Tuesday, April 21, 2020

MAMA SALMA ATOA SARUJI MIFUKO 50 SHULE YA MSINGI KIDONGO CHEKUNDU BAGAMOYO.

 Mbunge wa kuteuliwa ambae pia ni mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Mama Salma Kikwete ametoa msaada wa saruji mifuko hamsini kwa shule ya msingi kidongo chekundu iliyopo kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo.


Alisema hatua hiyo ya kukabidhi saruji mifuko hamsini ni hatua ya mwanzo ya kutekeleza ahadi yake aliyoiweka kwenye mahafali ya darasa la saba ya kutoa mifuko mia moja ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

       
"Nimeahidi kutoa mifuko ya saruji mia moja lakini kwa sasa nimeanza na hii hamsini na baada ya muda nitamalizia iliyobaki" alisema mama Salima.



Aidha, mama Salma amewataka viongozi na wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona ambao umekua ukienea kwa kasi nchini na kuuwa watu wengi duniani kote.


Mama Salma Kikwete aliwasisistiza viongozi hao kufikisha ujumbe kwa familia zao na   wananchi katika maeneo yao juu ya umuhimu wa kuwa makini na ugonjwa huo wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19)


Naye Diwani wa kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo, Abdul Pyallah ameelezea furaha yake wakati wa kupokea mifuko hiyo kwani kwa kiasi kikubwa itainua maendeleo ya elimu shuleni hapo kwakuwa shule hiyo ina changamoto kubwa hasa za
madarasa hali inayoepelekea adha katika suala la kujifunza


Pyalla alisema yeye kama Diwani anapambana kutatua baadhi ya changamoto hivyo anapata faraja anapoona watu wenye moyo wa kujitolea kama mama Salma Kikwete wanapoingiza nguvu zao katika maendeleo ya kata hiyo.


Aidha viongozi wengine pamoja na kamati ya shule hiyo wametoa shukrani zao za dhati juu ya kutekelezwa kwa ahadi hiyo na moyo wa mama huyo wa kutoa na kumuomba asiwachoke kuwasaidia.
 
Sehemu ya Saruji hiyo iliyotolewa na mama Salma Kikwete katika shule ya msingi Kidongo Chekungu wilayani Bagamoyo.

 
Diwani wa kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo, Abdul Pyallah, akiwapanga watu kwa umbali wakati wa kumpokea mgeni rasmi mama Salma Kikwete, ikiwa ni tahadhari ya kujinga na maambukizi ya Virusi vay Corona.
 


No comments:

Post a Comment