Tuesday, September 17, 2024

MADAKTARI BINGWA WA MAMA SAMIA WAWEKA KAMBI MKOANI LINDI

 

Na Hadija Omary, LINDI.


Wananchi Mkoani Lindi wametakiwa kutumia siku sita za ujio wa madaktari bingwa na ubingwa bobezi wa Rais Samia kupata huduma za kibingwa kwa karibu katika hospitali za Wilaya  za Mkoa huo


 

Rai hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dkt Kheri Kagya Jana  septemba 16, 2024 wakati wa kuwapokea madaktari hao bingwa na bingwa bobezi wa Rais Samia katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa lindi kisha kuwakabidhi kwa waganga wakuu wa halmashauri sita za mkoa huo



Madaktari hao watakuwepo kwa muda wa siku 6 kuanzia Jana Septemba 16 hadi 21 wakitoa huduma za kibingwa kwenye hospitalli zote za halmashauri Mkoani Lindi lengo likiwa  kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi na wananchi pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa afya kwa ngazi ya halmashauri kutoa huduma hizo za kibingwa.



Dkt. Kagya ametaja madaktari waliopokelewa ni pamoja na madaktari bingwa wa huduma za magonjwa ya kike na uzazi, upasuaji, mfumo wa mkojo, magonjwa ya ndani, huduma za mifupa, watoto, ganzi na usingizi.



Amesema huduma hizo zitatumia bima na kwa wagonjwa wasio na bima watamuona daktari na Kuchangia Kiasi kidogo kwa utaratibu wa kawaida kama atahitajika kupata huduma nyingine ikiwemo vipimo, upasuaji na dawa.



Awali, akizungumza Mwakilishi kutoka Wizara ya afya ambaye pia na mratibu wa madaktari hao waliotoka hospitali mbalimbali hapa Nchini  Faraja Mgeni amewakumbusha Madaktari kwenda kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kuzingatia maadili ili kutimiza lengo la Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Wizara ya Afya kwa wananchi huku akiomba waganga wakuu kwenye halmashauri kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kutimiza majukumu yao.





Thursday, September 12, 2024

MAGEUZI MAKUBWA WAKALA WA VIPIMO (WMA)

 

Na Albert Kawogo 


SERIKALI kupitia Wakala wa vipimo nchini (WMA)imefanya mageuzi makubwa yanayolenga kumlinda mlaji kwenye huduma na ubora wa vipimo vinavyotumika kwenye sekta za biashara, afya na mazingira.


 Mtendaji Mkuu wa WMA Alban Kiula amesema hayo jana wakati akiongea Jijini Dar es Salaam na Wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ukiwa ni mfululizo wa vikao vya Taasisi za Umma zilizoko chini ya msajili wa hazina. 


Kiula alisema WMA ina jukumu kubwa la kuilinda jamii kwenye athari zinazotokana na matokeo ya upimaji usio sahihi katika biashara na maeneo mengine mtambuka.


"Unaweza usiione hii hali lakini kuna madhara makubwa kijamii yatokanayo na upimaji usio sahihi hasa kiuchumi" Alisema Kiula


Mtendaji Mkuu alisema jukumu la WMA  haliishii tu kwenye kusimamia na kudhibiti vipimo bali pia taasisi hiyo inatoa ushauri wa kitaalam kuhusiana na vipimo Kwa serikali, mashirika ya umma na Taasisi binafsi.


Pia Kihula alisema moja ya mafanikio makubwa ya WMA ni kuongezeka kwa idadi ya vipimo vinavyohakikiwa na kuendelea na ununuzi wa vifaa vya kitaalam ambapo yote haya yameipa thamani taasisi hiyo


Akizungumza kwa niaba ya Wahariri Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Deodatus Balile alisema kazi kubwa ya kupongezwa imefanywa na WMA lakini bado changamoto ipo kwenye uchache wa watendaji kwakuwa jukumu lao kama WMA lina wigo mpana wa kiutendaji hasa kwenye yale maeneo yanayogusa walaji Kwa bidhaa za chakula na vifaa vya ujenzi.

Tuesday, September 10, 2024

SHARIFA MKWANGO MWENYEKITI MPYA TWFA MKOA WA LINDI

 






NA HADIJA OMARY, LINDI.

Sharifa Mkwango ameshinda kuwa Mwenyekiti mpya wa chama cha mpira wa miguu Wanawake  (TWFA) Mkoa wa Lindi atakaehudumu nafasi hiyo kwa muda wa miaka mitano  baada ya kushinda kwa Kura za ndio

Uchaguzi huo umefanyika Jana huko Manispaaa ya Lindi ambao ulihusisha pia nafasi za wajumbe wawili wa kamati tendaji ambao ni Bi. Subira  Mwangata na Beatrice Victor pamoja na nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa (TWFA) Bi.Sifa Mwaya 

Akifungua mkutano huo  Afisa Michezo wa Manispaa  ya Lindi Jamal Lisuma  kwa niaba ya Katibu tawala wa Wilaya ya Lindi hudhaifa Rashid aliwataka  viongozi watakaochaguliwa kutatua changamoto zilizopo Katika Mkoa wa Lindi upande wa soka la Wanawake ikiwemo kuongeza vilabu vya timu za Wanawake na kuanzisha ligi ya Wanawake Ngazi za Wilaya na Mkoa 

Amesema lengo la hayo yote ni   kutafuta vipaji vya wachezaji  hao wanawake wanaoweza kuunda timu ya Mkoa inavyoweza kushiriki ligi kuu ya Wanawake Tanzania Bara.

