Thursday, August 18, 2016

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU USAFIRISHAJI WA MAZAO YA MISITU KIHOLELA

hel
Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongoakitoa ufafanuzi leo, Mpingo House jijini Dare Salaam, kuhusu upigaji marufuku usafirishaji wa magogo ya miti kwenda nje ya nchi, magari kubeba mbao yakiwa yamefunikwa, pikipiki na baiskeli kubeba mkaa kwenda sehemu moja hadi nyingine mijini na vijijini. Kulia ni  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo hel1

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongo (Kushoto)  wakizungumza na Waandishi wa habari  leo, Mpingo House jijini Dare Salaam, kuhusiana na utaratibu kusafirisha  mazao ya misitu ikiwemo mkaa ambapo mfanyabiashara anayefanya biashara hiyo, atapaswa kuwa na vigezo ambavyo Serikali inavihitaji, na atakaekwenda kinyume hatua za kisheria zitachukuliwa  dhidi ya muhusika.
...................................................................................................


WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  imepiga marufuku usafirishaji wa mazao ya misitu ikiwemo mkaa ambapo mfanyabiashara anayefanya biashara hiyo, atapaswa kuwa na vigezo ambavyo Serikali inavihitaji, tofauti na hapo sheria itachukua mkondo wake.

Imesema zuio hilo linakwenda sambamba na kupiga marufuku usafirishaji wa magogo ya miti kwenda nje ya nchi, magari kubeba mbao yakiwa yamefunikwa, pikipiki na baiskeli kubeba mkaa kwenda sehemu moja hadi nyingine mijini na vijijini.
   
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisema uamuzi huo ni moja ya mikakati ya kukusanya maduhuli stahiki ya rasilimali za misitu na kuwabana wakwepa ushuru.

Alisema moja ya majukumu ya TFS, ni kuhakikisha inaanzisha na kusimamia rasilimali za misitu ili zisaidie ustawi wa taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo ni lazima wananchi wafahamu kuwa ni kosa kuvuna hovyo misitu na bidhaa zake bila kibali.

Mtendaji  huyo alisema kila zao linalotokana na misitu ni lazima lilipiwe ushuru stahiki na kukatiwa risiti, hivyo kukwepa kufanya hivyo kwa kutumia njia mbalimbali zinazokatazwa ni kuvunja sheria na kuiibia serikali mapato.

“Mazao ya misitu, ikiwemo mikaa ni kosa kuuzwa na kusafirishwa bila kuwepo kibali na risiti. Muuza mkaa lazima uwe na risiti, na wewe mnunuzi tukikukamata na gunia la mkaa na huna risiti utawajibika.

“Tunataka kuhakikisha maduhuli ya mazao ya misitu yanakusanywa ili kupata matumizi endelevu ya rasilimali za misitu hivyo ni biashara hii ya miti, mkaa na mazao ya nyuki inatakiwa iwe wazi.

“Ni marufuku kusafirisha mazao ya misitu usiku, kama mtu ana vigezo vyote tunavyovihitaji kusafirisha mazao ya misitu anatakiwa kusafiri kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni, ikipita hapo, weka pembeni gari mpaka asubuhi,” alisema.

Aidha alisema TFS chini ya Wizara ya Maliasili ina Meneja miti kwenye kila wilaya, ambao wanafanya kazi kwa karibu na Maofisa Watendaji wa vijiji ambao hushirikiana kutoa vibali kwa kuvuna miti stahiki kisheria na kutoa risiti.

Alisema risiti hizo pamoja na vigezo vingine ikiwemo kuwa na usajili wa TFS, leseni ya biashara na namba ya utambulisho wa mfanyabiashara (TIN), hati ya kusafirisha mazao ya misitu humfanya mfanyabiashara kuruhusiwa kuendelea na biashara ya mazao ya miti nchini.

Profesa Silayo alisema TFS wataendelea na majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipozungumza na watumishi wa wizara hiyo mapema mwezi uliopita.

Baadhi ya maagizo hayo likiwemo la kupunguza vizuio kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, Silayo alisema wanafanya utafiti kujua kizuizi gani kitolewe na kipi kibaki sambamba na kubana uvunaji holela wa misitu.

Alisema lengo lao si kukamata magogo baada ya kuvunwa bali ni kuzuia misitu isiharibiwe hivyo inapotokea, hutumia vizuio hivyo kukagua na kukamata nyara hizo za serikali ili kuongeza maduhuli kwa mujibu wa sheria.

“Tumeanza kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, ambayo kiuhalisia yana ukweli mkubwa kwa hiyo tunataka kuondoa vizuizi visivyo na tija lakini pia kuwasisitizia watu wetu kule vituoni kuzingatia weledi.

