Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Mheshimiwa Zainabu Rashidi Kawawa, akizungumza na wananchi katika Halmashauri ya Chalinze kuhusu kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi ya Corona.
......................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Mheshimiwa
Zainabu Rashidi Kawawa, amewataka wananchi wilayani humo kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wizara ya
Afya dhidi ya Mapambano ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya
Corona yaani COVID-19.
Mheshimiwa Kawawa ametoa maagizo hayo
jana katika ziara yake aliyoifanya na timu ya Mapambano dhidi ya homa kali ya
mapafu ya halmashauri ya Chalinze Katika Vijiji vya Lugoba, Msata, Kiwangwa na Mji Mdogo wa Chalinze.
Kawawa alitoa
tahadhari kwa wananchi hao kwa kueleza hali halisi ya gonjwa hili la COVID-19
lilivyoikumba Dunia, ikiwemo Tanzania na mikoa yake.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaeleza
wananchi hali halisi ya tatizo hili kwa kuwajuza kuwa hata Mkoa wa Pwani kuna
wagonjwa wa Corona, hivyo tuna kila Sababu ya kuchukua tahadhari za kujikinga
na huu ugonjwa.
Katika mazungumzo yake aliwataka
wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na safari zisizo na ulazima ili
kulinda Afya zetu na familia zetu.
Aidha aliwataka wananchi kutumia
Balakoa kama kinga dhidi ya maambukizi ya Corona na kutumia vitakasa mikono na
maji yanayotiririka kunawa mikono muda wote, pia alitumia muda kutoa onyo kwa
wafanyabiashara watakaopandisha bei kwa vitendea vinavyotumika katika Mapambano
dhidi ya homa kali ya mapafu.
"Ole wao watakao pandisha holela
bei ya vifaa vinavyotumika katika Mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu kama
ndoo, sabuni, vitakasa mikono, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwa
ni pamoja na kufungiwa biashara zao." Kawawa alisema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya
Dkt Kyungu, alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa mara moja endapo wataona mtu
yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Corona bila kuchelewa kwa hatua zaidi, na
kuwataka wananchi kufuata kanuni na miongozo iliyotolewa na wizara ya Afya
dhidi ya Mapambano ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona,
COVID-19.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka, alitoa maelekezo kwa watendaji wa
halmashauri kuanzia ngazi ya Kijiji hadi wilaya kuelimisha wananchi namna ya
kupambana na Corona sanjari na kuwataka wananchi wa Chalinze kula vyakula vya
vitamini"C" ili kuimarisha kinga za miili kama njia mbadala ya
kupambana na Corona.
"Tutumie vyakula vya vitamini C
na mboga za majani, kwani hivi vyote vinapatikana Katika Mazingira yetu ili
kupambana na janga hili. Mkurugenzi alisisitiza.
No comments:
Post a Comment