Monday, July 29, 2024
Sunday, July 28, 2024
SWEETBERT NKUBA AAHIDI KULETA MABADILIKO TLS.
KATIBU MKUU CCM, DKT NCHIMBI AZURU KABURI LA HAYATI MKAPA.
NANI KUUKWAA URAIS WA TLS UCHAGUZI WA IJUMAA?
Na Mwandishi Wetu
KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambao unatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa wiki hii zinaendelea kupamba moto ambapo wagombea wanaendelea kunadi sera wakitaka kufanya mabadiliko kwenye taasisi hiyo.
Mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Sweetbert Nkuba, alisema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa anataka nafasi hiyo ili akapambane na mawakili ambao hawana sifa ya kufanyakazi hiyo.
TLS ni taasisi muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mfumo wa sheria na haki nchini Tanzania na kwa mwaka huu wagombea wa nafasi ya urais kwenye uchaguzi huo watakuwa sita, ambao ni Boniface Mwabukusi, Emmanuel Muga, Ibrahim Bendera, Paul Kaunda, Revocatus Kuuli na Sweetbert Nkuba.
Nkuba alisema anauzoefu wa muda mrefu wa uongozi katika ngazi mbalimbali na kuomba achaguliwe kwenye nafasi hiyo ili afanikishe vipaumbele vitano ikiwemo kuwaunganisha wanachama wa TLS na kuhakikisha maslahi ya kiuchumi ya wanachana wa chama hicho yanazingatiwa.
“Nikichaguliwa nitahakikisha wanachama wote wa TLS wanakuwa na bima ya afya, bima ya maisha, nitaaanzisha kituo cha malezi kwa wanachama wanaochipukia, kuimarisha uhusiano baina ya wanachama wa TLS, Serikali, mahakama na jamii kwa ujumla,” alisema Nkuba
Mgombea mwingine Wakili Paul Kaunda amejinadi kuwa yeye si mgeni kwenye uongozi kwani amefanyakazi kwa miaka 10 katika maeneo mbalimbali ya sheria hasa sheria za jinai na madai na ni mdau mkubwa sana kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda yaani akili bandia (AI).
Alisema kwamba yeye pia siyo mgeni wa kuongoza taasisi kama TLS kwani 2019 -2020 alipata bahati ya kutumika kama Mjumbe wa Baraza la Uongozi na Mjumbe wa Kamati ya Sheria na Katiba ya TLS kwa miaka mitano.
“Nimedhamiria kuleta heshima kwa TLS na nyote ni mashahidi kwamba heshima ya chama hiki imeshuka sana kwa hiyo nitakwenda kurejesha heshima hasa sisi mawakili tunapowawakilisha wateja wetu wakiwa polisi, magereza na mahakamani,” alisema
Naye Ibrahim Bendera alisema amefanyakazi ya uwakili kwa miaka 18 upande wa Tanzania Bara na miaka 19 kwa upande wa Zanzibar hivyo amejipima na kuona anatosha kuongoza chama hicho hasa wakati huu ambapo Rais wa chama hicho ataongoza kwa miaka mitatu badala ya mwaka mmoja.
“Zamani Rais alikuwa anahudumu kwa mwaka mmoja sasa kwa mwaka mmoja siyo rahisi kuleta mabadiliko kwa hiyo baada ya mabadiliko na kuweka ukomo wa miaka mitatu nimeona nitapata nafasi ya kulieleza Baraza la Uongozi maoni yangu na mpango mkakati wa TLS unaisha mwaka huu kwa hiyo nitaweka msukumo wa kutengeneza mkakati mpya,” alisema
Alisema kwa mwaka TLS yenye wanachama 12,000 inapata wastani wa bilioni 1.2 na inalipa mishahara inayofikia shilingi milioni 80 kwa mwezi hivyo akichaguliwa atahakikisha anapunguza gharama za matumizi na kuwawekea mazingira mazuri mawakili vijana waweze kupata uzoefu.
Revocatus Kuuli yeye alisema yeye amekuwa wakili kwa miaka 13 Tanzania Bara na wakili Zanzibar kwa miaka minne na kwamba katika mawakili 13 waliosajiliwa na Mahakama ya Afrika iliyopo mkoani Arusha yeye ni miongoni mwao.
Alisema anafanyakazi pia kwenye Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya IRMCT yenye Makao yake Makuu Geneva Uswis na Arusha Tanzania na kwamba ametumikia nafasi mbalimbali serikali na ngazi yake ya mwisho serikalini alikuwa ofisa Wizara ya Katiba na Sheria.
