE kilicho hudhuriwa na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari vya kanda ya Ziwa, Jana 1/05/2018 mkoani Mwanza.


Tuesday, May 1, 2018

MAADHIMISHO YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI KUFANYIKA DODOMA KITAIFA.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe anatarajiwa kuwa  mgeni rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini .

Akizungumza na  Waandishi wa Habari  Jijini Dodoma , Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Nevile Meena alisema mada mbalimbali zitakazojadiliwa ni pamoja na  changamoto zinazovikumba vyombo vya habari katika kipindi cha miaka 27 tangu Azimio la Windhoek, Namibia, lilipopitishwa linalohusu uhuru wa vyombo vya habari.

 Akieleza zaidi alisema, Kilele cha Maadhimisho hayo kitafikiwa      kesho, Mei 3, mwaka huu, mkoani Dodoma, ambapo siku moja kabla kutakuwa na majadiliano kuhusu hali ya vyombo vya habari nchini ambayo yatafunguliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

“Tutapata Wakati muafaka wa kujadili mada kuu ya changamoto zetu, pia kutakuwa na mada nyingine zitakuwa zinaendelea katika vikundi, ikiwemo inayohusu mitandao ya kijamii kama inatakiwa kudhibitiwa au watumiaji ndio wajidhibiti wenyewe,” alisema Meena.

Pamoja na hayo alisema kutakuwa na mada kuhusu unyanyasaji wa kingono ndani ya vyombo vya habari, na kuona kama suala hilo bado ni kikwazo hasa kwa waandishi wanawake kupata nafasi za juu kwenye vyombo vya habari.

Aidha Katibu huyo wa TEF alisema, kutakuwa na mada kuhusu usalama wa waandishi wa habari, ni kiasi gani waandishi wanakuwa salama wanapofanya kazi zao katika maeneo mbalimbali.

“Suala la haki za kupata habari, japo limeingizwa kwenye sheria tangu mwaka 2016 na kanuni zake Februari mwaka huu, na namna gani mwandishi anaweza kudai haki hiyo,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Klabu za Waandishi Tanzania (UTPC), Jane Mihanzi aliyataja maadhimisho hayo kuwa ni fursa kwa wadau wa habari kujadili namna vyombo vya habari vilikotoka, vilipo na wapi vinaelekea.

” Sisi kama wadau wa habari tunaotambua na kuwajali wananchi kupata habari, tumekuwa tukisaidia waandishi kuwapamafunzo na vifaa vya kazi,”alisema. 
Kwa upande wake mwakilishi wa Mfuko wa Habari Tanzania (TMF), Razia Mwawanga alisema kupitia maadhimisho hayo wanahabari na jamii kwa ujumla wataelewa umuhimu na wajibu wa kuwajibika.

Alisema,japo kuwa taaluma hii ina vikwazo vingi kuna ,waandishi watapaswakuwajibika kwa kujitolea ikiwa ni pamoja na  kuhamasika kuacha kuandika habari kwa mazoea na bafala yake wajikite katika kuandika habari zenye maslahi za kueleza wajibu wa serikali kwa umma na umma kwa serikali yao.

  Hata hivyo alisema fani ya uandishi habari inapaswa kujikita katika maadili ya uandishi bora kwa kuzingatia vigezo weledi na si vinginevyo  kwani hii itasaidia ukuwaji wa fani hiyo hapa nchini na kuondokana na uandishi wa kimazoea katika kutekeleza majukumu ya wanahabari ya kila siku.

MAGAZETI YA LEO TAREHE 01 MAY 2018.

Monday, April 30, 2018

BAGAMOYO YAZINDUA CHANJO YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiandaa sindano kwaajili ya uzinduzi wa chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
   
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akizungumza kabla ya kuzindua chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
.......................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga amesema mtu atakaekwamisha zoezi la chanjo ya Saratani ya shingo ya Kizazi atachukuliwa hatua za kisheria.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema serikali inapanga mikakti ya kuboresha Afya za wananchi wake ili waweze kutumikia taifa pamoja na kuihudumia wenyewe na familia zao.

