Monday, August 15, 2016

DC HANDENI APIGA MARUFUKU MCHEZO WA BAO NA POOL TABLE KATIKA WILAYA YAKE.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bw.Godwin Gondwe amepiga marufuku wananchi wa wilaya yake kucheza mchezo wa bao na "pool table" wakati wa mchana muda ambao ni wa kufanya kazi ili kutekeleza falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya "Hapa kazi Tu".

Gondwe alitoa kauli hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mambo mbalimbali yanayohusu wilaya yake ya Handeni ambapo alisema katika wilaya hiyo baadhi ya vijana hawana muamko wa kufanya kazi badala yake wamekua wakijishughulisha na kucheza bao na "pool table" vitu ambavyo haviwaletei maendeleo.

"Nimekataza vijana katika wilaya yangu kucheza michezo ya bao na "pool table" wakati wa kazi na nimewahamasisha kushiriki shughuli za ufugaji na kilimo kwa ajili ya kujiletea maendeleo na kuondokana na hali ya umasikini" alisema Gondwe.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwashauri wakazi wa Handeni kujishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara ikiwemo alizeti, ufuta na ufugaji wa mbuzi na kuku ili waweze kujipatia fedha zitakazowasaidia kujikimu kimaisha.

Pia Gondwe alisema kuwa wamekubaliana na Idara ya Ardhi wilayani humo kutenga maeneo maalum ya uwekezaji kwa vijana ambapo Serikali itawawezesha kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kilimo.

Amewataka vijana kujiunga katika vikundi waweze kupatiwa fedha ambazo kila Halmashauri imetenga kwa ajili ya vijana na wanawake na watumie mikopo hiyo kujikwamua kimaisha kwa kufanya shughuli za ujasiliamali.

Akizungumzia tatizo la ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo, Gondwe alisema bado anaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tatizo la maji wilayani Handeni linapungua ili wananchi waweze kuondokana na adha hiyo ambayo inawakabili kwa muda mrefu.

Alisema wananchi wa Handeni hasa wanawake wanapata tabu ya kutafuta maji safi na salama ingawa Serikali bado inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma hiyo kwa uhakika. 
 

Na Abushehe Nondo (MAELEZO). kwa hisani ya  jiachie blog.

MGOMO WA MABASI BAGAMOYO LEO TAREHE 15-08-2016



Madereva wanaofanya safari kutoka Bagamoyo kwenda Dar es Salaam, leo wamegoma kutoa huduma hiyo ili kuishinikiza Halmashauri ya Bagamoyo kupunguza Ushuru unaotozwa katika kituo cha mabasi Bagamoyo ambao ni shilingi 2000 kutoka shilingi 500 ya zamani.

Akizungumzia swala hilo makamo Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Dar Bagamoyo, Hassani Manamba, alisema madereva wamefikia  uamuzi huo kutokana na kiwango cha ushuru kuwa kikubwa kinachotozwa  kila gari inapotoka kituoni.

Alisema Halmashauri imebandika Tangazo la kubadilisha bei hiyo bila ya kuwashirikisha wahusika ambao ni madereva, ili kukubaliana au kutokubaliana na bei hiyo mpya.

Nae Makamo Mwenyekiti wa Sakosi wa umoaja wa Madereva, Manja Diksoni Mwaibula, alisema swala la kupandisha ushuru katika kituo cha  mabasi Bagamoyo halikushirikisha wadau wa usafirishaji jambo ambalo limeleta usumbufu katika utekelezaji wake.

Alisema awali malipo yalikuwa shilingi mia tano kila Gari inapotoka  ambapo sasa kila Gari inatakiwa kulipa shilingi elfu mbili kila inapotoka kituoni jambo ambalo madereva wameligomea.

Aliongeza kuwa malipo ambayo yapaswa kulipawa kila Gari inapotoka kituoni ni vigumu kutekelezeka kwakuwa kama gari itatoka mara nne kwa siku inapaswa kulipa shilingi elfu nane wakati bado hesabu ya mwenye  gari, mafuta  nk. "hii ni kutuwekea mazingira magumu ya kufanya  kazi hii", Alisema.

BAGAMOYO KWANZA BLOG imemtafuta Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Aliy Aliy Issah, ambae amekiri kuwepo kwa mabadiliko hayo na kusisitiza kuwa hiyo ni sheria iliyopitishwa kwenye Baraza la  madiwani na kusainiwa na waziri ambapo madereva walipelekewa  Tangazo kwaajili ya utekelezaji.

Mwenyekiti huyo wa Halmashauri alisema swala malipo ya ushuru ni mikakati ya Halmashauri katikia kuongeza  pato la ndani na  kwamba sheria hiyoimepitishwa kwa mujibu wa utaratibu ingawa kwenye utekelezaji wa sheria mbalimbali kunakuwa na changamoto zake.

Kufuatia hali hiyo Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, alifika katika  kituo cha mabasi ambapo aliwataka madereva kukutana na uongozi wa Halmashauri ili kujadili swala hilo na kulipatia ufumbuzi.

Abiria mbalimbali walionekana kuzagaa  katika kituo  hicho cha mabasi Bagamoyo bila ya kupata usafiri, ambapo baadhi yao wamekuwa wakikodi bajaji kwa gharama ya shilingi 5000 kutoka  Bagamoyo mpaka  Bunju, huku wengi wao wakishindwa kusafiri na  kulazimika kurudi nyumbani.

Wakizungumzia  hali hiyo Abiria katika kituo cha mabasi Bagamoyo wamesema hali hiyo imewaathiri kiuchumi kwakuwa  wengi wanaosafiri asubuhi wanwahi sehemu zao za kazi ambapo watu wengi leo wameshindwa kufika maofisini.