Kwa upande wake Bi Sharifa Mkwango Mwenyekiti mpya wa (TWFA) ameahidi kufanya uhamasishaji kwa Jamii kuona Umuhimu wa kuwekeza Katika Michezo kwa watoto wa Kike.

Katibu wa kamati ya Uchaguzi Fidea Mnunduma amewapongeza wajumbe kwa kutimiza wajibu wao na kutenda haki  kwenye uchaguzi huo  na kwamba Kura zimepigwa vizuri hakuna zilizoharibika kila Mmoja ametumia  haki yake kwa kutimiza wajibu wake


"Kamati ya uchaguzi inawashukuru wajumbe wote  kwa ushirikiano uliouonysha lakini Leo mmeweza kupata viongozi wapya wa TWFA kamati ipo itadumu kwa miaka minne kama mutakuwa na tatizo lolote  kamati imefungua milango njooni mtuone"

Monday, September 9, 2024

DKT. BITEKO ASHIRIKI DUA YA MZEE MAJID NSEKELA

 




Na Alodia Dominick, Kyerwa.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dkt. Doto Biteko ameiasa jamii kuwa na utaratibu wa  kuwatunza na kuwajali  wazazi wao, amesisitiza upendo miongoni mwa jamii na kuendelea kuwaombea ambao hawapo hai.


Dkt. Biteko ameyasema hayo Septenba 7, 2024 akiwa Nyakatuntu, wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera wakati aliposhiriki katika dua ya kuwaombea baba mzazi na ndugu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela



“ Tuendelee kuwakumbuka na kuwaombea ndugu na wazazi waliotangulia mbele za haki ni jambo zuri na wajibu wetu tuliobaki, Sheikh wetu katika mawaidha yake ameliongelea kwa uzuri sana. Tulitilie maanani na sote tuendelelee kufanya hivi, na kama huwa hatuwafanyii hivi ndugu zetu, hatuna budi tuanze kwa moyo wote.” Amesema Dkt. Biteko.

 


“Ndugu zangu tusisahau mapito yetu, Katika mapito huwa kuna watu, Katika watu hawa, kuna wazazi wetu, Kama wazazi wako wapo hai, mmoja au wote au wale waliokulea, jua nawe una wajibu wa kuwalea na kuwatunza, siyo kifedha tu bali pia kwa mahusiano mema hasa ya kihisia kwa kuwa hivyo ndivyo impendezavyo Mungu.”ameongeza Dkt Biteko 


Ametolea mfano wa  Rais wa awamu ya pili, Marehemu Ally Hassan Mwinyi, Mzee Rukhsa kuwa aliiasa jamii kuwa maisha hapa duniani si kitu ila ni hadithi tu na kuwa wayafanye maisha yao yawe hadithi nzuri. 


"Kwa dua hii, kwa umati huu, kwa wanafamilia hawa wa Nsekela inadhihirisha bayana kabisa kuwa maisha ya Mzee wetu, Alhaji Tibihika Mussa Nsekela, na wengine tuliowaombea dua leo hapa yameacha hadithi nzuri kwa sisi tuliobaki hili ni jambo zuri la kujifunza.”

 

Aidha, Dkt. Biteko ameendelea kuiasa jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao wanapotoka, kuendelea kuishi kwa upendo sambamba na kuishukuru familia hiyo kwa kumualika kushiriki katika dua hiyo.

 

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali  imeendelea na jitihada zake mbalimbali za kuwaletea maendeleo wananchi wa Nyakatuntu kwa kutekeleza miradi mbalimbali katika Wilaya ya Kyerwa  na tayari imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi wa barabara.


Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuber amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Majid Nsekela kwa kuandaa dua hiyo kwa ajili ya baba yake na kusema kwa kufanya hivyo inaonesha anaipenda familia yake na dini yake ya kiislamu.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Majid Nsekela amesema kuwa tukio hilo kwao ni la kihistoria na wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo.


“Kwa dua hii ya leo tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko pamoja na kuwa na kazi nyingi amejumuika nasi hapa na wote mliopo nasi leo kwa upendo wenu na familia yote imefurahi na inawashukuru,” amesema  Nsekela.


Aidha, Majid amewakumbusha na kuwatakia heri wananchi wa Nyakatuntu kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za 

Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu kwa kuchagua viongozi wanaofaa.