Aliongeza kuwa, Bagamoyo ina mikakati ya kukuza uchumi kwa kujenga viwanda hivyo ni wazi kuwa wanaotakiwa kufanya kazi katika viwanda hivyo ni watu wenye afya nzuri isoyokuwa na mgogoro.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa chanjo za magonjwa mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ameigiza Halmashauri ya Chalinze kuangalia madeni ya madaktari na kuwalipa ili kuwaondolea manung'uniko ambayo yanaweza kuzorotesha utendaji kazi wao.

Alisema yapo malalamiko kwa madaktari ambao hawalipwi fedha za kuitwa kazini kwa matukio ya dharula nje ya muda wa kazi (On-call Allowance) ambayo ni haki yao kimsingi.

Ameitaka Halmshauri ya Chalinze kufanya haraka kuwalipa madaktari On-call Allowance ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi muda wowote wanapohitajika.

Alisema Serikali imetenga bajeti kubwa katika wizara ya Afya ili kuboresha huduma za afya hivyo Halmashauri nazo zinapaswa kuongeza bajeti zake katika sekta ya afya ili kuwajengea mazingira rafiki madaktari na watumishi wa afya kwa ujumla. 

Aidha, alimtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai kuchukua hatua za dhati kuhakikisha zahanati ambazo hazina madaktari anapeleka madaktari ili kuwasogezea wananchi huduma za afya ambazo kwa sasa wanatembea umbali mrefu licha ya kuwepo zahanati kwenye maeneo yao.

Awali wakichangia mada katika semina elekezi iliyofanyika shule ya Kikaro Halmashauri ya Chalinze washiriki wa semina hiyo walisema wananchi wanakabiliwa na changamoto ya kufuata huduma za afya mbali na maeneo yao hali inayopelekea kushindwa kuwapatia watoto wao chanjo.

Walisema vipo baadhi ya vijiji mwananchi analazimika kutumia shilingi elfu nane ili kumpeleka mtoto akapate chanjo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai alisema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa wilaya ili kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo ambayo tayari kuna Zahanati lakini hakuna Daktari.

Alisema tatizo la upungufu wa madaktari katika Halmashauri hiyo limetokana na watumishi walioondolewa kutokana na kuwa na vyeti feki hivyo idara ya afya katika Halmashauri hiyo ni miongoni mwa wathirika ambapo mpaka sasa wanasubiri watumishi wengine watakaopangiwa na wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (TAMISEMI) ili kuziba mapengo hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashuri ya Chalinze Saidi Zikatimu alisema ataiongoza Halmashauri hiyo katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa watumishi ili nao wafanye kazi kwa moyo na bidii.

Alisema ni kweli serikali imetenga fedha kwaajili kuboresha sekta ya afya ambapo Halmashauri ya Chalinze imepoke zaidi ya shilingi milioni 440 kwaajili ya kuboresha huduma katika vituo vya afya na Zahanati na milioni 400 kwaajili ya kituo cha afya ambapo ujenzi wake unaendelea.

Chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi imezinduliwa rasmi hii leo jumatatu ya tarehe 30 Aprili katika Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze ambapo walengwa ni wasichana wenye umri wa miaka 14.
 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akivaa koti la udaktari ikiwa ni maandalizi ya kuzindua chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Watumishi wa halmashuri ya Chalinze wakifutilia kinachoendelea kwenye semina elekezi kuhusu chnjo ya mlango wa kizazi kwa wasichana iliyofanyika shule ya Kikaro kata ya Miono.
 Mwenyekiti wa Halmashuri ya Chalinze Saidi Zikatimu akizungumza katika semina hiyo.
 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai akitoa maelekezo kwa washiriki.



Washiriki wa semina hiyo wakifuatilia maelezo yanayotolewa.

Muwezeshaji akitoa semina kwa washiriki.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwa na viongozi wa dini katika picha ya pamoja.