Naye Wakili Emmanuel Muga alisema amekuwa wakili kwa miaka 12 hivyo amejipima na kuona kuwa anaweza kumudu majukumu ya kuwasimamia mawakili wenzake kama atachaguliwa kushika nafasi hiyo kwenye uchaguzi ujao.
Alisema amekuwa mwenyekiti wa TLS mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili akianzia 2019 mpaka 2021 na kwamba fursa hiyo ndiyo ilimpa nafasi ya kuwafahamu mawakili na mahitaji yao na nini kifanyike ili chama hicho kiweze kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
“Nikiwa mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Dar es Salaam nilifanikiwa kuunda kamati nane na zilileta mageuzi makubwa sana tunayoyaona kwa Chapter ya chama chetu hapa Dar es Salaam kwa hiyo mafanikio haya ndiyo yamenifanya nione ninaweza kuongoza chama hiki kwa ubora,” alisema
Boniface Mwabukuzi alisema anataka nafasi hiyo ili kuleta mageuzi ambayo kwa muda mrefu yameshindikana ikiwemo kupambana na mafisadi kwenye chama hicho na nje ya chama.
Alisema TLS kwa muda mrefu imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kusaidia wanachama kutokana na watu wanaochaguliwa kuiogopa serikali hali ambayo iliwafanya washindwe kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa TLS.
Thursday, July 25, 2024
SHAHIDI AELEZA MUME WAKE ALIVYOPIGWA NA NATHWANI MPAKA KUZIMIA.
Na Mwandishi Wetu
SHAHIDI Kiran Lalit Ratilal (52), ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jinsi mume wake alivyopigwa na mshtakiwa Bharat Nathwan (57) hadi kupoteza fahamu kutokana na ugomvi ambao ulikuwa unaendelea wa baina yao kuhusu ujenzi uliyokuwa unaendelea katika eneo la makazi yao.
Nathwan pamoja na mke wake Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, Kiran alidai kuwa anakumbuka Julai 21, 2023 alikuwa nje ya akiendelea na majukumu yake nanpia shughuli za mapambo zilikuwa zinaendelea nyumbani kwake mafundi wakiweka vigae.
Alidai kuwa, mshtakiwa Sangita alitoka ndani akaanza kupaza sauti akitaka atoe malighafi (material) yote yaliyokuwepo kwenye kibaraza hicho, wakati yote yapo upande wa Kiran Lalit Ratilal na sio upande wake.
"Aliendelea kupaza sauti mimi nikamjibu kwamba nitaondoa baada ya mafundi kumaliza kazi, nilipomjibu akaanza kutumia lugha chafu akidai hataki kusikia chochote na kwamba niondoe uchafu wangu,"
"Nilijaribu kumuelewesha, lakini hakunielewa ndipo nilipompigia simu mume wangu akakuchukua dakika tano aafika pale, wakati anafika na mume wa mshtakiwa Sangita nae akafika kwa maana ya Bharat,"alidai Kiran
Kiran alidai kuwa baada ya waume zao kufika kwa pamoja, akajaribu kumuelewesha Bharat kutokana na aliyoyasema mke wake (Sangita), lakini hakumulewa na pia mume wake alijaribu kuwaelewesha nankuwataka wakayazunguze lakini hawakuelewa.
"Sangita alianza kutumia maneno machafu tena, na nilipomuelewesha mume wake kuhusu maneno machafu ya mke wake alikaa kimya, mume wangu akaniambia kama hawajamuelewa awaache,"alidai
Alidai kuwa baada ya kumalizia hiyo sentensi, Bharat alimrukia mume wake na kuanza kumpiga kwa kumkandamiza kifuani na kumpiga mateke.
"Aliendelea kumpiga mume wangu nilipoenda kuamulia Bharat alinishika kichwa changu na kukitumbukiza kwenye ndoo ambayo ilikuwa na mchanganyiko wa saruji na kisha akaendelea kumpiga mateke,"
" Watu wote waliyokuwepo kwenye eneo hilo wakaanza kumsukuma Bharat ndipo alipoanicha mimi na kumfuata tena mume wangu akaanza kumpiga akadondoka chini akapoteza fahamu, muda huo uso wangu, macho na masikio yalikuwa yamejaa saruji ila nilikimbia kumsaidia ila hakuweza kuamka,"alidai Kiran
Kiran alidai kuwa alimuita mtu wa ofisini ili aweze kumsaidia ndipo alipompa simu yake akaanza kuchukua picha, mshtakiwa Sangita baada ya kuona hivyo alichukua simu hiyo ili aitupe wakati hayo yote yanaendelea mume wake alikuwa amelala chini.
