Wednesday, April 8, 2020

KAWAMBWA AKABIDHI PIKIPIIKI TATU KWA KIKUNDI CHA BODABODA (UMABOS G4)

 
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) akikabidhi pikipiki tatu kwa kikundi cha waendesha bodaboda kilichopo kitongoji cha Benki kata ya Dunda jimboni humo, pembeni yake ni Diwani wa Dunda, Dickson Makamba.

 Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) akizungumza na wanakikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4). 
....................................


Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa amekabidhi pikipiki tatu kwa kikundi cha waendesha bodaboda kilichopo kitongoji cha Benki kata ya Dunda jimboni humo.


Pikipiki hizo ambazo zimenunuliwa kutokana na mkopo uliotolewa na halmashauri ya Bagamoyo kwa vijana, zimekabidhiwa kwa kikundi hicho kinachojulikana kwa jina la Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4).


Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, Mbunge huyo wa jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa amewapongeza vijana hao kwa kuchangamkia fursa na kwamba wao ni mfano wa kuigwa.


Alisema Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli inawajali wananchi wa hali ya chini ndiomana kila halmashauri kuna mfuko kwaajili ya vijana, kinamama na walemavu ambapo makundi hayo hukopeshwa na kurejesha bila ya riba.


Kawambwa amefurahishwa na kikundi hicho kwa kitendo chao cha kuchangamkia fursa kwa kusajili kikundi haraka na kupata mkopo wa halmashauri.


Alisema amefurahishwa kwakuwa yeye alikuwa miongoni mwa washauri wa kikundi hicho toka kuanzishwa kwake jambo ambalo limepa faraja kuona kuna vijana wanaopenda kujituma kwa kujishughulisha na shughuli za halali.


Alisema serikali haiwezi kumpa fedha mtu mmoja mmoja lakini inatoa kwa vikundi ili iwe rahisi kuwahudumia watu wengi wenye uhitaji kwa wakati mmoja.


Aliongeza kuwa,  kikundi hicho kinavyokuwa na kuongeza pikipiki kitasaidia vijana wengine ambao wataendesha pikipiki za kikundi huku nao wakijipatia kipato cha kujikimu na familia zao.


Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Dunda, Dickson Makamba amewapongeza vijana hao na kusema kuwa hao ni vijana wa mfano katika kata yake.


Alisema kikundi hicho hakina muda mrefu toka kuanzishwa kwake lakini mafanikio yake ni makubwa katika kipindi kifupi ukilinganisha na vikundi vingine ambavyo vina muda mrefu.


Aihda, Makamba alisema iko haja ya kuendelea kukisimamia kikundi hicho ili kiweze kufikia malengo yake waliyojiwekea.


Makamba alimueleza Mbunge kuwa, iko haja ya kuwaongezea nguvu vijana hao kwa kuangalia uwezekano wa kuwatafutia bajaji ili waendelee na kazi ya kusafirisha abiria wao hata katika kipindi cha mvua.


Awali akisoma taarifa ya kikundi Katibu wa kikundi hicho Abdalla Shabani Jongo alisema malengo yao ni kupata pikipiki tano na kwamba mpaka sasa wamefanikiwa kupata pikipiki tatu tu.


Alisema pikipiki hizo tatu walizopkoe ambazo zimetokana na mkopo wa shilingi milioni nane kutoka Halmashauri ya Bagamoyo zinawawezesha kupata fedha ya marejesho ili waendelee kujenga uaminifu kwa halmashauri na baadae waweze kukopa fedha nyingi zaidi kwaajili ya kujiendeleza kiuchumi.
 
Diwani wa kata ya Dunda wilayani Bagamoyo, Dickson Makamba, akizungumza na wana kikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4). 
 
 Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, alipowasili katika ofisi ya kikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4).
 
 Vijana wa kikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4). wakifurahia mara baada ya makabidhiano hayo yalihudhuriwa na Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa. 

No comments:

Post a Comment