“Tayari tumeanza kutumia mashine za kielektroniki za malipo yaani EFD kwenye vizuio vyetu mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro na tutaendelea kuzisambaza maeneo mengine mara tu TRA watakapoziingizia program yao ya malipo,” alisema.

Alisema wana changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vitendea kazi hususan magari lakini wanafanya jitihada mbalimbali kuhakjikisha wanazitatua ili misitu iwe na mchango kwenye pato la taifa.
    
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali Misitu wa  TFS, Mohammed Kilongo, alisema kitakwimu asilimia 94 za kaya zote takriban milioni tisa nchini zinatumia mkaa kama nishani kuu, huku maeneo ya mijini pekee ikiwa na asilimia 38 za watumia mkaa.


“Mahitaji ya miti ni mita za ujazo 62.3 huku uwezo ukiwa ni mita za ujazo 42.8 hivyo uharibifu wa misitu unafika hekta 372,000 kwa mwaka sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye miti,” alisema Kilongo.

Alisema kwa takwimu hizo, miti na misitu nchini imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa na kusababisha uhitaji wa hekta mpya 185,000 za misitu inayotakiwa kupandwa maeneo mbalimbali ya nchi.

“Upungufu huu ni kichocheo cha uvunaji haramu na holela ndani ya misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata ndani ya hifadhi za taifa hivyo suala la kuilinda ni jukumu letu sote, kila gunia lazima lilipiwe ushuru,” alisema.

Pia alisema katika jitihada za kurudisha misitu iliyopotea, upo mkakati wa kitaifa wa kupanda miti ambapo kwa kila wilaya imepewa jukumu la kupanda miti milioni moja na nusu kwa mwaka chini ya uangalizi wa Meneja misitu wa wilaya husika.

Wiki kadhaa zilizopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam, alisema nchi inageuka jangwa kutokana na misitu mingi kukatwa kiholela huku maduhuli ya serikali yakipotea.

Kauli hiyo inaonekana kuanza kuzaa matunda baada ya TFS kuamua kuongeza kasi ya usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki nchini kwa siku za hivi karibuni hatua ambayo inadaiwa kuwa endelevu.

TFS inasimamia jumla ya misitu 506 nchini ikiwemo ya asili na kupandwa, pamoja na kusimamia jamii takriban milioni 9.2 za nyuki walioko kwenye misitu hiyo maeneo mbalimbali ya nchi.


GOOD NEWS FOR ALL YAANDAA MAOMBI KUMUOMBEA RAIS.

Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Good  News For All, Askofu  Dkt. Charles Gadi akifanya maombi mara baada ya kuongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa  idara ya habari  Maelezo jijini Dar es  Salaam.GAD

Askofu Dr. Charles Gadi akiongea na wanahahabari hawapo pichani kuhusu mkutano wa maombi ya kitaifa wa kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dk. John Pombe Magufuli. maombi hayo yatafanyika geita hivi karibuni
......................................................................................................


Askofu Dkt Charles Gadi ametoa wito kwa wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli,katika mchakato wake wa kuamishia serikali makao Makuu ya nchi Mkoani Dodoma kwani ni uamuzi wa kijasiri na upaswa kuungwa mkono.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini dare Es Salaam Askofu Gadi amesema kuwa jitihada zinazofanywa na Rais magufuli ni kubwa kwani jitahada zinaonekana wazi za kuimarisha mji wa Dodoma na ili uweze kutumika kama makao makuu ya nchi.

‘’Serikali inafanya kazi nzuri kinachotakiwa ni kumtia moyo Rias wetu ili jambo ili lifanikiwe na kuhamisha serikali ili kutimiza mpango wa muda mrefu wa kuhamisha serikali kutoka Dar es Salaam na kwenda Dodoma’’alifafanua askofu Gadi

Aidha amesema Serikali imejipanga na inaandaa mazingira mazuri kwa watumishi wake watakao hamia huko kupata mahitaji yote muhimu wanayohitaji,na kuongeza kuwa jambo hilo litaharakisha maendeleo katika mikoa jirani na Dodoma.

Ameongeza kuwa imekua ni kawaida ya baadhi ya watu kulalamika kila linapotokea jambo bila kusikiliza na kufatilia jambo hilo kwa makini,amewaomba watanzania wasiwe watu wakulalamika kulaumu na badala yake wawe watu wakusiliza na kufata maelekezo.

Ameongezea kuwa watafanya maombi ya kumuombea  Rais John Magufuli na viongozi wa serikali katika mji wa buselesele wilaya ya chato mkoani Geita agosti 25 mwaka huu,kuombea mvua,amani,upendo na mshikamano baina ya serikali na wananchi wake.

 ‘’Maombi haya ni ya kumuomba Mungu alifanye taifa letu kuwa taifa bora kwa uchumi,astawi wa watuwake na linaloongoza kwa amani na mafanikio katika kila sekta ‘’alifafanua Askofu Gadi.