"Nilifikiria njia ya kumsaidia mume wangu, mafundi walimbeba hadi sakafu ya pili ndipo akaanza kuzinduka akapewa maji, wakamkimbiza hospitali kwa ajili ya kupata huduma ya kwanza. Niliondoa saruji baada ya mume wangu kuzinduka, aliulizia simu yake akaanza kupiga simu,"
"Niliona wanaume wawili wakiwa wamevaa nguo za polisi, taratibu macho yangu yakaanza kupoteza uono kwa sababu ya ule mchanganyiko. Waliniambia natakiwa niende Kituo cha Polisi Kati kuripoti wakanishauri niite gari la wagonjwa kwa sababu nilikuwa siwezi kutembea vizuri,"alidai
Alidai alifanikiwa kuita gari hilo, wakati hayo yote yakiendelea Bharat aliendelea kutoa maneno machafu na za kitishio ya maisha, gari hilo lilimpeleka hadi kituoni hapo akapewa fomu moja akiwa na mume wake akampelekwa Hospitali ya Mnanzi Mmoja kwa matibabu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 6,2024, baada ya Wakili wa washtakiwa hao Edward Chuwa kuomba ahirisho kwa sababu alikuwa anakwenda kwenye shauri lingine mahakama ya juu, siku atamuuliza maswali ya dodoso shahidi.
MAAFISA UANDIKISHAJI DAFTARI LA MPIGA KURA KAGERA WALA KIAPO
Na Alodia Dominick, Bukoba,
Maafisa uandikishaji ngazi ya wilaya na maafisa ugavi mkoani Kagera wamekula kiapo ili kwenda kutekeleza shughuli mbalimbali za tume huru ya Taifa ya uchaguzi.
Watu hao wa wameapishwa Julai 25,2024 na Hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Bukoba Frorah Kaijage uapisho uliofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa huo.
Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili mgeni rasmi Jaji mstaafu Mbarouk S Mbarouk amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi zao kwa ueledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hilo na kuwaelekeza wengine ambao hawakuwahi kushiriki zoezi kama hilo.
“Wakati wa uboreshaji wa daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura, jambo hili ni muhimu na litasaidia kuleta uwazi wa zoezi zima pia mawakala watasaidia kuwepo uwazi ili kupunguza kuwepo kwa vurugu zisizo za lazima”
Aidha alisema kuwa, tume imetoa vibali 157 vya asasi za kiraia kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na waangalizi wa zoezi la uboreshaji 33 watakaotazama zoezi la uboreshaji daftari la mpiga kura.
Kwa upande wake mratibu wa uandikishaji mkoa wa Kagera Mapinduzi Severian ametaja vituo vya uandikishaji mkoa wa Kagera kuwa vitakuwa 1,778 katika majimbo tisa na halmashauri 8 za mkoa huo.
Hadi sasa wameshafanya usaili kwa watendaji ngazi ya vituo na watakuwa na mafunzo ya siku mbili kuanzia Agosti 02 hadi Agosti tatu mwaka huu.
“Uandikisha katika mkoa wetu utaanza Agosti 05 hadi Agosti 11, mwaka huu, hivyo niwaombe wananchi uandikishaji utakapoanza basi wajitokeze kwa wingi na wakajiandikishe vituo vitakuwa karibu na wananchi”
Aidha amesema kwa upande wa wilaya ya Muleba ambapo kuna visiwa vingi wamesha andaa boti na watendaji wa kwenda kufanya kazi huko hivyo hawatarajii changamoto yoyote katika zoezi la uandikishaji.
Naye mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Jacob Nkwela amesema kuwa, wao kama manispaa wamejipanga kuendesha zoezi la uandikishaji kikamilifu.
Amesema manispaa wanazo kata 16 na mitaa 66 ili wananchi waweze kujiandikisha kwa urahisi wameweka vituo 85 ambavyo vitakuwa katika maeneo rafiki kila mmoja kujiandikisha kiurahisi na kila mmoja atawajibika kwenda kuboresha taarifa zake na wale ambao wametimiza miaka 18 wanatakiwa wakajiandikishe.