Saturday, August 20, 2016

MWIMBAJI WA TAARAB BI. SHAKIRA SAID AFARIKI DUNIA GHAFLA.

index
MWANAMUZIKI MKONGWE WA TAARAB BI. SHAKIRA  SAID AMEFARIKI GHALA USIKU MARA BAADA YA KUMALIZA KUSWALI NYUMBANI KWAKE MBAGALA CHARAMBE AMBAPO AMEANGUKA GHAFLA NA KUPOTEZA MAISHA.
  BI. SHAKIRA ALIKUA HAUMWI.. MAREHEMU ATAKUMBUKWA KWA WIMBO MAARUFU
“NIKIMKUMBUKA WANGU MARIDHAYAMACHO YANALIA MOYO UNACHEKA”  HABARI HIZI  ZIMETHIBITISHWA NA MWANAE , MPAKA SASA MWILI WA MAREHEMU  UPO NYUMBANI UNASUBIRI TARATIBU ZA KUPELEKWA HOSPITALI KWA AJILI YA KUHIFADHIWA….!!
ADDO NOVEMBER RAIS SHIRIKISHO LA MUZIKI TANZANIA MAWASILIANO  0754396367

Friday, August 19, 2016

KESI APITISHWA KUCHEZEA YANGA.

index
Kamati ya Sheria na Haki za wachezaji imepitisha usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara huku ikiwa imepitisha jina la Hassan Ramadhani ‘Kesi’ kuitumikia Young Africans kuanzia msimu huu 2016/17 baada ya kuona kuwa hana tatizo katika usajili badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Young Africans kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.
Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Young Africans wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. 

TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.

Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea.

 Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa.

PAMOJA FILM YAPEWA SIKU SIKU 7 KUWASILISHA VIELELEZO VYA KAZI ZAO

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo akionyesha moja ya nyaraka zilizokiukwa na Kampuni ya Usambazaji wa Filamu nchini ya Pamoja Film Company wakati wa kikao baina ya Bodi ya Filamu Tanzania na kampuni hiyo ya usambazaji wa filamu. Bi Fisoo amewaasa wadau wa filamu kufuata sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya filamu nchini.
............................................................................................


Bodi ya Filamu Tanzania imetoa siku saba kwa Kampuni ya Usambazaji wa Filamu ijulikanayo kama ‘Pamoja Film Company’ kuwasilisha nyaraka za filamu zake ili kukagua na kuhakikisha kama wamefuata sheria na kanuni zinazosimamiwa na bodi hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kampuni hiyo kubainika kukiuka baadhi ya sheria na kanuni za usambazaji zikiwemo za kutowasilisha miswada ya filamu (script) kabla ya kuanza kurekodi, kuzitangaza kazi hizo kwenye mitandao ya kijamii bila ya kuzifikisha Bodi ya Filamu Tanzania Kwa ajili ya ukaguzi pamoja na kufanya kazi za utengenezaji na usambazaji wa filamu bila kibali.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo alipokuwa akiongea na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Lufingo Exaud kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza kuwa kukiuka sheria na kanuni zinazosimamiwa na bodi ni kosa kisheria.

“Natoa siku saba kwa Kampuni hii kuwasilisha miswada ya filamu zake 12 alizozitangaza na kuzisambaza kinyume cha sheria pamoja na kuleta maelezo kwa maandishi ya kujieleza sababu zilizowapelekea kufanya kazi hizo bila kibali kutoka bodi”,alisema Fissoo.

Filamu hizo zilizotolewa na Kampuni hiyo bila kufuata sheria na kanuni ni; Spompompo, Tanga Raha, Buku 10, Jirani Hafugiki, Mke Sahihi, Chanzo, Ahsante, Je Alaumiwe, Mwaka wa Tisa, Nyaraka na Kanya Boya.

Fisoo ameongeza kuwa Bodi imefanya jitihada kubwa kutoa elimu kwa umma kupitia njia za vipeperushi, kuandaa na kushiriki mikutano na makongamano ya kitaifa na kimataifa, kushiriki maonesho na maadhimisho ya kisekta na kitaifa ikiwa na lengo la kuwaelemisha wadau wa filamu kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta hiyo nchini.

Aidha, amewaonya wadau wote wa filamu kuacha kukiuka sheria na kanuni zinazosimamia tasnia ya filamu nchini kwani kufanya hivyo ni kosa kubwa kisheria, “tunawaonya wadau wote kuacha mara moja tabia hii” alimalizia.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni hiyo, Lufingo Exaud amekiri makosa yake na ameahidi kulipa faini za makosa yote, pia ameomba msamaha mbele ya Bodi hiyo na kuapa kuwa hatorudia tena. Kwa kumalizia ameahidi kuwa balozi mzuri wa Bodi ya Filamu Tanzania na yupo tayari kuwapa elimu wadau wengine wa filamu nchini ili waweze kufuata sheria na kanuni zinazoongoza sekta hiyo.

Mbali na kuahidi kushirikiana na bodi hiyo, Lufingo ameusifia utaratibu wa bodi wa kurahisisha upatikanaji wa vibali kwani kwa sasa baada ya kuwasilisha muswada wa filamu kwa ajili ya ukaguzi utapatiwa kibali ndani ya muda wa siku saba za kazi.

KIINGILIO MECHI YA SERENGETI BOYS, NA AFRIKA KUSINI SH 2,000, 5,000

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kiingilio cha Sh 2,000 kwa mzunguko na Sh 5,000 kwa jukwaa kuu wakati timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakapocheza na Amajimbos ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Madagascar, mwakani.

Mchezo huo utakaoanza saa 9.00 alasiri Jumapili Agosti 21, 2016 kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi – Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam utachezeshwa na Mwamuzi Noiret Jim Bacari wa Comoro akisaidiwa na Mmadi Faissoil na Said Omar Chebli wakati mezani atakuwa Ali Mohamed Adelaid huku Kamishna wa mchezo huo atatoka Somalia ambaye anaitwa Amir Abdi Hassan.

Jumamosi Agosti 6, 2016, Serengeti ilitoka sare ya 1-1 na Afrika Kusini katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, Mji ulioko Kusini – Magharibi mwa jiji la Johannesburg, mabao yote yalipatikana kipindi cha pili yakiwa ni ya penalti kwa kila upande. Afrika Kusini ndio walioanza kupata penalti katika dakika 65 iliyofungwa na Luke Gareth kabla ya Ally Msengi kuisawazishia Serengeti Boys katika dakika ya 70.

Penalti ya Afrika Kusini ilitokana na mmoja wa mabeki wa Serengeti Boys kumfanyia madhambi Linamandla Mchilizeli wa Amajimbos ndani ya eneo la hatari wakati ile ya Serengeti Boys ilitoakana na beki Luke Donn wa Amajimbos kunawa mpira eneo la hatari. Mwamuzi wa mchezo huo alikuwa, William Koto kutoka Lesotho.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema: “Watanzania wakaribie Chamazi, waje kutushangilia ili tushangilie ushindi kwa pamoja kikosi changu kiko vema na ninamshukuru Mungu kwa hilo, akili yangu na akili za wachezaji wangu ni kumuondoa Msauzi (Afrika Kusini).”