 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwa na maafisa tarafa pamoa na viongozi wengine waandamizi katika picha ya pamoja.

WATATU WAFA NA 530 WAKUTWA NA DALILI ZA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI PWANI

Mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Yudas Ndungile akitoa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa mmoja wa wanafunzi, wakati wa uzinduzi wa zoezi ya chanjo hiyo kwa watoto wenye umri wa miaka 14 ,kimkoa yaliyofanyika kituo cha afya mkoani,Kibaha.
..........................

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

JUMLA ya akinamama 20,815 waliofanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi mkoani Pwani katika kipindi cha miaka mitatu kati yao 530 walikutwa na dalili za awali za saratani hiyo,ambapo watatu walifariki.

Aidha kati ya akinamama hao waliofanyiwa uchunguzi akinamama 412 walitibiwa matibabu na  115 walipata rufaa ya kwenda Oceanroad na hospitali ya Taifa ya Muhimbili  kwa matibabu zaidi.

Akitoa takwimu hizo ,wakati wa uzinduzi wa zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka 14 ,kimkoa yaliyofanyika kituo cha afya mkoani,Kibaha,mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Yudas Ndungile alisema , ipo changamoto ya kutojua idadi ya vifo kamili kwa kuwa wengi hupata rufaa.

Pamoja na hayo ,alisema ipo haja ya kuona ukubwa wa tatizo hilo kwa kuangalia afya mapema na watoto wa mashuleni kupata chanjo.
Ndungile alisema jumla ya watoto wa kike 18,823 waliopo shule na nje ya shule mkoani hapo watapatiwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi mwaka huu.

Alielezea, tayari wameshapokea chanjo na wataanza kuzitoa katika vituo mbalimbali vya huduma.

Ndungile aliitoa shaka jamii kuwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ni salama ,haina madhara na haiathiri uwezo wa binti kupata watoto hapo baadae
” Serikali imethibitisha usalama wa umadhubuti wa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ndiyo maana imeiongeza kwenye mpango wa Taifa wa chanjo ili iweze kusaidia kudhibiti tatizo hilo kwa akinamama”:!
Ndungile alieleza mwaka 2018 chanjo itatolewa kwa wasichana waliofikisha umri wa miaka 14 na ili kupata kinga kamili walengwa watahitaji kupatiwa dozi mbili.

Alisisitiza chanjo hiyo huwakinga wasichana wasipate saratani ya mlango wa kizazi pindi wawapo watu wazima wakiwa na familia zao.

“Nchini Tanzania saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti ” Saratani hizi mbili kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya wakinamama vitokanavyo na saratani”alibainisha Ndungile.

Kwa upande wake ,Mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Dkt.Tulitweni Mwinuka alisema ,wamezindua chanjo hiyo kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Alielezea ,kiwilaya wamezindua chanjo hiyo kwa wasichana 100 kituoni hapo na wanatarajia kufanikisha na kuleta matokeo kutokana na chanjo hiyo .
Akizindua zoezi hilo ,kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Pwani,mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama aliwataka wanafunzi wa kike kuacha kujiiingiza kwenye vitendo vya ngono mapema ili kujiepusha kuingia kwenye hatari ya kupata magonjwa ya zinaa,ukimwi na hata saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema moja ya sababu zinazosababisha saratani hiyo ni kuwa na wanaume wengi ,kuvuta sigara ,wenye mitala, na kuanza mapema kufanya ngono.
“Acheni kujiingiza kwenye mapenzi mapema ni hatari katika maisha yenu, ukivua sketi ,na mwanaume akavua suruali jua kuna hatari ya kuhatarisha maisha yako kwa magonjwa yanayosababishwa kutokana na ngono”
“Jizuieni hadi hapo mtakapoolewa ,msikimbilie ngono za haraka,mtapata saratani”: alisisitiza Mshama.

Mshama aliwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 14 kupata chanjo hiyo kwani haina madhara.