Aidha,  wamlisema kuwa, katika  hali kama hiyo serikali pia inapata hasara kwakuwa  haiwezi kupata mapato yake kupitia ushuru  kwakuwa Madereva  wa magari yote wamegoma jambo am balo litadhoofisha pia uchumi wa Halmashauri.

Abiria hao wameitaka Halmashauri ya Bagamoyo kukaa chini na wadau wa Usafirishaji Bagamoyo ili kuona namna ya kutatua tatizo hilo ili kufikia muafaka utakaoleta manufaa kwa pande  zote tatu, kwa maana ya Madereva, Halmashauri na Abiria.  
Makamo mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Dar. Bagamoyo, Hassani Manamba, akimueleza Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, hayupo pichani, sababu iliyowafanya wagome.
 Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, akiwasikiliza madereva katika kituo cha mabasi Bagamoyo, leo baagda ya Madereva hao kugomea ushuru wa shilingi 2000 kwa kila Gari inapotoka getini bada la ya shilingi 500 ya awali.
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawmbwa akizungumza na madereva wa kituo  cha mabasi Bagamoyo ambao wamegoma kutoa huduma usafiri kutoka Bagamoyo kwenda Makumbusho Dar es Salaam.
 Dereva wa Basi la Bagamoyo Dar. Mr. Ngomuo, akielezea kilichopelekea kugoma.

Sunday, August 14, 2016

RAIS WA ZANZIBAR ATANGAZA MSIBA NA KUSEMA KUWA MAZISHI YA MZEE ABOUD JUMBE KUFANYIKA KESHO ZANZIBAR.

unnamed

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akitoa taarifa rasmi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya pili Mzee Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea leo Mji Mwema Dar es Salaam na kuzikwa kesho katika viwanja vya nyumbani kwake Migombani Unguja.[Picha na Ikulu.]15/08/2016.
………………………………………………………………………………….
Kwa masikitiko makubwa, naomba kuwaarifu kuwa, leo tarehe 14 Agosti 2016, Mzee wetu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia.

 Kama mnavyofahamu, Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu wa Zanzibar awamu ya pili, ambaye vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Marehemu Mzee Aboud Jumbe amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na umri wake.

Msiba huu umetokea nyumbani kwake Mji Mwema, Dar es salaam. Maziko ya marehemu yatafanyika kesho tarehe 15 Agosti 2016 saa 7.00 mchana ambapo maiti yake itasaliwa katika Masjid Mshawar, Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani.

Kufuatia mchango  na juhudi mkubwa ambazo marehemu Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi alizichukua katika uhai wake kwa kuitumikia, kuiongoza na kuijenga Zanzibar pamoja na nafasi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi yetu imekabiliwa na msiba mkubwa kwa kifo cha kiongozi huyu mahiri.  

Kutokana na msiba huu mkubwa kwa nchi yetu, natangaza rasmi siku saba za maombolezo, kuanzia kesho tarehe 15 Agosti 2016. 

Katika kipindi hicho chote bendera zote zitapepea nusu mlingoti.  Kadhalika utaratibu wa maziko utafuata wasia ambao mwenyewe marehemu aliutoa wakati wa uhai wake.

Tunaungana na wanafamilia wote katika kipindi hiki kigumu cha msiba.  Naomba kutumia nafasi hii kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote.  Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie kauli thabit marehemu mzee wetu na amlaze pahala pema peponi, Amin.
Inalillahi wainnailaihi rajiun 

RAIS DKT JOHN MAGUFULI ATOA SALAMU ZA RAMBI RAMBI KUFUATIA KIFO CHA MZEE ABOUUD JUMBE

taa

MZEE ABOUD JUMBE MWINYI, AFARIKI DUNIA.

Aliyekuwa Rais wa awamu ya pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza  la mapinduzi Zanziba, Aboud Jumbe  Mwinyi, amefariki dunia hii leo nyumbani kwake mji mwema,  wilaya  ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, Taarifa ya  kufariki kiongozi huyo ambae pia aliwahi kuwa makamo wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliinea kwenye  mitandao ya kijamii mchana wa  leo.

Kufuatia Kifo hicho cha Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Dkt. John Pombe  Magufuli amemtumia salama za rambi rambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dkt. Aliy Mohamed Sheni.

Marehemu mzee Aboud Jumbe ambae alizaliwa Tarehe 14 juni 1920 amefariki akiwa na miaka 96 ambapo katika uhai wake alikuwa Rais wa pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na makamo wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (7 Aprili 1972 hadi 30 Januari 1984).

Katika salamu zake za rambi rambi Rais Magufuli alimtaja marehemu Aboud Jumbe kuwa  ni mtu mwenye mchango kubwa kwa Taifa  la Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu walioshiriki kupigania Uhuru wa Tanganyika.

Aidha, Rais Magufuli aliongeza kuwa  Marehemu Aboud Jumbe alikuwa ni mtu aliyejitoa kupigania  Uhuru, Haki, na maendeleo ya watu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Marehemu Mzee Aboud Jumbe  Mwinyi wakati uhai wake alitoa wasia ya kwamba pindi atakapofariki  katika mazishi yake kusiwe na bendi za muziki, wala kusipigwe mizinga na kuongeza kuwa jeneza lake lisifunikwe na bendera ya Taifa wala ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wasia huo wa marehemu Aboud Jumbe aliutoa  wakati wa mazishi ya aliyekuwa  rais wa awamu ya nne wa Zanzibar aliyefariki tarehe 15 Machi 2000.

Mungu ailaze roho ya Marehemu Aboud Jumbe  Mwinyi peponi, Aamiyn. Innaa lillaahi Wa innaa ilayhi Rajiuun. (Hakika sisi sote ni wa MwenyeziMungu na kwake yeye tutarejea).