TAKUKURU KAGERA YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 277.
TAKUKURU KAGERA YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 277.
Na Alodia Babara, Bukoba.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kurejesha jumla ya Sh 277.8 milioni zilizokuwa zimeporwa katika taasisi mbalimbali za umma na vyama vya ushirika, katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
Katika kipindi hicho, taasisi hiyo pia imefanikiwa kushinda kesi 45 kati ya 50 zilizofikishwa mahakamani, hatua inayoonesha mafanikio katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Hajinas Onesphory, amesema hayo Novemba 11, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba mwaka huu 2026.
"Miongoni mwa fedha zilizorejeshwa ni Sh milioni 100 zilizohusishwa na ubadhiliu wa fedha za mradi wa maji katika Kijiji cha Katare, Wilaya ya Bukoba Vijijini"amesema Onesphory
Fedha nyingine ni Sh 25.8 milioni zilizotokana na malipo yasiyo halali yaliyohusisha mtumishi wa TANESCO Kyerwa na mzabuni, pamoja na Sh 26.1 milioni za wakulima wa kahawa wa Kyamulaile AMCOS zilizokuwa zimetumiwa kwa manufaa binafsi na karani wa chama hicho James Mlinda.
Onesphory amezitaja fedha nyingine zilizorejeshwa kuwa ni Sh 59.2 milioni katika Chama cha Ushirika wa Kahawa Wilaya ya Ngara (Ngara Farmers), Sh15 milioni katika Kijiji cha Rwinyana na Sh 5.5 milioni katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.
Aidha, TAKUKURU imefanikiwa kurejesha Sh 26.6 milioni katika Manispaa ya Bukoba, Sh 5.3 milioni Omkishanda AMCOS na Sh 5.2 milioni zilizokuwa katika akaunti ya kikundi cha wanawake wavuvi (WAVUKE), Kata ya Nkwenda, Wilaya ya Kyerwa.
Amesema fedha hizo zote zilirejeshwa baada ya TAKUKURU kufanikiwa kushinda kesi mahakamani, ambapo watuhumiwa walikutwa na hatia na kupewa adhabu mbalimbali, ikiwemo vifungo vya jela na faini kulingana na makosa yao.
Katika hatua nyingine, Onesphory amesema taasisi hiyo imefuatilia matumizi ya Sh bilioni 8.9 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 67 ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU Mkoa wa Kagera imepokea jumla ya taarifa 252 kutoka kwa wananchi na vyanzo mbalimbali, ambapo taarifa 131 zilihusu tuhuma za rushwa, huku taasisi hiyo ikiendelea kuimarisha ushirikiano na wananchi katika kudhibiti vitendo vya rushwa na kulinda rasilimali za umma.
Dickson Laurian mkazi wa manispaa ya Bukoba amepongeza hatua zinazochukuliwa na TAKUKURU huku akiwataka kuongeza uwajibikaji na ujasiri katika kushughulikia maswala ya rushwa.
Eginatha Mukama amesema, TAKUKURU waendelee kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo,kuwasaidia wananchi wanaotapeliwa ili kurejeshewa fedha zao na kuchunguza watumishi na viongozi wanaotuhumiwa kwa rushwa.


Comments
Post a Comment